https://tpc.googlesyndication.com/simgad/8045142562622600543


Recent Post

Sunday, March 30, 2014

Simba yachapwa 2-1 na Azam, huku Yanga nayo ikipigwa bao 2-1 na Mgambo Shooting jijini Tanga



Timu ya Azam FC, leo imefanikiwa kuifunga bao 2-1 timu ya Simba, iliyojitoa kabisa katika mbio za ubingwa na kuziacha Yanga na Azam wakipumuliana kuwania taji hilo la Tanzania Bara.

Mabao ya Azam yalifungwa dakika ya 15 kupitia kwa Khamis Mcha na John Bocco dakika ya 56, wakati bao la Simba la kufutia machozi lilipatikana dakika ya 45 kupitia kwa Joseph Owino.

Katika mechi iliyopigwa katika Uwanja wa Mkwakwani mjini Tanga, Yanga walishindwa kufurukuta baada ya kukubali kichapo cha bao 2-1 kutoka kwa timu ya Mgambo Shooting, yenye maskani yake Kabuku, wilayani Handeni, mkoani Tanga.

 

Mbio za urais zamkumbuka Mbunge wa Moshi Vijijini Dkt Cyril Chami

Mbunge  wa Moshi  Vijijini Dkt  Cyril Chami.

Na Mwandishi Wetu, Moshi 
Jinamizi la Urais linazidi kutikisa medani za siasa nchini, baada ya Mbunge wa Jimbo la Moshi Vijijini, Dk. Cyril Chami (CCM) kudai anaandamwa na mtandao wenye malengo ya Urais 2015.
 
Dk. Chami amedai kiini ni mbabe mmoja ambaye hakumtaja, mwenye uwezo wa fedha kukasirishwa naye, baada ya kukataa maagizo yake kwamba amsaidie swahiba wake anayewania Urais mwaka 2015.
“Niliikataa kazi hiyo kwa sababu haina maslahi kwa Taifa wala Moshi Vijijini…Mimi nitamuunga mkono mgombea Urais yeyote atakayechaguliwa na mkutano mkuu wa CCM,”alisema Dk. Chami.
Dk. Chami aliongeza kusema,”Haitanishangaza ikithibitishwa kuwa mbabe huyu ndiye anatoa fedha kuufadhili mtandao huu wa wahalifu, japo hii ni kazi ya Polisi na ni kazi inayoendelea,”
Mbunge huyo amedai mtandao huo, ndio ambao umefungua  akaunti yenye jina lake na picha katika mtandao mashuhuri wa kijamii wa Facebook na kumchonganisha na wapiga kura wake na CCM.
Katika taarifa yake Dk. Chami amedai akaunti hiyo inatumika kumchonganisha na chama chake pamoja na viongozi wakuu wa CCM ili asiteuliwe kugombea ubunge mwaka 2015.
“Kwa kujifanya wao ni mimi, wanapingana na misimamo yote ya CCM. Kwa mfano, wanadai kuwa kwenye mchakato unaoendelea wa Bunge la Katiba, mimi napendelea serikali tatu,”amelalamika.

Pendo Njau:Tanzania sina mpinzani

Na Kambi Mbwana, Dar es Salaam

BONDIA wa ngumi na mateke nchini (Kick Boxing), Pendo Njau, amesema kwamba kwa Tanzania imekuwa ngumu kupata mapambano ya kuonyesha uwezo wake, hali inayompa wakati mgumu.

Akizungumza jijini Dar es Salaam, Pendo alisema kuwa wanawake wengi wameshindwa kupata mwamko wa kuingia katika mchezo huo unaozidi kushuka thamani yake siku hadi siku.

Alisema changamoto za ukosefu wa watu wa kupanda nao ulingoni kwenye ngumi na mateke ndio zilizomfanya Japhet Kaseba ahamie upande wa ngumi za kawaida kwa ajili ya kutafuta maslahi.

“Ili uwe bondia mzuri lazima uwe na watu wa kupanda nao ulingoni, hivyo kwa upande wetu wa ngumi na mateke, changamoto za kukosa wanawake wa kupigana nao kunaleta utata.

“Naumiza kichwa jinsi ya kulinda kiwango changu bila kupanda ulingoni, hivyo huu ni wakati wa kutafakari kwa kina mfumo wangu wa maisha,” alisema.

Pendo anatokea katika klabu ya ngumi ya Kaseba, ambaye leo anacheza na Thomas Mashali, katika Ukumbi wa PTA Sabasaba, jijini Dar es Salaam.

DC Rweyemamu asisitiza umuhimu wa michezo wilayani Handeni


Na Kambi Mbwana, Dar es Salaam

MKUU wa wilaya Handeni, Muhingo Rweyemamu, amesisitiza umuhimu wa jamii kuweka mkazo katika kuibua vipaji kwa ajili ya maendeleo ya vijana na wanaoshiriki katika sekta ya michezo.

Akizungumza jijini Dar es Salaam hivi karibuni, DC Rweyemamu, pichani, alisema kuwa vipaji ni muhimu kuendelezwa kwa maendeleo ya Tanzania kwa ujumla.

Alisema hali hiyo inamfanya aweke mipango ya kuanzisha mashindano mbalimbali, hasa yanayoshirikisha vijana wadogo kwa kuwakuza kimichezo.

“Hii ni changamoto na dhamira ya kila mmoja wetu kufanya juhudi za kuendeleza vipaji vya vijana wetu kwa ajili ya kuwapatia mwanga mzuri.

“Hii ndio sababu tunajaribu kuwaza namna ya kuhakikisha watoto wote wanaanza kucheza tangu wakiwa katika shule za msingi,” alisema.

Kwa mujibu wa DC Rweyemamu, anajipanga kuanzisha mashindano ya vijana wadogo kwa ajili ya kuwakuza katika minajiri ya kuboresha vipaji vyao.

Saturday, March 29, 2014

Ajali ya treni mkoani Dodoma jana

Treni iliyopata ajali wilayani Mpwapwa mkoani Dodoma jana baada ya kusombwa na maji ikionekana pichani.

Pinda kukabidhi tuzo za Mwanamke Bora mjini Dodoma leo

WAZIRI Mkuu, Mizengo Pinda kesho atakuwa mgeni rasmi katika hafla ya kukabidhi Tuzo ya Mwanamke Bora wa Mwaka 2013-14, itakayowakutanisha wanawake wanne itakayofanyika kesho katika Ukumbi wa The African Dream mjini Dodoma.
Waziri Mkuu, Mizengo Pinda ndiye atakuwa mgeni rasmi katika utoaji tuzo.
Mkurugenzi Mtendaji wa Global Publishers, ambayo ndiyo iliyoratibu zoezi hilo, Eric Shigongo, alisema jana kwamba shughuli hiyo itakuwa ni hitimisho la kazi kubwa ya kupokea na kuchuja kura zilizotumwa na wasomaji kumtafuta mwanamke bora ambaye ni nembo kwa taifa.
Prof. Anna Tibaijuka.
“Zoezi hili lilifanyika kwa muda wa miezi tisa, kuanzia Juni mwaka jana hadi Machi mwaka huu. Awali kabisa watu walitakiwa kutuma majina ya wanawake wanaowaona ni bora ili wapigiwe kura, watu waliitikia vizuri sana, kwani jumla ya majina 150 yalitumwa katika kipindi cha miezi miwili.

Matumla alia na changamoto kwenye masumbwi


Na Kambi Mbwana, Dar es Salaam

BONDIA wa ngumi za kulipwa hapa nchini, Mbwana Matumla, amesema kwamba mchezo wa masumbwi unahitaji uvumilivu, hasa kutokana na changamoto za ukosefu wa wadhamini.

Akizungumza jijini Dar es Salaam, Matumla alisema ukosefu wa wadhamini unawafanya mapromota wengi kukosa moyo wa kuendeleza mchezo huo.

Alisema kwa mabondia wanaocheza ngumi, wanapaswa kujenga ujasiri na uvumilivu mkubwa ili waweze kufikia ndoto zao katika masumbwi.

“Bila kuwa na uvumilivu mambo yanaweza kuwa magumu zaidi, maana wakati mwingine mtu anakosa pambano ili kuonyesha uwezo wake.

“Hii ni mbaya kwakuwa inashusha kiwango cha bondia husika, jambo linalotufanya sisi mabondia kupata changamoto kadhaa ya kulinda viwango vyetu,” alisema Matumla.

Matumla ni mmoja wa mabondia wenye viwango vizuri, licha ya kukutana na changamoto za ukosefu wa mapambano ya kuwania mikanda mbalimbali ndani ya nje ya nchi.

Friday, March 28, 2014

MMJKT Mabingwa wa ngumi Mkoa wa Dar es Salaam

Bondia Hamisi Mputeni kushoto akioneshana umwamba wa kutupiana makonde na Victor Njaiti wakati wa mpambano wao katika mashindano ya klabu bingwa mkoa wa Dar es salaam juzi. Njaiti alishinda kwa pointi.
 Na Mwandishi Wetu
TIMU ya MMJKT jana imeibuka mabigwa wa mashindano ya mkoa wa Dar es salaam baada ya kuvipiku vilabu nane vilivyoweza kujitokeza kushiliki mashindano hayo na kutawazwa kuwa bingwa wa mkoa baadhi ya mabondia waliocheza fainal za mashindano hayo ni Hamisi Mrisho wa 'MMJKT' alisambalatishwa kwa pointi na bondia Oscar Richard wa 'Urafiki'   na Omari Mohamed wa urafiki akichezea kichapo kutoka kwa mwenzie John Mwambinga, na bondia anaekuja kwa kasi ya ali ya juu akitokea timu ya Ashanti ya ilala kwa sasa akichezea timu ya 'MMJKT'  alifanikiwa kumpiga John Christian wa 'Mgulani' Saleh Abdallah wa mgulani alishindwa kutamba mbele ya  Undule Langson wa Magereza.

Wananchi Handeni walalamika kuporwa ardhi yao


Na Kambi Mbwana, Aliyekuwa Handeni
WANANCHI wa Kijiji cha Komsala, wilayani Handeni, mkoani Tanga, wamemlalamikia mwekezaji anayejulikana kwa jina la Amina Singa, kuwa anapora ardhi zao, huku serikali ya Kata Kwamatuku, ikishindwa kuwatetea wakulima wadogo na kuelemea upande wa mwekezaji.
Katibu wa Baraza la Kata ya Kwamatuku, Nassib Bakari, pichani.
Mwandishi wa habari hizi alitembelea katika kijiji hicho na kufanya mazungumzo na wananchi sambamba na Baraza la Kata juu ya mgogoro huo unaosababisha malalamiko mengi kutoka kwa wakulima hao.
Mjumbe wa Baraza la Kata ya Kwamatuku, Mwanahamisi Nyata, pichani.
Akizungumza kwa huzuni kubwa, mkulima aliyejitambulisha kwa jina la Hausi Zuberi, alisema kuwa mwekezaji huyo amechota eneo lake, kama alivyofanya hivyo kwa wananchi wengine waliopakana na shamba lake.
 Mkuu wa Wilaya ya Handeni, Muhingo Rweyemamu pichani.
Alisema hali hiyo imewafanya waishi kwa mashaka wakiamini kuwa ataendelea na tabia yake hiyo, licha ya kumiliki eneo zaidi ya heka 120 hali ya kuwa anashindwa kulilima.
Hausi Zuberi, mmoja wa walalamikaji wa migogoro ya ardhi katika Kata ya Kwamatuku, wilayani Handeni, mkoani Tanga.
“Mwekezaji huyu ni kero kubwa kwetu kwasababu amechota maeneo yetu wakulima tusiopungua 6 baada ya kuvuka mbele ya mpaka wake, hali inayotufanya tuishi kwa hofu tukiamini kuwa ataendelea kutupora,” alisema.

Naye Paulina Athon Simbaulanga, alisema kuwa uporaji huo umebarikiwa na Baraza la Kata, baada ya kutembelea eneo hilo, jambo linalowafanya waamini kuwa kuna njia ya mkato iliyopitwa katika kufanikisha uporaji huo.

“Amina alikuja kijijini kwetu na kuomba heka 60, lakini sasa ana heka 120 na bado anapora sisi tusiokuwa na hata heka 5, licha ya yeye kumiliki eneo kubwa.

Thursday, March 27, 2014

Mwili wa marehemu, John Tupa, Mkuu wa Mkoa wa Mara waagwa rasmi leo


Mwili wa aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Mara, John Gabriel Tupa, ukitolewa kwenye makazi yake kwa ajili ya taratibu nyingine za mazishi yake.

Mwili wa marehemu ukiagwa
 Waombolezaji wakiwa msibani kwa Mkuu wa Mkoa wa zamani wa Mara, John Tupa.

TAZARA waomba kadi za uanachama Simba


Na Kambi Mbwana, Dar es Salaam
KLABU ya Simba, Makao Makuu, imeombwa kufanya haraka kuwapatia kadi za uanachama wapenzi wote wanaopatikana katika Tawi la Simba la Shirika la Reli la Zambia na Tanzania (TAZARA), ili kuwapatia nafasi ya kushiriki shughuli za kimaendeleo.
Wadau wakiwa katika picha ya pamoja baada ya uzinduzi wa tawi la TAZARA, lenye maskani yake jijini Dar es Salaam. Mwenye fulana ya mistari na kofia nyeusi ni Katibu Mwenezi wa tawi hilo, Alfredy Mdemu. Mwenye fulani nyekundi Mwenyekiti wa Kamati ya Mashindano ya Simba, Swed Mkwabi.

Akizungumza leo mchana jijini Dar es Salaam, Katibu Mwenezi wa tawi hilo, Alfredy Mdemu, alisema kuwa tawi lao lenye watu 176, ni wanachama 60 wenye kadi za klabu hiyo ya Simba SC.

Alisema hali hiyo inawapa wakati mgumu jinsi ya kuwabana katika kuiletea maendeleo, huku wakiamini kuwa wote wana mapenzi na klabu yao.

“Tumejitahidi kufungua tawi hili kwa ajili ya kuhakikisha kuwa wanachama wote wanafanikisha mambo ya kimaendeleo ya Simba, hivyo tunaomba kwa dhati kabisa klabu yetu iwape kadi wale walioomba,” alisema.

Naye Makamu Mwenyekiti wa tawi hilo, Amri Hussein, alisema kuwa wamefuata taratibu zote za kuwaombea uanachama watu wote wanaopatikana katika tawi lao la TAZARA.

“Endapo tutafanikiwa kuzipata kadi za wanachama wote wanaopatikana kwetu, hata sisi viongozi wao tunaweza kutafuta namna ya kuwabana kwa ajili ya kushiriki mambo ya kuiendeleza klabu yetu,” alisema.

Klabu ya Simba ni miongoni mwa klabu zenye wapenzi wengi, ikiwa ni kutokana na kuasisiwa kwake mwaka 1936, kama ilivyokuwa Yanga SC.

SIWEZI KUVUMILIA: Wimbo wa uwanja Simba, Yanga hauna kiitikio

Na Kambi Mbwana, Dar es Salaam
WIMBO wowote usiokuwa na kiitikio huwa haueleweki. Hata uwe mzuri vipi, maana yake na uhondo wake hutoweka.


Ndivyo ninavyoweza kusema kila ninaposikia wimbo wa ujenzi wa Uwanja kwa timu za Simba na Yanga. Kwa bahati mbaya, wimbo huu ni mzuri lakini namna unavyoimbwa na ukosefu wake wa kiitikio ni tatizo kubwa kwa wadau wote.


Hapa siwezi kuvumilia. Siwezi kuvumilia kwa kuona wimbo huu unazidi kuimbwa bila kuwa na kiitikio. Kwanini nasema hivi? Klabu ya Yanga imeanzishwa mwaka 1935. Mwaka mmoja baadaye ikaanzishwa Simba, yani mwaka 1936.


Ni miaka mingi sana. Lakini tangu wakati huo, wamekuwa na wimbo wao wa ujenzi wa uwanja. Kila siku wimbo huu unaimbwa na hayaonekani matunda yake.


Hii ni aibu kubwa. Azam iliyoanzishwa miaka ya hivi karibuni, sasa inamiliki uwanja wa kisasa maeneo ya Chamaz, jijini Dar es Salaam.


Lakini hawa wanaojiita wakongwe bado wanaendelea kupiga porojo zao kila uchwao. Ona, Simba wao wameanzisha kampeni za ujenzi wa uwanja maeneo ya Bunju. Lakini njia wanazopitia hadi kukamilisha unagundua zina ukakasi.

Alliance wasifiwa kwa juhudi za kuendeleza michezo

Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
MKURUNGENZI  Mtendaji wa Shule  na kituo cha kukuza michezo ya vijana cha Alliance School Sports Academy, James Bwire amesema timu ya Alliance inayotoka kituo hicho ikipanda daraja, ubigwa wa Ligi Kuu utahamia jijini Mwanza.

Akizungumza jijini Mwanza, baada ya kumalizika kwa mechi kati ya Alliance na timu ya Chuo cha Biashara (CBE), alisema vijana wanaondaliwa na kituo hicho watabadilisha soka nchini na kuleta changamoto ligu kuu.


Bwire alisema vijana wa timu ya Alliance waliopo daraja la nne hivi sasa wanaandaliwa na kupewa mafunzo ya kimichezo ngazi ya kimataifa ndio maana wanashinda  mechi zao zote ndani na nje ya nchi.


“Kituo chetu kinaandaa vijana wa michezo  kwa malengo, unajua zipo timu zinapanda daraja na kushiriki ligi kuu kwa kubahatisha na kushuka kwa muda mfupi, sisi hilo hatutaki ndio maana yapo masomo ya jinsi ya kucheza mpira uwanjani.

Klabu ya ngumi yaangukia wadau wa ngumi

Na Kambi Mbwana, Dar es Salaam

KLABU ya Ngumi ya Msisiri, yenye maskani yake Kinondoni, jijini Dar es Salaam, imeendelea kuomba hisani ya wadau wa ngumi ili kuwasaidia vifaa kwa ajili ya kumudu kuucheza mchezo huo wa masumbwi hapa nchini.


Akizungumza jana jijini Dar es Salaam, Kocha wa klabu hiyo, Daudi Muhunzi, alisema kwa kupata msaada zaidi wa vifaa, wanaweza kumudu kasi ya usshindani iliyopo.


Alisema klabu yao ina changamoto nyingi, hivyo wadau ni wakati wao kujitokeza kwa wingi kuwasaidia vifaa vya mchezo huo.


“Tunaomba wadau wote wajitokeze katika klabu yetu na kutusaidia kutupatia vifaa mbalimbali ili tuweze kusonga mbele.


“Naamini mpango huu ukifanikiwa, kila kitu kitakuwa kizuri kwa namna moja ama nyingine, ingawa kijana mwenzetu Yusuph Mlela, amekuwa wa kwanza kutupatia vifaa kadhaa,” alisema.


Mlela aliipatia klabu hiyo vifaa vya ngumi kama vile glove, clip bandeji, proctecta na gumshit.

Wednesday, March 26, 2014

Kaseba:Nimepata dawa ya Mashali



Na Kambi Mbwana, Dar es Salaam
BONDIA wa ngumi za kulipwa hapa nchini, Japhet Kaseba, amesema kwamba tayari ameshapata dawa nzuri ya kumtandika mpinzani wake Thomas Mashali, katika pambano linalotarajiwa kupigwa Machi 29, katika Ukumbi wa PTA Sabasaba, jijini Dar es Salaam.
Pambano hilo linalogusa hisia za wengi, linasubiriwa kwa hamu na wadau wengi, huku kila mmoja akiwa na imani ya bondia wake kuibuka na ushindi.
Akizungumza jana jijini Dar es Salaam, Kaseba alisema kwamba amepata dawa sahihi ya kumpiga mpinzani wake, baada ya kugundua udhaifu wake.
Alisema mara kadhaa Mashali amekuwa bondia ambaye ana uwezo mzuri, lakini huwa anaingiza uhuni anapokuwa ulingoni, jambo linalomfanya yeye awe makini zaidi.
“Nimepata dawa ya kumpiga Mashali ikiwa ni pamoja na kuzalisha matamanio zaidi ya kuibuka na ushindi katika pambano hilo.
“Naamini hatakuwa na madhara yoyote katika yangu, hivyo sina shaka maandalizi ninayofanya yataniweka kileleni, ukizingatia kuwa nina mipango kabambe katika tasnia ya masumbwi hapa nchini,” alisema.
Aidha, Mashali yeye alikaririwa na vyombo vya habari kuwa hana hofu juu ya pambano lake, akiamini kuwa atamziba mdomo Kaseba.

Tukigundua michezo ni ajira, tutaziepuka siasa uchwara

Na Kambi Mbwana, Dar es Salaam


WACHEZAJI wengi duniani wanaishi kifalme kwa kumiliki kiasi kikubwa cha pesa kutokana na vipaji vyao. Wachezaji kama vile David Beckham, watakumbukwa na utajiri wao, kiasi cha kufikia kutajwa kama moja ya wachezaji waliowahi kuwa na fedha nyingi.
Umati wa watu ukionekana katika moja ya mechi ilizokutanisha timu kongwe za Tanzania, Simba na Yanga. Hizi ni fedha tupu.

Katika urafiti uliofanywa na mtandao wa goal.com, ulibaini kuwa Beckham aliwahi kuwa na utajiri wa kiasi cha Dola Milioni 261, huku akifuatiwa na Lionel Messi wa Barcelona, akiwa na Dola Milioni 149, wakati Cristiano Ronaldo wa Real Madrid akitajwa kuwa na Dola Milioni 145.


Utafiti huu ulifanyika Machi mwaka jana, ikiwa ni ishara kuwa kwa kutumia miguu yao uwanjani, wachezaji hawa walifanikiwa kuvuna fedha nyingi mno. Si wachezaji wa soka tu, ila michezo yote kwa ujumla inaingiza fedha nyingi kwa wanamichezo wengi duniani.


Wachezaji kama vile Floyd Mayweather, Manny Pacquiao, Tiger Woods, Lebron James, Roger Federer, Kobe Bryant, Phil Mickelson, Peyton Manning na wengineo kwa nyakati kadhaa wametajwa kuvuna fedha nyingi kwa vipaji vyao.


Ndio hapo utakaposhangaa kuna tofauti gani kati ya Pacquiao na bondia Francis Cheka, kutoka mkoani Morogoro? Kwa vipaji hawana tofauti yoyote. Wawili hawa wanatofautishwa na mfumo wa nchi zao wanapotoka. Tanzania sisi tunaendekeza sana siasa, wakati wenzetu wanawaza kupiga hatua kwa maendeleo yao na vipaji vyao.


Haya ni mambo yanayoshangaza na kuhudhunisha kupita kiasi. Hivyo siku tutakapojua michezo ni ajira, basi tutaziepuka siasa uchwara. Unaweza kujiuliza, kwanini wingi wa Makampuni na taasisi kibao hazina mpango wowote wa kusaidia michezo mingine, ukiacha mpira wa miguu?

Timu ya uendeshaji wa huduma za afya wilayani Korogwe, mkoani Tanga

Meneja wa Bima ya Afya – Mkoa wa Tanga, Bw. Ally Mwakababu (kushoto) akitoa maelezo ya utangulizi wakati wa ufunguzi wa kikao cha Timu ya Uendeshaji wa Huduma za Afya ya Halmashauri (CHMT) kikijadili mchakato wa kubadirisha sheria ndogo ya Mfuko wa Afya ya Jamii (CHF) kwenda katika Mfumo wa Afya ya Jamii Mijini wa Tiba kwa Kadi (TIKA). Kikao hicho cha kwanza kilifanyika jana Machi 25, 2014 katika ukumbi wa Halmashauri ya Mji wa Korogwe, Tanga. Pembeni ni mgeni rasmi aliyekaribishwa kufungua kikao hicho, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Korogwe, Bw. Lewis Kalinjuna (katikati) na Mganga Mkuu wa Halmashauri ya mji Korogwe, Jerry Mwakanyamale (kulia).
 Mganga Mkuu wa Halmashauri ya mji wa Korogwe, Jerry Mwakanyamale (Kulia) akiongea wakati wa kumkaribisha mgeni rasmi Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Korogwe, Bw. Lewis Kalinjuna (Katikati) katika ufunguzi wa kikao cha Timu ya Uendeshaji wa Huduma za Afya ya Halmashauri (CHMT) kikijadili mchakato wa kubadirisha sheria ndogo ya Mfuko wa Afya ya Jamii (CHF) kwenda katika Mfumo wa Afya ya Jamii Mijini wa Tiba kwa Kadi (TIKA). Kikao hicho cha kwanza kilifanyika leo Machi 25, 2014 katika ukumbi wa Halmashauri ya Mji wa Korogwe, Tanga. Pembeni ni Meneja wa Bima ya Afya – Mkoa wa Tanga, Bw. Ally Mwakababu (kushoto).

Tuesday, March 25, 2014

Maoni kuelekea pambano la Kaseba na Mashali

Hivi karibuni watakutanishwa miamba miwili ulingoni wote wakiwa na nywele zilizotengenezwa kwa mtindo wa rasta, 
Miamba hiyo  ambayo mara nyingi huwa ndio gumzo la watu mitaani hususani wapenda mchezo wa ngumi kwa tabia zao na vibwekwa vyao  kwa raia wa kawaida, hao si wengine bali ni Japhet Kaseba na bondia mtukutu Thomas Mashali, pichani, Jumamosi ya Machi 29 katika Ukumbi  PTA, Sabasaba.

Kwa Mfano - bondia Thomas  mashali “samba asiyefugika – kama anavojiita” alizaliwa Sept 1989 na kukulia mitaa ya manzese jijini dare s salaam,akiwa mtoto mtundu,mkorofi,mgomvimgovi  na mpenda michezo kama ilivyo kwa mdogo wake Charles mashali ambaye na yeye pia  alikuwa  bondia mzuri aliyetokea kuwashinda na  kuwasumbua mabondia wengi kama kina Francis Miyeyusho na alishawahi kuchukua Ubingwa wa Taifa kabla ya kuachana na mchezo wa ngumi kwa kuumia bega.
Alishindwa kuendelea na mchezo wa ngumi na kumuachia Thomas mashali ambae ni mkubwa kwa Charles mashali aliyeanza mchezo wa  ngumi akiwa mdogo na kupigana mapambano  katika kumbi za colin na manyala park  za manzese na hapo udogoni amewahi kucheza na kina Ramadhan miyeuyusho,
Raston Phili ‘moto wa tipa’ na  marehemu papa upanga na kuwa kivutio cha wengi  ulingoni na kero kwa wengine uraiani kwa tabia yake ya kuwapigapiga  watu na kuwaonea wasio na hatia na kuendekeza ubabe usio na maana akiwa kama tembo wa mitaa ya manzese kwa tabia yake  hiyo kulimfanya awe anakwenda jela  mara kwa mara na kumpotezea dira imara katika masumbwi  na kukaa muda mrefu bila kupigana mpaka pale kuna wakati ametoka jela na kurudi tena gym kama ilivyo kawaida yake kiasili anapenda sana mazoezi na michezo alikuwa akijifua kuuweka mwili wake fiti.

Yanga mikononi mwa Mahakama Kuu

SHIRIKISHO la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limepokea amri ya Mahakama Kuu (Kitengo cha Kazi) kukamata Sh. milioni 106 za klabu ya Yanga kutokana na mapato ya mlangoni kwenye mechi zake ili kuwalipa waliokuwa wachezaji wake Stephen Malashi na Wisdom Ndlovu.

Akizungumza jijini Dar es Salaam leo, Msemaji wa TFF, Boniface Wambura, alisema kuwa tayari wameanza utekelezaji wa amri hiyo ambapo katika mechi ya Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) dhidi ya Rhino Rangers iliyochezwa Machi 22 mwaka huu mjini Tabora wamezuia Sh. 9,221,250 ambazo ndizo zilizokuwa mgawo wa Yanga katika mchezo huo ulioingiza jumla ya Sh. 38,655,000.

Wachezaji hao walifungua kesi kortini kupinga mikataba yao na klabu hiyo kuvunjwa bila kulipwa haki zao za kimkataba. Malashi na Ndlovu walishinda kesi hiyo, hivyo korti kuwapa tuzo hiyo ya sh. milioni 106.

Tunawakumbusha wanachama wetu (klabu za Ligi Kuu, vyama vya mpira wa miguu vya mikoa na vyama shiriki) kuzingatia mikataba wanayoingia na watendaji wao wakiwemo wachezaji, makocha na maofisa wengine.

Iwapo wanataka kuvunja mikataba ya ajira wafuate taratibu kwa vile hakuna mkataba ambao hauelezi jinsi ya kuvunjwa iwapo upande mmoja unataka kufanya hivyo.

LinkWithin

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...