https://tpc.googlesyndication.com/simgad/8045142562622600543


Recent Post

Monday, June 10, 2013

Viwanja vya michezo mikoani vikarabatiwe



SIWEZI KUVUMILIA
Na Kambi Mbwana, Aliyekuwa Morogoro
KWA SIKU mbili ya wiki iliyopita, nilikuwapo mkoani Morogoro nikishiriki kwa namna moja ama nyingine kazi za kijamii, yakiwapo mazishi ya msanii Albert Mangweha ‘Ngwair’.
 Watu wakiangalia tukio katika Uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro......
Watu wakiwa wamepanda juu ya Uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro.

Nikiwa pale, niliweza kutembea sehemu mbalimbali kwa ajili ya kuangalia kinachonifurahisha na kile kitakachonikera pia. Safari yangu haikuishia hotelini au msibani tu, ila kuna wakati nililazimika kutembea kona hii na kutokea kule kwa ajili ya kusoma pia mazuri na mabaya ya mji wa Morogoro.

Mengi nimeyaona ambayo yalipita kama zinavyopita vitu vingine, ingawa juu ya Uwanja wa Jamhuri Mjini Dodoma nikishindwa kusahau, maana najua tusipokuwa makini viwanja hivi vitapotea asilani.

Uwanja wa Jamhuri kama vilivyokuwa viwanja vingine, hasa wa Kaitaba,  ni vibovu mno. Sijui hata hii ligi viwanja visivyokuwa na ubora vinatumika kwa mtindo gani. Najua serikali ina changamoto nyingi, hasa Chama Cha Mapinduzi (CCM), ambao ndio wamiliki wa viwanja hivi, ila ni vyema tukaviendeleza au kuvitunza ili hata ligi zetu ziwe na mashiko.

Kwa mfano, Uwanja wa Kaitaba umekuwa ukilalamikiwa kila wakati na wadau, wanamichezo na jamii kwa ujumla. Katika kuangalia mazingira mazima ya viwanja hivi, huwezi kuamini kuwa eti kuna timu kubwa za ligi au ngazi ya mkoa zinashiriki mashindano kwa kutumia uwanja kama huo.
Hii Siwezi Kuvumilia hata kidogo. 

Ni wakati wetu sasa kufanya mambo yenye maana kwa jamii nzima. Najua pia CCM ina rasilimali fedha na watu pia, hivyo haiwezi kukosa uwezo wa kuviendeleza viwanja hivi.

Viendelezwe na kutunzwa maana pia vina heshima kubwa, hasa kwa kuona vimeanza kutumiwa tangu nchi hii ni changa na leo tumegonga nusu karne, yani miaka 50 ya Uhuru.

Kwa bahati mbaya au nzuri, unapotaka kuelezea viwanja vya michezo katika kila mkoa, ni dhahiri wahusika watakuwa CCM. Viwanja kama vile Mkwakwani Tanga, Jamhuri Morogoro, Jamhuri Dodoma, Sokoine Mbeya, Majimaji Songea na vinginevyo vingi ni mali ya CCM.

Ni wakati sasa kujaribu kutafuta mbinu mbadala za kuvitunza au kuviendeleza viwanja hivi kwa ajili ya maendeleo ya michezo. Wakati huu ambao tunatafuta wadau, kama vile Said Bakheressa ambaye kwa mapenzi yake ameamua kujenga uwanja kwa ajili ya timu yake ya Azam FC, uliopo Mbagala, si vyema kuviachia viwanja hivi vife.

Nasema hivyo maana hata wachezaji wanaoshiriki ligi yetu Tanzania, huenda wakakosa viwango, hasa wanapokutana na wachezaji wenye mazoezi imara, huku wengi wao wakiwa majeruhi kila wakati.

Mchezaji anapokuwa majeruhi kila mara, ni wazi anakosa kiwango cha kumuwezesha kufikia malengo yake uwanjani. Mwili wake unakosa nguvu na akiendelea hivyo, ni wazi atapoteza soka lake.

Nadhani kwa kulisema hili, mambo yatakwenda sawa kwa wadau hawa kukaa pamoja kutafuta mbinu nzuri za kuendeleza viwanja vya michezo. Uwanja kama huu wa Jamhuri Morogoro, ukiuangalia tu, huwezi amini kama kuna ligi inachezwa ndani yake.

Ukiacha ukuta uliozunguushwa matangazo, lakini wenyewe ulivyo, unaokena ni mbovu, hivyo ni wazi tunatakiwa tujuwe namna gani tutaendeleza michezo, kwanza kwa kuwa na viwanja bora, ligi nzuri yenye ushindani.

Wakati huu ambao kila mtu anataka mafanikio katika sekta ya michezo, basi tutafute namna bora ya kuendeleza hivi viwanja vyetu, hata kama bajeti zetu ni ndogo.

Kama hivyo haitoshi, wale wanaojitangaza kwa kupitia viwanja hivi, naamanisha wale waliopachika matangazo yao kwenye kuta, basi wakae na kutafakari namna gani ya kuvitunza viwanja hivi.

Huu ndio ukweli. Bila hivyo, tutaendelea kukuza wachezaji wengi, wasiokuwa na mahala kwa kuonyesha viwango vyao, maana mtu anapocheza katika viwanja visivyokuwa na ubora, ataishia kuumwa mwili, kutegua miguu na kesho tunamuhitaji katika michuano ya Kimataifa kwa timu zetu au wale wanaoitwa kwenye timu za Taifa.

Hakika siwezi kuvumilia na kuna haja ya kujiangalia upya, maana huu si mwendo mzuri tunaopita, hasa kwa kuangalia viwanja hivi vinaachwa bila matunzo na hivyo hivyo vinatumiwa kwenye ligi kubwa.
0712 053949
0753 806087

No comments:

LinkWithin

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...