https://tpc.googlesyndication.com/simgad/8045142562622600543


Recent Post

Saturday, June 22, 2013

Kigoda ataka wananchi wake watazame mjadala wa maji na kujifunza kero za shida ya maji



Na Mashaka Mhando, Handeni
MBUNGE wa Handeni, Dkt Abdallah Kigoda, amewataka wananchi wa jimbo lake kutazama mijadala inayoendelea ya kuchangia bajeti ya Wizara ya Maji ili wajifunze na kuona kwamba tatizo la maji si la wilaya yake bali ni tatizo la kitaifa.
Abdallah Kigoda, Mbunge wa Handeni

Akizungumza juzi kwenye mji mdogo wa Mkata wakati akizindua kisima cha maji kilichojengwa na taasisi ya Kiislamu ya Afrikanbrunnen ya watu wa Ujerumani, alisema wananchi wa Handeni wasijue kwamba tatizo la maji ni la wilaya yake pekee.

"Wiki iliyopita wabunge wamekuwa wakielezea matatizo ya maji katika maeneo yao kiasi kwamba hawakuipitisha wakataka ikafanyie marekebisho ili ije na suluhisho la upatikanaji wa maji, niliwapigia simu watu wangu tazameni muone siyo sisi tu tunaolilia maji," alisema.



Hata hivyo, mbunge huyo ambaye ni Waziri wa Viwanda na Biashara, alisema wakati akigombea ubunge aliahidi kulitafutia ufumbuzi tatizo la ukosefu wa maji ili aweze kupunguza tatizo hilo kwa wnaanchi wake wilayani humo.

Alisema katika mji wa Chanika, makao makuu ya wilaya hiyo katika kipindi cha hivi karibuni ameweza kufungua visima 19 ambavyo kwa kiasi fulani kimepunguza kero ya maji na hivi sasa anatarajia kuchimba visima vingine maaeneo ya Manga, Kwandugwa na maeneo mengine.

Alisema anaishawishi serikali kufikisha maji kutoka mradi wa mto wami ili yaweze kufika katika mji wa Manga uliopo mpakani na wilaya ya Bagamoyo kusaidia tatizo hilo ikiwemo kuchimba visima katika maeneo mbalimbali kwa kushirikiana na wafadhili mbalimbali.

Awali mmoja ya wafadhili wa taasisi hiyo ya Afrikanbrunnen Bw. Raphael Khalili, alisema mwaka jana walipofika katika eneo hilo la Mkata waliwashuhudia wananchi wakitumia maji ambayo yalikuwa machafu na tatizo la maji eneo hilo lilikuwa ni la kutisha.

Alisema walirudi nchini Ujerumani na walipokaa na ndugu zao na watu wengine walichanga na kuamua kuwachimbia kisima hicho ili kuwasaidia kupunguza tatizo hilo ambapo kisima hicho kitaweza kusaidia watu wapatao 20,000.

Alhaj Mohamed Hassain alisema alifanikisha mradi wa kisima hicho kutoka kwa taasisi hiyo kutokana na kuguswa na tatizo la maji na kutaka kushirikiana na mbunge huyo kusaidia kutatua kero ya maji wilayani Handeni.

No comments:

LinkWithin

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...