Na Kambi Mbwana, Dar es Salaam
UMOJA wa Wamiliki wa Malori Tanzania (TATOA) umelalamikia
ongezeko la bei za bima, ukisema hazijazingatia uhalisia wa soko, pamoja na
kukosa uhalali kwa kuwa hazijashirikisha wadau wa sekta ya usafiri pamoja na
jamii kwa ujumla.
Msemamaji wa Umoja wa wamiliki wa Malori Tanzania,
Bwana Elias Lukumay akizungumza na waandishi wa habari kuhusiana na malalamiko
ya kampuni yake kuhusiana na ongezeko la bima. Kulia kwake ni Makamu mwenyekiti
wa TATOA, Bi Angellina Ngalula.
Makamu Mwenyekiti wa Umoja wa Wamiliki wa Malori
Tanzania, Bi Angellina Ngalula akisisitiza jambo wakati akizungumza na
waandishi wa habari kuhusiana na malalamiko ya umoja wao ya kupanda kwa bei za
bima kwa asilimia 400. Kushoto kwake ni msemaji wa TATOA, Bwana Elias Lukumay.
Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake, msemaji wa TATOA
Bwana Elias Lukumay, alisema wanasikitishwa na mamlaka ya uthibiti wa bima
Tanzania (TIRA) kuongeza malipo ya bima kwa asilimia 400 bila kutoa sababu za
msingi lakini pia bila kushirikisha wadau.
‘Majaribio yetu ya kuzungumza na TIRA yameshindika baada ya TIRA
kutojibu barua wala mawasiliano rasmi ya kukutana nao, tofauti na makubalino yetu
ya kikao cha mwezi wa pili, kati yetu na wao ambapo tulikubaliana kuwa na kikao
kabla ya mazungumzo baina ya wadau na umma juu ya swala hili’ alisema Lukumay.
Akielezea zaidi kuhusu malalamiko hayo, Lukumay alisema vigezo
maalumu vya kupandisha bei hizo haviko bayana lakini pia ushindani wa biashara
haukuzingatiwa.
‘TATOA inaamini kuna njia nyingi za kufata ili kupandisha bei,
lakini kubwa zaidi ni kuacha soko lijiendeshe lenyewe, kwani tuko kwenye soko
huria’ alisema Lukumay.
Kwa upande wake makamu mwenyekiti wa TATOA, Bi Angellina Ngalula,
alisema ongezeko hili la bei ni kubwa mno kwa mara moja na litapunguza
ushindani wa makampuni ya usafirishaji ya ndani, lakini pia litaongeza bei za
usafirishaji kwa kiwango kikubwa sana na hivyo kuumiza uchumi wa nchi na
mwananchi wa kawaida ataathirika kwa bei za bidhaa kupanda.
‘Sababu za TIRA kupandisha bei sio za msingi, sababu kama
udanganyifu na kuongezeka kwa kesi za bima pamoja na ajali za barabarani, sio
sababu tosha za kupandisha bima kwani kufanya hivyo kutaongeza malalamiko
zaidi, na pia kuwavunja moyo wateja waaminifu’ alisema Bi Ngalula.
Bi Angellina pia alitoa wito kwa wahusika, yaani TIRA, kuacha tamaa
na kutokuendeshwa na genge la makampuni ya bima na kurudi kwenye meza ya
majadiliano ili kuweza kupata muafaka kwa mujibu wa taratibu na sheria za nchi
kwa maendeleo ya taifa.
‘Bila TIRA kurudi kwenye meza ya majadiliano TATOA itabidi ichukue
hatua mbadala kama kwenda mahakamani na kugomea bei hizi mpya, jambo ambalo
litasababisha usumbufu kwenye uchumi wetu’ alisitiza Bi Ngalula.
No comments:
Post a Comment