Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
HALI ya utata
imeonekana kugusa hisia za watu wengi kutokana na kifo cha msanii Albert
Mangwea, huku ripoti yake ikifanywa siri, hivyo kushindwa kuurudisha mwili wa
marehemu nchini Tanzania kwa ajili ya mazishi yake.
Marehemu Ngwea, enzi za uhai wake
Kwa siku tatu sasa,
mazishi ya Ngwea yamekuwa yakisogezwa mbele kwa madai kuwa ripoti yake
haijamilika. Awali, mwili wa Ngwea ulitarajiwa kufika Tanzania Alhamis, lakini
danadana ilianza hadi sasa kutarajiwa kuletwa mwili wake siku ya Jumatatu au Jumanne.
Kama hivyo ndivyo,
mwili wa Ngwea una dalili za wazi kuzikwa Alhamis, hasa kama utaratibu wa kuagwa
katika Viwanja vya Leaders Club utabaki kama ulivyopangwa.
Akizungumza kwa
masharti ya kutajwa jina lake, mtu wa karibu ndani ya Kamati ya Mazishi,
haelewi kwanini kifo cha Ngwea kinakuwa cha utata, hadi ujio wake Tanzania
kushindwa kueleweka.
Ingawa maandalizi kwa
kila hatua yamekuwa yakifanyika, lakini Hospitali ya Dk Hellen nchini Afrika
Kusini, imekuwa ikishindwa kutoa majibu ya ripoti ya msiba huo.
Akizungumza na Handeni
Kwetu, Rais wa Shirikisho la Muziki Tanzania, Addo Novemba, alisema kuwa kamati
yao haiwezi kufanya vitu kinyume na ripoti ya hospitali hiyo.
“Na sisi tunasubiria
ndugu yetu aletwe ili shughuli za mazishi yake zifanyike kwa Watanzania wote
washiriki kwa namna moja ama nyingine, hivyo tunaomba tuwe na subira katika
hili,” alisema.
Kuna kila dalili kuwa
Ngwea ataletwa Tanzania Jumanne kama sio Jumatatu, hivyo utaratibu wa mazishi
yake kuendelea kama ulivyopangwa na Kamati ya Mazishi.
Msiba wa Ngwea
umegusa hisia za watu wengi, huku kwa sasa watu wakikutania nyumbani kwa kaka
yake, Kenneth Mangwea, ambaye pia ndio mwenyekiti wa Kamati hiyo ya mazishi.
Aidha, wadau
mbalimbali wamekuwa wakijitokeza kusaidia kwa namna moja ama nyingine, hasa
katika suala la michango.
No comments:
Post a Comment