Na Kambi Mbwana, Dar es Salaam
BEKI wa Yanga, David Luhende ameongezwa kwenye kikosi
cha Taifa Stars kwa ajili ya mechi dhidi ya Uganda (The Cranes) kuwania tiketi
ya kucheza Fainali za Afrika kwa Wachezaji wa Ligi za Ndani (CHAN)
zitakazofanyika mwakani nchini Afrika Kusini.
Devid Luhende kulia akiwajibika uwanjani katika mechi za Ligi Kuu. Sasa ameitwa katika kikosi cha timu ya Taifa, Taifa Stars.
Kocha Kim Poulsen amesema kutokana na uamuzi huo wa
kumuongeza beki huyo wa kushoto amemuondoa mchezaji mmoja kwenye kikosi chake.
Mchezaji huyo ni mshambuliaji Zahoro Pazi wa JKT Ruvu.
Taifa Stars inayodhaminiwa na Kilimanjaro Premium
Lager sasa itaingia kambini kwenye hoteli ya Tansoma jijini Dar es Salaam,
Julai 3 mwaka huu badala ya Julai 4 mwaka huu kama ilivyokuwa imepangwa awali.
Mechi ya Uganda itachezwa Julai 13 mwaka huu, saa 9
kamili alasiri kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam wakati ile ya marudiano
itachezwa wiki mbili baadaye jijini Kampala, Uganda.
Wachezaji wanaotakiwa kambini ni Aggrey Morris (Azam),
Aishi Manula (Azam), Ally Mustafa (Yanga), Amri Kiemba (Simba), Athuman Idd
(Yanga), Frank Domayo (Yanga), Haruni Chanongo (Simba), John Bocco (Azam), Juma
Kaseja (Simba), Juma Liuzio (Mtibwa Sugar) na Kelvin Yondani (Yanga).
Wengine ni Khamis Mcha (Azam), Mrisho Ngasa (Simba),
Mudathiri Yahya (Azam), Mwadini Ali (Azam), Mwinyi Kazimoto (Simba), Nadir
Haroub (Yanga), Salum Abubakar (Azam), Shomari Kapombe (Simba), Simon Msuva
(Yanga) na Vincent Barnabas (Mtibwa Sugar).
No comments:
Post a Comment