Na Kambi Mbwana, Dar es Salaam
Wachezaji wawili kutoka
Tanzania wamechaguliwa miongoni mwa 50 waliofanyiwa majaribio nchini Uganda kwa
ajili ya kuingia katika kituo cha kuendeleza vipaji (centre of excellence)
kilichoko Doha nchini Qatar kupitia mpango wa kukuza vipaji wa Aspire Football
Dream.
Msemaji wa TFF, Boniface Wambura
Taarifa iliyotumwa katika vyombo vya habari na Ofisa Habari wa Shirikisho la Soka nchini (TFF), Boniface Wambura, alisema kuwa Abdulrasul Tahir Bitebo
(15) ambaye ni mshambuliaji kutoka Kituo cha Uwanja wa Karume, na Martin Omela
Tangazi (14) ambaye ni beki kutoka Kituo cha Ukonga ndiyo waliochaguliwa kutoka
Tanzania kuingia katika kituo ambapo watakaa kwa mwezi mmoja kabla ya kusaini
mkataba rasmi wa kuendelezwa.
Wachezaji wengine
walikuwa wakitoka katika nchi za Uganda na Kenya. Mchezaji mwingine aliyefuzu
katika nafasi tatu zilizokuwepo ni kutoka nchini Kenya.
Mpango wa Aspire
Football Dream unafadhiliwa na Mtoto wa Mfalme wa Qatar katika nchi 16 duniani,
na kwa hapa nchini uko chini ya Idara ya Ufundi ya Shirikisho la Mpira wa Miguu
Tanzania (TFF).
TFF ina jumla ya vituo
14 vya kuendeleza vipaji kupitia mpango huo wa Aspire Football Dream. Vituo
hivyo ni Karume, Kigamboni, Tandika, Kawe, Ukonga, Kitunda, Mbagala, Magomeni,
Makongo, na Tabata vilivyo katika Mkoa wa Dar es Salaam. Vingine ni Bagamoyo
kilichopo mkoani Pwani, Morogoro, Arusha na Moshi mkoani Kilimanjaro.
Kituo kingine cha kuendeleza vipaji (centre of excellence)
cha Aspire kipo Dakar nchini Senegal.
No comments:
Post a Comment