https://tpc.googlesyndication.com/simgad/8045142562622600543


Recent Post

Monday, November 30, 2015

Rais Dr John Magufuli, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa wamtembelea Makamu wa Rais ofisini kwake leo

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli, (kushoto) akizungumza na Makamu wake, Mhe. Samia Suluhu Hassan (katikati) na Waziri Mkuu, Majaliwa Kassim Majaliwa, wakati Rais na Waziri Mkuu walipomtembelea Makamu Ofisini kwake Ikulu jijini Dar es Salaam, leo Nov 30, 2015 kwa mazungumzo. Picha zote kwa hisani ya OMR
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli (kushoto) akiagana na  Makamu wake, Mhe. Samia Suluhu Hassan (katikati) na Waziri Mkuu, Majaliwa Kassim Majaliwa (kulia) baada ya mazungumzo yao yaliyofanyika Ofisini kwa Makamu wa Rais Ikulu jijini Dar es Salaam, leo Nov 30, 2015. Wa pili (kulia) ni Naibu Katibu wa Makamu wa Rais, Mohamed Khamis.

Mchumi na Mwenyekiti wa zamani wa Chama Cha Wananchi CUF amtembelea Rais Magufuli, ampa tano kuukwaa urais

Mwenyekiti wa zamani wa wa Chama Cha Wananchi (CUF) Prof Ibrahim Lipumba amemtembelea Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Dkt John Pombe Magufuli na kumpongeza kwa Hotuba nzuri. Pia Prof Lipumba amesifu na kuunga mkono Juhudi za Mhe Rais katika kupambana na wakwepa kodi na wahujumu uchumi.

Kasi ya RC Makalla yautikisa Mkoa wa Kilimanjaro, afanya ziara za kushtukiza

Na Mwandishi Wetu, Moshi
MKUU wa Mkoa Kilimanjaro, Amos Makalla, amefanya ziara ya kushtukiza katika masoko manne ya Manispaa ya Moshi pamoja na dampo za kukusanyia uchafu, ili kujionea hali ya usafi na utendaji kazi katika mkoa huo. Katika ziara hiyo, RC Makalla alitumia muda huo kuwaagiza watendaji wake, hususan katika mchakato mzima wa kuifanya Moshi iwe kwenye usafi.
Mkuu wa Mkoa Kilimanjaro, Amos Makalla mwenye miwani, akikagua soko lililopo kwenye Manispaa ya Moshi, mkoani humo, baada ya kufanya ziara ya kushtukiza kujionea hali ya usafi katika maeneo mbalimbali ya mkoa huo.
Akizungumzia ziara yake hiyo, Makalla alitoa siku tatu kwa watendaji wa Manispaa ya Moshi kuhakikisha kwamba lundo la takataka katika soko la Kwasadala linaondoshwa haraka iwezekanavyo. Alisema hawezi kukubali kuona Manispaa hiyo inashuka kiwango chake cha kuifanya Moshi inaendelea kuheshimika katika suala zima la usafi.

Sunday, November 29, 2015

Watanzania waaswa kuwasomesha watoto wao kwenye vyuo vya ufundi

WATANZANIA wametakiwa kuwapelewa watoto wao katika vyuo mbalimbali vya ufundi stadi elimu inayo zalisha ajira nyingi kuliko vyuo vikuu hapa nchini ili kuepukana na tatizo la ajira. Inadaiwa kuwa watu wanaojiajiri ni wengi wanao toka katika vyuo vya ufundi kuliko wanano maliza vyuo vikuu kutokana na wanao toka vyuo vikuu wanategenea kuajiliwa huku wa vyuo vya ufundi wakijikita kujitengenezea ajira na kuachana na utegemezi kutoka kwa wazazi.

Kauli hiyo imetolewa na mwenyekiti wa bodi ya vyuo vya Veta kamda ya nyanda za juu inayo jumuisha mikoa ya Iringa, Ruvuma na Njombe, Kabaka Ndenda, juzi katika mahafari ya kwanza kwenye chuo pekee ya wilaya cha Veta Makete, alisema kuwa  vijana wengi wanao maliza katika vyuo vya ufundi wanauhakika wa kujiajiri kuliko wanao enda vyuo vikuu.
Alisema kuwa wananchi wamekuwa wakiona ni bora kumpeleka mtoto wake katika chuo kikuu kuliko kumpeleka katika vyuo vya ufundi, alisema kuwa Tanzania kutokana na ulivyo mfumo wa ajira watoto ni bora wakapelekwa katika vyuo vya ufundi ili kutengeneza ajira.

Mohamed Dewiji MO anyakua tuzo nyingine Afrika Kusini


IMG_3351
Mfanyabiashara maarufu ambaye pia ni Afisa Mtendaji Mkuu wa Makampuni ya MeTL Group, Mohammed Dewji akitembea kwenye 'Red Carpet' mara baada ya kuwasili katika hotel ya Hilton Sandton jijini Johannesburg, Afrika Kusini kwenye hafla ya utoaji tuzo iliyoandaliwa na jarida maarufu la Forbes na kutunukiwa tuzo ya "Forbes Africa Person Of the Year 2015".Story na picha zote kwa hisani ya Zainul Mzige.

MFANYABIASHARA na  mtu mwenye taasisi ya kusaidia jamii, Mohammed Dewji maarufu kama Mo ametunukiwa tuzo ya jarida maarufu la Forbes ya  "Forbes Africa Person Of the Year 2015" katika hafla iliyofanyika Novemba 27 mwaka huu jijini Johannesburg, Afrika Kusini. Mfanyabiashara huyo pia ni Afisa Mtendaji Mkuu wa Makampuni ya Mohammed Enterprises T Ltd (MeTL Group) kampuni iliyoanzishwa na na baba yake katika miaka ya 1970 ambayo sasa imekua na kujikita katika viwanda vya nguo, usagaji nafaka, utengenezaji wa vinywaji baridi, usindikaji wa mafuta ya kula, usindikaji wa chai  na kuendesha mashamba ya mkonge ambapo tayari anashea ya asilimia 40 ya soko.

Mo ametwaa tuzo hiyo kwa kuwashinda watu watano mashuhuri barani Afrika. Watu hao ni Nkosazana Dlamini Zuma, mke wa Kwanza wa Rais wa Afrika Kusini, Jacob Zuma. Mama huyo kwa sasa ndiye Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika (AU). Mwingine ni Rais wa sasa wa Nigeria, Muhammadu Buhari aliyetambuliwa kutokana na kuanzisha vita dhidi ya rushwa nchini mwake. Aidha wapo Arumna Otei, mchumi mahiri raia wa Nigeria ambaye kwa sasa ni Makamu wa Rais wa Benki ya Dunia. Pia alikuwemo Mwandishi maarufu wa vitabu wa Nigeria, Chimanda Ngozi Adichie ambaye moja ya vitabu vyake vinaelezea picha halisi ya Afrika inavyofikiriwa duniani.

LADHA ZA WASANII WETU: Mwana wa Kitwana, wimbo wa kimahaba kutoka kwao Jagwa Music

Na Kambi Mbwana, Dar es Salaam
Muziki aina ya mnanda ni kati ya aina ya muziki uonekanao ni wa kihuni.  Ingawa upo muziki wa Bongo Fleva ambao nao unaitwa wa kihuni miaka ya 2005 kushuka chini, ila huu wa mnanda umezidi. Na kuonekana kwake ni muziki wa kihuni unatokana na aina ya mashabiki wake na jinsi wanavyojiweka. Muziki wa mnanda una nguvu sana. Unapopigwa mtaani, basi unaweza kukuta mashabiki wake wametoka Bagamoyo na maeneo mengine ya mbali kabisa. Na idadi kubwa ya watu hao ni wale wanaojihusisha na vitendo vya uhuni. Kwa mfano, ni rahisi kuona mtu anakwenda kuangalia muziki huo mtaa Fulani huku akiwa na burungutu la bange au dawa nyingine za kulevya.
Na wadau hao hutumia hadharani. Kwa wanaofuatilia muziki huu watakubaliana na mimi, hususan katika ngome za muziki huu kama vile Tandale, Mwananyamala, Kigogo, Mbagala na kwingineko unapopita mara kwa mara wanapoalikwa vijana hawa. Binafsi ni aina ya muziki niupendao sana. Naupenda mno muziki wa mnanda. Na kuupenda kwangu kumetokana na jinsi ya uimbaji wao. Wasanii wanaoimba muziki wa mnanda wa asili ni wenye vipaji kupita kiasi. Aidha licha ya kufanya kazi zao katika wakati mgumu hususan uhaba wa vyombo vya muziki, lakini nyimbo zao huwa nzuri sana.
Huyu ni mmoja wa wapiga vyombo wa muziki aina ya mnanda. Anaonekana anapiga kisturi.

Unaweza kushangaa kwenye shughuli wanakuja na spika ndogo, kinanda kidogo na hutegemea kuazima meza, kisturi au vinginevyo ili kupiga na kuchanganyia muziki wao. Katika video ya wimbo uitwao Mwana wa Kitwana kutoka kwa kundi la Jagwa Music watakubaliana na mimi. Ni wimbo mzuri na video iliyochangamka sana. Katika video hiyo marehemu Sharo Milionea amecheza kama Mwana wa Kitwana ambaye ni masikini, lakini anampenda msichana mzuri aitwae Jokate Mwigelo. Na Jokate pia anapendwa na Yusuf Mlela, anayeonyesha kuwa anajimudu kiuchumi.

Jamaa hawa wanavutana sana, lakini mwisho wa siku Sharo milionea anaonekana kushinda vita hii, kwa sababu msichana mwenyewe anampenda. Mashairi yanasisimua, hasa pale msanii anaposema “umenifanya niwe jasiri mbele yao sasa mimi ni jabali”. Kuna sehemu pia anasema, “umeonyesha huwa mind na tena hauna mpango nao”.  Pia mwanzo alionyesha hofu kidogo pale alisema kwamba mwanzo wa mapenzi yao waliamua kufanya iwe siri, hii ni kwa sababu mapenzi yao yalizunguukwa na vikwazo vingi, hususan ugumu wa maisha. Jagwa wanasema, “Moja ya vikwazo choka mbaya na hali duni niliyokuwa nayo mimi ohoo”. Baada ya kulalamika sana, akilalamikia upendo wake na ugumu wake wa maisha, anaingiza maneno matamu yenye kutia moyo kwamba hatokatishwa tamaa, bali atakaza uzi mpaka awe pamoja na mrembo huyo.

Ni mashairi mazuri ya ushindi. Mtu anapokuwa anafuatilia msichana mzuri, lazima kuwe na changamoto kadhaa. Hii ni kwa sababu vizuri vinapendwa na wengi.  Omba sana Mungu. Pia jaribu kuchunguza, unayempenda ana ndoto na wewe? Katika kuchunguza upendo wako, usiangalie hali yako ya mfukoni, ila angalia thamani ya moyo wako. Katika kusikiliza wimbo huu, najifunza mengi sana. Lakini pia nafarijika mno. Je, umewahi kupata muda wa kuhudhuria shoo za muziki wa aina ya mnanda? Mimi nimewahi, ni muziki mzuri mno unaovutia kusikiliza hata kuangalia wanavyocheza wahusika. Mnanda bwana, hata ukiruka ruka kachura umekwenda na biti. Ukichuchumaa na kulia, inapenda zaidi.

Saturday, November 28, 2015

RC Kilimanjaro apiga stop likizo za Ma DC, wakurugenzi na wakuu wa idara

Na Mwandishi Wetu, Kilimanjaro
KATIKA hali inayoonyesha ni joto kali la kuwatumikia Watanzania, Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Amos Makalla, amepiga marufuku likizo za Wakuu wa wilaya, Wakurugenzi na Wakuu wa Idara kwenye mkoa wake ili kutekeleza kwa vitendo hotuba na maagizo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dr John Pombe Magufuli.

RC Makalla aliyasema hayo jana katika kikao cha kazi na wakuu wa wilaya, wakurugenzi wa halmashauri, wakuu wa idara wa halmashauri na Kamati ya Ulinzi na usalama ya mkoa huo kwa ajili ya kupeana mikakati ya majukumu ya kuwatumikia Wana Kilimanjaro na Watanzania kwa ujumla, ikiwa ni hatua nzuri ya kwenda na kasi ya Dr Magufuli.

Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Amos Makalla, akizungumza na Wakuu wa Wilaya, Wakurugenzi na Wakuu wa Idara katika Mkoa huo ili kujipanga katika majukumu mbalimbali ya kuwatumikia wana Kilimanjaro na Watanzania kwa ujumla. Picha na Mpiga Picha Wetu.
Baadhi ya watendaji wa Mkoa Kilimanjaro wakimsikiliza kwa makini Mkuu wa Mkoa huo, Aamos Makalla alipozungumza nao jana. Katika kikao hicho, RC Makalla alipiga marufuku likizo kwa Wakuu wa Wilaya, Wakurugenzi na Wakuu wa Idara ili kujipanga na maagizo yaliyotolewa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dr John Pombe Magufuli.

Alisema kuwa Dr Magufuli ameagiza mambo mengi mazuri na yenye kuhitaji utendaji uliotukuka, ikiwamo elimu bure, mikakati ya kubana matumizi, kupambana na maradhi mbalimbali, ugonjwa wa kipindupindu, usimamizi wa pembejeo na kuzuia pia matukio mbalimbali yenye kugharimu pesa, sanjari na mapambano ya dawa za kulevya na uwadijibikaji kazini.

“Hakuna muda wa kupoteza katika kufanyia kazi maagizo ya rais Magufuli, hivyo sote kwa pamoja tunapaswa kujipanga na kwenda na kasi ya serikali yetu ili kuhakikisha kwamba nchi yetu inapiga hatua kubwa kama yalivyokuwa makusudio yetu ya kuhakikisha watoto wanasoma bure, hivyo sitaki kusikia likizo kutoka kwa Ma DC, Wakurugenzi na Wakuu wa Idara katika Mkoa wetu wa Kilimanjaro. “Suala la kubana matumizi, pembejeo kwa wakulima, vita ya madawa ya kulevya na mengineyo yanapaswa kuanza sasa, huku tukihakikisha kwamba maadhimisho ya siku ya Uhuru yanajikita zaidi kwenye suala zima la usafi kuanzia kaya, mtaa au kijiji  na kwingineko,” Alisema Makalla.

Friday, November 27, 2015

Mwili wa marehemu Alphonce Mawazo kuagwa kesho kwenye uwanja wa Furahisha jijini Mwanza

Mkutano wa Naibu Katibu Mkuu Chadema Salum Mwalimu na Wanahabari Jijini Mwanza hii leo.
Na:Binagi Media Group
Mwili wa aliekuwa Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo Chadema Mkoa wa Geita Marehemu Alphonce Mawazo, kesho unatarajiwa kuagwa Jijini Mwanza kabla ya kusafirisha kwenda Mkoani humo kwa ajili ya Mazishi.

Kaimu Katibu Mkuu wa Chadema Salum Mwalimu, amesema Marehemu Mawazo ataagwa Kitaifa kwa taratibu za chama hicho, katika uwanja wa Furahisha Jijini Mwanza.

Amesema ratiba hiyo itatanguliwa na ratiba ya kifamilia ya kuuaga mwili huo, ambayo itafanyika asubuhi Nyegezi Jijini Mwanza ambako ni nyumbani kwa Mchungaji Charles Lugiko ambae ni baba mdogo wa Marehemu Mawazo hiyo ikiwa ni baada ya mwili wake kutolewa katika Hospitali ya Rufaa Bugando ulikohifadhiwa.

BREAKING NEWS: Rais Magufuli amsimamisha kazi Kamishna wa Mamlaka ya Mapato Tanzania TRA Rished Bade na kumteua Philliph Mpango kukaimu nafasi yake

MOTO umeendelea kuwaka katika serikali ya awamu ya tano, baada ya rais Dkt. John Pombe Magufuli kumsimamisha kazi Kamishna wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Rished Bade na kumteua Philiph Mpango kukaimu nafasi yake. 

Turudie uchaguzi Zanzibar ili wananchi wampate wanayemhitaji, iwe ni Dk Shein au Seif

ILI uwe rais unahitaji kuwa na wananchi. Wananchi ndio kila kitu. Hawa ndio wanaopaswa kupiga kura ili wakuchaguwe wewe kwa ajili ya kuwaongoza. Na inafahamika kwamba uongozi ni kuonyesha njia. Ikiwa uamuzi wao ni wewe kuwa rais wao, watafanya hivyo. Ikitokea upande mmoja hautaki, basi demokrasia ikifuatwa, watamchagua yule yule wampendaye. Kama hivi ndivyo, kwanini Zanzibar isirudie Uchaguzi wao baada ya ule wa awali kufutwa kutokana na matatizo kadha wa kadha? Wafuasi wa CCM wanaamini Dk Ali Mohamed Shein angeshinda kama sharia zingefuatwa. Maalim Seif Sharrif Hamad naye anasema alikuwa mshindi na ndio maana akajitangaza kama rais mpya wa Zanzibar anayesubiri kuapishwa tu.
Rais wa Zanzibar Dk Ali Mohamed Shein kushoto, akisalimiana na Maalim Seif Shariff Hamad, katika matukio yaliyowakutanisha mara kadhaa nchini Tanzania.
Kwa nini alitangaza? Si kwa sababu aliamini Wazanzibar wanamuhitaji? Kama wanamuhitaji, hapana shaka watamchagua tena hata uchaguzi ukifanyika usiku wa maneno. Sitaki kuamini kuwa kurudia kwa uchaguzi kutamfanya Seif ashindwe wakati anaamini alishinda kwa kura nyingi. Na siwezi kuamini kwamba Shein aliyeshindwa katika uchaguzi huo uliyofutwa atashinda, wakati wananchi ni wale wale. Kurudia kwa uchaguzi, mshindi atakuwa yule anayependwa na kuhitajiwa na Wazanzibar wenyewe.
Hivyo basi, bila kujali vyama vyetu, dini zetu, koo zetu au elimu zetu. Shime Wazanzibar na Watanzania wote kwa ujumla tunapaswa kuafikiana na kurudia uchaguzi huo ili wapiga kura waamue wenyewe, kidemokrasia tu. Hakuna mbora kati ya Shein na Seif. Mbora ni Mzanzibar mwenyewe. Kamwe tusisikilize maneno ya waropokaji. Tujali zaidi udugu wetu, uhusiano wetu na nchi yetu. Turudie uchaguzi huu kwa Amani. Aliyechaguliwa na Mungu kuwa kiongozi wetu atakuwa tu, hakuna wa kumzuia. Wewe kama ni mfuasi wa CUF, kipende zaidi chama chako, ila mwisho wa siku jenga uzalendo pia kwa nchi yako. Na ikiwa ni Mwana CCM, unapaswa kujua bila nchi hakuna chama chako cha siasa. Hivi kwa mfano tukianza kugombana, kutoana roho, hao tunaowapigania watamuongoza nani? Na je, wote tunaweza vita? Wote tunaweza kupaa angani kujihifadhi katika nchi za wenzetu kama watakavyofanya wanasiasa tunaotaka kuwapigania?

Makontena 349 yenye thamani ya zaidi ya sh bilioni 80 yapotea bandarini, serikali yaamuru kukamatwa kwa maofisa kadhaa wa bandari, yazuia hati zao za kusafiria

Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
TAHARUKI imetokea Bandarini baada ya kugundulika kuwa makontena 349 yamepotea na kuisababishia hasara serikali kwa zaidi ya Sh Bilioni 80. Waziri Mkuu Mh Kassim Majaliwa pichani, leo ameamuru kukamatwa kwa maafisa kadhaa wa Mamlaka ya Mapato (TRA) na wengine kufukuzwa kazi kutokana na kufanya ziara ya kushtukiza Bandarini na kukuta uozo huo ulioitia hasara serikali na aibu kubwa.
Maafisa hao wametakiwa kusalimisha hati zao za kusafiria ikiwa ni kitendo cha kibaya cha kutoweka kwa makontena bayo ambayo data za Mamlaka ya Bandari inazo lakini katika mtandao wa TRA hayaonekani.

Mwenyekiti wa CCM Taifa, Ndugu Jakaya Mrisho Kikwete akiendelea na shughuli za kuijenga CCM

Mwenyekiti wa CCM Dkt Jakaya Mrisho Kikwete akizungumza na Katibu Wa Halmashauri Kuu Itikadi na Uenezi, Ndugu Nape Nnauye na Katibu wa Halmashauri Kuu Oganaizesheni Ndg Mohamed Seif Hatibu katika ofisi yake Makao Makuu ya CCM, ofisi ndogo ya Lumumba jijini Dar es salaam, jana 26th Nov 2015.
Mwenyekiti wa CCM Dkt Jakaya Mrisho Kikwete akizungumza na Mwanasheria wa CCM Ndg Godwin Kunambi nje ya Ofisi ndogo ya Makao Makuu ya CCM Lumumba Jijini Dar es salaam, jana Novemba 26, 2015.

Ratiba ya kuagwa na maziko ya marehemu Alphonce Mawazo wa Chadema hii hapa, Lowassa, Sumaye na Mbowe kuongoza maombolezo

Ratiba ya shughuli ya utoaji heshima za mwisho na mazishi ya Kamanda Mawazo
Leo Siku ya Ijumaa, Novemba 27 saa 2 asubuhi, mwili wa Mpiganaji na Kiongozi wetu Alphonce Mawazo utachukuliwa Hospitali ya Bugando kuelekea nyumbani kwa Baba yake mdogo, eneo la Nyegezi-Swea kwa ajili heshima za familia kabla ya kuelekea Viwanja vya Furahisha ambapo Viongozi waandamizi wa UKAWA, wakiongozwa wa Mwenyekiti wa CHADEMA Taifa, Freeman Mbowe, Mgombea Urais Edward Lowassa, Waziri Mkuu Mstaafu Fredrick Sumaye, wabunge wa UKAWA, wataongoza maelfu ya wakazi wa Jiji la Mwanza na vitongoji vyake kutoa heshima za mwisho kwa mpendwa wao Mawazo.
Baada ya Viwanja vya Furahisha, mwili wa Mpiganaji Mawazo utasafirishwa kuelekea Geita kwa ajili ya kuwapatia nafasi wakazi wa Mkoa wa Geita kumuaga Kiongozi wao siku ya Jumamosi, Novemba 28 kuanzia asubuhi mapema ambapo baadae mchana mwili huo utapelekwa Mji Mdogo wa Katoro, mkoani Geita, ambapo pia wananchi watapata fursa ya kumpatia heshima za mwisho na kumuaga Mawazo ambaye alikuwa ni Mgombea wao wa Ubunge wa Jimbo la Busanda.
Baada ya wakazi wa Katoro kushiriki tukio hilo, mwili wa Kamanda Mawazo utapelekwa nyumbani kwao kijijini Chikobe tayari kumhifadhi kwenye nyumba ya milele shambani kwake, siku a Jumapili, Novemba 29, baada ya familia, ndugu, jamaa na wakazi wa kijiji hicho kutoa heshima zao za mwisho.
Tumaini Makene
Msemaji Mkuu Chadema

Thursday, November 26, 2015

Uzinduzi wa siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia zazinduliwa mkoani Kilimanjaro

Brass Band ya Chuo cha Polisi Moshi ikiongoza maandamano ya uzinduzi wa kampeni ya siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia kanda ya kaskazini .

MGODI UNAOTEMBEA: Ardhi ni mali, Magufuli aungwe mkono kwa vitendo

Na Kambi Mbwana, Dar es Salaam
NI Dr John Pombe Magufuli tu, rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Kila kona anatajwa yeye. Kwenye usafiri wa umma, daladala na mabasi anatajwa yeye. Kwenye maeneo ya huduma za kijamii kama vile hospitali, shuleni na kila kona anazungumziwa yeye. Hii inaonyesha ni dalili njema za kukubalika kwa mwanasiasa huyo ambaye hivi karibuni alitangazwa kuwa rais wa Tanzania. Kutajwa kwa Magufuli kumetokana na kuanza vema katika ngwe yake ya uongozi, akifanyia kazi kwa vitendo yale aliyozungumzia kwenye kampeni zake, akiwa mgombea urais wa Tanzania, kwa kofia ya Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dr John Pombe Magufuli, pichani.
Siku chache tangu alipoingia madarakani, Magufuli amepiga marufuku safari za nje ya nchi kwa viongozi wa serikali ili serikali yake kuokoa mabilioni ya shilingi yaliyokuwa yanatumika katika kugharamia safari. Mbali na hilo la safari, pia amezuia sherehe za Siku ya Uhuru, 9 Desemba, akiamini kuwa ni njia ya kuokoa pesa. Awali Magufuli alitangulia pia kuzuia pesa za wabunge zilizotengwa kwa ajili ya sherehe yao. Jambo hili na mengine linatia moyo mno. Angalau sasa watu wanaweza kupata picha ya namna gani Dr Magufuli ataiongoza nchi hii kwa mafanikio makubwa. Ni kutokana na hilo, naamini Dr Magufuli anastahili pongezi naa kuungwa mkono pia kwa aliyozungumza na hata yale asiyozungumzia pia. Kwa mfano, asilimia kubwa ya Watanzania wanaishi vijijini.

Na watu wa vijijini wanaishi kwa kutegemea kilimo. Kama hivyo ndivyo, kazi ya kilimo haiwezi kukamilika kama hakuna ardhi ya kutosha. Maeneo mengi ya nchi, hususan vijijini kumekuwa na shida kubwa ya ardhi.Vigogo na wafanyabishara wamekuwa wakigawana ardhi kubwa, jambo linalowafanya wananchi masikini wakose maeneo ya kulima. Hili halikubaliki. Serikali ya Magufuli ilifanyie kazi suala hili kwa vitendo. Ndio alionyesha kulipinga wakati wa kampeni zake, ila kwakuwa ameshafanikiwa kuwa rais, ni wakati wa kulitatua. Utumike utaratibu mzuri wa kuipima ardhi na kufanya utafiti ni kwa kiasi gani ardhi imeporwa na watu wasiokuwa na nia njema kwa walalahoi. Tunajua si wote wameipora, ila pia wapo waliofanya hivyo. Tuwajue wanaomiliki ardhi kihalali na wale waliojimilikisha wenyewe.

Wapo watu wanaomiliki heka zaidi ya 120 na bado wanaingia kwenye vieneo vya walalahoi. Kesi nyingi za ardhi zinazoendeshwa vijijini zinaishia kwa masikini kuonekana wana makosa. Hili linasikitisha. Namna gani Dr Magufuli ataungwa mkono? Nadhani ili suala hilo lifanyiwe kazi kwa vitendo, ni wakati wa Wakuu wa Mikoa kujipanga kikamilifu. Kila Mkuu wa Mkoa asimamie kuundwa kwa Kamati ya Ardhi katika wilaya husika. Kamati ya Ardhi iwe na wajumbe mchanganyiko, akiwamo Mkuu wa wilaya na Mkurugenzi. Kamati hii na Mwenyekiti, Katibu na wajumbe wake kadhaa. Kamati hii iwe na mamlaka ya kutembelea katika maeneo mbalimbali ya wilaya husika kuchunguza, kusikiliza kero za ardhi. Kamati hii pia iwe na mamlaka ya kutatua kero ndogo ndogo. Baada ya kukamilisha utendaji kazi wake, Kamati hii itawasilisha kwenye Kamati ya Ardhi ya Mkoa, ambayo hapana shaka Mwenyekiti wake anaweza kuwa Mkuu wa Mkoa husika, ambapo baadaye itawasilisha mezani kwa Waziri Mkuu na Mheshimiwa Rais. Utaratibu huu utumike katika kila wilaya na Mkoa.

Wednesday, November 25, 2015

Tamasha la NSSF Handeni Kwetu 2015 halitafanyika

TANGAZO
Tamasha la Utamaduni la NSSF Handeni Kwetu limefanyika Handeni Mjini mara mbili mfululizo, mwaka 2013 na 2014. Tamasha hili limefanyika kwa mafanikio makubwa. Limeendelea kupokea wageni na vikundi mbalimbali hata nje ya wilaya ya Handeni. Mipango iliyokuwapo ni kulifanya tamasha liwe na mvuto kwa kuhakikisha kwamba linaandaliwa vizuri zaidi. Mwaka huu mwanzoni tulipokea maoni kutoka Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA), wakisema kulingana na hadhi ya tamasha la NSSF Handeni Kwetu, kibali chake kinapaswa kutoka BASATA na si Halmashauri tena. BASATA walisema hivi kama taratibu za matamasha makubwa yanavyofanyika.

Hili limetupa moyo mkubwa. Mwanzo tuliamini hatutaweza, ila tumeweza. Wakati sisi tunaona ni tamasha dogo, kumbe wadau wakubwa wa sanaa wanajua ni tamasha kubwa. Bahati iliyoje? Vyuo mbalimbali vya sanaa vimekuwa vikifundisha wanafunzi wao kwa kupitia tamasha la NSSF Handeni Kwetu, hususan lile la mwaka 2013. Ni kutokana na kiu ya kulifanya tamasha hili liwe na mvuto mkubwa zaidi, mwaka huu halitafanyika. Hii ni kwa sababu mwaka huu ulijawa na matukio mengi makubwa, ukiwamo Uchaguzi Mkuu.
Si kwetu tu, ila kwa wadau mbalimbali. Kutofanyika kwa tamasha hili si kigezo cha kusema NSSF Handeni limekufa. Yapo matamasha mengine ambayo mwaka huu hayajafanyika. 


Naomba hii iwe taarifa rasmi kuwa tamasha hili kwa mwaka huu halitafanyika, ila kutofanyika kwake mwaka huu ni sehemu ya maandalizi ya mwaka 2016. Maandalizi yake yatakuwa bab kubwa mno. Tutakuwa tunaambizana hatua kwa hatua. Tamasha la mwakani litakuwa na matukio tofauti tofauti. Kilele cha tamasha hili kitashangaza wengi. Tunatamani tamasha la mwakani liwe kubwa zaidi, ukizingatia kuwa kupata kibali cha BASATA, ndio kusema wataalamu wao watakuwa bega kwa bega na sisi. Tunatamani pia NSSF Handeni Kwetu iwe zaidi ya siku moja. Tunatamani pia tamasha hili lizidi kupokea wageni kutoka nje ya Tanzania ili kuchochea maendeleo. Tunafanyia kazi changamoto mbalimbali zilizojitokeza, ikiwamo sapoti kutoka kwa wadau mbalimbali. Tunatamani tamasha lijalo liwe la utamaduni na biashara pia. 

Kwa walioathiriwa na kutofanyika kwa tamasha hili msimu huu wa 2015 tunatoa pole. Tunawaomba wajipange kwa mwaka ujao. Na tunaamini kuwa watafurahia zaidi. Msimu ujao wa NSSF Handeni Kwetu 2016 utakuwa wa aina yake.
By Kambi Mbwana, Mratibu Mkuu
kambimbwana@yahoo.com
0712053949

Monday, November 23, 2015

Msiba wa Alphonce Mawazo waibua mapya, Chadema wafungua kesi Mahakama Kuu Kanda ya Mwanza

Mwenyekiti wa Chadema Freeman Mbowe akitoa taarifa kwa wananchi baada ya Chadema Kufungua Kesi Mahakama Kuu Kanda ya Mwanza kupinga kuzuiliwa kwa mwili wa Marehemu Mawazo kuagwa Jijini Mwanza.

Na George Binagi, Mwanza
Chama cha Demokrasia na Maendeleo Chadema leo kimefungua kesi katika Mahakama Kuu Kanda ya Mwanza, ili kuiomba Mahakama hiyo kutengua zuio la kuuaga mwili wa aliekuwa Mwenyekiti wa chama hicho Mkoa wa Geita Marehemu Alphonce Mawazo, lililotolewa na Jeshi la Polisi Mkoani Mwanza kutokana na hofu ya kiusalama pamoja na uwepo wa ugonjwa wa Kipindupindu.

Katika kesi hiyo, Chadema inawakilishwa na Mawakili watatu ambao ni James Millya, John Mallya pamoja na Paul Kipeja ambapo mlalamikaji ni Charles Lugiko ambae ni baba mdogo wa Marehemu Mawazo. Mahamaka hiyo chini ya Jaji Lameck Mlacha, imesikiliza malalamiko ya upande wa washtaki na kuahirisha kesi hiyo hadi kesho ambapo imeamuru mlalamikiwa ambae ni Mkuu wa Polisi Mkoa wa Mwanza pamoja na mwanasheria Mkuu wa Serikali kupelekewa nyaraka za kesi hiyo kabla ya kusikiliza utetezi wao hapo kesho.

Bima ya afya NHIF yakanusha kudaiwa na Hospitali ya Rufaa Mbeya



Na Mwandishi wetu,Dar es salaam Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya nchini umekanusha kuwepo kwa madai yaliyotolewa na Hospital ya Rufaa  Mkoani Mbeya kuwa  wanaudai Mfuko jumla ya shilingi bilioni 2 na kwamba wanaudai Mfuko kutoka mwezi Juni, 2015.  Akizungumza jijini Dar es salaam Kaimu Mkurugenzi Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya  Ndugu Michael Mhando amesema madai yaliyotolewa na Hospital hiyo ya Rufaa Mkoa wa Mbeya  hayana ukweli wowote nakwamba mfuko huo  unalipa madai baada ya mtoa huduma kuwasilisha kwenye Mfuko. Amesema madai   ya mwisho ya Hospitali hiyo kulipwa ni ya mwezi Agosti, 2015. Madai ya mwezi Septemba, 2015 yamewasilishwa kwenye Mfuko tarehe 4/11/2015 ambayo mpaka sasa yana siku 15 tu. Kwa hiyo Hospitali ya Rufaa ya Mbeya tumewalipa madai yao yote na kwa mwaka huu wa 2015 kuanzia Januari hadi Agosti 2015 tumewalipa kiasi cha shilingi bilioni 4.3.

 Madai mengi ambayo yamekuwa yakiwasilishwa kwao yamegubikwa na udanganyifu mkubwa hali inayowafanya kuchukua muda mrefu katika uhakiki wake ikiwemo kuwapigia simu wagonjwa waliopewa huduma za matibabu.  Aidha Mhando amesema mfuko huo unatoa onyo kali kwa watoa huduma ambao wamekuwa bado wakijihusisha na udanganyifu wa aina yoyote kwa kuwa haitawaonea haya kuwafutia usajili na kuwafikisha katika vyombo vya sheria.  Amesema Mfuko pia unazidi kutoa rai kwa watoa huduma kutumia fursa zinazotolewa na Mfuko katika kuhakikisha huduma za matibabu zinaboreshwa kwa wanachama na Watanzania kwa ujumla.

Rais Magufuli apiga stop sherehe za Sikukuu ya Uhuru

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Kwa mujibu wa Sheria ya Sikukuu za Kitaifa (The Public Holidays Act, Cap 35) pamoja na Sheria zingine zinazompa mamlaka Rais kutangaza siku yoyote kuwa sikukuu au mapumziko, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli ameamua kuwa maadhimisho ya Sherehe za Uhuru na Jamhuri zitakazofanyika tarehe 9 Desemba, 2015, yatumike kwa kufanya kazi.
Kwamba maadhimisho ya Uhuru ya mwaka huu (2015) yatatumika kama kichocheo cha kujenga tabia ya kufanya kazi (Uhuru na Kazi) katika Taifa letu. Mheshimiwa Rais ameelekeza Watanzania wote siku hiyo waitumie kwa kufanya kazi mbalimbali kama vile, mashambani, maofisini, sokoni, viwandani na usafi wa miji yao katika kutimiza dhana ya Uhuru na Kazi kwa vitendo.
Aidha, kwa kuwa Sherehe za Uhuru na Jamhuri huendana na Maandalizi mbalimbali ambayo yanatumia fedha, kwa kuzingatia kuwa siku hiyo itaadhimishwa kwa kufanya kazi, fedha zilizokuwa zimetengwa kwa ajili ya sherehe hiyo sasa zitumike kwa shughuli zingine za kijamii ikiwa ni pamoja na kupambana na maradhi hasa kipindupindu, kununulia dawa za hospitali, vitanda vya hospitali n.k. kadri kamati za maandalizi zitakavyoamua.
Ieleweke kuwa sherehe za Uhuru na Jamhuri ni muhimu katika kuadhimisha kumbukumbu ya uhuru wa nchi yetu. Hivyo, sherehe hizi zitaendelea kuadhimishwa kila mwaka kama kawaida kuanzia mwaka 2016.
Gerson Msigwa

UNIDO yapiga jeki viwanda vidogo vya mafuta ya alizeti mkoani Dodoma

IMG_2196
Meneja Mkuu wa kiwanda cha kuzalisha mafuta ya alizeti cha Glory Farm & Agricultural Products, Justin Nyamoga akitoa maelezo jinsi kiwanda hicho kinavyofanya kazi zake kwa Mratibu Mkazi wa Mashirika ya Umoja wa Umoja wa Mataifa na Mwakilishi wa Shirika la Maendeleo (UNDP), Alvaro Rodriguez (wa pili kushoto) aliyeambatana na Mkurugenzi Mkazi wa Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP), Awa Dabo (kushoto), Mwakilishi Msaidizi wa Shirika la UNFPA, Dk. Hashina Begum (kulia) pamoja na Mwakilishi Mkazi wa Shirika la FAO nchini, Patric Otto kukagua miradi inayofadhiliwa na Umoja wa Mataifa mjini Dodoma. 

Na Mwandishi wetu
Kutoratibiwa kwa mbegu za alizeti na ukosefu wa mitaji umeelezwa kuwa changamoto kubwa kwa wasindikaji wadogo wa mafuta ya mbegu ya alizeti katika kuendesha viwanda vyao kwa gharama nafuu. Hayo yameelezwa na Wakala wa uendelezaji Kongano la Mafuta ya Alizeti wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Maendeleo la Viwanda (UNIDO) Vedastus Timothy wakati akizungumza na waandishi wa habari walioambatana na Mratibu wa mashirika ya Umoja wa Mataifa nchini Tanzania, Alvaro Rodriguez.

Mratibu huyo alikuwa Dodoma kwa shughuli mbalimbali za ukaguzi wa miradi pamoja na kuhudhuria shughuli za bunge la Tanzania lililomalizika jana. Timothy alisema kwamba pamoja kuwepo kwa taarifa za kuwepo kwa mbegu za kutosha nchini Tanzania,hali halisi inayoelezwa na wasindikaji inaashiria kwamba sekta hairatibiwi vyema kwani wasindikaji hukaa muda mrefu bila kuwa na mbegu za kusindika.

Aidha alisema kwamba mbegu za alizeti zinazovunwa kuanzia Aprili hadi Julai na huwa na bei nafuu kipindi hicho lakini kama wasindikaji wakikosa mitaji na kununua mbegu chache, msimu unapoisha hawawezi tena kuendelea kufungua viwanda vyao.
Alisema kwamba wasindikaji hao wanakumbana na kiwango kikubwa cha riba kuanzia asilimia 20 kwenda juu , riba ambayo inakwamisha maendeleo ya viwanda hivyo.

CCM, Mwakalebela waendelea kumng'ang'ania mchungaji Peter Msigwa mjini Iringa

Aliyekuwa mgombea ubunge jimbo la Iringa Mjini, Fredrick Mwakalebela, kushoto akiwa na Katibu wa CCM Iringa Mjini, Elisha Mwampashe wakati wanazungumza na waandishi wa habari kufuatia kesi waliyofungua dhidi ya Mchungaji Peter Msigwa.

Na Mwandishi Wetu, Iringa
CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) wilaya ya Iringa Mjini kimekanusha kufutwa kwa kesi yao dhidi ya Mkurungenzi wa Manispaa hii pamoja na mbunge wa Jimbo la Iringa mjini mchungaji Peter Msigwa. Akizungumza na waandishi wa habari katibu wa ccm wilaya ya Iringa mjini, Elisha Mwampashe alisema kuwa taarifa zilizosambaa sehemu mbalimbali sio za kweli.

“Nimekuwa nikipigiwa simu nyingi toka jana nikipewa taarifa kuwa kesi yetu imetupiliwa mbali na imeenea sana kwenye mitandao ya kijamii na maeneo mbalimbali ukweli ni kwamba kesi ya uchaguzi namba tano ya 2015 haijafutwa,”alisema Mwampashe. Mwampashe ameongeza kuwa kesi hiyo bado haijapangiwa siku ya kusikilizwa wala kupangiwa jaji wa kuendesha kesi hiyo hivyo anashangaa kuaona taarifa zinazendelea kuenena mitaani.
Baadhi  ya waandishi wa habari wa mkoani Iringa, wakisikiliza hoja za aliyekuwa mgombea Ubunge wa jimbo la Iringa Mjini, Fredrick Mwakalebela na Katibu wa CCM wilaya ya Iringa Mjini, Elisha Mwampashe, hawapo pichani.

“Ifahamike kuwa mahakamani kuna shauri la msingi  ambalo lilikuwa na kupinga matokeo na kuna  shauri dogo  namba 28 la mwaka 2015 ndio lilikuwa likizungumziwa jana kwa lengo la kuomba kupunguziwa dhamana kutokana na sheria kuruhusu kufanya hivyo,” alisema.

Mwampashe amemalizia kwa kuwataka wananchi  na wanachama wa CCM kuendelea kuwa na subra kwa kuwa haki yao ya msingi itapatikana mahakamani. Kwa upande wake Fredrick Mwakalebela aliyekuwa mgombea ubunge jimbo hilo, aliesema kuwa shauri lililofutwa ni la kuomba kupunguziwa pesa ya dhamana.

Saturday, November 21, 2015

Soma Hotuba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa John Pombe Joseph Magufuli wakati anazindua Bunge jana mjini Dodoma

Mheshimiwa Spika;
Niko hapa leo kutimiza matakwa ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Ibara ya 91 Ibara ndogo ya kwanza inayonitaka kulihutubia na kulifungua rasmi Bunge hili. Naomba nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutujalia uzima na afya njema, na kutuwezesha kuwepo hapa siku ya leo. Aidha nitumie fursa hii kuwakumbuka wenzetu ambao, kwa namna na nafasi mbalimbali, walishiriki katika mchakato wa uchaguzi huu na kwa bahati mbaya walipoteza maisha yao kabla ya mchakato haujakamilika. Kwa hao wote waliotangulia mbele za haki ninamuomba Mwenyezi Mungu azirehemu roho zao na awape pumziko la amani. Nitumie nafasi hii kuwapa pole ndugu na jamaa ambao ndugu zao walifariki na wengine kupata ulemavu wakati wa mchakato wa uchaguzi huu.
Pia natoa pongezi kwako wewe Mheshimiwa Spika, Job Ndugai na Mheshimiwa Naibu Spika, Dkt. Ackson Tulia kwa kuchaguliwa kwenu kuongoza Bunge letu la 11. Waheshimiwa Wabunge wamewapa imani yao, na mimi kwa nafasi yangu nawahakikishia imani na matumaini yangu makubwa kwenu. Sina shaka Mheshimiwa Spika, chini ya uongozi wako Bunge letu limepata kiongozi mahiri, makini na mweledi.
Aidha, niwapongeze Wabunge wote kwa kuchaguliwa kuwa wabunge wa Bunge hili la 11. Aidha, nitumie nafasi hii kuwapongeza wale wote waliochaguliwa katika nafasi za udiwani katika kata mbalimbali kote nchini. Natoa pongezi hizi kwa dhati kabisa kabisa kwa sababu kuu mbili:
• Kwanza, ni kwa sababu ushindani katika uchaguzi wa mwaka huu ulikuwa ni mkubwa sana kuanzia ndani ya vyama vyetu na baadae katika Uchaguzi Mkuu uliohusisha na kushindanisha wagombea toka vyama tofauti.
• Pili, nawapongeza kwa sababu wananchi wamewapa imani na ridhaa ya kuwawakilisha katika kipindi ambacho matarajio yao kwa Awamu ya Tano ya uongozi wa nchi yetu ni makubwa sana. Watatupima kwa namna tutakavyokidhi kiu na matarajio yao. Sote tuliahidi kuwatumikia wananchi, na kutokana na utumishi wetu kwao tuweze kutatua matatizo yao mbalimbali, na kuongoza mabadiliko makubwa ya kiutendaji, usimamizi wa matumizi ya mali za umma na rasilimali za taifa, na ugawaji wa rasilimali hizo kwa haki. Mimi na Mheshimiwa Samia Suluhu, Makamu wa Rais tuliwaahidi wananchi kuwa tutawatumikia na tutahakikisha kuwa katika utumishi wetu tutawajali wananchi wote, lakini zaidi wananchi wa kawaida. Naamini wenzangu pia ndicho mlichoahidi na daima tukumbuke kuwa kazi zetu na mipango yetu yote tutakayoipanga na kuisimamia italenga katika kuwanufaisha watu wetu.
Mheshimiwa Spika;

Friday, November 20, 2015

Angalia jinsi sherehe za kuapishwa kwa Waziri Mkuu Mheshimiwa Majaliwa Kassim Majaliwa

 Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan, akisalimiana na kuwapongeza baadhi ya Wabunge wapya wa bunge la 11, walipokutana kwenye viwanja vya Ikulu ndogo Chamwino wakati wa sherehe za kuapishwa Waziri Mkuu mpya wa awamu ya Tano, Mhe. Majaliwa Kassim Majaliwa zilizofanyika leo Nov 20, 2015 mjini Dodoma. 
 Rais Dkt. John Pombe Magufuli, akimwapisha Mhe. Majaliwa Kassim Majaliwa, kuwa Waziri Mkuu wa awamu ya tano, wakati wa sherehe hizo zilizofanyika leo kwenye Viwanja vya Ikulu ndogo Chamwino mjini Dodoma.
 Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan, akisalimiana na Mbunge wa Ilemela, Angelina Mabula kwenye viwanja vya Ikulu ndogo Chamwino wakati wa sherehe za kuapishwa Waziri Mkuu mpya wa awamu ya Tano, Mhe. Majaliwa Kassim Majaliwa zilizofanyika leo mjini Dodom

UN wazindua mradi wa kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi, Chamwino mkoani Dodoma

ALVARO KUPANDA MTI-2
Mratibu Mkazi wa Mashirika ya Umoja wa Umoja wa Mataifa na Mwakilishi wa Shirika la Mpango wa Maendeleo (UNDP), Alvaro Rodriguez akipanda mti kama ishara ya uhifadhi mazingira baada ya kuzindua mradi wa kupunguza na kukabiliana na mabadiliko ya Tabianchi kwa kutumia nishati jadidifu ya jua (Mitigating Climate change in vulnerable communities of Dodoma region, Machali village, Chamwino District), katika Kijiji cha Machali A, wilaya ya Chamwino mkoani Dodoma katika utekelezaji wa moja kati ya malengo ya maendeleo endelevu (SDGs).
ALVARO MWAGILIA MAJI-3
Mratibu Mkazi wa Mashirika ya Umoja wa Umoja wa Mataifa na Mwakilishi wa Shirika la Mpango wa Maendeleo (UNDP), Alvaro Rodriguez akimwagilia maji kama ishara ya uhifadhi mazingira baada ya kuzindua mradi wa kupunguza na kukabiliana na mabadiliko ya Tabianchi kwa kutumia nishati jadidifu ya jua (Mitigating Climate change in vulnerable communities of Dodoma region, Machali village, Chamwino District), katika Kijiji cha Machali A, wilaya ya Chamwino mkoani Dodoma katika utekelezaji wa moja kati ya malengo ya maendeleo endelevu (SDGs).

Thursday, November 19, 2015

Wasamaria wema waombwa kusaidia matibabu kwa dada Joyce Mwambepo



Ndugu Wasamaria wema,Wakati huo huo kwa niaba ya Michuzi Media Group, Ankal amejitolea kusaidia uratibu wa kufanikisha matibabu ya dada Joyce. Hivyo unaweza kuwasiliana naye kwa email issamichuzi@gmail.com ama whatsapp namba +255 754 271266 kwa jina la Ankal.
Hivyo ndiyo kusema jumla ya Tshs. 2,565,270/-  tayari zimekusanywa kumsaidia dada yetu huyu anayeteseka. Kwa niaba ya mgonjwa tunashukuru sana kwa msaada huo, hana cha kuwalipa zaidi ya kuwaombea kwa Mola mzidishiwe pale mlipopungukiwa.
Wakati huo huo kwa niaba ya Michuzi Media Group, Ankal amejitolea sio tu kuchangia bali pia kusaidia uratibu wa kufanikisha matibabu ya dada Joyce. Hivyo unaweza kuwasiliana naye kwa email issamichuzi@gmail.com ama whatsapp namba +255 754 271266 kwa jina la Ankal.



Napenda kutumia fursa hii kukushirikisha habari ya kusikitisha kuhusu dada Joyce Mwambepo (pichani akiwa na mwanaye wa miaka 4, na miguu yake iliyopooza) mkaazi wa Sinde jijini Mbeya. Dada huyu mwenye umri wa miaka 27 anaishi na bibi yake mwenye umri wa miaka 80 pamoja na huyo mwanaye.

GAPCO Tanzania yadhamini shindano la Kilimanjaro Marathon za kilomita 10

Meneja Masoko wa GAPCO Tanzania, Caroline Kakwezi (Wa pili kutoka kushoto) akishiriki katika uzinduzi wa Kilimanjaro Marathon 2016 ambapo GAPCO ilitangaza kudhamini mbio za kilomita 10 kwa walemavu. Wengine kutoka kushoto ni Meneja Masoko wa Kampuni ya Bia Tanzania Oscar Shelukindo, Meneja wa Bia ya Kilimanjaro Pamela Kikuli, Mkurugenzi Msaidizi wa Michezo katika Wizara ya Habari, Michezo na Utamaduni, Alex Nkenyenge na Meneja Mawasiliano wa Tigo John Wanyancha.
Meneja Masoko wa GAPCO Tanzania, Caroline Kakwezi (Wa tatu kutoka kushoto) akishiriki katika picha ya pamoja mara baada ya kumaliza uzinduzi wa Kilimanjaro Marathon 2016 ambapo GAPCO ilitangaza kudhamini mbio za kilomita 10 kwa walemavu. --- GAPCO, kampuni ya mafuta inayoongoza Tanzania imetangaza udhamini wake wa mbio za Kilimanjaro Marathon 2016 kilomita 10 kwa walemavu. 

Akitangaza udhamini huo jana wakati wa uzinduzi wa mashindano hayo ya Kilimanjaro Marathon, Meneja Masoko wa GAPCO Tanzania, Caroline Kakwezi alisema GAPCO inaona fahari kudhamini mbio hizo za kilomita 10 kwa walemavu. “Tumeshuhudia mbio hizi za Kilimanjaro Marathon zikikua tangu tuanze kudhamini mwaka 2011 na pia kufurahia faida wanayopata washiriki na jamii inayozunguka maeneo ambayo mbio hizi hufanyika kila mwaka. Tunayo furaha kufanya kazi na Wild Frontiers ambao ndio waandaaji wa mashindano haya,” alisema Kakwezi. 

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni Mheshimiwa Kassim Majaliwa

Hatimae kile kitendawili kigumu cha nani atakuwa Waziri Mkuu wa serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wa awamu ya Tano chini ya Rais, Dr John Pombe Magufuli kimeteguliwa leo baada ya kutangazwa Kassim Majaliwa kuwa Waziri Mkuu. Jina la Majaliwa halijatarajiwa na wengi kuwa atatangazwa kuwa Waziri Mkuu mpya baada ya Mizengo Pinda aliyestaafu.

Wednesday, November 18, 2015

Twanga Pepeta yapata pigo, Mwinjuma Muumini ang'oa nyota wake watatu, akiwapo Dogo Rama, Salehe Kupaza na Jojoo Jumanne

Na Kambi Mbwana, Dar es Salaam
BENDI ya Twanga Pepeta imepata pigo zito baada ya Mkurugenzi wa bendi ya Double M Sound, Mwinjuma Muumini kuwanyakua wanamuziki watatu ambao ni Dogo Rama, Salehe Kupaza na Jojoo Jumanne.
Mwanamuziki Dogo Rama enzi hizo wakati yupo bendi ya The African Stars, Twanga Pepeta, sasa amejiunga na bendi ya Double M Sound.
Kuondoka kwa wanamuziki hao ambao sasa wanaelekea nchini Msumbiji kuweka kambi ili kuimarisha bendi hiyo, kutaleta mshike mshike katika bendi hiyo inayomilikiwa na mjasiriamali Asha Baraka.

Mwanamuziki Dogo Rama aliyeibuliwa na Twanga Pepeta miaka kadhaa iliyopita aliuthibitishia mtandao huu kuwa ameamua kuhama rasmi katika bendi yake hiyo na kuhamia katika bendi ya Double M Sound.


Kuondoka kwa wanamuziki hao watatu katika kipindi  cha kuelekea mwishoni mwa mwaka kutapokewa kwa hisia tofauti na wadau wa muziki wa dansi nchini, ambapo Twanga imeendelea kubaki kileleni kwa kutegemea zaidi sauti na uwezo wa kutunga nyimbo wa Kupaza, aliyepika vibao moto moto.

Kujengwa kwenye hifadhi ya Bahari Golden Tulip kwazua maswali ya sheria ya mita 60


Kumekuwa na sheria na kanuni mbalimbali zinazoundwa, ingawa wakati mwingine hushindwa kutekelezeka kwa wakati. Ukifika katika hoteli ya Golden Tulip utakuta jinsi eneo hilo linavyozidi kujengwa na kuendelezwa kama lilivyokutwa na mpiga picha wetu. Kujengwa kwa eneo hili lililokuwa pembezoni mwa Bahari ya Hindi ni kinyume cha sheria ya Hifadhi ya Bahari. Tumeshuhudia maeneo mengi yakivunjwa kwa nyumba zao baada ya kubainika yamejengwa katika hifadhi ya bahari. Haijafahamikaa mara moja kama eneo hili limeruhusiwa kuendelezwa, ikiwa ni tofauti na jengo la Hoteli ya Golden Tulip
Sheria za Hifadhi ya bahari inasema ni marufuku kujenga nyumba mita 60 ilipokuwa bahari. Hali hii imeonekana kuwa tofauti baada ya kukuta hifadhi hii ikionekana kuanza kujengwa na kuanza kuzua maswali mengi kwa wadau wa maendeleo na Waanzania kwa ujumla wanaofuatilia mambo ya maliasili na utalii. Kibao hiki kinaonyesha jinsi eneo hilo lilivyotengwa kwa ajili ya kujenga jambo ambalo ni kinyume cha sheria za mita 60 za bahari.
Gari likipita katika barabara inayoelekea katika barabara ya Golden Tulip Hoteli, ambayo pia inaonekana eneo hilo lililowekwa mabati kwa ajili ya kuanza kulijenga kama lilivyokutwa na mpiga picha wetu. na chini mkazi wa jiji la Dar es Salaam akipita katika eneo hilo, huku ikionekana ramani mbalimbali za ujenzi huo.

Taasisi ya Doris Mollel yapongezwa na serikali

DSC_1839
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Mhe. Saidi Meck Sadiki akizungumza mbele ya wanahabari, madaktari na baadhi ya akina mama waliokuwa na watoto waliozaliwa kabla ya wakati maarufu kama Njiti (Hawapo pichani). Kushoto ni DoriS Mollel ambaye ni Mwanzilishi na Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya Doris Mollel Foundation (DMF) na wengine ni maafisa kutoka Hospitali ya Taifa Muhimbili.
Na Andrew Chale, Dar es Salaam
SERIKALI ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imepongeza juhudi binafsi zinazofanywa na Taasisi ya Doris Mollel Foundation (DMF) katika harakati zake za kusaidia watoto wanaozaliwa kabla ya wakati (njiti) na mambo ya elimu hapa nchini huku ikiahidi kuendelea kushirikiana nayo kufikia malengp yake. Kauli hiyo imetolewa mapema leo na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Mhe. Saidi Meck Sadiki wakati wa kupokea vifaa maalum vya kusaidia watoto njiti vilivyotolewa na taasisi hiyo ya Doris Mollel Foundation tukio lililofanyika katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili jengo la Watoto.

“Tunatambua mashine hizi ni bei kubwa na Serikali pekee yake haina pesa hivyo kwa kusaidiana na wadau kama hivi n faraja sana na tunapongeza juhudi hizi za taasisi ya DMF kwa kujitokeza kusaidia mashine kwa watoto njiti” ameeleza Mkuu wa Mkoa huyo.
Mkuu wa Mkoa huyo aliongeza kuwa, Mashirika mengine yaendelee kujitokeza kusaidia huduma za kijamii ikiwemo vifaa kama taasisi ya Doris Mollel kwani asilimia 100 ya wagonjwa na watu wengine wenye mahitaji katika tiba wanakimbilia Dar es Salaam hasa Hospitali ya Muhimbili. “Tunaomba tena mukipata nyingine musisite kutiletea hapa maana Mkoa huu unapokea wagonjwa wengi kutoka maeneo mengi ya Tanzania na vifaa vya tiba mara nyingi vinakuwa ni vichache, Huko mikoani wanapewa rufaa waanakuja hapa pia hivyo DMF musisite kuja tena” alimalizia Mkuu wa Mkoa huyo.

Daraja la Mbweni JKT lipo mbioni kukamilika, lapokewa kwa shangwe na wananchi jijini Dar es Salaam

Daraja lililokuwa linawasumbua mno wakazi na wananchi wa Mbweni JKT, sasa linaelekea mwishoni, hali iliyoanza kuwafurahisha wananchi hao waliokuwa wakisumbuka kuvuka eneo hilo lililokuwa linajaa maji mara kwa mara yanayotoka baharini.

Katika pita pita ya mitandaoni, tuliona picha hizi ambazo tayari zimeshapokewa kwa shangwe kutokana na wananchi hao kuanza kulitumia. Ikumbukwe kwamba kutokuwapo kwa daraja hili kulileta usumbufu mkubwa kwa wananchi. Kabla ya uwapo wa daraja hili, magari yalilazimika kupita kwenye maji na pengine yanapokuwa mengi kushindwa kuvuka. Ni kutokana na daraja hili, shukrani za dhati ziende kwa JKT wanaojenga daraja hili, serikali Kuu kwa kupitia Mkuu wa Wilaya Kinondoni, DC Paulo Makonda na watendaji wote waliohakikisha kwamba utengenezaji wa daraja hili unakamilika ili kuondoa adha kwa wakazi na wananchi wa Mbweni JKT.

Mkazi mmoja wa Mbweni aliyeshindwa kutaja jina lake alitumia muda mwingi kuwasifu wahusika kwa kulisimamia vyema daraja hilo litakalokuwa mkombozi kwa wananchi wa eneo hilo na wote wanaoishi jijini Dar es Salaam.
Picha ya daraja hili la Mbweni JKT ilipigwa kwenye gari.

Tuesday, November 17, 2015

Rais Magufuli asaini kitabu cha maombolezo ya vifo vya watu 130 nchini Ufaransa katika ubalozi wa Ufaransa Tanzania

Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dokta John Pombe Magufuli amesaini kitabu cha Maombolezo katika Ubalozi wa Ufaransa jijini Dar es salaam kufuatia vifo vya watu zaidi 130 vilivyotokea November 15, 2015 kutokana na mashambulizi ya ugaidi mjini Paris, Ufaransa.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akimpa pole Balozi wa Ufaransa nchini Tanzania Malika Berak kufuatia vifo vya Watu zaidi 130 vilivyotokana na mashambulizi ya kigaidi.

Pamoja na kutia saini kitabu cha maombolezo, Mheshimiwa Dr. Magufuli ametoa salamu za pole kwa Rais wa Ufaransa Mheshimiwa Francois Hollande na kumuombea uvumilivu na ustahimilivu katika kipindi hiki kigumu.

Dokta Magufuli ambaye amepokelewa na Balozi wa Ufaransa hapa Nchini Bibi Malika Berak amesema Tanzania imeguswa na vifo hivyo na inaungana na Ufaransa katika kipindi hiki kigumu cha majonzi.

Aidha Rais Magufuli amewaombea majeruhi wote wa tukio hilo wapone haraka ili waweze kuungan a na familia zao na kuendelea na shughuli zao za kila siku. Katika hatua nyingine Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dokta John Pombe Magufuli amewasili Mjini Dodoma jioni hii kwa shughuli mbalimbali za kikazi. Mheshimiwa Magufuli amesafiri kwa gari kutoka Dar es salaam hadi Dodoma na taarifa ya shughuli atakazozifanya mtaarifiwa baadaye.

LinkWithin

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...