https://tpc.googlesyndication.com/simgad/8045142562622600543

Recent Post

Monday, December 31, 2012

SALAMU ZA MWAKA MPYABY KAMBI MBWANA
NATUMIA fursa hii kukushukuru wewe ambaye umekuwa bega kwa bega tangu kuanzishwa kwa blog hii ya Handeni Kwetu. Ingawa blog hii ilianzishwa rasmi mwaka jana mwishoni, lakini ilinichukua miezi takribani 10 kuitendea haki.

Kwanini nasema hivyo? Kutokana na kubanwa na majukumu mengine, iliniwia vigumu kuingiza kazi mbalimbali kwa ajili ya kuwapa uhondo wasomaji wangu, ambao licha ya changamoto hizo lakini walikuwa na mimi.

Wakati nausubiria mwaka mpya

Mpenzi msomaji, najiona kuwa ni mwenye bahati sana. Kwani katika kipindi cha wiki ya mwisho ya mwezi Desemba, tumeweza kuingiza wasomaji wapya zaidi ya 4000, kiasi ambacho ni kikubwa mno katika blog inayochipukia.

Naamimi wingi huo unatokana na kufanya kazi kwa moyo nikiwa na melengo zaidi ya kupeana habari mbalimbali. Ndugu msomaji wangu, napenda kutangaza kuwa blog hii haichagui.

Nimekuwa mwepesi kuandika kila ninachoweza. Na kuanzishwa kwa blog hii kumetokana na kuwa na malengo mawili makuu. Lengo la kwanza ni kutafuta mahali kwa kusemea, nikiona kuwa kazi ya uandishi wa habari, nipo kwenye vyombo vya watu vya habari.

Hivyo kama wakati mwingine naweza kubanwa na sera ya kampuni, ingawa changamoto hizo sijakutana nazo hadi muda huu, basi blog ya ‘Handeni Kwetu’ itanipa nafasi ya kusema kila ninachojisikia ili mradi tu nisivunje sheria za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kuzungumza na wasomaji wetu na ujumbe wangu kufika kwa wakati.

Lengo la pili ni kutafuta namna gani naweza kuwaunganisha Watanzania wanaoishi ndani na nje ya nchi, bila kusahau wakazi na wananchi wa wilaya ya Handeni yenye changamoto nyingi.

Nashukuru kwa dhati. Nashukuru maana nimepata mwangaza kugundua kuwa kazi zangu zinapendwa. Na ndio maana nimekuwa mwepesi kuandika makala za aina mbalimbali, ikiwamo kolamu ya ‘Mgodi Unaotembea’, ‘Mambo Fulani Muhimu’, ‘Siwezi Kuvumilia’ na zote ninazoandika katika uwepo wa kazi yangu ya uandishi wa habari na uchambuzi wa makala zangu ambazo pia hupatikana katika gazeti la Mtanzania, linalochapishwa na Kampuni ya New Habari 2006 Ltd, yenye maskani yake jijini Dar es Salaam Tanzania.

Habari za aina mbalimbali za michezo, siasa, afya, burudani na sanaa kwa ujumla, bila kusahau biashara, afya na nyinginezo. Katika kulisema hilo, napenda kusema mwaka mpya wa 2013 nitakuwa makini zaidi.

Nitafanya kazi kwa moyo wote. Wewe kama mdau wa ‘Handeni Kwetu’, usisite kunishauri na kunikosoa kwa njia mbalimbali, ikiwapo safu iliyoandikwa TOA MAONI YAKO KUHUSU HANDENI KWETU.

Kwakuwa sisi ni marafiki na ndugu moja, usisite pia kunitumia habari yoyote, picha unayoona inafaa kuonwa kwenye blog ya ‘Handeni Kwetu’ ili iwe elimu kwa wasomaji wote.

Napenda kumaliza kwa kumshukuru tena Mungu pamoja na wewe kwa kuniunga mkono katika kipindi chote cha mwaka 2012 na mwaka mpya wa 2013, huku nikiamini kuwa tutaendelea kuwa pamoja wakati wote.

Asanteni sana na tuendelee kushirikiana.

Kocha mpya wa Simba Patrick Liewing atua DarNa Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
Kocha mpya wa Simba, Mfaransa, Patrick Liewing pichani, aliyeshika nguo nyekundu mkononi, amewasili leo saa saba za mchana kwa ajili ya kuinoa timu ya Simba. Uongozi wa Simba, kwa kupitia Katibu Mkuu wao, Evodius Mutawala, alikuwa miongoni mwa wadau wa michezo waliompokea Liewing katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Nyerere.

Kocha huyo anawasili huku akiikuta timu ya Simba ikiwa chini ya Jamhuri Kihwelo Julio, kocha ambaye amekuwa na mapenzi makubwa na klabu hiyo kila wakati kwa kitendo chake cha kukubali kuinoa timu hiyo.

Mengi juu ya ujio wa kocha huyo raia wa Ufaransa, yatasikika baada ya kufanya mazungumzo ya mwisho na kuingia makubaliano rasmi ya kuinoa Simba, yenye kipindi kikubwa cha kurudisha imani kwa wapenzi na wanachama wao.

Simba ilimaliza mzunguuko wa kwanza wa ligi ya Tanzania kwa kushika nafasi ya tatu, nyuma ya timu ya Yanga na Azam FC.

Pikipiki au bajaji? Kumbe Bodaboda..Matumizi mabaya ya usafiri wa pikipiki yanasababisha ajali nyingi za barabarani, kama alivyokutwa dereva huyu wa bodaboda aliyesheheni mzigo na kushinda chombo chake anachoendesha. Picha hii ilipigwa leo na mtaalamu wetu. Duh? Kweli bodaboda nouma.

Salamu za mwaka mpya za Dayna NyangeMambo vipi ndugu zangu? Napenda kuchukua nafasi hii kuwatakia maandalizi mema ya mwaka mpya. Mungu atupe nguvu na neema zaidi katika mwaka 2013 utakaoanza kesho. 

Mwaka 2012 tutaukumbuka kwa mengi yapo mema na mabaya. Naomba nikuombe radhi wewe kwa lolote ambalo niliwahi kukukosea, nawe kama ulinikosea sina tatizo nawe tangu sasa.

Pia naomba nitoe shukrani zangu kwa wote waliohusika ktk mafanikio yangu ya kimuziki. 

Dayna Nyange

Naamini wengi mlikuwa mstari wa mbele katika kunishauri, kunipongeza na kunikosoa nilipokosea. Shukrani nyingi zwafikie radio presenter, dj's, radio na tv zote Tanzania na Afrika, maana bila nyinyi kuzicheza nyimbo zangu nisingefika hapa.
Hapo vipiiii
 
Waandishi wa magaazeti mlikuwa mstari wa mbele katika kuona nafika mbali kwa kuandika habari zangu na kufika hata vjijini. Nachukua fursa hii kuwashukuru pia blogs mbalimbali.

Mlikuwa mstari wa mbele kwakuandika habari na ku-post hata baadhi ya show zangu ambazo mmenipa heshma ya kufika mbali zaidi na kusikika hata nje ya nchi mchango wenu ni mkubwa.
Pozi za Dayna Nyangeeeeee

Pia requester wa media sina cha kuwalipa nawashukuru sana na nitabaki kuwaheshimu kwani mmetoa mchango mkubwa kwa kuomba nyimbo zangu media na zikachezwa.

Na amini ni mchango mkubwa sana ktk game hasa kwetu wasanii Nitabaki kuwaheshimu na kuwathamini siku zote. Bila kuwasahau wasanii wenzangu walikuwa nami bega kwa bega katika kunishauri na kunisaidia kwa chochote.

Pia ma dj wa club mbalimbali, mmekuwa chachu ya mzk wangu pale mlipoonesha ushirikiann wenu kwangu.

Pia Waandaaji wa (show) matamasha  madogo na makubwa nawashukuru sana sana kwa kuniamini na kukubali kufanya kazi na mimi siwasahau ma-producers wa video na Audio  na studio mbalimbali kwa kunifanyia kazi za uhakika na jamii ikanikubali kwa kazi hizo.

Wote kwa pamoja naamini sasa ni kama ndugu. Nawaomba muonyeshe tena moyo huwo na mwaka ujao na mingine kwani kaz nzur ni yenye kushirikiana.

Msisite kama ntawakosea naomba msisite kunikanya na kunisamehe. Napenda wote na kuwajali. Nawatakia  mwaka mpya.

Its me Dayna Nyange ‘Mkali wao’

Rage amejificha kwenye kofia ya Jeshi la Polisi Siwezi Kuvumilia

Aden Rage, mwenyekiti wa Simba

Na Kambi Mbwana, Dar es Salaam
JESHI la Polisi kwa kupitia Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Charles Kenyela, halijawatendea haki wanachama wa Simba, zaidi ya 698 waliopanga kufanya mkutano wao jana, Travertine Hoteli, Magomeni.

Jeshi hilo ambalo kimsingi linatakiwa kutoa ulinzi kwa kila Mtanzania, lilijitetea kuwa wameupinga mkutano huo kwa madai eti wanachama hao hawajafuata sheria na taratibu.

Sawa, huenda wanachama hao walikosea, lakini kitendo cha kukaa kimya hadi kutoa uamuzi siku moja kabla ya mkutano hakikubaliki.

Ni dhahiri Jeshi la Polisi limechukua uamuzi wa kuukataa mkutano huo, kwasababu ya kupokea barua kutoka kwa uongozi wa Simba, walioomba mkutano huo uzuiwe kwa sababu wanazojua wenyewe.

Hii sio haki na siwezi kuvumilia kuona baadhi ya watu wanafanya mambo kama Taifa hili ni lao peke yao. Kwanini nasema hivi? Jeshi la Polisi linapaswa kujua kwa mujibu wa Katiba ya Simba, mkutano ule ulikuwa sahihi.

Wanachama hao waliitisha mkutano wao kwa kubebwa na Ibara ya 22, kifungu cha pili cha Katiba yao, ukizingatia kuwa tayari walishatoa taarifa za siku 30 za kutaka viongozi kwa kupitia Kamati ya Utendaji ya klabu hiyo, iitishe mkutano wa wanachama wote.

Simba kwa kupitia mwenyekiti wao, Ismail Aden Rage, walikataa hata kwa kujibu kwa maandishi kama wao walivyotumiwa na wanachama hao, badala yake walipita uchochoroni au kwenye vyombo vya habari na kusema wanachama hao ni wahuni. Kweli wanachama hawa ni wahuni?

Ikumbukwe kuwa wanachama hawa wanaoitwa ni wahuni ndio walioshiriki kwa namna moja ama nyingine, kumuweka madarakani Rage na viongozi wengine wa Simba.

Lakini pamoja na huo uhuni wao, wanachama hawa katika kuandaa mkutano wao walikuwa sahihi, wakitoa taarifa halali, hivyo polisi wao walipaswa kutoa ulinzi tu na sio kuingia kwenye dhambi ya viongozi wa Simba.

Sina lengo la kuunga mkono kundi hilo linalotaka mkutano wa Simba, lakini pia sio kawaida yangu ya kuchekea hata yale mabaya yanayofanywa na waliokuwa madarakani.

Huwa sipendi kuchekea vitu ambavyo vinaongeza chuki kati ya viongozi na jamii, ikiwamo jeshi la polisi ambalo kwa hakika limefanya uamuzi wa kufurahisha watawala badala ya watawaliwa, ukizingatia kila mmoja ana haki sawa kama Katiba ya nchi inavyoeleza.

Kenyela, aliamua kuupinga mkutano huo kwa kuusaidia uongozi wa Simba, walioandika barua ya kuomba msaada Desemba 28, ikiandikwa na Katibu Mkuu, Evodius Mtawala bila hata kupima kuangalia mchakato ulivyokuwa.

Kweli? Kenyela kumbuka upo kwenye nafasi ya kutumikia Watanzania wote na sio viongozi wachache wa Simba, akiwamo Rage ambaye pia ni mbunge wa Tabora Mjini.

Kama kweli ulikuwa na nia ya kuukataa mkutano huo, basi usingesubiri hadi upelekewe barua na Simba. Najiuliza, kama Simba wasingepeleka barua hiyo ya kuomba msaada kwa jeshi la polisi, mkutano huo usingefanyika?

Kwa mtindo huu, tunaweza kuibua hisia hasi kutoka kwa viongozi wa Simba na wanachama. Sakata kama hili lipo pia katika siasa.

Mara nyingi polisi wamekuwa wakitumia mbinu mbovu za kupambana na vurugu. Njia hiyo si sahihi. Lazima Polisi kwa kupitia Kenyela wajuwe wanachokifanya kipo kwa ajili ya watu wachache au la.

Kwa mujibu wa Katiba ya Simba, wanachama wanapofikia idadi ya watu 500 wanaweza kuitisha mkutano, kama wanataka kuijadili klabu yao.

Hili lilifuatwa. Rage na jopo lake hana uwezo wa kupinga mkutano ule, maana uliandaliwa kwa kufuata sheria zote, ikiwamo taarifa Makao Makuu.

Kama Rage angekuwa na utawala wa sheria na ushirikiano na wanachama wake, angekuwa muungwana kwa kuwa miongoni mwa watakaohudhuria mkutano huo.

Lakini anakimbia kivuli, huku akijificha nyuma ya kofia za polisi, akijua kuwa wataweza kufanyia kazi ujanja wake, nasema hivi kwakuwa namfahamu vyema Rage.

Pamoja na kumfahamu Rage, pia naelewa kuwa wengi wasiomjua Rage wanaweza kujikuta wanaingia katika lawama bure na kuleta mgogoro mkubwa zaidi.

Tuombe Mungu wanachama wa Simba wawe waelewa, lakini kama sio hivyo, kuna siku balaa kubwa linaweza kujitokeza, hasa kwa kupewa vizingiti kwasababu zenye matege.

Kenyela anasema, ‘Jeshi la Polisi haliwezi kufanya kazi kwa kupitia nakala,’ mwisho wa kunukuu. Kama kweli, kwanini kauli hiyo isitoke tangu mwanzo wa tarehe iliyopangwa hadi wasubirie barua ya Simba?

Kenyela usiingie kwenye dhambi ya kutumikishwa na viongozi wa michezo wasiokuwa na majibu sahihi kwa wanachama wao, na usijaribu kujiingiza kwenye vurugu na askari wako, ulinzi shirikishi kwasababu ya mtu mmoja.

Kenyela uamuzi wako hauna nia ya kuzima moto zaidi ya kuuwasha, wanachama waliozuiwa kufanya mkutano wao, wakati wamefuata taratibu zote watashindwa kukubali matakwa ya mtu mmoja yawaendeshe.

Kinyume cha hapo, labda Kenyela uniambie kuwa sheria ya saa 48 ya kupeleka barua rasmi jeshi la polisi, inaweza kutumika kama wanachama hao watakuletea barua yao leo jumatatu na wakikubaliwa wakutane Jumatano.

Wakati mwingine uamuzi wetu tunaochukua inabidi tutumie busara na kuangalia matokeo yake, maana si sahihi kuuzima moto kwa kunyunyiza petroli juu yake.

Rage habebeki, ndio maana anaona kuruhusu wanachama hao wafanye mkutano wao kwa haki kama Katiba inavyosema, anaweza kukalia kuti kavu.

Wasiwasi Kamanda Kenyela anajua janja hii? Siwezi Kuvumilia, ndio maana nimeamua kuandika ukweli huu nikiamini kuwa, Kenyela ni mwelewa na atakuwa makini zaidi siku nyingine kadhia kama hii inapojirudia.

0712 053949
0753 806087

Tetea msimamo wako wa kimapenzi


Mapenzi matamu ehee?
 
Na Kambi Mbwana, Dar es Salaam
HII ni Jumatatu ya mwisho kwa mwaka huu 2012 kabla ya kuipokea mwaka mpya utakaoingia siku nne zinazokuja.

Jumatatu hii inatufanya tuendelee kuwa pamoja katika kona ya uhusiano wa kimapenzi na kimaisha.

Nakushukuru kwa dhati kwa wewe uliyeijali na kuithaamini kona hii katika kipindi chote cha mwaka huu, huku nikiamini utaendelea kuniunga mkono.

Nitakuwa mchoyo wa fadhira kama nitashindwa kukushukuru wewe, maana unatumia muda wako mwingi kuisoma na kuamua kunipigia simu kwa ajili ya kuchangia yanayoandikwa humu kila mwisho wa wiki.

Ndugu msomaji wangu mpendwa, katika mapenzi hakuna kitu kizuri kama kuheshimu maamuzi ya moyo wako na pia kusimama kwenye msimamo wako. Nasema hivyo, maana wengineo wanayumba kwakukosa msimamo.

Wanajua fika kuwa wameamua kukaa sehemo moja, lakini kwa sababu hiyo wanajikuta wakisikiliza maneno ya watu, jambo linalomvuruga kichwa chake na kuamua kwa mikono yake kuvunja uhusiano wake, iwe ni wa ndoa au uchumba.

Hilo ndio jambo kubwa na baya mno. Bila kuwa na msimamo wako, kamwe huwezi kufurahia mapenzi yako, maana duniani hakuna aliyekuwa sawa.

Kila mtu ana mapungufu yake. Hata hivyo katika hilo, huwezi kusikiliza majirani wanasema nini.

Huwezi kusikiliza marafiki zako wanakwambia kitu gani. Ndio anaweza kuwa tofauti mpenzi wako kwa marafiki au ndugu zako, ila jua kabisa hupo kwa ajili ya watu hao wanaokwambia maneno ya kila aina yanayohusu mtu wako.

Wapo watu waliobarikiwa uongo. Ni hao wanaoweza kukwambia mtu uliyekuwa naye havutii kimuonekano wake, ila mwisho wa siku wewe mwenyewe ndio muamuzi wa jambo hilo, hivyo lazima uwe makini.

Ukiyumba wewe, hata uhusiano wako utayumba. Utaachana bure na mtu wako kwasababu ya hao wapita njia.

Ndio maana nasema lazima uwe na msimamo na uheshimu maamuzi ya moyo wako. Nasema hivyo, maana moyo hauwezi kudanganya.

Unapopenda hakuna mwingine anayeweza kutoa hoja ya aina yoyoye ikasikilizwa. Hapo lazima uwe makini.

Hapo lazima ujuwe ubaya wa mtu wako au uzuri wake wewe mwenyewe ndiyo unayejua, hivyo hakuna haja ya kujua watu wanasema nini.

Bila hivyo utayumba. Na mbaya zaidi tabia hiyo itaendelea kukusumbua katika maisha yako yote, kitu kitakachokufanya ubadilishe wapenzi au waume kila siku ya Mungu. Hawatakoma hao. Baaada ya kuachana na wako watahamia huko utakapokwenda.

Ndio kazi yao, maana hawapendi kukuona umetulia na kufurahia mapenzi kwasababu yako ya kuyumbishwa. Lazima ujitambuwe na kujifanyika marekebisho wewe mwenyewe.

Mapenzi ni matamu kweli, ila ni baada ya kujielewa na kuheshimu uhusiano wako. Ukiheshimu wewe mwenyewe na kusimama kwenye msimamo wako, hakuna mtu wa kukuletea habari za ajabu ajabu na ukazisikiliza.

Hata kama mtu huyo atakuja kwa nia ya kumponda mpenzi wako, mume wako au mke wako, unaweza kuwa mkali na kumkimbiza mtu huyo, endapo utabaini umedhalilishiwa mwendani wako, hali ya kuwa ndio chaguo lako.

Hakuna njia ya mkato katika hilo. Msimamo tu ndio kila kitu. Wapo marafiki ambao muda wao mwingi ni kuwaponda wapenzi wa wenzao na wenyewe wakacheka. Maana rafiki ni muhimu mno kwake kuliko mtu wake.

Huo ni ujinga. Ila kinachotakiwa hapo ni kuwa mkali, maana wanachotaka wao ni kuona uhusiano wako unakufa, hivyo lazima ujuwe.

Lakini ukiwa mkali kwa watu wenye tabia hizo, watakuogopa na kukuheshimu pia.

Huo ndio ukweli wa mambo. Na ukifanya hivyo, uhusiano wako, ndoa yako itadumu na kuwa kuwa yenye furaha wakati wote.

Jifanyie marekebisho msomaji wangu kwa faida ya uhusiano wako, maana mengi yasemwayo ukiyachekea utafadhaisha moyo wako.

0712 053949
0753 806087


Sunday, December 30, 2012

Digitali kuanza na jiji la Dar es Salaam kesho Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, January Makamba


Na Kambi Mbwana, Dar es Salaam
SERIKALI kwa kupitia Wizara ya Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, imetangaza rasmi kuwa kuanzia kesho Desemba 31, Tanzania itaanza kuingia kwenye mfumo mpya wa urushaji wa matangazo wa kutoka Analogy kwenda kwenye Digitali.
Taarifa ya Naibu Waziri, January Makamba, ilisema kuwa uamuzi huo unatokana na kurejea tangazo lao la Februari 23 mwaka huu juu ya usitishwaji wa matangazo ya televisheni kwa kutumia teknolojia ya analojia kwenda teknolojia ya dijitali.

Makamba alisema maandalizi ya kuzima mitambo ya analojia kuanzia 31 Desemba 2012 yamekamilika kwa mujibu wa makubaliano ya nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Hata hivyo, serikali ilitangaza kuwa uzimaji wa mitambo ya analojia utafanyika kwa awamu kama ifuatavyo, ikianzia na jiji la Dar Es Salaam-31 Desemba, Dodoma & Tanga, Januari 31, Mwanza Februari 28, Moshi & Arusha Machi 31,  wakati Mbeya itakuwa ni Aprili 30.
“Tumeamua kuanza kuzima mitambo hiyo kwa Jiji la Dar es Salaam kwanza ili kutoa fursa kwa makampuni yenye leseni kusimika mitambo ya utangazaji wa dijitali katika mikoa mingine, huku tukiamini kuwa makampuni hayo yamejipanga kukamilisha usimikaji wa mitambo hiyo katika mikoa minane katika miezi minane ijayo.

Mitambo ya analojia itakayozimwa kesho ni ile iliyopo Kisarawe na Makongo. Vituo ambavyo siku ya tarehe 1 Januari 2013, vitapaswa kuanza kutangaza matangazo kwa mfumo wa dijitali ni TBC1, ITV, EATV, Channel 10, StarTV, DTV, CapitalTV, TumainiTV, ATN, MlimaniTV, C2C, CTN, CloudsTV na Efatha,” alisema.

Alisema Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) inafanya jitihada za kutosha kuhakikisha kwamba makampuni yenye leseni za kusambaza ving’amuzi yanakuwa na ving’amuzi vya kutosha na vingine vimeagizwa ili kukidhi mahitaji ya baadaye na vile vilivyopo sokoni vina ubora unaokubalika.

Vilevile, Serikali kwa kushirikiana na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania itahakikisha kwamba zoezi la uhamaji linafanyika bila usumbufu na kero kwa wananchi. Makampuni yanayouza ving’amuzi yameagizwa yaimarishe huduma kwa wateja wakati wa kuuza ving’amuzi na hata baada ya ununuzi iwapo wananchi watakuwa na matatizo na ving’amuzi.

Zoezi hili la uhamaji ni muhimu sana kwa maendeleo ya nchi yetu. Tutakapokuwa tumekamilisha uhamaji, huduma za mawasiliano na utangazaji zitapanuka na kuwa bora zaidi. Kwa mfano, itawezekana sasa kuangalia televisheni kupitia simu zetu za mikononi.
“Vilevile, itawezekana, kwa bei nafuu kabisa, kwa mtu mwenye uwezo wa kutengeneza vipindi kukodisha chaneli yake na kutangaza vipindi vyake. Vilevile, bei za mawasiliano na utangazaji zitashuka, na tutakuwa tumepiga hatua kubwa kwenye mapinduzi ya teknolojia duniani, ambayo nchi yetu haiwezi kubaki nyuma,” alisema.

Makamba alisema serikali kwa kushirikiana na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania itaendelea kutoa elimu kwa wananchi kuhusu uhamaji huu na kutarajia kupata ushirikiano wa karibu kutoka kwa wadau wa sekta ya utangazaji na wananchi kwa ujumla katika kipindi cha uzimaji wa mitambo ya utangazaji wa televisheni ili kufanikisha zoezi la uzimaji wa mitambo ya utangazaji ya teknolojia ya analojia.

Uhamaji huu hautahusu televisheni za wananchi zinazopata matangazo kupitia madishi (nyungo) (satellite) au nyaya (cables). Hivyo, wananchi wanaopata matangazo kupitia DStv, Zuku, na nyinginezo wataendelea kupata matangazo yao kama kawaida.TAARIFA KWA WAWEKEZAJI WAPYA KATIKA KILIMO CHA MITI YA MBAO, KARATASI NA NGUZO.


Wadau wakiangalia vitalu vya miti

 Fresh Farms & Tours (T), biashara tanzu ya Anesa Co.Ltd (Nyaluke Business Empire); inajishughulisha na upandaji, utunzaji na uendelezaji wa mashamba ya miti ya mbao, karatasi na nguzo-mkoani Iringa.
Vilevile inahusika na uvunaji na usambazaji wa mazao ya miti, (mbao na nguzo za umeme) sambamba na ufugaji.
Fresh Farms ilianzisha programu maalumu, mapema mwaka jana; inayolenga kuwawezesha watanzania wengine kuwekeza katika kilimo cha miti kwa urahisi.
Tayari makumi ya watanzania wamechangamkia fursa hii. Fresh Farms & Tours (T) tunapenda kuwaarifu wale wote wenye nia ya kuwekeza nasi, kuwa kuanzia Februari Mosi, 2013 kutakuwa na mabadiliko ya bei na gharama za uendeshaji kwa mashamba ya miti.
Mashamba tunayoyauza laki sita kwa sasa; bei mpya itakuwa milioni moja; na yale tunayouza laki nane gharama yake itakuwa milioni moja na nusu.
Bei hizi hazitawaathiri wateja wa awali na wale ambao wamekwisha wasilisha oda zao. Fresh Farms & Tours (T) tunaendelea kuboresha huduma, taarifa na usaidizi kwa wote wanaowekeza nasi.
Fresh Farms & Tours (T) tunakutakia heri ya Mwaka mpya wa 2013 na tunakukumbusha ile salamu yetu(motto); "Greening the world and Feeding People".
IMETOLEWA NA:
Albert Nyaluke Sanga, (SmartMind)
Mtendaji Mkuu-Fresh Farms & Tours(T),
(C) 2012

Rutainurwa atangazwa promota bora 2012
Na Kambi Mbwana, Dar es Salaam
SHIRIKISHO la Ngumi la Kimataifa (IBF) katika bara la Afrika, Ghuba ya Uajemi na Mashariki ya Kati limemtamngaza Lucas Rutainurwa wa Kampuni ya Kitwe General Traders ya jijini Dar es Salaam kama Promota wa mwaka 2012.

Akitangaza uamuzi huo, Rais wa shirikisho hilo, Onesmo Ngowi, alisema Ruinurwa alifanikisha Watanzania wawili kuwa mabingwa wa IBF katika bara la Afrika, Ghuba ya Uajemi na Mashariki ya Kati.

Katika harakati zake za kuipa Tanzania sura ya kimataifa katika tasnia ya ngumi za kulipwa Rutainurwa na kampuni yake ya Kitwe General Traders waliandaa mapambano makubwa mawili ambayo yalizidi maandalizi ya mapambano yote yaliyowahi kufanyika Tanzania kwa miaka ya karibuni.

Mwezi April mwaka 2012, Rutainurwa na Kitwe General Traders waliandaa pambano lililowakutanisha mabondia Francis Cheka na Mada Maugo wote wa Tanzania kugombea mkanda wa IBF bara la Afrika, Ghuba ya Uajemi na Mashariki ya Kati katika ukumbi wa PTA jijini Dar-Es-Salaam. Katika mpambano huo bondia Francis Cheka aliibuka kidedea baada ya kumsimamisha Maugo katika raundi ya nane.

Francis Cheka alitetea vyema mkanda wake huo tarehe 26 Desemba jijini Arusha alishinda kwwa points bondia Chimwemwe Chiotcha kutoka nchini Malawi katika pambano lao la raundi 12.

Mwezi wa nane mwaka 2012, Rutainurwa na Kitwe General Traders waliandaa mpambano mwingine kati ya bondia Ramadhani Shauri wa Tanzania na Sunday Kizito kutoka Uganda kugombea mkanda wa IBF katika bara la Afrika.

Katika mpambano huo bondia Ramadhani Shauri wa Tanzania alimsimamisha Sunday Kizito kutoka Uganda katika raundi ya 9 na kutangazwa kuwa bingwa mpya wa IBF.

Kupatikana kwa mabingwa hao, kumeifanya Tanzania kuwa nyumbani kwa mabingwa wawili wa IBF na hivyo kuiweka nchi hii katika ngazi moja na chache duniani hususa katika bara la Afrika zikiwemo Afrika ya Kusini, Ghana, Morocco, Algeria na Cameron.

Umasikini wa Handeni waumiza wengiWakazi wa moja ya vijiji vya wilaya ya Handeni kama walivyopigwa picha na Handeni Kwetu hivi karibuni.Na Mwandishi Wetu, Handeni
WAKAZI wa wilaya ya Handeni mkoani Tanga wametajwa kuishi kwa umasikini unaofikia 80%, huku watu hao wakiishi kwa kipato cha sh 1000 kwa siku hali inayosababisha kuwa na maisha duni kutokana na kutotumika vyema fursa za kiuchumi zilizopo.
Hayo yamebainishwa na juzi na Katibu Tawala ya Wilaya hiyo John Tike, wakati akisoma risala ya uzinduzi wa mradi wa mafunzo ya ujasiriamali kwa vijana wa Moto wa Nyika, unaofadhiliwa na Shirika la Kazi Duniani ILO, kupitia asasi ya kiraia maendeleo ya jamii (CDMT).
Alisema idadi hiyo ni kubwa  kwa wananchi wa kawaida kupata kipato hicho hali inayosababisha kurudisha nyuma kasi ya maendeleo na umaskini kutawala kutoka na kukosa kipato cha kuweza kujikimu kwa familia.
“Tukiwatumia vijana hawa vizuri katika mradi huu wataweza kuleta ushindani wa maendeleo katika wilaya hii, ikiwa tu watajituma kwa lengo la kuleta mabadiliko kwani wao ndio chachu ya mabadiliko nchini,” alisema Tike.
Tike alisema ikiwa mradi huo watauzingatia wataweza kuboresha maisha yao na yafamilia zao kwa ujumla pia tatizo la ajira litapungua kwa kiasi kikubwa kwani sasa watakuwa wamepewa elimu ambayo watahitajika kuifanyia kazi baada ya hapo.
Nae Kaimu Mkurungezi wa Wilaya hiyo Julius Mhando alisema kuwa moja ya vipaumbele katika Halimashauri hiyo ni kuhakikisha kipato cha mtu mmoja mmoja kinakuwa kutoka 1000 ya sasa hadi kufika 3000 kwasiku .
Alisema katika kulitekeleza hilo wameanda mpango wa jamii shirikishi kwa kuunda vikundi vya watu 10 hadi 20 na kubuni mradi watakaoweza kuuendesha na Halimashauri kuwawezasha ufadhili wa mradi huo ili kujiletea maendeleo.
“Tunachokifanya ni kuunda vikundi vya nguvukazi na kuviweka pamoja  kisha kuwatafutia ufadhili wa vitendea kazi kama ni kilimo tunawatafutia pembejeo za kilimo na eneo la kulima chini ya usimamizi wa maofisa ugani,” alisema Mhando.

Vifo 5 vya wasanii vilivyotikisa Tanzania 2012Marehemu Steven Kanumba

Na Kambi Mbwana, Dar es Salaam
HII ni Jumamosi ya mwisho kabla ya mwaka huu kumalizika na kuuanza mwaka mpya wa 2013. Ni mwaka uliokuwa na matukio mengi katika sekta karibia zote.
Sharomillionea kabla ya umauti wake
 
Sio kisiasa, kimichezo na kiutamaduni. Pande zote hizo zimeguswa na matukio ambayo kwa kiasi Fulani yaliumiza watu na kuwaacha njia panda kwa kiasi kikubwa.

Hapa nitaelezea japo kwa ufupi matukio ya kisanaa na burudani hasa ya vifo yaliyotokea kwa mwaka huu, ambayo kwa kiasi kikubwa yalitikisa katika viunga hivyo nchini.

 Mariam Khamis, enzi za uhai wake

Yalichanganya kiasi kwamba hadi sasa, ukimuuliza mtu anayefuatilia sanaa nini anakumbuka kwa mwaka huu, ni wazi atakwambia misiba isiyopungua mitano ya wasanii wetu.

Misiba ambayo imeacha pengo kubwa. Watu bado wanaendelea kulia na kuumizwa na misiba hiyo. Tena misiba mingine mitatu imetokea ndani ya kipindi cha mwezi mmoja ule wa Novemba.

Tuanze na msiba wa kwanza uliogusa watu wengi na kulifanya jiji zima litetemeke. Kila mdau wa sanaa aliumia. Si mwingine, bali ni msiba wa Steven Kanumba, uliyotokea nyumbani kwake Sinza Vatcan, jijini Dar es Salaam, Aprili 7.

Kifo cha msanii huyo wa filamu hapa nchini kilihuzunisha wengi. Siku ya Aprili 8, takribani vyombo vya habari vyote viliripoti msiba huo na kufanyia mwendelezo katika kipindi cha zaidi ya siku 30.

Msiba huo inadaiwa ulitokana na ugomvi wa kimapenzi kati yake na msanii mwenzake Elizabeth Michael, maarufu kama (Lulu), ambaye hadi leo yupo rumande.

Mwili wa Kanumba uliagwa katika viwanja vya Leaders Club, kabla ya kuzikwa makaburi ya Kinondoni, huku msiba wake ukivunja rekodi kutokana na kujaza watu wengi.

Jiji zima lilifurika watu. Tax zilifanya kazi pamoja na bodaboda zilizobeba watu kuwatoa sehemu moja kwenda nyingine, hasa wale waliokuwa na haraka ya kufika eneo la tukio.

Kwa mwaka huu, msiba wa Kanumba ndiyo uliyokusanya watu wengi kwa mara moja, hasa kutokana na umahiri wake katika kazi, akicheza filamu nyingi zinazopendwa hadi leo.

Kanumba tayari alishaanza kuvuka nje ya mipaka ya Tanzania kwa kucheza filamu zaidi ya tatu za Kimataifa, ikiwamo ile ya Dar to Lagos.

Baada ya msiba huo kupoa na watu kuendelea na maisha ya kawaida, mwishoni kabisa mwa mwaka huu, msiba mwingine ulitokea katika tasnia ya taarabu, Mariam Khamis kupoteza maisha.

Mwanadada huyo aliyekuwa anafanya kazi na TOT Taarab, chini ya Malkia wa Mipasho Tanzania, Khadija Omari Kopa, alifariki kutokana na matatizo ya uzazi na kuacha kichanga.

Mwanadada huyu alizikwa katika makaburi ya Magomeni Ndugumbi, ikiwa ni siku moja tu baada ya kifo chake. Kutokana na imani ya dini yake ya Uislamu, mwimbaji huyo alizikwa mapema.

Msiba wa Mariam uligusa watu wengi katika tasnia hiyo ya taarabu, wakijitokeza watu wengi wa kushiriki mazishi yake. Hata hivyo, bado hajaweza kufikia hata robo ya watu waliomzika marehemu Kanumba.

Msiba wa Mariam Khamis ulikuwa mzito kwa wadau wa taarabu hapa nchini, ukizingatia kuwa alikuwa na mashabiki waliopenda kazi zake alipokuwa kwenye kundi hilo linalomilikiwa na Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Wakati watu wanaendelea kutafakari maisha ya sanaa na wasanii hapa nchini, wadau walishtushwa na taarifa za msiba wa msanii wa zamani wa Kaole, Khalidi Mohamed, maarufu kama Mlopelo, kilichotokea Novemba 23.

Msiba wa msanii haujatingisha sana, labda ni kwasababu hakucheza nafasi zinazokaa kwenye fikra za watu kichwani au maisha ya Kaole Sanaa Group yalivyokuwa yakishuka kwa kasi.

Ilikuwa hadi mtu amuelezee sana ndio mtu akumbuke sura yake au kumuona kwenye picha yake. Hata hivyo pengo lipo, maana kila mtu ana umuhimu wake katika jamii.

Msiba wa Mlopelo bado ukiwa mbichi, taarifa za kifo cha John Maganga nazo zilisikika na kuzidi kuwaacha watu kwenye maswali mengi wakiangalia namna gani habari hizo zinakuwa nyingi kwa wasanii.

Taarifa za kifo cha Maganga zilichanganya watu wengi, tangu Novemba 25, wakipishana siku moja, ukingatia kuwa msiba huo ingawa haujafikia mshtuko wa Kanumba, ila wengi walimjua na kuheshimu kazi zake za sanaa hapa nchini.

Moja ya kazi aliyocheza marehemu Maganga ni ile ya Mrembo Kikojozi iliyofanya vyema katika tasnia hiyo ya filamu Tanzania.

Maganga alizikwa makaburi ya Kinondoni, lakini siku aliyokuwa anazikwa, mwingine ulitokea, huu ukiwa mkubwa zaidi kwa wasanii na wadau wa sanaa kwa ujumla.

Msiba huu ulikuwa ni wa Hussein Mkiety, maarufu kama Sharomillionea, uliyotokea Novemba 27 mwaka huu. Kijana aliyeibadilisha kabisa soko la sanaa ya vichekesho. Wengi walizoea kuigiza wamevaa vinyago.

Lakini ujio wake ukawa na matunda zaidi. Mwonekano wake wa usafi zaidi, lakini bado alichekesha. Ni kazi nzuri. Marehemu Sharomillionea alikufa kwa ajali ya gari wilayani Muheza na kuzikwa katika makaburi ya kijiji chao cha Lusanga, wilayani humo.

Ukitaka kupanga misiba iliyogusa hisia za wengi, basi huu wa Kanumba ulishika nafasi ya kwanza na Sharomillionea akishika namba mbili, ingawa utaratibu huu ni mchungu zaidi, maana kiubinadamu huwezi kufananisha kupendeza kwa misiba.

Handeni Kwetu ilikuwapo katika mazishi ya msanii huyo wa vichekesho aliyeliza wengi mkoani Tanga na Tanzania kwa ujumla, huku umati wa watu ukifunga katika mtaa mzima nyumbani kwa Sharomillionea.

Pamoja na vifo vya wasanii hao, kazi zao, uwezo wao utaendelea kukumbukwa na wengi, huku kazi iliyobakia ni kuwaombea kwa Mungu ili wakapumzike kwa amani.

0712 053949
0753 806087

Saturday, December 29, 2012

Pole sana


Rais Jakaya Mrisho Kikwete akimjulia hali  Padri, Ambros Mkenda wa Kanisa Katoliki la Mpendae mjini Zanzibar anayeuguza majeraha katika taasisi ya mifupa ya Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (Moi) jijijini Dar es salaam leo, baada ya kupigwa risasi sehemu za mdomoni na watu wasiojulikana. Picha na MpigaPicha wetu.

Simba wapigwa 3-0 na Tusker leo Taifa


Kiungo wa Simba, Mussa Mudde, akijaribu kupiga shuti mbele ya mchezaji wa Tusker ya Kenya, katika mchezo wao wa kimataifa wa kirafiki uliopiga leo katika Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam. Katika mchezo huo, Simba walipigwa bao 3-0.

Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
KOCHA Mpya wa Simba, Mfaransa Patrick Liewig, aliyetarajiwa kuwapo uwanjani wakati kikosi hicho kilipomenyana na Tusker FC katika mchezo wa kirafiki kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam ameshindwa kutokea uwanjani hapo na kuwaacha midomo wazi mashabiki wa timu hiyo.

Awali katika taarifa yake, Simba ilidai kwamba Liewig angetambulishwa rasmi kuinoa timu hiyo wakati wa mchezo huo, lakini kukosekana kwake ni jambo lililowaacha njia panda mashabiki wa timu hiyo waliofurika kwenye kumshuhudia kocha wao mpya.

Mechi hiyo ambayo ilitarajiwa na mashabiki wa timu hiyo kwamba watashuhudia kikosi kamili kikishuka dimbani ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya duru la pili la Ligi Kuu Tanzania Bara itakayoanza mwezi ujao, badala yake ni kikosi B cha timu hiyo ndicho kilichoanzishwa.

Tusker FC ambao siku kadha zilizopita waliinyuka Yanga bao 1-0, waliendeleza makali yao na kuzichapa timu za hapa nchini baada ya kuinyuka Simba mabao 3-0 katika  mchezo wa kirafiki uliofanyika kwenye dimba la Taifa, Dar es Salaam jana.

Mabao mawili ya Jesse Were na moja la Fredrick Onyango yalitosha kuitoa kimasomaso Tusker katika mchezo ambao mashabiki wa Simba walishindwa kupata burudani kutoka kwa nyota wao wa kimataifa kutokana na kutokuwapo katika mchezo huo.

Katika mchezo huo, Simba ilianza kumtumia tena kiungo wake mshambuliaji, Haruna Moshi 'Boban', aliyeingia kipindi cha pili kujaribu kuweka mambo sawa, lakini mambo yaliendelea kuwa magumu kwa kikosi hicho cha Wekundu wa Msimbazi.

Boban alicheza mechi hiyo akitokea kwenye adhabu ya kufungiwa mechi kadha za duru la kwanza la Ligi Kuu Bara kwa madai ya kwamba ni utovu wa nidhamu.

Kama timu tumeona hilo sio tatizo na kwamba kocha wetu mtu atatua hapa nchini Jumatatu. Kuhusu wachezaji wengi, Okwi (Emmanuel) na kipa wetu Abel Dhaira na Sunzu (Felix) watatua hapa nchini kesho (leo).

Kuhusu wale wachezaji waliokuwa kwenye timu ya taifa, Kapombe (Shomari), Ngassa (Mrisho) na wengineo watajiunga rasmi na timu Jumatatu.

Katika mchezo wa jana, Simba ilijaribu kufanya mabadiliko kadha ya kuwaingiza wachezaji wake, Boban, Edward Christopher, Nassor Chollo, Emily Isyaka, Salum Kinje, Jonas Mkude na Ramadhan Singano, lakini hakukuwa na mabadiliko yoyote na hivyo hadi mwisho wa mchezo, Simba ilikubali kipigo.

Simba: William Mwete, Haruna Shamte, Paul Ngalema, Hassan Hatibu, Komain Keita, Mussa Mudde, Haroun Athuman, Abdallah Seseme, Abdallah Juma, Ramadhan Chomo, Kiggy Makassy.

Tusker FC: Samwel Odhiambo, Luje Ochieng, Jeremiah Bright, Mana Odhiambo, Joseph Shikokoti, Khalid Aucho, Edwin Ombasa, Fredrick Onyango, Jesse Were, Robert Omonuk. Refa: Hashim Abdallah kutoka Dar es Salaam.

LinkWithin

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...