Sasa kutumia mawakala kufanya kazi za kibenki
Yatarajia kusogeza huduma karibu na wananchi
Na Kambi Mbwana, Dar es Salaam
MAENDELEO ya kukua kwa sayansi na teknolojia yanasababisha
maisha kuwa rahisi zaidi, jambo ambalo linaleta tija kwenye jamii kwa namna
moja ama nyingine.
Mkurugenzi Mtendaji wa CRDB Bank, Dk. Charles Kimei, akizungumza na wageni waalikwa katika uzinduzi wa huduma yao mpya ya Fahari Huduma iliyozinduliwa mwishoni mwa wiki iliyopita.
Nchi nyingi duniani zinasonga mbele katika Ulimwengu huo wa
sayansi, hasa kutokana na kukaa chini katika kuhangaikia ubinifu wa kila aina,
kama sehemu ya kujiletea maendeleo.
Wasanii kutoka THT walipokuwa katika uzinduzi wa Fahari Huduma kutoka CRDB.
Hapa Tanzania, zipo Taasisi, Kampuni, Mashirika pamoja na
benki zinafanya bidii kubuni kwa ajili ya kwenda na wakati, kama sehemu ya
kupambana na changamoto mbalimbali.
Nasema hili baada ya kuhudhuria uzinduzi wa huduma mpya ya
benki ya CRDB, inayojulikana kama ‘Fahari Huduma’. Huduma hii inahusu uwekaji
pesa, kutuma na kupokea kwa njia ya wakala.
Yani leo badala ya kwenda kwenye matawi ya benki ya CRDB
kuweka pesa au kutoa, bila kusahau kulipa bili mbalimbali, mtu anakwenda kwa
wakala aliyekuwa karibu naye na kufanya huduma zote anazohitaji.
Haya ni maendeleo makubwa katika biashara za kibenki,
ukizingatia kuwa nazo zinakabiriwa na changamoto kubwa, ikiwapo masharti kwenye
biashara, au fedha zisizopungua Milioni 700 kwa kila tawi moja.
Katika mazungumzo yaliyofanyika mwishoni mwa wiki iliyopita,
Mkurugenzi Mtendaji wa benki ya CRDB, Dk. Charles Kimei, anasema kuwa ni ngumu
benki kuwa na matawi mengi, maana fedha zinazohitajika ni nyingi mno.
“Leo hii CRDB tunapohitaji kuweka tawi letu la kibenki
katika eneo lolote, tunahitaji kutenga fedha zisizopungua Milioni 700, kwa
kuweka vitu vyote vinavyohitajika katika biashara za kibenki.
“Hii ni sababu inayozifanya benki nyingi tukiwapo sisi CRDB
kutokuwa na matawi mengi, jambo ambalo linatufanya tukae chini na kubuni mbinu
nyingi za kuwafikia wateja wetu,” alisema Kimei.
Mkurugenzi huyo anasema kwa kulijua hilo, benki yao imekuwa
‘busy’ kutafuta nafasi ya kuwafikia wateja wao, ambapo wao ndio wa kwanza
kubuni huduma ya tawi linalotembea.
Tawi hili lipo ndani ya gari, ambapo hupita sehemu mbalimbali,
kwa ajili ya kuwafikishia wateja wao huduma za benki karibu, jambo ambalo kwa
kiasi Fulani lilipokelewa vizuri.
Kimei anasema kuwa pamoja na kubuni huduma hiyo, bado
wamezidi kuwaza kwa ajili ya kusogeza biashara zao na kufikia kuizindua Faharai
Huduma, ambapo sasa mawakala watafanya kazi zote zinazohusu mambo ya fedha
yanayofanywa katika benki zao nchi nzima.
“Kama wateja walilazimika kwenda kwenye tawi la benki yetu
kufanya muamala wa kifedha, kama vile kuangalia salio, kuweka fedha, kutoa,
kulipa bili za kampuni mbalimbali bila kusahau ada, sasa atafanya hayo kwa
kupitia wakala wetu ambao tunaamini watakuwa kila kona.
“Hii sasa inayafanya maisha yawe rahisi zaidi, ukizingatia
kuwa si lazima mtu aje kwenye benki zetu, kwakuwa watakachofuata huku hata mawakala
pia wamewezeshwa juu ya hilo,” alisema Kimei.
Mkurugenzi huyo anasema kuwa kikubwa watakachofanya ni
kuwapa elimu mawakala wote wakatakaopitishwa kutokana na vigezo vilivyowekwa,
huku wakisitiza uamini wa mawakala.
Anasema pia wapo kwenye mpango wa mawakala wote wanaofanya
kazi kwa Kampuni ya Vodacom, M-Pesa na Airtel Money kuingizwa katika biashara
hiyo, kama njia ya kuwapatia huduma bora wateja wao.
Kimei anasema Tanzania imekuwa na kiwango kidogo cha watu
wanaotumia huduma za kibenki, huku ikikadiriwa kuwa jumla ya watu wanaotumia
huduma hizo kuwa ni asilimia 12.
Kwasababu lengo lao ni kuwafikia Watanzania wengi zaidi,
hivyo wameaamua kuingiza huduma hiyo ya Fahari Huduma ambapo ilizinduliwa
katika Hoteli ya Kilimanjaro Kempinski.
Matawi 15 yanayotembea yamekuwa yakitoa huduma za benki ya
CRDB, pamoja na huduma ya benki kwa kupitia simu ya mkononi, (Sim banking),
ambayo inawawezesha wateja wao kufanya muamala kwa kupitia simu zao za
mikononi, moja ya huduma zenye ubora wa aina yake.
Mkurugenzi huyo anasema lengo la CRDB ni kutoa huduma nzuri
kwa ajili ya wateja wao, hivyo katika hili wanaamini kuwa Fahari Huduma itakuwa
mkombozi na chachu ya maendeleo ya Taifa.
Katika kuhakikisha kuwa huduma hizo zinafanikiwa kwa kiasi
kikubwa, CRDB wameazimia kutumia pia
baadhi ya ofisi za Shirika la Posta Tanzania (TPC), ambapo makubaliano hayo
yameshafanyika kwa ajili ya kuwasogezea wateja wao huduma zao.
CRDB wanasema kuwa mawakala wote watakaopitishwa kwa ajili
ya kutoa huduma hizo ni wale waaminifu na watakaohakikiwa kwa uangalifu wa aina
yake, ili kutimiza malengo, hasa kwa kufuata pia masharti yaliyowekwa na Benki
Kuu ya Tanzania juu ya huduma hiyo mpya.
“Kwa kuanzia, lazima mtu anayehitaji kuwa wakala wa CRDB awe
na biashara iliyodumu kwa miaka miwili pamoja na kuwa na mtaji wa kutosha kwa
ajili ya kutoa huduma ya miamala mbalimbali.
“Kwa upande wa wateja wa benki, kutegemeana na huduma
wanayotaka kutoka kwa wakala, anapaswa kwenda na kadi ya benki ya CRDB yenye kadi ya
TemboCardVisa, TemboCardMasterCard na TemboCardFahari,” alisema Kimei,
Mkurugenzi Mtendaji wa CRDB.
Anasema kuwa miamala yote inayofanyika kwa wakala ni salama,
maana mtu anapoweka au kutoa pesa anapata uthibitisho huo kwa njia ya meseji
kwenye simu ya mkononi pamoja na risiti.
Mara baada ya mpokeaji kupata uthibitisho wa kutumiwa fedha,
anaweza kuzichukua na kufanya matumizi yake kadri anavyoona inafaa, utaratibu
ambao utakuwa mkombozi kwa Taifa, huku huduma hiyo ikiwa ni kama ile
inayotolewa na wahasibu wa fedha (tellers).
Kimei anasema kwamba kwa kupitia huduma hiyo, mawakala wao
wataweza kutoa huduma ya kutoa pesa kwenye akaunti za wateja wa benki ya CRDB,
kutuma fedha kwa watu walio na wasiokuwa na akaunti za benki, kupokea pesa
zilizotumwa na wateja kwa kupitia mawakala wa FahariHuduma au kupitia
SimBanking.
Huduma nyingine ni pamoja na kupokea marejesho ya mikopo
mbalimbali ya benki ya CRDB, kulipia Ankara mbalimbali, kuhamisha fedha kwenda
kwenye akaunti nyingine ndai ya benki yao, kuangalia salio sambamba na kuchukua
kadi ya benki ya CRDB.
Mkurugenzi huyo anasema kuwa wanaamini huduma hiyo
kufanikiwa, wateja wote Tanzania wataishi maisha mazuri zaidi, maana popote
pale atakapokuwapo, atakuwa karibu na benki yake.
“Naomba wateja wetu waipokee huduma hii ya FahariHduma, huku
tukiamini kuwa watu wote wataiweka kichwani mwao huduma hii maana imekuja
kuwakomboa pia wafanyabiashara.
“Maisha yatazidi kuwa rahisi kutokana na huduma hii, hivyo
naamini CRDB, tutaendelea kuwa karibu na wananchi wote, ukizingatia kuwa sehemu
yoyote ya Tanzania tutakuwapo, kama vile wilayani na vijiji pia kama wakala
atajitokeza na kufanya biashara hiyo,” alisema.
Kufanyika kwa huduma hiyo, ni mwendelezo wa kutumia vyema
maendeleo ya sayansi na teknolojia, huku baadhi ya wilaya ambazo zimekuwa
zikikosa huduma za kibenki kuwa wananchi wao watanufaika kwa kiasi kikubwa na
huduma za FahariHuduma kutoka benki ya CRDB.
+255 712053949
+255 753806087
No comments:
Post a Comment