https://tpc.googlesyndication.com/simgad/8045142562622600543

Recent Post

Friday, March 17, 2017

Rais Magufuli afuta agizo la vyeti vya Waziri Mwakyembe

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli akizungumza na Wanahabari Mkoani Dodoma kuhusiana na kufuta agizo lililotolewa jana na Waziri wa Katiba na Sheria kuhusu Wananchi wanaohitaji kufunga ndoa kuanzia mwezi Mei mwaka huu kuwa na vyeti vya kuzaliwa. Rais Mhe. Dkt. Magufuli ameagiza utaratibu wa awali uendelee kutumika kwasababu wananchi wengi wa Tanzania hawana vyeti, hivyo wangekosa haki hiyo ya kufunga ndoa. Kushoto kwake ni Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Jordan Rugimbana. PICHA NA IKULU

Usambara Development yatoa msaada wa saruji wilayani Lushoto

 Wanafunzi wa shule ya secondari viti kata ya shume wilayani Lushoto wakipokea mifuko ya saruji yenye thamani ya shilingi laki tano kwa ajili ya ujenzi wa choo kutoka kwa taasisi ya USAMBARA DEVELOPMENT INITIATIVE (UDI) ikiwa ni katika kuchangia juhudi za Mh. Mbunge wa Mlalo mh. Rashid Shangazi za kuleta maendeleo jimboni hapo.
 Diwani wa kata ya Vuga wilayani Lushoto mh. Dhahabu jumaa akipokea miche ya miti kutoka kwa taasisi ya USAMBARA DEVELOPMENT INITIATIVE , ikiwa ni juhudi za kuendeleza na kutunza mazingira wilayani Lushoto, pichani anayekabidhi ni katibu Mkuu wa UDI DIckson shekivuli na naibu katibu Mkuu Frank shempemba.

Thursday, February 23, 2017

Jumia yazindua huduma za ndege

 Ofisa Habari wa Kampuni ya Jumia Travel, Geofrey Kijangwa (kulia), akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, kuhusu kampuni hiyo kuzindua huduma za ndege. Kushoto ni Meneja Mkazi wa Kampuni hiyo, Fatema Dharsee. 

Na Dotto Mwaibale
KAMPUNI ya Jumia Travel imetangaza kuwa imezindua huduma za ndege kwa ajili ya wasafiri, hatua ambayo itapelekea kutanua wigo wa huduma zake. 

Uzinduzi huu unakuja kipindi ambacho Kilele cha Mkutano wa Pili wa Masuala ya Anga Afrika ukifanyika nchini Rwanda. 

Kwa sasa mtandao huo nambari moja kwa huduma za hoteli barani Afrika unatoa huduma za ndani na nje ya nchi kwa kushirikiana na mashirika makubwa ya ndege yakiwemo Precision Air, Kenya Airways, Rwandair Express, Qatar Airways, Emirates, Ethiopian Airlines, South African Airways, KLM, Fly Dubai, Turkish Airlines, Air Arabia, Air Seychelles miongoni mwa nyinginezo.
 Meneja Mkazi wa Kampuni hiyo, Fatema Dharsee akizungumza na wanahabari.

TAYODEA yapongezwa kuinua uchumi wa vijana jijini Tanga

Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Tanga,Mhandisi Mwanasha Tumbo akizungumza wakati wa uzinduzi wa akibadhi vifaa vya vijana wa mradi wa WEKEZA (Wezesha Ustawi Endelevu kiwango cha Elimu Kuzuia Ajira kwa watoto) kulia ni Mkurugenzi wa Tayodea, David Chanyegea na kushoto ni Katibu Tawala wa wilaya ya Tanga,Faidha Salim

 Mkurugenzi wa Tayodea, David Chanyege akizungumza wakati wa halfa hiyo kushoto kwake ni Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Tanga,Mhandisi Mwanasha Tumbo ambaye pia ni Mkuu wa wilaya ya Muheza.

Wednesday, February 22, 2017

Semina yakutanisha vijana mbalimbali kujadili changamoto zao


Bwana Jackson Oganga akiwa anatoa maelezo kwa vijana jinsi ya kupata 'Scholarship' katika zinazotolewa sehemu mbalimbali.
Mwakilishi wa Asasi ya Kiraia  Global Peace Foundation (GPF) Tanzania aliyewakilisha katika Semina hiyo Bi. Anna Mwalongo akielezea kwa kifupi kuhusu Asasi hiyo.

Wajasiriamali watembelewa katika maeneo yao nchini Tanzania

Mkurugenzi wa Kampuni ya Namaingo Business Agency, Ubwa Ibrahim akiwa katika moja ya mikoa kukagua na kuimarisha shughuli za Wajasiriamali wanachama wa kampuni hiyo katika mikoa mbalimbali nchini. Tayari hadi leo ameshafanya ziara katika mikoa ya Iringa, Tabora, Kigoma, Manyara, Arusha na Kilimanjaro.

Mafunzo yanayotolewa na kampuni hiyo kwa wajasiriamali zaidi ya 400,000 nchini ni. ufugaji wa kuku wa chotara, sungura, samaki pamoja na kilimo bishara cha mbogamboga na matunda.

Pia husaidia kupatika kwa masoko ya bidhaa hizo, pamoja na kuwaunganisha katika taasisi mbalimbali za kifedha ili kupata mikopo kirahisi. Imeandaliwa na Richard Mwaikenda.

Tuesday, February 21, 2017

Bayport yatoa kompyuta nne kwa shule za Msingi Dodoma Mjini

Naibu Waziri wa Kazi, Ajira na Vijana, Anthony Mvunde (kulia) akipokea msaada wa Kompyuta Nne kwa Meneja Masoko na Mawasiliano wa Taasisi ya Kifedha Bayport Tanzania, Ngula Cheyo mjini Dodoma leo asubuhi. Kushoto ni Meneja wa Kanda ya Kati wa taasisi hiyo, Kushoto ni Meneja wa Kanda ya Kati wa taasisi hiyo, Christopher Kihwele. 

Na Mwandishi Wetu, Dodoma
TAASISI ya Kifedha ya Bayport Financial Services, jana imemkabidhi kompyuta nne Naibu Waziri wa Vijana, Kazi na Ajira, Mheshimiwa Anthon Mavunde kwa ajili ya shule za Msingi za Majengo, Chigonge, Mahomanyika na Uhuru zilizopo mjini Dodoma.
Baadhi ya wanafunzi wa shule ya msingi Majengo, wakinyoosha mikono juu katika tukio la kukabidhiwa kompyuta nne za Bayport Financial Services, zikipokewa na Naibu Waziri wa Kazi, Ajira na Vijana, Anthony Mavunde.

Makabidhiano hayo yalifanyika katika shule ya Msingi Majengo, ambapo kompyuta hizo zina lengo la kuongeza kiwango cha elimu mkoani Dodoma. Akizungumza leo mjini Dodoma, Meneja Masoko na Mawasiliano wa Bayport Financial Services, Ngula Cheyo, alisema kwamba msaada huo wa kompyuta umetokana na dhamira yao ya kusaidia jamii kwenye sekta ya elimu kama njia ya kuikomboa jamii.

Alisema kwamba si mara ya kwanza kusaidia sekta ya elimu kutokana na kujitokeza mara kadhaa kujenga madarasa, kununua thamani za shule pamoja na kudhamini mikopo ya elimu ya juu na vitabu. 
Baadhi ya walimu wa Shule ya Msingi Majengo, wakisoma shairi mahususi kwa ajili ya Naibu Waziri wa Kazi, Ajira, Vijana, Anthony Mavunde wakati anakabidhiwa kompyuta nne kutoka kwenye taasisi ya Bayport Financial Services.

“Bayport tuna lengo la kuikwamua jamii katika maendeleo kwa kuhakikisha kwamba tunakuza kiwango cha elimu, hivyo kama sehemu ya kuunga mkono juhudi za serikali kuhamia Dodoma, tumeamua kutoa kompyuta nne kwa kuboresha miundo mbinu ya elimu ili nchi yetu isonge mbele.

Monday, February 20, 2017

Mkuu wa wilaya Muheza ajionea zoezi la upasuaji wa macho Kituo cha Afya Ubwari

MKUU wa wilaya ya Muheza Mkoani Tanga,Hajat Mhandisi Mwanasha Tumbo katika akiingia kwenye kituo cha Afya Cha Ubwari leo wakati alipokwenda kuangalia zoezi la upasuaji wa macho kwa wakazi wa wilaya hiyo wanaokabiliwa na matatizo mbalimbali ikiwemo ya mtoto wa Jicho iliyoendeshwa na Taasisi ya Medewell Charitable Health Centre kulia ni Mganga Mkuu wa wilaya hiyo,Mathew Mganga na kushoto ni Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo, Luiza Mlelwa.Baadhi ya wazee waliofanyiwa upasuaji wakisubiri zoezi la kupatiwa dawa na miwani
Baadhi ya wananchi waliofanyiwa upasuaji wakisubiri zoezi la kupatiwa dawa na miwani.

Mbunge wa Mkuranga aongoza tukio la kuchangia damu Dar es Salaam

Mgeni rasmi wa kongamano la kuchangia damu lililoandaliwa na Tanzania Yemen Professional Foundation (TYPF), Abdallah Ulega ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Mkuranga akizungumza umuhimu wa kila Mtanzania kujitolea damu ili kuinusuru jamii yake. Picha zote na Mpiga Picha Wetu.


Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
MBUNGE wa Mkuranga, Mheshimiwa Abdallah Ulega, mwishoni mwa wiki aliongozana na Balozi wa Kuwait nchini Tanzania, Jasem Al Najem, katika tukio la uchangiaji wa damu lililoandaliwa na Taasisi ya Tanzania Yemen Professional Foundation (TYPF), lililofanyika katika Ukumbi wa City Garden, jijini Dar es Salaam. Katika tukio hilo, watu mbalimbali walishiriki katika uchangiaji damu kama sehemu ya kutatua changamoto ya upungufu wa damu kwa wenye uhitaji, wakiwamo akina mama wajawazito, ajali za barabarani na majanga mengine.
Balozi wa Kuwait nchini Tanzania, H.E Jasem Al Najem akitolewa damu katika tukio la kuchangia damu lililofanyika mwishoni mwa wiki katika Ukumbi wa City Garden, jijini Dar es Salaam.


Akizungumza katika uchangiaji huo, Mbunge Ulega alisema kwamba jukumu la kuchangia damu linamuhusu kila Mtanzania, huku akiwataka watu kujenga mazoea ya kujitolea damu ili kuondoa upungufu wa damu.

Alisema kwamba mahitaji ya damu kwa nchi yetu ni makubwa, hivyo amefarijika kwa kupata mwaliko wa kuwa mgeni rasmi sambamba na kuongoza tukio hilo la uchangiaji wa damu, akiamini amejitolea jambo la msingi na la lazima.

Monday, February 13, 2017

Mke wa Rais Magufuli atembelea wasiojiweza mkoani Singida

NA MWANDISHI MAALUM, SINGIDA
MKE wa Rais Mheshimiwa Mama Janeth Magufuli pamoja na Mke wa Waziri Mkuu Mama Mary Majaliwa wametoa rai kwa Wanzania kujenga tabia ya kusaidia watu wasiojiweza na wenye mahitaji maalumu.
Mke wa Rais Mama Janeth Magufuli na mke wa Waziri Mkuu Mama Mary Majaliwa wakilakiwa kwa furaha walipowasili katika Makazi ya Wazee Wasiojiweza Sukamahela wilaya ya Manyoni mkoani Singida leo.
Wake hao wa viongozi pia wamewatahadharisha watumishi wanaofanya kazi katika vituo vya kulelea wazee wasiojiweza wahakikishe misaada inayotolewa na wadau mbalimbali inawafikia walengwa bila ya kuchakachuliwa.

Wameyasema hayo leo (Jumatatu, Februari 13, 2017) wakati walipotembelea Makazi ya Wazee wasiojiweza na walemavu watokanao na ugonjwa wa ukoma ya Sukamahela wilayani Manyoni Mkoani Singida. Katika kituo hicho wamekabidhi tani 7.5 za vyakula mbalimbali ukiwemo mchele, unga wa sembe na maharage, ambapo Mama Janeth amewataka viongozi wa kituo kuhakikisha chakula hicho hakichakachuliwi.

Akizungumza na wazee wa makaazi hayo, viongozi mbalimbali na wananchi wanaozunguka eneo hilo Mama Janeth amesema “Naomba chakula hiki kitunzwe vizuri na hakikisheni kinawafikia walengwa na kisichakachuliwe hii ni sadaka,”.

Kwa upande wake Mama Mary amewaomba wadau mbalimbali kujitokeza na kuwasaidia wazee wanaoishi katika makaazi ya kulelea walemavu na wasiojiweza nchini kwa sababu wanakabiliwa na changamoto nyingi. “Watanzania wote popote mlipo tukumbuke kutembelea vituo vya kulelea wazee kikiwepo na hiki tulichokitembelea leo cha Sukamahela na kutoa misaada mbalimbali kkwa kadri tutakavyojaaliwa,” amesema.

DC Muwango ataka ardhi iliyovamiwa irejeshwe

Mkuu wa wilaya ya Nachingwea Mhe Rukia Muwango akisisitiza umuhimu wa kufanya mazoezi.

Na Mathias Canal, Lindi
Mkuu wa wilaya ya Nachingwea Mhe Rukia Muwango ameitaka Halmashauri ya Wilaya hiyo irejeshe maeneo yote ya wazi yaliyo vamiwa na kutumika kinyume cha matumizi yaliyolengwa.

Dc Muwango ametoa agizo hilo mjini Nachingwea kwenye uzinduzi wa kampeni ya kitaifa ya kudhibiti magonjwa yasioambukiza na yanayoweza kuzuilika kupitia mazoezi na michezo.

Uzinduzi huo uliofanyika katika uwanja wa kumbukumbu ya Sokoine ambapo Alisema kuwa yeye kama mwenyekiti wa kamati ya ulinzi na usalama ya wilaya hiyo anatambua na anazotaarifa za kutosha kuwa maeneo mengi ambayo yalitengwa kwa ajili michezo na shuguli nyingine za umma yamevamiwa na kubadilishwa matumizi.
Mkuu wa wilaya ya Nachingwea Mhe Rukia Muwango akionyesha mfano wa ufanayaji mazoezi
Mkuu wa wilaya ya Nachingwea ambaye pia ni mwenyekiti wa kamati ya ulinzi na usalama wa Wilaya hiyo Mhe Rukia Muwango akifanya mazoezi katika uzinduzi huo.

Maonyesho ya utalii nchini Saudi Arabia yaipaisha Tanzania

Baaadhi ya watu mbalimbali wakitembelea banda la Tanzania, nchini Saudi Arabia, katika maonyesho ya utalii ya '(Travel and Tourism Pioneers Forum - 2017).

Na Mwandishi Maalum, Saudi Arabia
Ubalozi wa Tanzania nchini Saudi Arabia mwishoni mwa juma hili ulishiriki katika maonyesho ya Safari na Utalii yajulikanayo kama '(Travel and Tourism Pioneers Forum - 2017).

Maonyesho ya TPF 2017 ambayo hufanyika kila mwaka kwa uandalizi Al Awsat Expo chini ya uhisani wa Mwana Mfalme HRH Prince Dr. Seif al Islam bin Saud bin Abdulaziz, yamefanyika kwa mafanikio huku ubalozi wa Tanzania ukifanikiwa kwa kiasi kikubwa kutangaza utalii wa Tanzania.

Akizungumza katika maonyesho hayo, Balozi wa Tanzania nchini Saudi Arabia, H.E Hemed Mgaza, alisema kwamba maonesho hayo yalikuwa maalumu kwa wafanya maamuzi na viongozi wa asasi za utalii (decision makers and leaders and tourisma leaders) nchini Saudi Arabia.
Balozi wa Tanzania nchini Saudi Arabia, H.E Hemed Mgaza, mwenye suti nyeusi akizungumza jambo na wageni waliotembelea katika banda la Tanzania kwenye maonyesho hayo.

Alisema kwamba kuwa banda la Tanzania lilifanikiwa kuonesha vivutio vya utalii vya Tanzania ikiwemo mlima Kilimanjaro, mbuga za wanyama, hifadhi za taifa, maeneo ya kihistoria ya Zanzibar, kilwa na Bagamoyo. 

Saturday, February 11, 2017

Makamu wa Rais Tanzania aendeleza kasi ya mazoezi ya viungo mjini Dodoma


Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akisalimiana na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa wakati wa kukabidhi matembezi ya Uzinduzi wa Kitaifa wa Mazoezi ya Viungo kwa wananchi wote ya kupambana na magonjwa yasioambukiza, Makao Makuu ya nchi Dodoma.

Makamu wa Rais Mh.Samia Suluhu Hassan akishiriki mazoezi mapema leo asubuhi mjini Dodoma ikiwa ni sehemu ya kumuunga mkono Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa katika Uzinduzi wa Kitaifa wa Mazoezi ya Viungo kwa wananchi wote ya kupambana na magonjwa yasioambukiza, mjini Dodoma.Pichani kushoto ni Waziri wa Habari,Utamaduni,Sanaa na Michezo,Mh.Nape Nnauye.

Khadija Kopa ataka wanawake wajikwamue kiuchumiBaadhi ya nguo za maharusi zinavyoonekana katika duka la urembo na mitindo lililozinduliwa rasmi jana, huku mgeni rasmi akiwa ni mwimbaji wa muziki wa taarabu nchini Tanzania, Bi Khadija Kopa.

Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
MWIMBAJI wa muziki wa taarab nchini Tanzania, Bi Khadija Kopa, amewataka wanawake kuendelea kujikwamua kiuchumi wao wenyewe bila kusubiri kuwezeshwa na wanaume.
Khadija aliyasema hayo jana katika ufunguzi wa duka kubwa la kisasa la urembo na nguo za wanawake linalojihusisha pia na kupamba maharusi, kukodisha na kuuza nguo za maharusi, linalojulikana kama Taiba Beauty, linalomilikiwa na mjasiriamali Twaiba Ahmed Ally.
Mwimbaji mkongwe wa muziki wa taarabu nchini, Bi Khadija Kopa, akizungumza na waandishi hawapo pichani katika uzinduzi wa duka la nguo za wanawake na za harusi linalomilikiwa na mwanamama Twaiba Ahmed Ally.

Alisema kwamba wapo wanawake wanaoamini kuwa hawawezi kuendelea hadi wawezeshwe, jambo linalohitaji kupingwa vikali ili wanawake waweze kupiga hatua kiuchumi na kujikomboa wao wenyewe.
Mmiliki wa duka la nguo za maharusi lililopo mtaa wa Livingstone na Mkunguni, Bi Twaiba Ahmed Ally, katikati akikata keki ya uzinduzi wa duka hilo jana. Kulia ni mwimbaji wa taarabu nchini, Khadija Kopa akilishwa keki kama mgeni rasmi. Kushoto ni mtangazaji wa kipindi cha Ng'ari Ng'ari kutoka Clouds Tv, Sakina Lyoka.

Tuesday, January 31, 2017

CUF ya Profesa Lipumba yajibu mapigo ya ruzuku


Mkurugenzi wa Fedha na Uchumi (Taifa) wa Chama cha Wananchi (CUF), Thomas D.C Malima (katikati), akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari Makao Makuu ya Chama hicho jijini Dar es Salaam leo kuhusu ruzuku ya chama hicho iliyopokelewa kupitia akaunti namba 2072300456 ya Benki ya NMB Tawi la Temeke. Kulia ni Mkurugenzi wa Mipango na Uchaguzi, Mneke Jafar na Katibu Jumuiya ya Wanawake (JUKE), Salama Masoud.
Meza Kuu. Kutoka kulia ni Kamanda Mkuu, Athumani Hamadi,Mkurugenzi wa Mipango na Uchaguzi, Mneke Jafar, Mkurugenzi wa Fedha na Uchumi (Taifa) wa Chama cha Wananchi (CUF), Thomas D.C Malima, Katibu Jumuiya ya Wanawake (JUKE), Salama Masoud na Mjumbe wa Mkutano Mkuu Taifa, Masha Amour.
Wanahabari wakichukua taarifa hiyo.
Waandishi wa habari kutoka vyombo mbalimbali wakichukua taarifa hiyo. (Imeandaliwa na mtandao wa www. habari za jamii.com-simu namba 0712-727062)
Mkutano ukiendelea.


TAARIFA KWA UMMA 

The Civic United Front (CUF – Chama Cha Wananchi) chini ya Uongozi thabiti wa Mwenyekiti wake Mhe Profesa Ibrahim Haruna Lipumba kinaishukuru na kuipongeza Ofisi ya Msajili wa Vyama Vya Siasa kwa kukipatia Chama chetu Ruzuku yake inayopatikana kwa Mujibu wa Sheria ya vyama vya Siasa Namba 5 ya mwaka 1992.

Pamoja na Ruzuku ya CUF kuzuiwa kwa Muda wa miezi mine (4) kuanzia mwezi Septemba, 2016 hadi Desemba 2016 kutokana na sintofahamu ya uongozi wa Kitaifa wa CUF, Msajili hakuona haja ya kuendelea kuizuia wakati shughuli za chama zinafanyika kila siku. Kuendelea kuizuia Ruzuku halali ya chama ni kukizuia kufanya kazi zake halali za kisiasa ikiwa ni pamoja na kushiriki katika chaguzi mbali mbali za kiserikali zinazoendelea nchini. 

Waheshimiwa wanahabari, Baada ya Msajili wa Vyama vya Siasa kupitia katiba ya CUF ya mwaka 1992, Toleo la 2014 alijiridhisha kuwa Mhe Profesa Ibrahim Haruna Lipumba ndiye Mwenyekiti halali wa CUF kwa kuwa mchakato wa kukamilisha kujiuzulu kwake haukukamilika kabla yeye kutengua barua yake ya kujiuzulu.

Mnamo Tarehe 23 Septemba 2016 , Msajili aliandika barua kwa Katibu Mkuu wa CUF kumjulisha msimamo na mwongozo wa wake  kuwa  “Mwenyekiti wa Taifa wa CUF ni  Mhe Profesa Ibrahim Haruna Lipumba”

Baada ya Katibu Mkuu kupokea barua hiyo aliamua kupinga Uamuzi huo wa Msajili wa Vyama vya Siasa uliotokana na Malalamiko ya wajumbe wa Mkutano Mkuu wa Taifa wapatao 324 kati ya 343 ambao walilalamikia uvunjifu wa Katiba ya CUF unaofanywa na Katibu Mkuu Maalim Seif Sharif Hamad kwa Msajili wa Vyama vya Siasa.

Maaalim Seif na timu yake walienda mbali kwa “kuikimbia ofisi yake” iliyoko hapa Ofisi Kuu ya CUF Buguruni na kukimbilia Mafichoni kusikojulikana na kusababisha kushindwa kutekeleza majukumu yake ya kiutendaji.  Hivyo, Mwenyekiti wa Taifa aliamua kufanya mabadiliko ya Kurugenzi za Chama kwa kumujibu wa ibara ya 91(1)(f) ya katiba ya CUF, nainukuu:

“Mwenyekiti wa Taifa atateua kutoka miongoni mwa wajumbe wa Mkutano Mkuu wa Taifa, wajumbe wa Baraza Kuu la Uongozi Taifa au wanachama wajasiri kuwa wakurugenzi na manaibu wakurugenzi wa Chama pamoja Katibu wa Kamati ya Ulinzi na Usalama baada ya kushauriana na Makamu Mwenyekiti na kufikisha uteuzi huo mbele ya Baraza Kuu la Uongozi la Taifa kwa kuthibitishwa”. 

Kwa mujibu wa Ibara ya 95(3) ya Katiba ya CUF ya mwaka 1992, Toleo la 2014, Nainukuu:-
  “Naibu Katibu Mkuuatakayemfuatia Katibu Mkuu kwa madaraka ni Yule anayetoka upande tofauti wa Jamhuri ya Muungano na upande anotoka Katibu Mkuu”.  Kwa kifungu hicho, Katibu Mkuu anaposhindwa kutekeleza majukumu yake kwa sababu yoyote ile, Naibu Katibu Mkuu Bara ndiye anakaimu Ukatibu Mkuu mpaka atakaporejea ofisini kuendelea na majukumu yake.

Hii inatokana ukweli wa kikatiba uliowekwa kwenye ibara ya 105 (1) ya Katiba ya CUF ya mwaka 1992, Toleo la 2014, Nainukuu:-
  
 “Pale ambapo mwanachama yeyote wa Chama mwenye madaraka kwa mujibu wa masharti ya katiba hii, kwa sababu yeyote ile, hawezi kutekeleza kazi zake kwa muda, mwanachama anayemfuata kwa madaraka kwa mujibu wa katiba atakaimu nafasi yake”. 

Hivyo, kwa mujibu wa ibara hii na ile ya 95(3) Ni suala la kikatiba lisilo na shaka kwa Mheshimiwa Magdalena Sakaya (Mb) ambaye ndiye anayemfuata Katibu Mkuu kwa Madaraka kukaimu ofisi ya Katibu Mkuu mpaka atakaporejea ofisini kwake Buguruni. Kwa hiyo, Mhe Sakaya ataendelea kufanya majukumu yote ya Katibu Mkuu kwa mujibu wa Katiba ya CUF. Na Katibu Mkuu hapaswi kulalamika.

Kuhusu masuala ya fedha, Kwa mujibu wa kanuni ya jfedha ya mwaka 2014, ibara ya 22(2)(a) (B):-“Masuala yote ya fedha yanasimamiwa na Mkurugenzi wa Fedha na Uchumi na ndiye Mshauri Mkuu wa Katibu Mkuu kuhusu Masuala ya Fedha”. 

Na kwa kuwa Katibu Mkuu ni Ofisi siyo mtu, anapokuwa hayupo ofisini Naibu Katibu Mkuu Bara atatekeleza majukumu yote ya ofisi ya Katibu Mkuu kama Kaimu Katibu Mkuu.  Ni aibu kwa Mwalimu Seif kulalamika wakati anaijua katiba ya CUF na anajua kuwa amekimbia ofisi mwenyewe ndiyo maana Mhe Sakaya anafanya kazi alizozikimbia kwa kushirikiana na wakurugenzi walioteuliwa na Mwenyekiti wa Taifa kwa mujibu wa Katiba.

Waheshimiwa wanahabari, Chama Chetu kimepokea sehemu ya malimbikizo ya ruzuku ya CUF Kiasi cha Tsh. 369,366,671/=. Tumepokea Ruzuku hiyo kupitia Akaunti namba 2072300456 ya The Civic United Front (CUF-Chama cha Wananchi)  NMB Tawi la Temeke. Hii siyo akaunti Mpya ya Chama kama inavyodaiwa Maalimu Seif na genge lake.

Akaunti hii ilifunguliwa zaidi ya miaka Kumi iliyopita na Katibu Mkuu kwa ajili ya kupokea na kutoa fedha za CUF kwa wilaya ya Temeke. Na kwa mujibu wa Kanuni ya Fedha ya CUF ya mwaka 2014, ibara ya 23(1)(f) Nainukuu: -
  
“Chama ngazi ya Taifa kinaweza kufungua akaunti tofauti au kubadili matumizi ya akaunti iliyopo kwa ajili ya kazi au shughuli maalum kadri itakavyoona inafaa. Akaunti hizo zilizofunguliwa utawekwa utaratibu maalum wa kuzihudumia”.

Kwa kuzingatia hali iliyopo, Tuliona kubadilisha matumizi ya Akaunti ya The Civic United Front (CUF-Chama cha Wananchi), Tawi la Temeke itumike kupokelea Ruzuku ya Chama toka serikalini ili iweze kufikia katika mikono salama kwa ajili ya uendeshaji wa Shughuli za Chama.

Waheshimiwa wandishi, Baada ya kuipokea Ruzuku hiyo, tayari tumeshaitumia katika harakati za Kiuchaguzi katika Chaguzi za marudio ya Udiwani katika kata 14 ambapo CUF imefanya vizuri sana katika kata tatu (3) ambazo ni Nkome (Geita), Malya (Kwimba) na Kijichi (Temeke). 

Waheshimiwa wandishi, Ikumbukwe kuwa Tangu  Mwalimu Seif na Genge lake wakimbie Ofisi Kuu Buguruni Tarehe 23 Septemba 2016, shughuli za chama zilikuwa zikiendelea kufanyika japokuwa hatukuwa tunapata ruzuku toka Serikalini. Wanachama wetu walikuwa na ari zaidi ya kukichangia chama ili kuendeleza harakati za ukobozi wa Haki sawa kwa Wote. Kwa mapenzi makubwa ya Chama chake Mheshimiwa Mwenyekiti wetu Profesa Ibrahim Haruna Lipumba alikuwa Msitari wa mbele kukisaidia chama kwa kujitolea na hata kukikopesha chama ili tutekeleze Majukumu ya ujenzi wa chama.

Waheshimiwa wanahabari, Hii si mara ya kwanza Mhe Profesa kukisaidia chama Chetu. Ipo mikataba kadhaa ambayo Mwenyekiti wetu amewahi kukikopesha chama fedha zake mwenyewe.

Waheshimiwa wandishi, Ni jambo la kusikitisha kuwa kwa takribani mwaka mmoja hasa baada ya Mhe Profesa Lipumba kuwa nje ya uenyekiti wa Taifa wa CUF, Wilaya zote za Tanzania Bara zilisitishiwa Ruzuku toka Ofisi kuu wakati wilaya zote za Zanzibar zikiwa zinaendelea kupokea ruzuku. Kwa kweli huu ni uonevu mkubwa kwa wanaCUF wa Tanzania Bara na huu ni mpango wa Makusudi wa Maalim Seif na genge lake.

Baada ya kupokea Ruzuku hiyo, Tumeamua kuzipelekea ruzuku Wilaya zote za Tanzania Bara alau ruzuku ya miezi mitatu mitatu kwa kila wilaya. Mpaka sasa tumeshatuma ruzuku katika wilaya 82 ambapo Tsh. 66,300,000/= zimetumika. 

Ikumbukwe kuwa Wilaya zinazotakiwa kupokea ruzuku ni wilaya zote zilizofanya uchaguzi wa ndani ya Chama ambapo Jumla ya wilaya 104 zina uongozi halali wa chama. Kwa mantiki hiyo, wilaya 22 bado hazijapewa Ruzuku kutokana na matatizo mbalimbali ikiwemo Akaunti zao kuwa dormat kwa muda mrefu, na nyingine kutowasilisha akaunti namba zao ofisini. 

Hivyo, tunatoa wito kwa viongozi wa Wilaya zote wa CUF kwenda benki kuangalia taarifa ya fedha ya akaunti zao kisha kutupa taarifa. Lakini pia ni wajibu wao kufanya matumizi ya fedha hizo kwa mujibu wa sheria za nchi na kanuni ya Fedha za CUF kwa kuwa hizo ni fedha za umma.

Waheshimiwa wandishi, tumesikitishwa na tamko la inayojiita Bodi ya wadhamini ya CUF eti fedha zimeibwa na wanazuia viongozi wa wilaya wasichukue fedha zilizoko kwenye akaunti zao. Kwa mujibu wa ibara ya 98(1) nainukuu:- 

“ Kutakuwa na Bodi ya wadhamini itakayoteuliwa na Baraza Kuu la Uongozi la Taifa kwa mujibu wa sheria za nchi kwa kipindi cha miaka mitano (5) na mjumbe anaweza kuteuliwa tena baada ya muda kumalizika”. 

Ndugu wandishi, Bodi ya CUF iliteuliwa kwa mara ya mwisho Januari 2010, hivyo ilimaliza muda wake Januari 2015.  Haijawahi kuteuliwa tena na haijawahi kulipiwa Mchango wa kila mwaka RITA tangu 2013. Kutokana, sheria za nchi na katiba ya CUF, Bodi hiyo ni mfu kwa hiyo haina uwezo wa kushughulikia na kusimamia masuala yoyote ya fedha za CUF. How can a dead body talk about financial matters?. 

Wakiwa wanajua ukweli huo, bado wanakubali kutumika kwa maslahi ya Maalim Seif. Hii ni kuthibitisha kuwa “Mbwa mzee hafundishwi mbinu mpya za kuwinda”. Ni kweli Maalim Seif, Bashange na Katau wamezeeka, ni sawa mbwa wazee wasioweza kutumia mbinu mpya za kujijenga kwa wanachama wa CUF bali wanazidi kujifedhehesha. 

Ndevu zao ni ishara ya kupitwa na wakati. Ni bora watuachie vijana tujitanabahishe kwa mbinu za kisasa za kuiweka kweli ndani ya CUF na Watanzania kwa ujumla. Kama Maalim Seif alikuwa simba wa vita vya miaka 1980, kamwe hawezi kuwa simba wa vita ya 2016/2017. Huwezi kuwa Katibu Mkuu ambaye unapeleka Ruzuku Zanzibar kupitia Michango ya Wabunge lakini ukawa hutaki Wilaya za Tanzania Bara zipate Ruzuku. Huu ni ubaguzi uliokithiri na sisi hatutaukubali.

Tunaiomba ofisi ya Gavana wa Benki kuu kutupilia mbali ombi la Bodi ya wadhamini ya CUF isiyo halali kwa kuwa imepitwa na wakati na inakiuka hata katiba ya CUF ibara ya 98(1) na (2) inayotaka bodi iundwe na jumla ya wajumbe 9 ambapo 3 kati yao lazima wawe wanawake lakini bodi feki ya Mwalimu Seif ina wanaume watupu ndiyo maana wanailalamikia RITA eti wametoa siri za ufeki wao. 

Na kama wanahisi RITA wameghushi nyaraka, waende Polisi wakafungue mashitaka dhidi ya RITA, japokuwa nalo ni jambo gumu kwao maana wao ni Bodi mfu, hawana uwezo wa kushitaki wala kushitakiwa.

Waheshimiwa wanahabari, kwa sasa Maalim Seif anamlaumu kila mtu. Anamlaumu Jaji Mutungi kwa kusema ukweli, anawalaumu Wajumbe wa Mkutano Mkuu wa Taifa kwa kuupinga udikiteta wake Mkutanoni, anamlaumu Gavana wa Benki, anailaumu RITA, anamlaumu Jaji Kihiyo, anamlaumu Rais Shein, anamlaumu Jecha, anamlaumu Profesa Lipumba eti anakuja kuzuia asipewe urais wa Zanzibar lakini cha ajabu hajilaumu mwenyewe kwa udikiteta wake ndani ya CUF na tamaa yake ya kupenda fedha za Lowasa kuliko utu na thamani yake kwa jamii.

Mwisho, tunamtaka Mwalimu Seif na Genge lake waende kwa amani watuachie CUF yetu. Hata Mapalala ailianzisha CUF lakini alipoonekana anaisaliti aliamua kuiacha CUF kwenye mikono salama. “Yeye sasa ni Simba mzee hawezi mawindo ya wakati huu”.

Imeandaliwa na;-
Thomas D.C Malima
Mkurugenzi wa Fedha na Uchumi (Taifa)

Sunday, January 29, 2017

Rais Magufuli wa Tanzania ahutubia jengo jipya la Mwalimu Nyerere Ethiopia

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akiwahutubia Viongozi Wakuu wa Mataifa mbalimbali hawapo (pichani) katika Jengo jipya la Kituo cha Amani na Usalama kilichopewa jina Rasmi la Mwalimu Julius Nyerere, Addis Ababa nchini Ethiopia.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akijadiliana jambo na Rais wa Rwanda Paul Kagame wakati wakielekea katika Kituo cha Amani na Usalama cha Makao Makuu ya Umoja wa Afrika kilichopewa jina la Rais wa kwanza wa Tanzania Mwalimu Julius Nyerere, Addis Abba nchini Ethiopia. PICHA NA IKULU

Treni ya Kigoma yapata ajali

By Staff wa TRL
Leo saa 9:40 alasiri treni yetu ya Deluxe ilipokuwa ikirejea Dar kutoka Kigoma imepata ajali kati ya vituo vya Ruvu na Ngeta ambapo mabehewa 9 yamepata ajali . Kati ya hayo manne yameanguka, mawili yametenguka na matatu yameacha njia..

Imeripotiwa watu kadhaa wamepata majeraha mepesi isipokuwa mmoja ndiye aliyepata majeraha makubwa.amekimbizwa hospitali kwa matibabu zaidi. Hizi ni taarifa za awali..baada ya Kikosi cha uokoaji kikimaliza kazi ya kuinua mabehewa ndio taarifa ya Wahanga itakamilika! 

Wakati taarifa hii ikipatikana Waziri wa Sekta Profesa Mbarawa. Mkuu wa TRL Ndugu Kagosa Kamanda Kikosi cha Polisi Reli Mhandisi Chillery wako njia kuelekea katika eneo la ajali! . Sehemu ya treni ya Deluxe yenye mabehewa kumi iko njiani kuja Dar es Salaam inatarajiwa kufika saa 2 usku.

Kompyuta za Bayport mkoani Mara kuelekezwa shule za Kata

Mratibu wa Masoko na Mawasiliano wa Bayport Financial Services, Mercy Mgongolwa, akimkabidhi kompyuta sita Katibu Tawala wa Mkoa wa Mara, Mheshimiwa Ado Mapunda kwa ajili ya kuongeza ufanisi katika ofisi za umma mkoani Mara. Wengine kwenye tukio hilo ni watumishi wa Bayport, akiwamo Meneja wa Kanda ya Ziwa wa Bayport, Lugano Kasambala wa kwanza kushoto. Picha na Mpiga Picha Wetu Mara.


Na Mwandishi Wetu, Mara
SERIKALI ya Mkoa Mara kwa kupitia Katibu Tawala wake, Mheshimiwa Ado Mapunda, imewaagiza watendaji wa serikali mkoani humo kuhakikisha kompyuta walizopewa na Taasisi ya Kifedha ya Bayport Financial Services, zinaelekezwa kwenye shule za kata ili kuchangia ukuzaji wa kiwango cha elimu.

Mheshimiwa Mapunda aliyasema hayo mwishoni mwa wiki wakati anapokea kompyuta sita kutoka Bayport zilizoelekezwa katika Halmashauri ya Tarime, Rorya na Manispaa ya Musoma, huku kila ofisi ikipata kompyuta mbili ikiwa ni mwendelezo wa ugawaji wa vitendea kazi kutoka kwenye taasisi hiyo inayojihusisha na mikopo ya fedha taslimu kwa watumishi wa umma na wafanyakazi wa kampuni zilizoidhinishwa.

Akizungumza katika makabidhiano hayo, Katibu Tawala huyo alisema lengo la Mkoa wao ni kuona kiwango cha elimu kinapiga hatua kubwa, hivyo wameona msaada huo uelekezwe zaidi katika shule za kata kwa ajili ya kuhifadhi kumbukumbu muhimu za wanafunzi wao.

Alisema kufanya hivyo kutaongeza ukuzaji wa elimu ya wanafunzi wa mkoani Mara, ili iwe njia ya kuandaa wataalamu wazuri kwa kutumia vema teknolojia ya kompyuta inayoboresha utendaji wa kazi.

“Tunashukuru wenzetu wa Bayport wa Kanda ya Ziwa pamoja na Makao Makuu kwa kutuletea msaada huu mkubwa kwetu ambao kwa hakika tutautumia vizuri katika Mkoa huu wa Mara ili ulete tija kama mlivyokusudia wakati mnafikiria kusambaza.

“Ofisi yetu imeagiza kompyuta hizi zisambazwe katika baadhi ya shule za kata kwa kuzitumia kwa namna moja ama nyingine ili wanafunzi wetu wasonge mbele zaidi kwa kuanzia kurekodi vizuri takwimu zao kama njia ya kugundua tunafanya juhudi za kutuvusha hatua ya juu zaidi,” Alisema Mapunda.

Naye Mratibu wa Masoko na Mawasiliano wa Bayport Financial Services, Mercy Mgongolwa, alisema ndoto zao zinaelekea kukamilika kuhakikisha kwamba msaada wa kompyuta zao unafika kwa haraka kama walivyokusudia na kuuzindua mwaka jana jijini Dar es Salaam.

“Kompyuta tulizotoa Mara na Kanda ya Ziwa ni mwendelezo wetu wa kutoka kwenye kompyuta 125 tulizomkabidhi Mheshimiwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, huku 80 zikielekezwa mikoani na kuufanya mzigo wote ufikie 205 wenye thamani ya Sh Milioni 500,” Alisema Mercy.


Mbali na Mara, Bayport pia walikabidhi kompyuta mbili kwa Halmashauri ya Wilaya Misungwi, mkoani Mwanza na kuifanya Kanda ya Ziwa kuvuna kompyuta nane za taasisi hiyo ambapo pia ilitangaza kuwa utaratibu huo wa kufikisha kompyuta utaendelea katika wilaya na mikoa mbalimbali ya Tanzania Bara wakiamini utasaidia kuongeza ufanisi katika ofisi za umma.

Tukio la moto makazi ya askari mkoani Kilimanjaro lahamisha askari tisa

Kamishna wa Operesheni na Mafunzo ya Jeshi la Polisi,Nsato Marijani akiwasili katika eneo lilipo jengo la ghorofa ambalo ni makazi ya sakari lililoungua moto huku akiongozana na Mwenyeji wake Kamanda wa Polisi mkoa wa Kilimanjaro,Wilbroad Mutafungwa.
Jengo la ghorof mbili ,makazi ya askari Polisi wa vikosi mbalimbali mjii Moshi liliungua moto sehemu ya juu na kueteketeza vyumba tisa pamoja na mali za asakri waliokuwa wakiishi katika vyumba hivyo.

CCM mkoani Shinyanga yafanya kongamano la kuangalia ufanisi wake


Chama cha Mapinduzi wilaya ya Shinyanga Mjini katika mkoa wa Shinyanga kimefanya Kongamano ikiwa ni uzinduzi wa wiki ya Maadhimisho ya miaka 40 tangu kuzaliwa kwa Chama Cha Mapinduzi CCM Februari 05, mwaka 1977.


Kongamano hilo limefanyika leo Katika Ukumbi wa CCM mkoa wa Shinyanga na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wa wilaya ya Shinyanga mjini na mkoa wa Shinyanga,makada wa CCM na vyama vya upinzani na watu mbalimbali wenye mapenzi mema wakiwemo wanafunzi wa Shule ya sekondari Buluba na Kom sekondari.
Mada mbalimbali zilitolewa wakati wa kongamano hilo ikiwemo historia ya CCM na mafanikio ya chama hicho tangu kuanzishwa kwake mwaka 1977.

Katika kuadhimisha wiki ya maadhimisho ya miaka 40 ya CCM,Chama cha Mapinduzi wilaya ya Shinyanga kitashiriki katika shughuli mbalimbali za maendeleo katika ngazi ya matawi ikiwemo,kupanda miti,kusalimia wagonjwa,watoto yatima,walemavu,kutembelea shule,michezo na kufanya mikutano ya ndani badala ya mikutano ya hadhara.
Vyama asili vilivyozaa CCM ni Tanganyika African National Union (TANU) cha Tanganyika  na Afro Shiraz Party (ASP) cha Zanzibar vyote vikiwa ni vyama vya ukombozi.
Kauli mbiu ya maadhimisho ya miaka 40 ya CCM ni "CCM Mpya,Tanzania Mpya".

Tuesday, January 24, 2017

Balozi Mgaza apigia chapuo ‘Hapa Kazi Tu’ Saudi Arabia

Na Mwandishi Maalum, Saudi Arabia
WATANZANIA waishio nchini Saudi Arabia, wametakiwa kufanya juhudi za kuitangaza nchi yao pamoja na kuangalia namna ya kutekeleza kiu ya nchi ya viwanda kama ilivyoasisiwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dr John Pombe Magufuli.
Balozi wa Tanzania nchini Saudi Arabia, H.E Hemedi Mgaza, mwenye suti nyeusi, akifurahia jambo ofisini kwa Waziri anayeshughulikia Masuala ya Hijja na Umrah wa Serikali ya Saudi Arabia, Mhe. Dr. Mohammed Saleh Bin Taher Benten, alipofika ofisini kwake kujadiliana mambo mbalimbali ikiwamo hija ya mwaka huu wa 2017.

Baadhi ya Watanzania wanaoishi nchini Saudi Arabia, wakimsikiliza Balozi wa Tanzania nchini Saudi Arabia, H.E Hemedi Mgaza, hayupo pichani walipokutana katika kikao cha pamoja kwa ajili ya kuangalia fursa za kimaendeleo nchini Tanzania.

Hayo yamesemwa mwishoni mwa wiki mjini Jeddah, Saudi Arabia na Balozi wa Tanzania nchini hapa, H.E Hemedi Mgaza, alipofanya kikao na Watanzania waishio nchini hapa kama njia za kushirikiana na wadau hao kwa ajili ya kupeleka maendeleo ya uhakika nchini Tanzania na kuisimamia kwa vitendo kauli mbiu ya ‘Hapa Kazi Tu’.

Akizungumzia juu ya fursa ya uwekezaji nchini Tanzania, Balozi Mgaza alisema ni wajibu wa kila mmoja kufanya kazi kwa nafasi yake kwa ajili ya kukuza uchumi wa nchi yao. Alisema mbali na Watanzania hao kuwekeza kwao kama uwezo wanao, pia wanaweza kutangaza vivutio mbalimbali vya utalii kwa ajili ya kuchangia fursa hiyo ya watalii inayolipa duniani kote.

Monday, January 16, 2017

Watoto wawili waliokufa kwa kukosa hewa ndani ya gari waagwa

Wanafunzi wa Shule ya Msingi ya Mtakatifu Therese wakitoa heshima za mwisho mbele ya jeneza lenye mwili wa mwanafunzi mwenzao Maria Masala wakati wa ibada ya kuuaga mwili huo iliyofanyika Kanisa Katoliki la Mtakatifu Therese Ukonga Madafu Dar es Salaam jana.

MO Dewji akanusha kuzungumza kuhusu pesa za tetemeko la ardhi Kagera

Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
Mkurugenzi Mtendaji wa Makampuni ya Mohammed Enterprises Tanzania Limited (MeTL Group), Mohammed Dewji pichani chini, amekanusha taarifa ambazo zimesambaa katika mitandao mbalimbali ya kijamii kuwa amefanya mahojiano na kituo cha Redio cha Times FM kuhusu pesa zilizochangishwa katika Tetemeko la Ardhi la Kagera lililotokea mwezi Septemba, 2016. 

Dewji amesema hajafanya mahojiano na kituo chochote cha habari kuhusu tetemeko la Kagera na habari hiyo haina ukweli wowote zaidi ni mbinu ambayo imetumiwa na baadhi ya watu kwa ajili ya kuchafua jina lake na kampuni yake ya MeTL Group ambayo mpaka sasa ina wafanyakazi zaidi ya watu 28,000.

Aidha Dewji amesema ana imani na Serikali ya awamu ya tano na kuwatoa hofu Watanzania kuwa ataendelea kushirikiana na Serikali kusaidia jamii yenye uhitaji ikiwa ni sehemu ya ahadi yake ya kutumia nusu ya utajiri wake kusaidia watu wenye uhitaji.

“Nitumie nafasi hii kuwajulisha Watanzania wenzangu kuwa hii habari ambayo inasambazwa na watu katika mitandao ni ya uongo na haina ukweli wowote, sijafanya mazungumzo na media yoyote na mimi nilichangia pesa kwa nia nzuri, nina imani na Serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Rais Dk. John Magufuli kuwa inafanya kazi kwa faida ya watu wote bila kufanya ubaguzi,” amesema Dewji.

Katika ujumbe ambao unaonekana kusambaa katika mitandao mbalimbali ya kijamii ikiwepo Facebook, Instagram na WhatsApp imeandikwa kuwa MO Dewji amefanya mahojiano na Redio Times FM na kusema kama angejua mapema kuwa wahanga hawatopatiwa pesa hizo asingechangia

Mwandishi wa Habari za Michezo aliyefariki Zanzibar kuzikwa kwao Lushoto, Tanga

Mwandishi wa habari za Michezo wa Gazeti la Uhuru, Amina Athuman (pichani) amefariki Dunia jana asubuhi katika Hosptali ya Mnazi Mmoja mjini Zanziba alipokuwa amelazwa kwa matibabu.

Amina alilazwa Hospitalini hapo baada ya kuzidiwa (kushikwa na uchungu) kutokana na ujauzito na kukimbizwa kupata huduma katika hospitali hiyo ambpo alijifungua mtoto wa Kiume (Bahati mbaya) na yeye akaendelea kupatiwa matibabu hadi ulipomkuta umauti asubuhi ya leo.

Amina alikua mjini Zanziba kikazi alipokwenda kuripoti mashindano ya Kombe la Mapinduzi, ambapo alikuwa arejee jijini Dar es Salaam jana.

Kwa mujibu wa taarifa kutoka kwa familia, mwili wa marehemu utawasili leo jijini Dar es Salaam tayari kwa kuanza safari ya kuelekea wilayani Lushoto, mkoani Tanga kwa mazishi.

Mungu ilaze roho ya Marehemu Amina Athuman mahala pema peponi, Amina

LinkWithin

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...