https://tpc.googlesyndication.com/simgad/8045142562622600543

Recent Post

Thursday, June 06, 2013

Diamond auvuruga msiba wa Albert Mangwea, mwili wake kuzikwa leo hapa mkoani Morogoro, mashabiki wake kila mmoja anasema lakeNa Kambi Mbwana, Morogoro
WAKATI mwili wa Albert Mangwea ukitarajiwa kuzikwa leo hapa mkoani Morogoro, jana katika kuaga viwanja vya Leaders Club, mashabiki wa muziki wa kizazi kipya, walitoa kali baada ya kuacha msiba wa msanii Ngwair na kuanza kumkimbilia nyota mwingine wa muziki huo, Nassib Abdulmalilck, maarufu kama Diamond.
 Ngwair enzi za uhai wake
 Ngwair alivyoletwa juzi
Ngwair alivyoagwa jana.
Hiyo ilitokea jana katika Viwanja vya Leaders Club, Kinondoni, kulipofanyika tukio la kumuaga msanii Mangwea, aliyefariki nchini Afrika Kusini Jumanne ya wiki iliyopita na kuzua huzuni kubwa katika tasnia hiyo.

Mwili wa Mangwea uliwasili viwanjani hapo saa 2:00 ukitokea Hospitali ya Taifa, Muhimbili, alipohifadhiwa juzi, mara baada ya kuletwa ukitokea nchini Afrika Kusini alipofia.

Hali ya utata katika shughuli hiyo ilianza kuonekana tangu mapema, baada ya wadau na mashabiki kuanza kuzengea katika sehemu waliyokaa wasanii, ikionyesha kuwa walikuwa na shauku ya kuwashika wasanii waliokuwapo uwanjani hapo kwa ajili ya kumuaga mwenzao.
Vurugu za Diamond zilianza baada ya kumaliza shughuliza kumuaga msanii mwenzake, hivyo kuamua kuondoka uwanjani hapo, jambo lililosababisha umati wa watu kuanza kumkimbilia.

Hata hivyo jeshi la Polisi na vijana wa ulinzi wa usalama waliingilia kati, kwa ajili ya kudhibiti mwingiliano na haja ya mashabiki hao ambao kwa kawaida walianza kutishia usalama wao na tukio zima la kumuaga marehemu Ngwair.

Hata hivyo, hii si mara ya kwanza kwa Diamond, maana vurugu kama hizo ziliwahi kuibuka alipokwenda kwenye msiba wa msanii wa maigizo na filamu, marehemu Steven Kanumba na kujikuta idadi kubwa ya watu kutaka kumuona kwa ukaribu au hata kumshika mkono.

Awali, Diamond alimuelezea marehemu Ngwea kama moja ya wasanii wenye uwezo mkubwa wa kuimba, huku akiweza kuishi kwa upendo na wasanii wote, tangu alipojiingiza kwenye muziki.

“Nimeguswa sana na msiba wa Ngwair, naamini pengo lake haliwezi kuzibika, maana jamaa alikuwa na uwezo mkubwa mno katika tasnia hii, akitamba na nyimbo nyingi zilizowafurahisha watu wote,” alisema Diamond.

Naye Mbunge wa Kinondoni, Idd Azzan, alimuelezea Ngwea kama mhimili kwenye sanaa ya muziki wa kizazi kipya, huku akisema wadau, akiwamo yeye hataweza kuusahau mchango Ngwair.

“Ni mmoja wa wasanii mahiri mno katika tasnia nzima ya Bongo Fleva, hivyo naamini tutaendelea kumuenzi na kuhakikisha kuwa mchango unakuwa tunu katika soko la muziki huu,” alisema Azzan.

Watu wengi walijitokeza katika kumkuaga Ngwair, wakiwamo wanasiasa, viongozi wa serikali na vyama vya siasa, hasa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), waliowakilishwa na Mwenyekiti wa Baraza la Vijana Taifa (BAVICHA), John Heche, Msemaji wao Tumaini Makene na viongozi wengine ndani ya chama hicho kikuu cha upinzani kwa sasa.

Heche aliwahakikishia wasanii kuwa chama chao kitaendelea kupambana vikali kuibana serikali juu ya maslahi ya wasanii kwenye kazi zao, akiamini kuwa viongo wao, akiwamo mbunge wa Mbeya Mjini, Joseph Mbilinyi ‘Sugu’, Zitto Kabwe, John Mnyika na wengineo wanaendelea kuipigania sanaa nzima kwa kuwapo kwenye mijadala mikubwa ya kitaifa.

“Sisi kama Chadema tumekuwa hodari mno kupigania sanaa ya Tanzania, ndio maana tunasema tutafanya juhudi kubwa kuhakikisha kuwa wasanii wananufaika, ukizingatia kama msanii amefanya kazi nyingi na anakosa maendeleo, anaweza kupata matatizo hata kisaikolojia,” alisema Heche.

Kwa hakika, kila aliyepata nafasi ya kumuelezea marehemu Ngwea, aliitumia nafasi hiyo kumuombea dua njema marehemu Ngwair, sambamba na kuwataka wasanii watumie muda huo kumuombea dua njema.

Idadi kubwa ya wasanii walilimika katika viwanja vya Leaders Club, akiwamo Mrisho Mpoto, Ommy Dimpozi, Madee, Fid Q, Profesa Jay, AY, Mwana FA, Lady Jay Dee, Barnabas, Keisha, Dogo Dito, Q-Chillah, Kassim Mganga, Feroos, Joti na wakali kibao waliojitoa kwa hali na mali kwa ajili ya kumuaga marehemu Ngwea katika viwanja vya Leaders Club.

Marehemu Ngwair anatarajiwa kuzikwa leo katika makaburi ya Kihonda, mkoani Morogoro, huku idadi kubwa ya watu, wakiwamo wadau, mashabiki na viongozi mbalimbali wa Mkoa wakitajwa kushiriki katika msiba huu.

Kamati ya Mazishi iliyosaidiwa kwa kiasi kikubwa na Shirikisho la Muziki Tanzania, chini ya Rais wao, Addo Novemba, waliweka utaratibu mzuri, japo kasoro za hapa na pale hazikosekani katika matukio ya kuaga marehemu ambaye alikuwa na jina kubwa katika jamii yake.

Eneo alililozwa marehemu Ngwea, kuliwekwa uzio ambao ilibakizwa njia tu ya kupita watu waliokwenda kumuaga marehemu, huku nyuma ya mwili wa marehemu kukiwa na maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya viongozi mbalimbali, ndugu wa marehemu, Kamati ya Mazishi na wasanii wote, ikiwa ni sehemu ya kuhakikisha kuwa shughuli za uagaji zinafanyika bila kuleta hatari yoyote kwa waliokwenda Leaders Club.

Wakati wanamuaga marehemu Ngwea, kila mmoja alikuwa akitoa ishara anayojua mwenyewe, ikiwamo saluti, dua kwa Wakristo na Waislamu, wakiwa na haja ya kumuombea marehemu Ngwair.

Hapa mkoani Morogoro, hali ya utulivu imeonekana kuonekana, huku mashabiki mmoja baada ya mwingine wasikika wakizungumzia msiba huu ulioletwa kwa ajili ya maziko.


No comments:

LinkWithin

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...