Na Mwandishi Wetu, Dodoma
BUNGE leo limepitisha Bajeti ya Shilingi Trilioni 18.2, kwa ajili ya kutumika mwaka wa fedha wa 2013 na 2014, huku Wabunge 35 wakisema hapana katika mchakato wa kuipigia kura bajeti hiyo.
Waziri wa Fedha na Uchumi, Dk. William Mgimwa.
Aidha, Bunge zima lilikuwa na wabunge 270, huku 35 wakiikataa na wabunge 235 kusema ndiyo.
Kwa sababu hiyo basi, serikali
sasa itakuwa imepitisha bajeti yake, huku Waziri wa Fedha, Dk William Mgimwa,
akitumia dakika kadhaa jioni ya leo kujibu hoja za wabunge, yakiwamo malalamiko
ya msamaha wa kodi kwa bajaj na kusema kuwa wamesikiliza maoni ya wabunge.
Mara baada ya mchakato huo wa
upigaji wa kura kumalizika, Spika wa Bunge, Anne Makinda, alitumia fursa hiyo
kuikumbusha Wizara ya Fedha juu ya kusimamia vyema fedha hizo kwa ajili ya
kutumika kama zilivyopangwa kwa ajili ya maendeleo ya Taifa.
Hata hivyo, kulikuwa na
burudani ya aina yake katika upigaji wa kura wa kuipitisha bajeti hiyo, hasa
pale sauti za baadhi ya wabunge kusikika zikisema ‘maandamano’ na kushangaza
kwa kiasi fulani.
Wa kwanza kuulizwa juu ya
kuikubali ama kuikataa bajeti hiyo alikuwa ni Waziri Mkuu, Mizengo Peter Pinda,
ambaye bila ajizi aliipitisha moja kwa moja na kufuatiwa na mawaziri na manaibu
waziri, ambapo baadaye walifuata wabunge waliokuwa bungeni.
Hata hivyo, ukiacha Mbunge
machachali, Tundu Lissu kutoka Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema),
aliyeipitisha bajeti hiyo, wabunge wengi wa chama chake hawakuwapo bungeni.
Ndio hao waliokuwa wakiitwa na
kusikika wabunge waliokuwapo wakisema maandamano na kuleta kicheko kwa wabunge
wengine bungeni na wale waliokuwa wakifuatilia kikao hicho kwa televisheni.
No comments:
Post a Comment