Na Kambi Mbwana,
Dar es Salaam
KITUO Cha Polisi
Magomeni, jijini Dar es Salaam, kimeingia kwenye kashfa nzito, baada ya kudaiwa
kumuachia anayedaiwa kuhusika na ubakaji wa mtoto wa kike mwenye umri wa miaka
12 jina tunalo bila sababu za kueleweka.
Msamaria Mwema, Halima Athumani.
Msamaria mwema
aliyekuwa anafuatilia suala hilo la ubakaji, aliyejitambulisha kwa jina la
Halima Athuman, alidokeza juu ya suala hilo na kusema lilitokea Aprili 21,
maeneo ya Magomeni Makuti, jijini Dar es Salaam.
Katika hali ya
kushangaza, mmoja wa askari kutoka katika kituo hicho alitajwa kuwa alimpigia simu msamaria mwema huyo na kumwambia aachane na kesi
hiyo kwakuwa inaweza kumletea matatizo.
Mwanamama huyo
alisema kuwa mtoto aliyebakwa alikuwa anaishi na shangazi yake, Magomeni
Makuti, lakini usiku wa kumkia Aprili 21, alipanda kwenye daladala kwa nia ya
kwenda Kigamboni kwa mama yake mzazi Khadija Juma, baada ya kufanyiwa unyama
huo.
“Nikiwa kama binadamu
ambaye nipo sehemu ya jamii, niliamua kumsaidia mtoto yule, hata hivyo baada ya
kumbana kwa maswali aliamua kuniambia ukweli juu ya kufanyiwa unyama huo na
mume wa shangazi yake.
“Kwa bahati mbaya,
baada ya taarifa kufika polisi na baadaye madai ya ubakaji huo kuthibitishwa na
mmoja wa madaktari wa Hospitali ya Mwananyamala,” alisema.
Siku ya Aprili 21, yalifanyika
mazungumzo na Mkuu wa Kituo cha Polisi Magomeni, Mwanne Salum, hata hivyo kwa
mujibu wa sheria za jeshi la Polisi, hakuwa msemaji mkuu wa sakata hilo, ingawa
alikiri kulifuatilia kwa karibu kuangalia ukweli wake kwa ajili ya kulifikisha
suala hilo kwenye vyombo vya dola.
Hata hivyo, Mkuu huyo
alimtaka mwandishi wetu kuacha kuandika habari hizo, kwakuwa angehakikisha
sheria zinafuata mkondo wake ikiwa ni kufungua jalada lenye kumbukumbu namba
MAG/RB/5280/2013.
Tangu Aprili 21,
tuhuma hizo hazikupewa kipaumbele, hadi mtuhumiwa kuachiwa kabla ya kufikishwa
mahakamani, huku habari zake zikifanywa siri.
Taarifa hizi zilifika
katika meza ya Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Charles Kenyela, kabla
hajahamia Makao Makuu na kusema kuwa bado hakuwa na taarifa hizo.
“Ndio kwanza nasikia
kutoka kwako, ila ningeomba huyo anayelalamika kwenye tuhuma hizo, aje ofisni
kwangu nizungumze naye kwa ajili ya kujua kinachoendelea.
“Naomba umwambie huyo
msamalia mwema aje ofisini kwangu siku ya Jumatatu ya Mei 27 ili nijuwe sakata
lenyewe lilivyo na kutafuta suluhu kabla ya kuliandika kwenye vyombo vya
habari, maana si kila jambo linalotokea nalijua, ukizingatia kuwa nina watu
ambao nafanya nazo kazi,” alisema Kenyela.
Taarifa za kuachiwa
kwa mtuhumiwa huyo kinyemela ni mwendelezo wa kashfa mbalimbali zinazoliandama
jeshi la Polisi kila siku na kuzua hofu kwa wananchi wake, ambao wanategemea
uwapo wa jeshi hilo kwa ajili ya kulinda usalama wa raia na mali zao.
No comments:
Post a Comment