Na, Albert Sanga, Iringa
Wiki iliyopita nilifika katika
moja ya mifuko ya pesheni ili kujiandikisha kwa ajili ya utaratibu wa kujiwekea
akiba kwa mpango wa kuchangia kwa hiari. Baada ya kutoka katika ofisi za mfuko
huo wa pesheni nikiwa na fomu na makabrasha mengi nikakutana na mtu mmoja
ambaye maongezi kati yangu na yeye ndiyo yaliyonipelekea kuandika makala hii.
Mjasiriamali Albert Sanga, pichani.....
Rafiki yangu huyu ambaye ni
mfanyakazi alipigwa na bumbuwazi sana kuona ninaeleza habari za mfuko wa jamii.
Swali lake kubwa lilikuwa ni hili, “Je, mifuko ya hifadhi ya jamii inahusika na
wajasiriamali?” Haraka haraka nikabaini tatizo lake ya kuwa anafahamu kuwa
mifuko ya kijamii ni kwa ajili ya wafanyakazi walioajiriwa ama na serikali au
na mashirika na makampuni makubwa pekee.
Kutoka na maarifa na ufahamu
nilionao kuhusu mifuko hii ya hifadhi ya jamii; nilipata wasaa mzuri sana wa
kumuelekeza rafiki yangu huyu kwa kina kuhusu mifuko ya hifadhi ya kijamii na
namna inavyowagusa watanzania wote bila kujali ikiwa wapo serikalini, kwenye
sekta binafsi ama katika sekta isiyo rasmi.
Wajasiriamali ni sehemu ya
nguvu kazi ya jamii. Kile kinachowapata wale walioajiriwa kwa maana ya kuchoka
kiumri na kiafya, kutakiwa kupumzika baada ya miaka mingi ya kazi pamoja na
maandalizi ya maisha ya baadae; vivyo hivyo kinawahusu pia wajasiriamali.
Ndio maana baada ya kumaliza
mazungumzo na rafiki yangu huyu nikabaini kuwa ipo haja nishirikishane na
wajasiriamali wenzangu dhana nzima kuhusu umuhimu wa mifuko ya hifadhi ya jamii
na umuhimu wa mjasiriamali kujiandaa kustaafu katika ujasiriamali.
Ni vema tukafahamu kuwa mifuko
ya hifadhi ya jamii ina histoia ndefu nchini Tanzania. Awali kulikuwepo na
mifuko isiyo rasmi ya hifadhi ya Jamii (Informal safety nets) ambayo ilikuwa ni
vijana kusaidia wazee ama ukoo kusaidiana.
Kuanzia mwaka 1942, wakoloni
wakaja na utaratibu rasmi ambapo GEPF ilikuwa ya kwanza ikifuatiwa na NPF
(NSSF), 1964, PPF-1978, PSPF-1999 kwa kutumia shera ya mifuko ya hifadhi ya
jamii ya mwaka 1954. Sheria hizo za mifuko zilikuwa na utaratibu wa kisekta.
Lakini mwaka 2008 kuliundwa
mamlaka ya udhibiti wa mifuko ya hifadhi ya jamii ambapo utaratibu wa kuchangia
kwa hiari ulianzishwa. Hata hivyo sheria hii ilitanguliwa na sera ya hifadhi ya
jamii ya mwaka 2003.
Lengo la sera hii lilikuwa ni
kuweka mazingira mazuri ya taratibu mbalimbali za hifadhi za jamii, kuruhusu
mwanachama kuhama kutoa mfuko mmoja kwenda mwingine na stahili zake pamoja na
kuanzisha mifumo ya uchangiaji wa ziada kwa hiari.
Ni kutokana na sheria na
taratibu zilizoboreshwa ndipo kumekuwepo na fursa ya Mpango wa uchangiaji wa
Hiari ambapo watu mbalimbali kutoka serikalini, kutoka sekta binafsi na kutoka
katika sekta isiyo rasmi wanapata fursa ya kuwa wanachama katika mifuko hii ya
kijamii.
Hivyo utabaini kuwa
mjasiriamali yeyote anayo nafasi ya kujiunga na mfuko wa Hifadhi ya jamii na
kuanza kujiwekea akiba. Ni muhimu sana wajasiriamali kutafakari kwa kina maisha
ya baadae badala ya kujisemea “Atajua Mungu”. Maisha ya sasa na baadae kwa mjasiriamali
yamo katika maamuzi ya mjasiriamali mwenyewe. Unachoamua leo ndicho
utakachopata kesho.
Nimekuwa nikieleza mara kwa
mara katika chambuzi zangu kupitia safu hii; kuhusu athari za mabadiliko ya
kibiashara kwa wajasiriamali. Nimepata kueleza kuwa biashara za sasa zinahitaji
akili nyingi, ubunifu mwingi na kuona mbali kwa tofauti sana.
Hii ina maana kuwa wewe
mjasiriamali upende ama usipende kuna wakati biashara zinaweza kukoma. Kukoma
huku kuna namna mbili. Mosi ni kukoma mwendo wa kibiashara kutokana na
mabadiliko ya kimzunguko. Hapa ni pale unapojikuta biashara iliyokupa faida
jana leo imegoma na haina faida tena.
Pili: ni kukoma kwa biashara
kwa maana ya wewe mjasiriamali kuishiwa uwezo wa kuendelea na biashara. Kuna
wakati utafiki umri utakuwa umeenda sana, afya inaweza kuwa matatani au akili
yako mjasiriamali kuchoka kabisa; kiasi kwamba hakuna namna isipokuwa kuachana
na biashara.
Jawabu kwa kukoma kwa namba
mosi ni wewe mjasiriamali kubadilisha biashara ama kuingiza mbinu mpya katika
hiyo biashara iliyokoma. Jawabu la kukoma kwa pili ni wewe mjasiriamali
kustaafu. Hapa kwenye kustaafu ndipo ambapo wajasirimali wengi hawajui.
Kimsingi kama ilivyo kwa watu walioajiriwa, ndivyo ilivyo kwa mjasiriamali ya
kuwa kuna wakati utafika na utalazimika kustaafu katika ujasiriamali.
Wakati wafanyakazi hupangiwa
muda wa kustaafu, mjasiriamali unatakiwa ujipangie muda wa kustaafu. Kwa
mfanyakazi; tafsiri ya kustaafu ni pale
ambapo taifa linaona kuwa mtu amelitumikia vya kutosha hivyo yafaa apumzike.
Kwa upande wa wale wafanyakazi
walioajiriwa na serikali ama mashirika, inapofika wakati wa kustaafu walau
mwajiri na serikali wanakuwa wamejiridhisha kuwa huyu mstaafu anayoakiba
itakayomtosha kuishi katika maisha yake yaliyobaki hadi kufa. Akiba hii ndio
kile kinachoitwa mafao na pensheni.
Niseme tu kuwa nafahamu
changamoto inayowakumba wataafu wengi kuhusu pesheni ndogo wanayoendelea kulipwa
kila mwezi baada ya kustaafu; lakini lengo na mpango wa mtu kustaafu kwa sheria
za ajira za nchini ni kumsaidia kuishi maisha mazuri hata baada ya kustaafu
kwake.
Kwa kuwa nia yangu ni
kusemezana na wajasiriamali juu ya hatma yao ya kustaafu; naomba niachane na hayo
ya walioajiriwa bali nijikite kwa wajasiriamali wenzangu. Kama nilivyosema pale
juu ni kuwa katika ujasiriamali kuna kustaafu na kama hutaki kustaafu kwa
hiyari biashara zitakustaafisha kwa lazima.
Swali hapa linalokuja ni hili,
Je, mjasiriamali utaishije ukistaafu? Nimesema kuwa umri wa kustaafu kwa
mjasiriamali anajiamulia mjasiriamali mwenyewe. Unaweza kustaafu ukiwa na miaka
30, 45, 50, 60, 70 au katika umri wowote ule utakaojiamulia wewe mwenyewe.
Kama mjasiriamali ukiamua
kustaafu ukiwa na miaka 30 na tuchukulie umri wa kuishi wa mtanzania ni miaka
60+ (nimetumia kigezo cha ustaafu wa serikalini); ina maana kuwa utakuwa
umebakiza miaka 30 mbeleni. Je, katika miaka 30 ijayo utaishije? Vivyo hivyo
ikiwa utastaafu ukiwa na miaka 40, utakuwa na miaka 20 mbele.
Ukistaafu na miaka 50, utauwa
na miaka 10 mbele. Kubwa ninalotaka mjasiriamali ujiulize ni hili utaishije
ukifika wakati ambao biashara haziendi ama ule mda utakaokua umechoka kiumri na
kiafya kuweza kumudu biashara? Tumeona kuwa wenzetu walioajiriwa huendelea kula
pensheni yao hata baada ya kustaafu, Je, mjasiriamali unampango gani?
Ni vema nizitaje fursa zote
alizonazo mjasiriamali kujiandaa mapema kwa ajili ya kustaafu. Kwanza
mjasiriamali anaweza kuwekeza katika vitega uchumi vya muda mrefu ili vimsaidie
pindi atakaokuwa hawezi tena kufanya biashara (kustaafu).
Pili anaweza kusomesha watoto
kwa lengo la kuja kumsaidia baadae, tatu anaweza kuweka hisa ama kuwa na
biashara katika mifumo rasmi zitakazoweza kumfaa kwa miaka mingi baadae. Fursa
nyingine(ambayo ni ngeni kwa wajasiriamali weng) ni hii ya kuweka akiba katika
mifuko ya hifadhi ya jami
Hata hivyo kwa mazingira ya
ujasiriamali wa kitanzania sio wengi wanaoweza kumudu kuwekeza kenye vitega
uchumi vikubwa vya kuwasaidia miaka na miaka baadae. Pia sio wengi wanaoweza
kuwekeza katika hisa na biashara za mifumo rasmi. Sasa, wajasiriamali wa
kawaida wanafanyaje kujihami na maisha baada ya kustaafu katika ujasiriamali?
Suluhu inapatikana kupitia
fursa ya kujiunga na mifuko ya hifadhi ya jamii. Kwa kuwa mwanachama katika
moja ya mifuko hii inakupa wasaa mjasiriamali hata mwenye mtaji mdogo kabisa
kujiwekea akiba kidogo kidogo kwa ajili ya mafao ya kustaafu kwako.
Taratibu, sera na kanuni za
namna ya kujiunga zinatofautiana kutoka mfuko mmoja hadi mwingine sambamba na
aina ya mafao yanayotolewa. Hata hivyo kuna mifuko ambayo ina mafao mazuri mno
kwa ajili ya wajasiriamali.
Mathalani mifuko hii ina faida
mbalimbali ikiwemo mafao ya ujasiriamali (mtaji) pamoja na mikopo ya kibiashara
kupitia SACCOSS. Mbali na faida za kibiashara mifuko hii inakupa wasaa wa
kutoogopa kuhusu familia na afya yako wewe mjasiriamali kwa sababu wana mafao
ya matibabu, mikopo ya nyumba, mikopo ya samani, mafao ya elimu pamoja na mafao
ya uzazi.
Nitoe wito kwa wajasiriamali
wote nchini mjaribu kutembelea moja kati ya mifuko hii ya kijamii iliyokaribu
nanyi ili kupata maelekezo na namna ya kujiunga. Furaha yangu itakamilika pale
nitakapoona wajasiriamali wadogo na wakubwa wengi iwezekanavyo wakijiunga na
mifuko hii ya hifadhi ya jamii kwa ajili ya usalama wa ujasiriamali wao.
No comments:
Post a Comment