https://tpc.googlesyndication.com/simgad/8045142562622600543

Recent Post

Friday, January 31, 2014

Maoni na mtazamo wa mwananchi wa kawaida wilayani Handeni, mkoani Tanga

Yameandikwa na Rashid Hassan Kilo, kutoka kijiji  cha Misima, wilayani Handeni, mkoani Tanga katika mtandao wa facebook.

HAYA ni malalamiko ya watu wa kijiji cha Misima, wilayani Handeni mkoani Tanga, yameandikwa na Rashid Hassan Kilo, nikaona niyapachike hapa kutoka kwenye wall yake...... Sijaongeza wala kupunguza...

Habari za asubuhi "Wana wa Handeni"

Kwangu kumekucha salama hofu na mashaka ni kwenu. Hoja yangu leo ni juu ya matangazo yaliyozagaa kila kona ndani ya mipaka ya kijiji cha Misima yanayohusu kuchangia ujenzi wa maabala ya shule ya sekondari Misima katika mchanganuo ufuatao:
1. Nguvu kazi 10,000@
2. Ng'ombe 3000@
3. Mbuzi/kondoo 1000@
Labda niishie hapo kwanza kwakuwa mlolongo ni mrefu sana kwani ni zaidi ya vipau mbele 26 na viwango tofauti vya kulipia. Mwisho ni jina Mtendaji wa kijiji
S. KIDUNDA
VEO-MISIMA.
Japo tunajuwa haya ni maendeleo lakini kwanini tusingeitishwa mkutano na kupata ufafanuzi juu ya ghalama za ujenzi wa maabala hiyo, gawanya kwa idadi ya watu, mifugo, maduka, migahawa na vyanzo vyote vya vijiji 5 vya kata ya Misima?

Katika ibara ya 18(d) ya Katiba tuanayotumia sasa ya 1977 "Kila mtu anayo haki ya kupewa taarifa wakati wowote kuhusu matukio mbalimbali muhimu kwa maisha na shughuli za wananchi na pia kuhusu masuala muhimu kwa jamii."

Leo hili lakujenga maabala ni tukio muhimu sana kwetu na kwa vizazi vyetu ila jinsi ya uongozi wa kiimla wa Misima unavyotufanyia umeyatokomeza na unazidi kuyatokomeza kabisa maendeleo ya Misima.

Leo hii ni miaka mingi imepita bila kusomewa mapato na matumizi, lakini pia ni zaidi ya mwaka 1.6 tangu 18/10/2012 hatujafanya mkutano kwa viongozi kutuogopa kwa maovu yao, leo hatupo tayari kuchangia bila kupata mchanganuo unaoeleweka lakini pia hatupo tayari kutoa pesa kwa kwa viongozi wasio waaminifu.

Lakini la mwisho kiwango kilichowekwa ni kikubwa bora ingekuwa kila kaya 10000, lakini nguvu kazi? Kwa kipindi hiki ambacho wachangiaji wenyewe wanategemea chakula cha msaada toka serikalini? Ningeomba viongozi wangefanya mkutano kwanza na wanakijiji ili kujadiliana kwanza kuliko kutuogopa, mtatuogopa hadi lini?

Julio aitwa Mwadui FC Shinyanga

Na Kambi Mbwana, Dar es Salaam
KOCHA msaidizi wa zamani wa Simba, Jamhuri Kihwelo ‘Julio’, ameitwa katika kuinoa timu ya Mwadui FC inayoshiriki ligi daraja la kwanza, huku akisubiriwa kwa hamu kuona timu hiyo inapata tiketi ya kucheza Ligi Kuu ya Tanzania Bara.
Kocha wa zamani wa Simba, Jamhuri Kihwelo Julio ambaye yupo kwenye mipango ya kufundisha timu ya Mwadui FC.

Habari zilizotufikia katika chumba chetu cha habari zinasema kuwa tayari Julio ameshawasili katika timu hiyo kwa ajili ya kuanza taratibu za kuinoa timu hiyo.

Julio alikuwa kocha msaidizi wa Simba, hata hivyo alienguliwa akiwa sambamba na kocha wake mkuu, King Abdallah Kibadeni, jambo linalomuumiza kichwa hadi leo.

Akizungumza kwa njia ya simu, Julio alisema kuwa ni mapema mno kuelezea maisha yake ya soka, ikiwa ni miezi michache tangu alipoenguliwa Simba kwa mizengwe.

Pitia historia mpiga tumba wa Twanga Pepeta, MCD aliyezikwa juzi mkoani Kilimanjaro

Marehemu MCD enzi za uhai wake
Historia ya Marehemu Soud Mohammed Timbo (MCD) 1973-2014. Kama ilivyosomwa na Shemeji yake Bwana Mlanzi siku ya Maziko Jumatano tarehe 29-01-2014.

-Marehemu alizaliwa Mwaka 1973 mkoani Kilimanjaro.


-MCD alisoma katika Shule ya Msingi Mawenzi iliyopo Manispaa ya Moshi na alihitimu mwaka 1987. Alianza Masomo ya Sekondari katika Shule ya Shemsanga Korogwe Tanga kuanzia 1988-1992. Baada ya kumaliza masomo ya Sekondari alijiunga na Chuo cha Sanaa Bagamoyo.


-Baada ya kumaliza Chuo cha Sanaa Bagamoyo, alifanya kazi katika Bendi ya Diamond Sound "Wana Dar es salaam Ikibinda Nkoi", African Stars Band "Twanga Pepeta", Mashujaa Musica kwa muda mfupi na baadae alirejea katika Bendi ya African Stars "Twanga Pepeta" mpaka mauti yalipomfika.

Thursday, January 30, 2014

Mzee Yusuph: Tumejipanga kuwapa raha Morogoro

Na Kambi Mbwana, Dar es Salaam
MKURUGENZI wa kundi la Jahazi Modern Taarab, Mzee Yusuph, amewataka wadau wa muziki wajipange imara kwa ajili ya kupokea burudani zao katika onyesho la aina yake litakalofanyika Januari 31 katika Ukumbi wa Tanzanite Complex, uliopo mjini Morogoro.
Mzee Yusuph, pichani.
Akizungumza jijini Dar es Salaam jana, Mzee Yusuph, alisema kuwa amejipanga yeye na waimbaji wake kujibu maswali kwanini wao ni vinara katika muziki huo.

Alisema kuwa mkoa Morogoro ni kati ya ile inayopenda muziki wao, hivyo suala hilo limemfanya aone shauku ya kufanya kazi nzuri jukwaani kwenye onyesho hilo.

“Nimejipanga imara kama Mkurugenzi  kuwapatia burudani kabambe wadau na mashabiki wetu katika onyesho la mkoani Morogoro ambapo tutafanya vitu vya aina yake.

“Tutaimba nyimbo zetu mpya na zile za zamani ambapo wadau wetu wana kila sababu ya kuja kupata vitu vya aina yake kutoka kwetu Jahazi, lenye waimbaji hodari,” alisema.

Jahazi ni miongoni mwa makundi ya muziki wa taarabu yenye waimbaji wenye uwezo wa juu katika tasnia ya muziki wa taarabu hapa nchini, huku mashabiki wengi wakiwaunga mkono.

Mkuchika aelezea adha ya utawala bora na changamoto zake Tanzania

Kaptemo mstaafu George Mkuchika, pichani.
WAZIRI wa Nchi ofisi ya Rais anayeshuhulikia Utawala Bora, Kapteni mstaafu, George Mkuchika amesema migogoro ya ardhi, mauaji ya maalbino na vikongwe, wanachi kujichukulia sheria mikononi, rushwa pamoja na ujangili zinadaiwa kuwa moja ya sababu zinazochangia kuporomoka kwa Tanzania katika viwango vya utawala bora duniani.

Mkuchika aliyasema hayo alipokuwa akizungumza katika kikao cha 30 cha kamati ya ushauri wa mkoa wa Kilimanjaro (RCC) kikao ambacho ni cha kwanza kwa mwaka 2014 na maalum kwa ajili ya kujadili vipauumbele vya Bajeti ya Mkoa huo kwa mwaka 2014/2015.

Kaptein Mkuchika alisema kutokana na taarifa zilizotolewa hivi karibuni, Tanzania inashika nafasi ya pili kwa utawala bora nyuma ya Rwanda kwa nchi za ukanda wa Afrika mashariki nyuma ya Rwanda, 17 katika ukanda wa Afrika na 102  kati ya nchi 176  duniani ambapo kwa mujibu wa taarifa hizo Tanzania imeshuka kiwango katika ukanda wa Afrika katika kipindi cha miaka miwili.

CCM yaelezea mafanikio yake ikiwa ni kuelekea kwenye kilele cha maadhimisho ya miakaa 37 ya kuzaliwa kwake

Katibu wa NEC Itikadi na Uenezi Nape Nnauye akizungumza na waandishi wa habari kwenye ukumbi wa mkutano wa CCM Mkoa wa Mbeya.

Wakati CCM inatimiza miaka 37 tangia kuanzishwa kwake februari 5 mwaka 1977,Chama hicho kinajivunia sana mafanikio makubwa kiliyopata hasa katika kudumisha Umoja na Mshikamano kwa  Watanzania ,kutunza na kuilinda Amani ya nchi hii na kujenga misingi imara ya uchumi wa nchi,akizungumza na waandishi wa habari katika ukumbi wa mikutano CCM Mkoa wa Mbeya Katibu wa NEC Itikadi na Uenezi Nape Nnauye  alisema  sherehe za miaka 37 zimeanza nchi nzima na zilizinduliwa rasmi tarehe 26 na Makamu Mwenyekiti wa CCM (Zanzibar) Dk.Ali Mohamed Shein Unguja Zanzibar.

Kilele cha sherehe hizi  kitakua tarehe 2 februari ,Nape alisema “kwa nini tarehe mbili na sio tano ni kwa sababu tarehe tano ni siku ya kazi hivyo tumeona tufanye tarehe mbili ili tuwaruhusu watu wengi zaidi waweze kushiriki”.

Wadau kibao wamzika MCD mkoani KilimanjaroNa Kambi Mbwana, Dar es Salaam
HATIMAYE mwili wa mwanamuziki wa zamani wa bendi ya The African Stars, Twanga Pepeta, Soud Mohamed ‘MCD’ ulizikwa jana katika makaburi ya Njolo, mjini Moshi, mkoani Kilimanjaro na kuhudhuriwa na watu mbalimbali.


Wananchi na wadau wa muziki wakimzika Mpiga tumba wa zamani wa Twanga Pepeta, marehemu MCD.

Marehemu MCD alifariki juzi mjini Moshi baada ya kuugua kwa muda mrefu, huku akiacha pengo la majonzi makubwa katika tasnia ya muziki wa dansi nchini.

Akizungumza mara baada ya maziko ya MDC, Meneja wa bendi ya Twanga Pepeta, Hassan Rehani, aliwashukuru wadau mbalimbali waliofanikisha mazishi ya mpiga tumba wao huyo nguli nchini.

“Wadau mbalimbali waliweza kujitokeza kwa wingi katika vikao vya kujadili msiba wa MCD na hatimaye kufika nyumbani kwa  marehemu Moshi, mkoani Kilimanjaro.

“Twanga Pepeta imepata pigo zito kwa kuondokewa na MCD, ambapo pia tunaamini kuwa uwezo wake utaenziwa na wadau wote wa muziki wa dansi,” alisema.

MCD aliwahi kufanya kazi na bendi mbalimbali, ikiwamo Mashujaa Musica, ambapo pia walishirikiana na wadau walioguswa na msiba huo mzito.

Tuesday, January 28, 2014

Wadau wa ngumi wasifia mkutano wao


Na Kambi Mbwana, Dar es Salaam

KATIBU wa Ngumi za Kulipwa hapa nchini, Ibrahim Kamwe, amesema kwamba mkutano wao utakaofanyika Februari Mosi mwaka Vijana Hall Kinondoni, utakuwa na faida kubwa ya kujadili sekta hiyo ya masumbwi.


Akizungumza jana jijini Dar es Salaam, Kamwe alisema kwamba mkutano huo umepewa Baraka zote na Rais wa Oganaizesheni ya ngumi za kulipwa (TPBO), Yasin Abdallah.


Alisema kuwa anaamini wadau wote wa masumbwi, wakiwamo mapromota watajumuika pamoja kutafuta namna bora ya kuendeleza mchezo wa masumbwi hapa nchini.


“Huu ni mkutano wa kwanza unaofanyika nchini huku ukiwa na manufaa makubwa kwa sisi wadau wa masumbwi hapa nchini, hivyo naomba tujiandaye vizuri kwa maendeleo yetu.


"Mkutano utaanza mapema asubuhi, huku nikiamini kuwa kila kitu kitakwenda kama kilivyopangwa, ukizingatia kuwa mbali na mapromota, pia mabondia na makocha wa ngumi ni miongoni mwa wanaotarajiwa khudhuria,” alisema Kamwe.


Mchezo wa masumbwi unatajwa kati ya ile iliyopunguza makali yake, licha ya wadau mbalimbali katika tasnia hiyo kuendelea kuupigania ili ubaki katika mafanikio yake kama zamani.

Jumuiya ya Wazazi CCM Wilayani Kongwa yajipanga


Na Kambi Mbwana, Dar es Salaam

JUMUIYA ya Wazazi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), wilayani Kongwa mkoani Dodoma, Januari 29 itaandaa mechi ya kirafiki itakayokutanisha timu za Kata ya Segeri kwa ajili ya kusherehekea miaka 37 ya CCM tangu kuzaliwa kwake inayoadhimishwa Februari tano kila mwaka.


Akizungumza jana kwa njia ya simu kutoka mkoani Dodoma, Katibu wa Jumuiya hiyo, Hussein Mwaikambo, alisema kuwa lengo la mchezo huo ni kuwakusanya wadau wa michezo na kutafuta fursa ya kusherehekea kwa pamoja kuzaliwa kwa CCM.


Alisema kuwa lengo lao ni kutumia fursa hiyo kufurahia kuzaliwa kwa chama chao, wakiamini kuwa vijana watapata nafasi ya kubadilishana mawazo na kujiweka sawa kiafya.


“Katika kuelekea miaka 37 ya CCM ambapo kwa mwaka huu sherehe hizi zitafanyika mkoani Mbeya tumejipanga kwa sisi wilaya ya Kongwa kujipanga kwa vitu vingi ikiwapo mechi ya kirafiki ambayo wakati huu maandalizi yake yanaendelea.


Hili litakuwa tukio muhimu ambalo litatangazwa litakapokamilika, hasa kwa timu zitakazochaguliwa ambazo zitacheza baada ya vitu vyote kufanyika asubuhi hadi jioni,” alisema.


Kwa mujibu wa Mwaikambo, taratibu zote za sherehe hizo zitaendelea kuratibiwa ili kuhakikisha kuwa tukio hilo la burudani na michezo linafanyika kwa mafanikio makubwa.

Cheza Kidansi wakutana kuujadili muziki wa dansi


Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam

WADAU wa muziki wa dansi wanaotokea katika mkusanyiko unaojulikana kama Cheza Kidansi, juzi walifanya kikao cha kwanza na kuadhimia mpango wao kuwawezesha wanamuziki wa muziki huo na kuwakwamua kiuchumi.

Wadau wakijadiliana jambo katika kikao hicho cha Cheza Kidansi.
Kikao hicho kilifanyika katika Ukumbi wa Garden Breeze, ambapo kilihudhuriwa pia na mlezi wao Yusuph Mhandeni, maarufu kama Yusuphed Mhandeni, ambaye ni Mchumi wa Kata ya Makumbusho katika Chama Cha Mapinduzi (CCM).


Akizungumza katika kikao hicho, Yusuphed alisema kuwa mengi yaliyojadiliwa katika kikao hicho ni kuona muziki wa dansi unarudi katika chati yake ili wanamuziki wajimudu kiuchumi.


Alisema wanamuziki wengi wa dansi hawana maisha mazuri kuliko wenzao wa Bongo Fleva, hivyo hilo ni kati ya changamoto zinazoendelea kuwakumba.

Mwandishi wa habari aula uenyekiti UVCCM mkoani Kilimanjaro

Arnold Swai (wa kwanza kushoto)wakati wa upigaji kura, zoezi lilofanyika juzi, wilayani Hai kuziba pengo la nafasi ya Mwenyekiti
Mjumbe wa Halmshauri kuu CCM wilaya ya Hai, Fuya Kimbita, akizungumza katika zoezi la kupiga kura lililoshuhudia Mwandishi wa Habari Leo, Arnold Swai akiibuka kidedea.
Arnold Swai akihutubia baada ya kutangazwa Mwenyekiti Mpya kwa kushinda uchaguzi uliofanyika juzi. Swai alipata kura 151 kati ya kura 222 zilizopigwa
Mwenyekiti wa UVCCM mkoa wa Kilimanjaro, Fredy Mushi, akizungumza na wanajumuiya hiyo muda mfupi kabala ya uchaguzi ulioshuhudia ushindi wa kishindo wa Mwandishi wa Habari Leo, Arnold Swai kuwa Mwenyekiti wa UVCCM wilaya ya Hai.

Sunday, January 26, 2014

Madabida mgeni rasmi Diwani CupNa Kambi Mbwana, Dares Salaam
MWENYEKITI wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Dar es Salaam, Ramadhan Madabida leo atakuwa mgeni rasmi katika mashindano ya Diwani Cup yatakayofanyika kwenye Uwanja wa Shule ya Msingi Mbagala Kuu, iliyopo katika Kata ya Mbagala Kuu.
Timu za Kuzazi na Sansiro kutoka kata hiyo zitapambana kuwania zawadi ya kombe, ng'ombe na jezi seti ambazo ni zawadi za mshindi wa kwnza.

Madabida ndiye atakayekabidhi zawadi ya mshindi wa kwanza na ile ya pili ambaye ataondoka na jezi seti moja huku msindi wa tatu atapewa jezi seti moja.

Akizungumza jana, Diwani wa Kata ya Mbagala Kuu, Benson Malawandu, ambaye ndiye mwandaaji wa mashindano hayo alisema fainali hiyo inatarajiwa kuwa ya aina yake kutokana na kukutanisha timu zenye upinzani wa jadi.

Alisema kilichopelekea kumwalika Madabida katika mashindano ni kutokana na kiongozi kuwa ni mpenda michezo ambaye amekuwa akitoa kuhakikisha anasaidia vijana.
Malawandu akizungumzia mashindano hayo kwa ujumla alisema kwa kiasi kikubwa malengo yametimia.

Alisema wakati anayaanzisha alikuwa na malengo ya kukutanisha vijana pamoja, kutoa fursa kwa vijana kutumia michezo kwa ajili ya kujenga mshikamano na kuepukana na kukaa kwenye magenge.

"Malengo ya mashindano haya kwa asilimia kubwa yamefanikiwa sana, na ndio maana hata zawadi za washindi zilianza kutoka katika hatua za makundi kila timu iliiyoongoza ilipata jezi seti moja na mpira na zile za pili zilipata mipira," alisema.

"Pia kila timu iliyoshiriki nilitoa mpira mmoja kwa ajili yao kujiandaa, na katika hatua ya robo fainali kila timu pia ilipata zawadi ili kuongeza morali ya mashindano, aliongeza.

Pia alisema lengo lingine lilikuwa ni kukamilisha ilani ya chama chao ambacho kinaichukulia michezo kama ni ajira tosha kwa vijana ambayo inaweza kuwakomboa kiuchumi.

Wakati huo huo Malawandu alisema mashindano hao kuanzia sasa yatakuwa ni endelevu na ana mpango wa kuyafanya kila mwaka huku pia kwa sasa akijipanga na kamati yake kwa ajili ya kuanzisha na wanawake.

Wadau wa Cheza Kidansi wakutana kuujadili muziki wa dansiJANA kulikuwa na kikao cha wadau wa muziki wa dansi hapa nchini kilichoendeshwa na kundi la Cheza Kidansi, linaloendeshwa chini ya mlezi wao Yusuph Mhandeni, maarufu kama Yusuphed Mhandeni, ambaye pia ni Mchumi wa Kata ya Makumbusho wa Chama Cha Mapinduzi CCM.
 Wadau wa Cheza Kidansi wakiwa kwenye picha ya pamoja baada ya kikao cha kujadili maendeleo ya muziki wa dansi nchini. Wa pili kutoka kushoto ni Yusuphed Mhandeni, ambaye ndio mlezi wa kundi hilo.

 Katika kikao hicho, mengi yalijadiliwa yanayohusu maendeleo ya muziki wa dansi hapa nchini kwa ajili ya kuuwezesha muziki huo kufikia malengo.

LinkWithin

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...