Na Kambi Mbwana, Dar es Salaam
KOZI ya makocha wa ngazi ya pili (Intermediate)
inayosimamiwa na Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Dar es Salaam (DRFA),
inatarajiwa kufungwa Jumanne ijayo baada ya kudumu kwa wiki nne.
Kocha
mkuu wa Twiga Stars, Rogasian Kaijage akitoa somo kwa makocha wanashiriki kozi
ya ukocha ngazi ya pili ndani ya darasa kwenye Ukumbi wa Harbours Club,
Kurasini.
Kozi hiyo ilianza Juni 3 mwaka huu kwenye Ukumbi wa
Harbours Club, uliopo Kurasini chini ya Mkufunzi Rogasin Kaijage, ambaye ni
Kocha wa timu ya Taifa ya Wanawake ‘Twiga Stars’ ambapo makocha mbalimbali
pamoja na wachezaji wa zamani wamejitokeza kushiriki.
Ofisa Habari wa DRFA, Mohamed Mharizo alisema kozi
hiyo imekuwa na mafanikio na wanatarajia makocha walioshiriki katika kozi hiyo
watakuwa na mchango mkubwa katika kuendeleza mpira wa miguu katika mkoa wa Dar
es Salaan na Taifa kwa ujumla.
“Hadi sasa tunashukuru kuona tunafanikisha kozi hii
ambayo wengi wameitikia wito, mwisho wa kozi hii ndio mwanzo wa kozi nyingine.
“Lakini haya ya kozi ya makocha ni moja ya majukumu
ya Kamati ya Ufundi ya DRFA yaliyoainishwa katika Katiba, hivyo hili ni moja ya
shabaha yetu na mengine mengi mazuri yanafuata,” alisema Mharizo.
Kozi hiyo ni ya kwanza kuendeshwa na DRFA tangu
kuingia madarakani kwa uongozi mpya wa chama hicho Desemba 12, chini ya
Mwenyekiti wake Almas Kassongo.
No comments:
Post a Comment