Na Kambi Mbwana, Dar
es Salaam
CHAMA Cha Muziki wa
Hip Hop Tanzania (TUMA), kimetuma salamu ya rambirambi kufuatia kifo cha msanii
wake Langa Kileo, aliyefariki juzi katika Hospitali ya Taifa Muhimbili na
kuibua machungu upya kwa wapenzi wa muziki huo nchini.
Marehemu Langa Kileo enzi za uhai wake.
Wiki iliyopita, wadau
wa muziki wa Hip Hop walimpoteza Albert Mangweha ‘Ngwair’, aliyezikwa katika
makaburi ya Kihonda mjini Morogoro, huku mapema wiki hii msanii wa filamu, Jaji
Khamis Kash alifariki Dunia na kuleta hofu katika ulingo wa sanaa hapa nchini.
Akizungumza jana
jijini Dar es Salaam, Mwenyekiti wa Tanzania Urban Music Association (TUMA),
Fredrick Mkoloni, alisema kuwa Tanzania imempoteza msanii mwingibne mwenye
uwezo wa juu katika uimbaji wa muziki wa Hip Hop.
Alisema kwasababu
hiyo, TUMA wapo mstari wa mbele katika kipindi hiki kigumu cha mfululizo wa
vifo vya wasanii Tanzania, ambapo pia wamewataka wadau, mashabiki na wasanii
kwa ujumla kumuombea marehemu ili akapumzike kwa amani.
“Huu ni wakati mgumu
kwa Watanzania wote baada ya Langa naye kufariki Dunia, hivyo tunaomba ndugu
zetu tushirikiane katika kipindi hiki kigumu cha kuondokewa na ndugu yetu,
ikiwa ni siku chache baada ya kuzikwa Ngwair mkoani Morogoro.
“TUMA tutaendelea
kushirikiana kwa namna moja ama nyingine katika kifo cha Langa, huku tukiomba
na wasanii wote tushirikiane katika msiba wa ndugu yetu Langa,” alisema.
Wasanii mbalimbali
wameonyeshwa kupata mshtuko mwingine, akiwamo Kalapina, aliyeibuka na kusema
hofu imezidi kutawala na kumuombea marehemu aende akapumzike kwa amani.
Kalapina alisema kuwa
Langa ni miongoni mwa wasanii wenye kutoa mashairi mazito, hivyo Hip Hop
imezidi kukumbwa na wasiwasi wa aina yake kwa kuwapoteza vijana wao wenye
makali ya hali ya juu katika ramani ya muziki huo nchini.
“Langa ni msanii
mzuri mwenye uwezo wa juu, hakika nitamkumbuka kwa mengi, maana kifo chake ni
pigo kwa Watanzania na wadau wote kwa ujumla,” alisema Kalapina.
Naye Kala Jeremia,
alisema kuwa kifo cha Langa ni pigo zaidi katika muziki wa Hip Hop hapa nchini,
baada ya kurafiki katika Hospitali ya Muhimbili.
“Tutaendelea
kumkumbuka msanii mwenzetu Langa, maana wote safari ni moja,” alisema Kala
ambaye tuzo yake ya wimbo bora wa Hip Hop aliyposhinda ameamua kuipeleka katika
familia ya Ngwair kutokana na kuthamini mchango wake.
Ratiba ya kifo cha
Langa imepangwa kuwa msanii huyo ataagwa siku ya Jumatatu kuanzia saa saba
mchana, ambapo saa 10 alasiri atazikwa katika makaburi ya Kinondoni jijini Dar
es Salaam.
No comments:
Post a Comment