Na Kambi Mbwana, Dar es Salaam
TIMU kama Coastal
Union yenye maskani yake Tanga, ni wazi utaamini kuwa inanufaika kwa kiasi
kikubwa na uwepo wa kiwanda cha saruji kinachojulikana kama Tanga Cement.
Kikosi cha timu ya vijana, Coastal Union
Hii ni kwasababu wote
wanategemeana. Tanga Cement kama kiwanda, kinaweza kunufaika kwa kiasi kikubwa
na uwepo wa Coastal Union.
Timu hii tishio
katika soka nchini na yenye historia kubwa tangu kuanzishwa kwake, inatembelea
basi dogo aina coaster lenye maandishi ya aina mbalimbali, yanayoelezea bidhaa
za kampuni hiyo.
Hii ni kwasababu
kiwanda hicho ndicho kilichonunua basi hilo na kuwapa timu hiyo ya Coastal
Union, maarufu kama ‘Wagosi wa Kaya’.
Hata hivyo, tangu
kukabidhi kwa basi hilo, hakuna msaada mwingine
wanaotoa kwa timu hiyo. Awali
nilifikiri kuwa wao ndio wadhamini wakuu kwa timu hiyo kongwe mkoani Tanga.
Hakika siwezi
kuvumilia, maana licha ya Coastal Union kujitolea kwa kiasi kikubwa kwa kampuni
hii ya saruji ya Tanga Cement, kuwatangaza kila mahali, ila si wadhamini wao.
Ndio hapo ninapoanza
kushikwa na wasiwasi juu ya wadau wetu wa michezo Tanzania. Kwa Tanga Cement,
kama inashindwa kuwadhamini Coastal Union, inataka kudhamini nani?
Wao ndio wanaofanya
kazi kwa pamoja jijini Tanga. Wanategemeana kwa kila kitu. Nilifikiria watu wa
masoko wangeangalia mtaji wa mashabiki na nafasi ya Coastal kuwatangaza
kirahisi.
Coastal wanatoka
Tanga na kuelekea mikoa mbalimbali ya Tanzania, wakitangaza bidhaa za Kampuni
hiyo yenye mafanikio makubwa sokoni.
Sina lengo la
kuwalaumu Tanga Cement wala kulazimisha, ila ni ushauri tu, maana najua nao
wanaweza kunufaishwa zaidi na timu hiyo ya Wagosi wa Kaya katika soka Tanzania.
Huu ndio ukweli. Japo
kuwa wamejitolea wenyewe juu ya basi hilo waliloipa timu hiyo, ila isiwe mwisho
kuwasaidia ama kuwadhamini moja kwa moja.
Nasema hivi maana
timu za mikoani zinakabiriwa na changamoto nyingi mno, hasa ukosefu wa fedha za
kujiendesha.
Ndio maana licha ya
baadhi yao kuwa na wachezaji wenye uwezo wa juu, ila nguvu zao zinaishia
ukingoni, maana hakuna nyota wa soka anayeweza kucheza soka akiwa na njaa, ama
mawazo familia yake.
Timu kama vile Toto
African ya Mwanza, Villa Squad ya Kinondoni, zina njaa ya pesa, ukiacha zile za
jeshi, Azam FC, Mtibwa Sugar na Kagera Sugar zinazomilikiwa na wenye nazo.
Kama hivi ndivyo, ni
wakati wao basi wadau wa mikoani, matajiri kwa kupitia Kampuni zao, hasa Tanga
Cement kuingia makubaliano ya wazi juu ya kuwadhamini Coastal Union ya jijini
humo.
Hii itasaidia mno kuwafanya
wachezaji waonyeshe kiwango cha juu zaidi. Hii itazidi kuwaletea heshima
ukiacha basi waliloipa timu hiyo.
Tangu walikabidhi
gari hilo kwa Coastal Union, wamekuwa wakipata matangazo mengi, hasa kwa kuona
vijana hao wanajulikana na kuheshimika kwa kiasi kikubwa katika soka Tanzania.
Nikiwa kama mdau wa
michezo, ni wakati huu sasa kuwakumbusha juu ya kuwekeza katika michezo,
ukiwapo mpira wa miguu, hasa katika timu ya Coastal Union ya Tanga.
Ni wakati wao sasa
kuingia katika udhamini, badala ya kusaidia, kama walivyojitolea katika
kunununua basi hilo lisilozidi Milioni 50.
Milioni 50 kwa
matangazo haichukui hata mwezi mmoja, kwa kuangalia na gharama zinazohitajika
juu ya biashara hiyo, ila kwa Tanga Cement wao wameweza kujitangaza kwa miaka
miwili sasa kutokana na nembo za bidhaa zao kutembea kila kona kwasababu yaa
mgongo wa klabu ya Coastal Union.
Huu ndio ukweli wa
mambo, maana hakika nimeshindwa kuvumilia, ukizingatia kuwa Tanga Cement wana
kila sababu ya kuidhamini Coastal Union.
0712 053949
0753 806087
No comments:
Post a Comment