Na Kambi Mbwana, Dar es Salaam
KLABU ya Soka ya Simba, jana ilimkabidhi kocha wao wa zamani
Patrick Liewig jumla ya Dola 10,000, kwa ajili ya deni lake analoidai timu
hiyo, huku akitakiwa kutulia hadi mwezi Octoba kumaliziwa kiasi kilichobaki.
Kocha wa zamani wa Simba, Patrick Liewing
Liewing aliyekuwa kocha wa Simba, aliwasili nchini kwa ajili
ya kudai fedha zake Dola 16,000 ndani ya klabu hiyo, hivyo kulazimika kukaa na
viongozi wake wa zamani kwa ajili ya kulimaliza sakata hilo la deni lake.
Akizungumza jana jijini Dar es Salaam, Makamu Mwenyekiti wa
Simba, Joseph Itang’are, maarufu kama mzee Kinesi alisema wamemlipa Liewing kiasi
hicho cha fedha.
Alisema uamuzi huo umeafikiwa na pande zote mbili, hivyo
wanaamini kocha huyo wa zamani ataridhia na kurudi kwao ama kufanya analohitaji,
ukizingatia kuwa tayari wameshamlipa kisheria baada ya mazungumzo yao kufikia
pazuri.
“Mapema wiki hii tulizungumza naye na kumtaka atulie ili
tumuandalie fedha zake anazodai, ambapo tumefanikiwa kwa kiasi kikubwa na
kumtaka pesa zilizosalia, dola 6000 azipate mwezi 10 mwaka huu.
“Tunashukuru uamuzi huu ameukubali na tayari ameshasaini juu
ya uchukuaji huo wa dola 10,000, hivyo tuna amini kwa sasa hakutakuwa na tatizo
lolote kati ya Simba na Liewing, aliyekuwa kocha wetu hadi pale ligi ilipofikia
tamati,” alisema.
Kocha huyo amekomba pesa zisizopungua 16,450,000 kutoka kwa
mabosi wake hao, na kutuliza mzuka kutokana na moto aliokuja nao Tanzania,
akigoma kurudi kwao hadi alipwe fedha zake.
No comments:
Post a Comment