https://tpc.googlesyndication.com/simgad/8045142562622600543

Recent Post

Wednesday, July 30, 2014

Waimbaji wa nchi tano Afrika Mashariki kuchuana vikali

 Allan Kalinga-CEO for Afro-Euro Management Co. LTD
Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
WAIMBAJI kutoka nchi tano katika Kanda ya Afrika Mashariki hadi kufikia mwisho wa mwaka huu wanatarajiwa kushiriki katika shindano jipya la uimbaji liitwalo Shindano la Waimbaji wa Afrika Mashariki.

Shindano hilo ambalo limeandaliwa na Kampuni ya Afro-Euro Events Management Co. Limited, linatarajiwa kufanyika Jijini Dar es Salaam, na kuhusisha wasanii nguli kutoka Uganda, Tanzania, Kenya, Rwanda na Burundi.

Ofisa Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya Afro-Euro Management Co. LTD, Allan Kalinga, ambaye kwa sasa makazi yake yako nchini Uingereza, alisema kwamba wagombea  husika watachuana kuwania tuzo ya heshina ya juu kuvikwa taji la muimbaji bora wa eneo la Afrika Mashariki.

 "Umma wa Afrika Mashariki utahusishwa kuanzia mwanzo wa shindano hili hadi mwisho na hivyo mshindi atakayepatikana atakuwa chaguo la kweli la watu wa Afrika Mashariki, " alisema Kalinga.

MCHAKATO WA UTEUZI
Kalinga aliendelea kusema zaidi kwamba  kila nchi shiriki itafanya uteuzi wake wenyewe kuwatambua wanamuziki wake watano bora ambao watawakilisha katika fainali ya kikanda.

Fiesta kuanzia Mwanza Agosti 9Na Kambi Mbwana, Dar es Salaam
WAKAZI na wananchi wa jijini Mwanza, Tanzania, watapata fursa ya kuwa wa kwanza kushuhudia burudani za tamasha la muziki la Fiesta, litakaloanza Agosti 9, CCM Kirumba, Mwanza.

Kuzinduliwa kwa tamasha hilo, ni harakati za mwendelezo wa ziara za mikoani, ambapo wasanii mbalimbali wenye majina yao hupata nafasi ya kupanda jukwaani kutoa burudani.

Akizungumza jana jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi wa Utafiti na Matukio, Ruge Mutahaba, alisema kwamba maandalizi ya mwisho yanafanywa ili kuliweka pazuri tamasha hilo.

“Fiesta ni tamasha kubwa ambalo mashabiki nchini kote wanaliheshimu na kuona ni sehemu muafaka ya kupata burudani kabambe.

“Kwa mwaka huu wadau wa muziki wa jijini Mwanza watakuwa wa kwanza kuangalia maudhui na mikakati kabambe ya kuliweka juu tamasha hili linalotamba Tanzania,” alisema.

Wasanii mbalimbali nchini wanajiandaa kwa tamasha hilo, ambalo mara zote limekuwa eneo muafaka la kuwatangaza wasanii ndani na nje ya jiji la Dar es Salaam.

Sunday, July 27, 2014

Yusuf Manji avunja Kamati ya Utendaji, aunda mpya, Ridhiwan Kikwete awekwa kandoNa Kambi Mbwana, Dar es Salaam

MWENYEKITI wa klabu ya Yanga, Yusuph Manji, amevunja Kamati ya Utendaji kuanzia Julai 31 na kuunda mpya kwa ajili ya kusimamia na kuiendeleza klabu hiyo yenye maskani yake jijini Dar es Salaam.
Yusuf Manji, pichani.
Mbali na kuvunjwa kwa Kamati ya Utendaji, pia Manji ametangaza kuzivunja Kamati zote, ikiwamo ile ya kusimamia Jengo la Mafia, ambalo lilikuwa likisimamiwa na Mwenyekiti wake Ridhiwan Kikwete.
WAJUMBE WAPYA WA Kamati ya Utendaji ya YANGA ni hawa WAfuaTAO:

1.    Bw.Abubakar Rajabu                          -           Mradi wa Jangwani City

2.    Bw.Sam Mapande                              -           Sheria na Utawala Bora


3.    Bw.George Fumbuka                         -           Uundwaji wa Shirika


4.    Bw.Waziri Barnabas                           -           Vibali vya Hatimiliki na Mahusiano

na Wafadhili5.Bw.Abbas Tarimba                                -           Mipango na Uratibu


6.    Bw.Isaac Chanji na Bw.Seif Ahmed  -           Uendelezaji wa Mchezo


7.    Bw.Musa Katabalo                              -           Mauzo ya Bidhaa


8.    Bw.Mohammed Bhinda                      -           Ustawishaji wa Matawi


9.    Bw.David Ndeketela Sekione             -           Uongezaji wa Wanachama


10.  Bw.Mohammed Nyenge                    -           Utangazaji wa Habari, Taarifa,

Matangazo n.k.
Wajumbe wa Kamati ya Utendaji iliyoundwa upya watasimamia kimsingi kamati ndogo zifuatazo:


·                     Kamati ya Maadili                               -           Bw.Sam Mapande


·                     Kamati ya Nidhamu                            -           Bw.Sam Mapande


·                     Kamati ya Uchaguzi                           -           Bw. Sam Mapande


·                     Kamati ya Uchumi na  Fedha             -           Bw.George Fumbuka na Bw.Waziri

Barnabas

·                     Kamati ya Mashindano                       -           Bw.Seif Ahmed & Bw.Isaac Chanji


·                     Kamati ya Soka la Vijana na


Wanawake                                          -           Bw.Seif Ahmed &Bw.Isaac Chanji


·               Kamati ya Ufundi                                -           Bw.Seif Ahmed &Bw.Isaac Chanji


5.    Mwenyekiti na Makamo Mwenyekiti wa YANGA wanamategemeo makubwa kuwa waliotajwa hapo juu watahakikisha wana timiza malengo yaliyokusudiwa na YANGA ili“DAIMA MBELE, NYUMA MWIKO” mpaka hapo itakapoamuliwa kubadilishwa au kutenguliwa vinginevyo.


6.    Mwisho,tunawaomba ushirikiano wa dhati ili kuhakikisha kuwa YANGA inapiga hatua mbele na inafanikiwa katika kufikia malengo na mipango yake ya maendeleo ya muda mfupi na ya muda mrefu kwa manufaa ya Klabu, Timu na wana YANGA popote walipo duniani.

Pata picha mbili kali Rais Kikwete, Waziri Pinda walipokwenda kufuturu kwa Makamu wa Rais, Dkt Gharib Bilal

 Rais Jakaya Mrisho Kikwete, Waziri Mkuu Mizengo Pinda na Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe Mohamed Chande Othman, wakiongozana na mwenyeji wao Makamu wa Rais Dkt. Mohammed Gharib Bilali, wakati wakiwasili nyumbani kwa Makamu kwa ajili ya kushiriki katika halfa ya futari waliyoandaliwa na Makamu wa Rais Dkt Mohamed Gharib Bilali katika makazi yake Oysterbay jijini Dar es salaam juzi Ijumaa jioni Julai 25, 2014. Picha na OMR

Bunge la Katiba lazidi kukaliwa kooni

 Mwenyekiti wa Jukwaa la Katiba Tanzania (Jukata), Deus Kibamba (kulia), akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, wakati akitoa tamko kuhusu Bunge la Katiba litakaloanza Agosti 5, 2014 ambapo walishauri Bunge hilo likae wiki mbili badala ya miezi miwili kama ilivyopangwa ili kupunguza matumizi makubwa ya fedha za Umma. Kutoka kushoto ni Mjumbe wa Kamati na Uongozi Jukata Omar Ali Omar,  Meneja Habari na Mawasiliano wa Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP), Kenny Ngomuo, Makamu Mwenyekiti wa Jukata, Hebron Mwakagenda na  Mratibu wa Jukata, Diana Kidara.
 Makamu Mwenyekiti wa Jukata, Hebron Mwakagenda, akisoma tamko hilo.

Thursday, July 24, 2014

Kumekucha tamasha la Saba la Muziki wa Cigogo 2014

Na   Andrew Chale, Dodoma

SHAMRA shamra za tamasha la Muziki wa Cigogo zitatarajia kulipuka hiyo kesho Julai 25, kwenye kijiji cha Chamwino Ikulu, Mkoani hapa kwa kushuhudia vikundi zaidi ya 30, vikiwasha moto wa ngoma na muziki wa kitamaduni  hu ku Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Dk. Rehema Nchimbi  akitarajiwa kulifungua rasmi.


Katika kukuza na kuendeleza sanaa nchini, tamasha hilo ambalo kwa mwaka huu ni la msimu wa  Saba (7) likifahamika kama (Wagogo music festival 2014)  lenye kauli mbiu  ‘Utamaduni na Amani’ linatarajia kulindima kwa siku tatu, Julai 25 hadi 27, Kijijini hapo  Chamwino Ikulu.


Akizungumza na waandishi wa habari  katika mkutano uliofanyika mapema leo kwenye ukumbi wa Maktaba ya Mkoa wa Dodoma, Mkurugenzi mkuu wa tamasha hilo, Dk. Kedmon Mapana,  wa Kituo cha Sanaa Chamwino (Chamwino Arts Center-CAC) alisema jumla ya vikundi  31 vinatarajiwa kushiriki tamasha hilo.


“Tamasha la Wagogo mwaka huu ni la saba, ambapo shamrashamra ya tamasha hilo zinatarajia kuanza majira ya saa nane mchana Mkuu wa Mkoa atakapolifungua rasmi huku tukitaraji pia kuwa na wageni wasiopungua 1000” alisema Dr. Kedmon Mapana.


Na kuongeza kuwa, kituo hicho cha CAC  kimekuwa kikiandaa tamasha hilo kila mwaka huku lengo kuu likiwa ni kudumisha mila na tamaduni za Wagogo.

Taasisi ya Handeni Kwetu Foundation kuzinduliwa August 5

Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam 
SIKU chache baada ya kusajiliwa rasmi chini ya Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto, Taasisi inayojulikana kama Handeni Kwetu Foundation, imepangwa kuzinduliwa August 5 mwaka huu, katika Ukumbi wa Vijana Social Hall, Kinondoni, jijini Dar es Salaam.

Kuanzishwa kwa taasisi hiyo ni kutafuta namna ya kusaidiana na serikali katika mambo mbalimbali, ikiwamo Kujenga uwezo kwa jamii kujikwamua kiuchumi na kuhamasisha utawala.

Akizungumza hilo, jijini Dar es Salaam, Msemaji wa taasisi hiyo, Kambi Mbwana, alisema taasisi hiyo imeanzishwa na itafanya kazi zake bila kuvunja masharti yaliyowekwa na serikali ili kuhakikisha kuwa malengo yaliyokusudiwa yanapatikana.

Alisema kuwa taratibu za kuelekea kwenye uzinduzi huo zinaendelea kuwekwa katika hali ya kukutana pamoja kwa wageni walioalikwa kushuhudia uzinduzi huo wa aina yake.

“Kwa miezi kadhaa sasa taasisi ilikuwa kwenye mchakato wa usajili wake, hivyo baada ya kukamilika, kinachofuata sasa ni kuzindua ili ianze kazi zake kama ilivyokusudia.

“Taasisi hii itakuwa na Makao yake Makuu wilayani Handeni, lakini itafanya kazi zake nchi nzima na huko mbele itakuwa na ofisi katika kila eneo itakaloona inafaa,” alisema.

Sababu nyingine za kuanzishwa kwa taasisi hiyo ni kuleta ustawi kwa jamii katika njanya mbalimbali, kutoa mafunzo kuhusu kilimo bora na jinsi ya kutafuta masoko, kutoa elimu ya uraia na kuhamasisha misingi ya utawala bora, kutoa elimu na ushauri kuhusu mbinu bora za kuimarisha  afya na elimu ya msingi kuhusu Virusi vya Ukimwi na Ukimwi.

Malengo mengine ni kutoa elimu kuhusu makundi rika katika elimu ya uzazi, kuhamasisha na kushawishi jamii kuzingatia ustawi wa mtoto katika jamii, kufanya utetezi kwa makundi maalum ambayo haki zao zinakiukwa na kufanya tafiti mbalimbali zenye malengo ya kuboresha maisha ya jamii, kiuchumi na kijamii.

Semina ya kuelimisha jamii kuhusu Ukimwi yafana

DSC_0092
 Afisa Mradi wa Elimu ya Afya na VVU/UKIMWI kutoka UNESCO, Bw. Herman Mathias akitoa mada kuhusu tabia hatarishi zinazochangia maambukizi mapya ua VVU kwa Vijana katika warsha ya siku tatu ya Mradi wa SHUGA Redio inayofanyika katika Kituo cha Redio cha Nuru FM mjini Iringa.
Na Mwandishi wetu
Idadi kubwa ya Vijana hususan wa kike wenye umri kati ya miaka 15 hadi 24 wanaanza kufanya mapenzi katika umri mdogo jambo ambalo linaashiria hatari ya maambukizi ya VVU ikilinganishwa na  idadi ya Vijana wa Kiume.

Akitoa mada kuhusu tabia hatarishi zinazochangia maambukizi mapya ua VVU kwa Vijana katika warsha ya siku tatu ya Mradi wa SHUGA Redio inayofanyika katika Kituo cha Redio cha Nuru FM mjini Iringa, Afisa Mradi wa Elimu ya Afya na VVU/UKIMWI kutoka UNESCO, Bw. Herman Mathias, amesema hadi sasa kuna Asilimia 3.9 ya wasichana wenye umri huo wamepata maambukizi ya VVU ikilingaishwa na asilimia 1.7 ya wavulana.

Kufanya mapenzi pia katika umri mdogo kunachangia kwa kiasi kikubwa mimba za utotoni na kuathiri ustawi wa maisha ya wasichana. Wastani wa watoto wa kike 6,000 huachishwa masomo kila mwaka kutokana na mimba za utotoni.

Kutana na damu changa iliyotangaza nia ya kugombea ubunge jimbo la Nkenge (Chadema)

JOTO la kisiasa nchini kuelekea kwenye Uchaguzi Mkuu mwaka 2015 limezidi kushika kasi baada ya kijana, Edson Joel, kuonyesha nia ya kuwania Ubunge katika Jimbo la Nkenge, akitaka kujitosa kwa tiketi ya Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema).
 Edson Joel pichani akiwa kwenye moja ya majukumu ya kichama jimboni Nkenge.
Edson Joel mwenye kofia akiwa na timu katika moja ya shughuli za kijamii jimboni Nkenge.

Joel ameweka kambi yake ya wiki tatu jimboni humo akishiriki katika kazi mbalimbali za kijamii kwa ajili ya kuangalia namna ya kuwaingilia jimboni humo na lengo lake la kuwatumikia Watanzania, hususan wa Jimbo la Nkenge kutimia.

Joel aliuhakikishia mtandao wa Handeni Kwetu Blog kuwa anazo sifa na nguvu ya kuwatumikia Watanzania kwa kupitia chama chake cha Chadema. Habari mbalimbali juu ya siasa na wanasiasa Tanzania zitaendelea kukujia live...

Monday, July 21, 2014

Miss Kanda ya Mashariki kufanyika August nane mwaka huu

Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
SHINDANO la urembo la kumpata malkia wa Kanda ya Mashariki limepangwa
kufanyika Agosti 8 mwaka huu kwenye Ukumbi wa hoteli ya Nashera
iliyoko mkoani Morogoro.


Akizungumza jana jijini Dar es Salaam, Mratibu wa
shindano hilo, Alex Nikitas, alisema kuwa warembo 14 ndio watachuana
kuwania taji la kanda hiyo.


Nikitas alisema kuwa shindano hilo litashirikisha warembo kutoka mikoa
ya Lindi, Mtwara, Pwani na wenyeji Morogoro.
Aliongeza kuwa maandalizi ya shindano hilo yako katika hatua za mwisho
na washiriki wanatarajia kuingia kambini mapema wiki ijayo kujiandaa
na kinyang'anyiro hicho.


"Mwaka huu tumejipanga kufanya shindano lenye ubora wa hali ya juu,
tunawaomba wadau wa sanaa ya urembo kujitokeza kushuhudia fainali za
kanda hii ambayo safari ya mshindi wa taifa itaanzia," alitamba
mratibu huyo.


Alisema kuwa warembo watakaoshika nafasi tatu za juu watapata nafasi
ya kuiwakilisha kanda hiyo katika fainali za Taifa "Redd's Miss
Tanzania 2014" zitakazofanyika mwezi Septemba mwaka huu.


Diana Laizer kutoka Morogoro ndiye mrembo anayeshikilia taji la kanda
hiyo ya Mashariki na katika fainali zilizopita za Redd's Miss Tanzania
alifanikiwa kuingia katika hatua ya 15 bora.


Mrembo Happiness Watimanywa wa mkoani Dodoma ndite anayeshikilia taji
la taifa na mwaka huu ndiye atakwenda kuiwakilisha Tanzania katika
fainali za dunia (Miss World).

LinkWithin

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...