Na Kambi Mbwana, Dar
es Salaam
INAHITAJI moyo wa
chuma mno kuendelea kusikiliza maneno machafu, kejeli kutoka upande mmoja wa
Muungano, yani Zanzibar, dhidi ya wenzao Tanzania Bara.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete akiwa na Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shen.
Ni matusi kupita
kiasi. Katika watu 10 mjini Zanzibar, nane kati yao wanaubwatukia Muungano,
wakiuita wa kinyonyaji na hauna manufaa kwao, tangu ulipoasisiwa mwaka 1964
kutokana na matakwa ya viongozi wawili, yani Hayati Baba wa Taifa, Mwalimu
Julius Kambarage Nyerere na Abeid Aman Karume, Rais wa kwanza wa Zanzibar.
Waasisi wa Bara na Visiwani, Marehemu Julius Nyerere na Abeid Aman Karume wakikubaliana juu ya Muungano huo.
Hawautaki hata
kidogo. Wanazungumza mengi kuelezea ukweli huo mbele ya jamii nyingine, hasa
Bara, ambao wo wameonekana kama ving’ang’anizi wa Muungano huo.
Si vibaya mtu kutoa
maoni yake, kusema kile anachokiamini, ila ubaya unakuja pale mtu huyo anapotoa
kashfa ili anayosema yasikilizwe na kueleweka.
Mengi yanasemwa, ila
binafsi naweza kuzungumzia sakata hilo kuwa linachangiwa kwa kiasi kikubwa na
ubaguzi, udini, ndio maana tunashuhudia mnyukano, kuchomeana nyumba za ibada,
hasa makanisa visiwani humo.
Zanzibar ambayo watu
wake wengi ni wenye dini ya Kiislamu, wanaona hakuna mwingine mwenye ruhusa ya
kuishi huko isipokuwa yule mwislamu.
Mtu yoyote mwenye
asili ya Bara, hasa akiwa Mkristo, basi hana nafasi ya kuishi Zanzibar kwa
raha, kama wao wanavyoishi Tanzania Bara.
Ni ajabu mno. Ingawa
Wazanzibar wengi wanaona Visiwani ni kwao peke yao, ila wenzao wa Bara
wameendelea kuwa kimya.
Ukimya huo
unachangiwa na roho ya upendo dhidi ya ndugu zao Zanzibar, ndio maana kwenye
mitaa yao bado wameendelea kuwapa hadhi ile ile na haki ile ile.
Japo ndio kuna
mapungufu mengi katika muungano wa Bara na Visiwani, lakini yanaweza
kuzungumzika kwa ajili ya kuuboresha na sio kuuvunja kama wanavyotaka baadhi
yao.
Zaidi ya hapo, huwezi
kutofautisha ubaguzi wa dini, ukabila uliokuwa kwa kiasi kikubwa katika nyoyo
za watu wa Zanzibar.
Wale wanaoona kuwa
kuendelea kuwa kwenye muungano huo, kunasababisha wachache wakose fursa ya
kuoiona Zanzibar inakuwa nchi huru, tena Taifa la Waislamu.
Hili si jambo lenye
mbolea kwa Zanzibar. Zanzibar ambayo licha ya wachache wasiojitambua
wakijipambanua kuwa wanaweza kusimama wenyewe, lakini bado wamekuwa wakitegemea
vitu vingi kutoka upande wa Bara.
Hili tukilisema, wapo
watakaobisha, hasa wale wanaaokesha kuomba siku moja Zanzibar ijitenge katika
Muungano huo na wafanikishe adhma yao ya kuwa Dola la Waislamu.
Na endapo suala hilo
litafanikiwa, basi hata wale waliozaliwa mjini Zanzibar ila wenye asili ya
Tanzania Bara, kuna uwezekano mkubwa watakimbizwa.
Baba wa Taifa,
Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, katika uhai wake alikuwa akilielezea suala
hili mara kwa mara.
Hakuonekana mwenye
kupenda kuona Zanzibar wanajitenga au Bara wanajitenga. Nyerere anayekumbukwa
na wengi duniani, alisikika mara kwa mara akisisitiza muungano wenye kujali utu
wa kila Mtanzania, bila kuangalia yeye ni mwenye asili ya Zanzibar au Bara.
Tumesikia au kuona
mara kwa mara matamko ya watu wa Zanzibar, wakiwamo viongozi wao wakisimama na
kuukosoa muungano huo kwa vitendo.
Kwa bahati mbaya,
wapo wanaokosoa muungano huo katika majukwaa ya kisiasa, lakini katika serikali
ya Umoja wa Kitaifa (SUK), wanabaki kimya.
Hawa ni wanasiasa.
Watu ambao wanachokisema kwa wakati huo, si watakachokitenda muda ujao.
Kwanini nasema hivyo?
Ukiangalia mfumo mzima wa vyama vingi Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, upande
wa Zanzibar wameelemea sana katika utawala wa Kiislamu.
Mtu anayekuwa
Muislamu, Visiwani Zanzibar ana nafasi kubwa kushinda katika Uchaguzi wowote,
ukiwapo Ubunge.
Si vibaya, hasa kama
aliyeshinda amechaguliwa na wananchi wake,
ukizingatia kuwa tupo katika
kuitetea vyema Demokrasia.
Angalia, licha ya
Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kuonekana kukubalika mno katika
siasa za Tanzania kwa miaka mitano hii, lakini Zanzibar haina nafasi.
Katika Uchaguzi Mdogo
wa Jimbo la Chambani, ambapo mshindi wake alikuwa ni mgombea ubunge kwa tiketi
ya Chama Cha Wananchi (CUF), Yussuf Salim Hussein, aliyepata kura 2708, Chadema
wao walipataa kura 12 tu, wakiwa na mgombea wao Siti Ussi Shaibu.
Chama Cha Mapinduzi
(CCM), wenyewe walipata kura 202 wakiwakilishwa na mgombea wao, Sarahan Said,
wakati kile chama kipya kilichotokea katika mgongo wa CUF, yani Alliance For
Democratic Change (ADC), ikiwakilishwa na Said Miraaj, ambaye pia ndio
mwenyekiti wa Chama hicho.
Kwa waliofuatilia
siasa za Zanzibar kwenye Uchaguzi huo wa Chambani watakubaliana na mimi kuwa
wapo waliosimama hadharani wakisema kuwa ADC kinasimamiwa na Kanisa, kama
kilivyokuwa Chadema.
Mtu anapotoa maneno
kama haya, ni wazi wananchi, hasa Zanzibar ambao siku zote wamekuwa
wakichukizwa na Ukristo, kamwe hawawezi kukipigia kura.
Nasema haya kwasababu
sipendi fitina. Kuacha kuuzungumza ukweli, ili niwafurahishe wale wazandiki,
wasiopenda ukweli.
Huu ndio ukweli wa
mambo. Kinachoongeza joto katika Muungano wa Bara na Visiwani, ni vita ya
ubaguzi wa dini.
Si kweli kama
Tanzania bara inanufaika kwa kiasi kikubwa na Muungano huo, ila wale wanaosema
hayo ndio wenye chuki, choyo na ubaguzi wa dini.
Ndio hao wanaotamani
Zanzibar iwe nchi ya Waislamu, jambo ambalo si sahihi hata kidogo, ukizingatia
kuwa suala hilo linaweza kuibua mizozo na migogoro kila siku.
Angalia, wakati
wanasiasa, hasa waliokuwa kwenye Chama tawala wanazungumza siasa zenye kujenga
zaidi, wenzao wameona njia sahihi ni kuupinga Muungano, wakiamini kuwa wananchi
wengi watawaunga mkono.
Ndio hapo zinazoitwa
taasisi za kidini, kama vile Uamsho walipoingia na kushika kasi na kuzua
taharuki ya aina yake.
Hawa walipita kila
kona kuhubiri dini na kuupinga muungano. Wenyewe wanaziita harakati za kuipa
hadhi ya juu ya Kitaifa na kuwa nchi kamili. Yani kuwa na mamlaka yake ndani na
nje ya nchi.
Kama vita hivi vya
mgogoro wa Muungano visingechochewa na ubaguzi wa dini, sidhani kama
majadiliano ya kuuboresha yasingefikiwa kwa pande zote mbili.
Kwa bahati mbaya
zaidi, wakati wananchi hao wanatafuta namna gani ya kuuvunja Muungano huo, kwa
kuangalia tofauti zetu za kidini, yani Uislamu na Ukristo, ukapenyezwa tena
mjadala wa Serikali tatu.
Huu ulipenya katika
Tume ya Maoni ya Katiba Mpya, chini ya Mwenyekiti wake, Jaji Joseph Sinde
Warioba.
Maoni haya
yalizungumzwa sana na baadhi ya viongozi wa kidini visiwani Zanzibar pamoja na
wachache kutoka CUF, chama kinachoongoza nchini kwa ushirikiano, kati yao na
CCM, chini ya Rais wake, Dk. Ali Mohamed Shein.
Mengi yanayosemwa
sasa ni kuzidi kupandikiza chuki miongoni mwa Watanzania. Yanayosemwa sasa
yatawapandisha hasira wengine na kuingia kwenye mgogoro, wakati pande mbili
hizi zimekuwa zikiishi kwa upendo na kuheshimiana kwa kiasi kikubwa.
Ni wakati wetu
Watanzania wote kwa kupitia Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, yani Bara na
Visiwani, kuona kuwa badala ya kutaka chokochoko za kugawana, wenzetu
walioendelea wanatafuta namna ya kuungana ili wapate nguvu zaidi.
Sidhani kama ni
sahihi Wapemba kupigania sana kuugawa Muungano huo, wakati wanajua fika Bara
wamezagaa wao kila mahali na hakuna anayekimbizwa.
Hata hivyo haitoshi,
tayari pande mbili hizi zimeleta mwingiliano wa kimaisha na kuwafanya waishi
kwa amani, furaha na amani ya aina yake.
Kwa bahati nzuri,
licha ya Visiwani kuonekana kushikilia kuuvunja muungano, wakieneza mno hoja za
udini, ila wenzao Bara wamekuwa wazalendo zaidi.
Ndio maana bado
wabunge wake wanaishi kwa upendo katika Bunge la Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania. Wanaendelea kulipwa posho, mishahara na stahiki zao zote.
Wanafanya na kupata
kila kinachostahili kama watumishi wa umma. Haya ni maisha yenye neema mno.
Badala yaendelezwe,
wanajitokeza wachache, makundi ya watu wakitaka kutugawa kwa kila wanavyotaka
wao.
Binafsi nimekuwa
muumini mkubwa wa Muungano huu wa Bara na Visiwani. Naupenda kwasababu hakuna
haja ya kuuchukia.
Sioni maana ya
kuuponda. Mwenye upendo kwa wengine, asiyekuwa mbaguzi, mwenye choyo katu
hawezi kuukataa Muungano huu, iwe mchana au usiku.
Na kama Muungano huu
una mapungufu, kasoro, hakuna njia ya kuuboresha? Sitaki kusema watu wa Bara
wote wanaotoa huduma za kijamii Zanzibar waondoke Zanzibar, japo naamini
watatoka huko kama kelele hizi, ubaguzi huu, choyo hiki kitaendelea kushika
hatamu kila siku ya Mungu.
Ni wakati wetu sasa
kila Mtanzania, bila kuangalia anatoka Bara au Visiwani kusimama mstari mmoja
kuwakataa wanaotaka kuuvunja Muungano huu.
Tena wale wanaoukataa
kwa kuingiza hoja za udini, ukabila, maana daima huo umesababisha mapigano na
kuyagawa Mataifa mengi.
Mwenye hoja za kutaka
kuuvunja Muungano, pia asisite kuelezea njia zinazoweza kuchukuliwa kwa ajili
ya kuunusuru Muungano huo unaopigiwa kelele.
Nayasema haya kwa
mapenzi makubwa na Taifa langu, maana kwangu hakuna zaidi kati ya Mzigua au
Mpemba.
Hawa wote ni ndugu
zangu na wana haki sawa ya kuishi katika moja ya vijiji, wilaya au mikoa ya
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Nikirejea katika
baadhi ya maneno ya Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere juu ya
kuupigia kelele Muungano huu, alisema kuwa baada ya Muungano huo kusambaratika
na Wazanzibar kujitenga, watagundua kuwa kumbe wao bado si wamoja.
Makundi mawili
yatajitokeza, moja Waunguja na wengine Wapemba. Wachache hao wanataka kujitenga
kwasababu ya Muungano wa Tanzania Bara na Visiwani.
Nje ya Muungano huu,
bado Zanzibar hawatabaki salama, kama itakavyokuwa upande wa Bara nao kujitenga
kwasababu za kijinga, hasa udini, ukabila nilioelezea katika makala haya.
Katika kuliweka sawa
jambo hili, shime viongozi wote wa vyama vya siasa na serikali ya Bara na
Visiwani kusimama kidete juu ya kuunusuru Muungano huu unaotikiswa kwa sasa.
Sio kweli kama kuna
mmoja ananufaika zaidi ya mwenzake na hata kama yupo, huyo anayenyonywa anayo
haki ya kupaza sauti yake juu kwa njia ya kutafuta suluhu.
Mungu ibariki Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania, Bara na Visiwani.
0712 053949
0753 806087
No comments:
Post a Comment