MGODI UNAOTEMBEA
Na Kambi Mbwana, Dar es Salaam
INAHITAJI akili ya
kiuwendawazimu kupita huku na kule kusifia mwendelezo mbovu wa siasa za
Tanzania, hasa baadhi ya vyama vya upinzani kufanya mambo ya kijinga.
Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe
Ni pale mwanasiasa anayejiona
anakubalika kwa wananchi wake, anaamua kwa makusudi kuvunja sheria za nchi. Huu
ni ujinga. Unahitaji kupingwa vikali na kila muhibiri wa amani.
Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi CCM na Rais wa Jamhuri ya Muunganao wa Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete.
Kwa wiki moja sasa, jiji la
Arusha limekuwa likitawaliwa na uvunjifu wa amani, taharuki na kusababisha
matatizo makubwa. Tangu siku ya Jumamosi ya Juni 15, wananchi wa Arusha
wamekuwa wakiendelea kuishi kwa mashaka na wasiwasi mkubwa.
Watu watatu wamefariki Dunia,
huku wengine kadhaa wakijeruhiwa vibaya, ikiwa ni baada ya bomu kurushwa katika
mkutano wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), huku ukihudhuriwa pia
na Mwenyekiti wao, Freeman Mbowe.
Ikumbukwe kuwa, matokeo ya
ghasia jijini Arusha si mara ya kwanza, maana kila siku kunakuwa na mgogoro
mkubwa na kuwaacha Watanzania wenzetu wakiwa hawaelewi cha kufanya.
Mara baada ya kutokea mlipuko
huo, Mbowe, kama mwenyekiti wa Chadema, alitangaza kuwazuia wabunge wote wa
chama hicho kuingia kwenye vikao vya Bunge.
Ni kauli tata sana kwa
maendeleo ya Taifa. Taifa ambalo, linahitaji bajeti bora yenye maslahi na
Watanzania wote. Lakini kuzuia wabunge kuhudhuria vikao vya Bunge, ni vitendo
vya kushangaza mno.
Kwa mujibu wa Mbowe, aliwazuia
wabunge kuhudhuria vikao vya Bajeti ili washiriki kwenye misiba ya waliokufa
kutokana na mlipuko huo wa Soweto, jijini Arusha.
Mbowe anatangaza hatua hii huku
akijua kuwa Chadema haipo Arusha peke yake. Chadema pia inahitaji kura za
wananchi wote, kama vile Tanga, Kilimanjaro, Mwanza, Mbeya, Morogoro, Iringa na
mikoa mingine kama kweli inahitaji kushika dola.
Lakini Chadema wao wameonekana
kuweka nguvu kubwa kwa jiji la Arusha, tena wakifikia hata kuvunja sheria za
nchi. Ndio hapo ninapoanza kujiuliza juu ya mwendo huu.
Tunahitaji viongozi
wendawazimu. Wale wanaoweza kufanya kazi bila kuogopa sura au mihemko ya
viongozi wa vyama vya siasa. Kwa mfano, sheria inajieleza juu ya vyama vya
siasa vinavyofanya vitendo vya vurugu na adhabu yake pia.
Tunahitaji sasa serikali kwa
kupitia Msajili wa Vyama vya siasa, John Tendwa kuwa makini zaidi. Jeshi la Polisi
nalo lihakikishe kuwa linasimamia vyema usalama wa raia.
Usalama ambao mara kadhaa
umekuwa hatarini kwasababu ya matakwa ya viongozi wachache wa kisiasa. Huu ndio
ukweli. Jeshi la Polisi Tanzania, mkoani Arusha lilizuia mikusanyiko isiyokuwa
na sababu.
Ili kuonyesha kuwa Chadema wana
lengo lao binafsi, waliamua kufanya mkutano bila hata kupewa kibali cha polisi.
Hapa Chadema walitegemea kitu gani?
Wanataka waendelee kuvunja
sheria wakijua wanaogopwa, hawawezi kuchukuliwa hatua za aina yoyote? Kila mara
wabunge wa Chadema wanafanya vitendo visivyokuwa vya kiungwana.
Mbunge kama vile Godbless Lema,
Tundu Lissu, Mbowe, Mchungaji Peter Msigwa wamekuwa wakijifanya wao ndio kila
kitu katika Taifa hili, jambo linaloibua maswali kede kede.
Kuheshimika kwao wanakuchukulia
vibaya, ndio maana matamshi yao mara kwa mara hayajengi jamii bora zaidi ya
kuibomoa kadri wanavyojua wao, lengo lao ni kuichafua serikali iliyopo
madarakani, chini ya Rais Jakaya Mrisho Kikwete, ambaye pia ni Mwenyekiti wa
Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Hii sio njia nzuri kamwe.
Tanzania inazidi kuingia kwenye migogoro kama hii kwasababu ya ujinga wa watu
wachache, ambao nashawishika kusema kuwa wana uchu wa madaraka.
Mara baada ya mlipuko kutoka
Jumamosi, Mbowe hakuonyesha kumfahamu mlipuaji huyo, zaidi ya kuwazuia wabunge
kuingia bungeni, akiwamo Zitto Kabwe, ambaye alipaswa kuwasilisha Bajeti ya
Wizara Kivuli ya Fedha na Uchumi.
Lakini siku moja baadaye, yani
Jumapili, Mbowe huyu huyu anatangaza kuwa anamfahamu vyema mlipuaji wa bomu,
akasema ni Polisi. Sasa kama ndio yeye, maana hakuna anayeweza kufanya uharifu
akachekewa, isipokuwa anahitaji kuchukuliwa hatua kali.
Kauli ya Mbowe inakwenda
sambamba na tamko la serikali Bungeni, kwa kupitia Waziri wa Nchi, Ofisi ya
Waziri Mkuu, William Lukuvi, aambaye alionyesha kupigwa na butwaa jinsi baadhi
ya Watanzania wenzetu wanavyopigania kuiharibia sifa nchi yetu.
Lukuvi akafika mbali zaidi kwa
kusema serikali itatoa Milioni 100 kwa mtu atakayetoa ushahidi wa wanaofanya
vitendo vya kiharifu, kama hivyo vya kulipua mabomu, huku nikiamini kuwa Mbowe
atatoa ushirikiano kwa kumtaja mtu huyo.
Kwa uelewa wangu na siasa za
Tanzania, zenye kila aina ya mihemko, kutoka baadhi ya vyama upinzani, sidhani
kama Chadema wangeweza kumuacha mhalifu, arushe bomu na kutokomea
kusipojulikana.
Chadema wasingefanya ujinga
huu. Wangemng’ang’ania. Kama wanaweza kushindana na polisi kwa kuwarushia mawe,
wakisema ukombozi unakaribia, kwanini wamuache mtu anayepiga bomu katika
mkutano wao wa kampeni?
Hapa nini kinatengenezwa? Kwa bahati
mbaya wale wasiokuwa na uelewa mzuri juu ya mambo ya kisiasa, wanajikuta
wakipumbazwa na janja za aina hiyo kwenye propaganda za kisiasa. Naweza kusema kuwa Chadema wao wenyewe wanafuga jini, hivyo walitafutie damu ya kulinywesha, tofauti na ile ya Watanzania inayomwagika bila sababu za msingi.
Angalia ajabu hii, mara baada
ya bomu kurushwa kwenye mkutano huo, mtu ambaye anadaiwa kurusha, hakuweza
kukamatwa mara moja kwasababu Polisi hawakupewa ushirikiano.
Ni pale walipoanza kurushiwa
mawe na wananchi kwenye tukio hilo, ambalo baadhi yao wamepoteza maisha. Siasa
za aina hii sio mahali pake. Kila mtu mwenye mapenzi mema na Tanzania ni wakati
wake sasa kuwa makini na kuwa mkali zaidi.
Watanzania tunadanganywa na
wanasiasa ambao wanatumia nguvu kubwa kuiweka nchi kwenye kisiwa cha umwagaji
damu. Wanasiasa wa aina hii wanatafuta kitu gani?
Hata kesho wakifanikiwa
kunyakua dola, wanataka waongoze watu wa aina gani? Inauma sana. Katika
kuliangalia hili, naona kufanikiwa kwake ni ngumu, maana kwa bahati mbaya wapo
wananchi wanaojifanya hawanazo.
Wanajifanya wana uchungu zaidi
na nchi hii kuliko Baba wa Taifa, ambaye licha ya kuhangaika kwa mambo mengi,
ila leo hii ametangulia mbele za haki.
Wapambanaji wengi
waliohakikisha kuwa mimi na wengine wenye umri wangu wanakuja kuishi katika
nchi hii. Nchi ambayo kutokana na uongozi bora, kuheshimiana na kupendana,
kulisababisha kutapakaa kwa sifa nzuri ya kisiwa cha amani.
Kisiwa cha amani ambacho leo
hii watu wanataka kugawanywa kwa dini zao, makabila yao na mikoa wanayotoka.
Leo hii jiji la Arusha, lenye sifa kemkem linanuka damu.
Kila siku Arusha kimewaka.
Kunanini? Nani kasema Arusha ni lazima damu zimwagike? Huu sio mwendo mzuri
hata kidogo. Ni wakati wetu sasa kila mtu kuwa makini na aweke msimamo.
Kwa wale wanaopenda mabadiliko
ya kiutawala, yani kutoka Chama Cha Mapinduzi (CCM) na kuingia upinzani, pia
sio sahihi kushinda kwa kurushiana mabomu na risasi za moto.
Wapo watu wanaocheka kwa
vitendo hivi. Hao wanajidanganya kuwa muda wa mabadiliko umefika. Sawa, lakini
mabadiliko hayo yana manufaa gani kama watu wanapoteza maisha?
Kwanini tusifuate sheria na
taratibu za kiungwana? Angalia, wabunge wa Chadema baada ya kususia Bunge,
walivamia jiji la Arusha, wakijifanya wao ndio wenye uchungu kuliko wengine.
Hizi ni janja za kisiasa tu.
Hakuna jipya linaloweza kufanywa kwa amani kama watu wanapita kwenye migongo ya
wananchi, bila huruma na kuangamiza roho za ndugu zetu na wengine kupata
majeraha na kuharibu nguvu kazi ya Taifa.
Wapo radhi watu wafe lakini wao
waendelee kujulikana katika mitaa na kaya zetu. Wapo radhi wafanye fujo
wakiamini kuwa vyombo vya habari vitawaandika pamoja na kupata mijadala kwenye
mitandao ya kijamii, ambayo imejaza wanasiasa uchwara.
Ni wale wanaoacha mambo ya
maana na kujadili upupu wa mabwana wakubwa hawa ambao wengi wao wanaishi maisha
yenye kila raha, wakati wanaowahadaa na kufariki wanalala njaa, wanakufa
masikini.
Wanadanganya kila wawezalo. Wanafanya
kila hira, lakini siku akitoka hapo anaingia tena bungeni kwa ajili ya
kutunisha mfuko wake kwa posho za serikali.
Kulikuwa na haja gani ya
viongozi wa Chadema kufanya mkutano bila kupewa kibali? Hizi si janja za kutaka
waandikwe? Mwisho wa siku wabunge watatu, akiwamo Tundu Lissu, Joyce Nkya,
Mustafa Akoonay wakikamatwa huku mwenyekiti wao, kinara wa yote hayo, Mbowe
akifanikiwa kutoroka.
Ametorokea kusipojulikana. Watu
wanajua ametoroka, walioandika wanaandika katika media zao. Kesho akikamatwa au
kujisalimisha polisi aandikwe tena.
Huku ni kusumbua umma. Huku ni
kutumia ujanja kujinufaisha kisiasa kwa mambo ya kijinga kabisa. Watanzania
tuyaseme haya ili kuelimishana kwa ajili ya Tanzania yetu.
Taifa linakabiliwa na
changamoto nyingi mno. Bajeti ya mwaka 2013/2014 imetangazwa huku ikishindwa
kujibu namna gani wananchi wanaweza kuishi maisha bora.
Kodi kubwa itakuwa migongoni
mwao. Bei za bidhaa zinazotumiwa na walalahoi zimeongezwa mara dufu. Biadhaa
kama vile mafuta ya dizeli, petrol zitawafanywa wananchi waishi mashakani.
Kuongezwa kwa kodi hizo,
kutaongezeka mfumko wa bei mara dufu. Nauli zitapanda na vyakula havitakatika.
Watu watakufa njaa. Hapa ndipo tunapohitaji vichwa vya wabunge wetu, badala ya
kuelemea kwenye mambo ya anasa, kupiga soga na kulinda umaarufu wao usipotee.
Tunayasema haya hata tutaitwa
makada wa CCM au wale wanaombiwa wapo kwenye ndoa, yani wananchi wanaounga
mkono siasa za Chama Cha Wananchi (CUF).
Nadhani kwa kulijua hili
tunapaswa kuwa makini zaidi. Tuambiane ukweli, maana kinachoendelea leo jijini
Arusha, kitakuwapo tena katika mikoa yetu, wilaya au vijiji vyetu.
Kama leo wanaokufa ni Wachaga
wanaounga mkono Chadema, basi kesho sumu
hiyo itahamia wilayani Handeni, Korogwe, Lushoto, maana nao wanafuatilia
masakata haya yanayofanywa kwa makusudi kama njia ya kulisumbua Taifa letu.
Nachukizwa na vitendo vya
kihuni. Natamani sheria ichukuwe mkondo wake. Kwa wale wanaofanya uhuni wa aina
hii wakibainika wakamatwe na kufunguliwa mashtaka au kuvifuta vyama vya aina
hii.
Najua hili ni jambo
litakalozusha ghasia na machafuko, maana watakimbilia kwenye huruma za
wananchi, lakini akheri ya pengo kuliko jino bovu.
Chadema ni kero na lazima
wajirekebishe, maana wanachofanya sasa, akipatikana kiongozi makini, asiyekuwa
na woga na anayesimamia vyema sheria zake, wanasiasa wengi kwenye vyama vya
aina hii wanastahili kutulizwa mihemko yao.
Mungu ibariki Tanzania.
+255 712053949
+255 753806087
Mwisho
No comments:
Post a Comment