https://tpc.googlesyndication.com/simgad/8045142562622600543


Recent Post

Monday, June 03, 2013

Wanakera na usajili wao wa magazetini



SIWEZI KUVUMILIA
Na Kambi Mbwana, Dar es Salaam
NI wazi sasa kila kinachosemwa kwa timu ya Simba na Yanga, basi ni usajili wao, baada ya ligi kumalizika na Yanga kufanikiwa kunyakua Ubingwa kutoka mikononi mwa mtani wao wa jadi.

Picha zikionyesha vikosi vya Simba na Yanga
Baada ya kumalizika ligi hiyo ambayo kwa upande wa Simba kulikuwa na machungu ya aina yake, sasa macho na masikio ya wadau wa soka Tanzania wanaangalia kwenye usajili.

Usajili ambao endapo unatumiwa vyema, basi wachezaji wanaoweza kupatikana ni wale wenye uwezo wa juu na kuzisaidia timu zao na sio wale ambao hata thamani ya mishahara yao haitafanana.

Hapa ndipo ninaposhindwa kuvumilia. Kweli siwezi kuvumilia, maana timu zetu za Tanzania, hasa hizi za Simba na Yanga, mara nyingi usajili wao ni kanyaga twende.

Usajili wa magazetini ambao unafanywa kwasababu ya kuonyesha sifa, hasa kwa kuwachukua wachezaji wasiokuwa na kiwango sahihi. Tena, wakati mwingine mchezaji anayesajiliwa kutoka nje uwezo wake unakuwa mdogo tifauti na mzalendo, yani mchezaji wa Tanzania.

Tunahitaji wachezaji wazuri kwa ajili ya kuendeleza soka letu. Hatuhitaji soka la magazetini, huku tunapoingia kwenye mechi za Kimataifa, walau tupige hatua.

Kwa wachezaji wanaostahili kucheza soka Tanzania kutoka nje ni wanaofanana na uwezo wa aliyekuwa mshambuliaji wa Simba, Emmanuel Okwi au akina Haruna Niyonzima kutoka nchini Rwanda, Hamis Kiiza wanaocheza soka Yanga.

Tuyaseme haya bila kuficha. Kwa mfano, kuna kasumba nyingine ya mtu ambaye hajui mambo ya ufundi, anachukua jukumu la kumsajili mtu bila kufanyia uchunguzi.

Kwa bahati mbaya, habari za usajili wake zinavumishwa na kugusa hisia za watu wengi, hivyo kuleta hatari ya kuangamiza soka letu. Wachezaji kama vile marehemu Patrick Mafisango na Okwi kutokuwapo ndani ya Simba pengo lao limeonekana.

Kwa mfano, msimu wa 2011 na 2012, Mafisango na Okwi waliipatia Simba ubingwa sambamba kuwezesha ushindi wa bao 5-0 dhidi ya Yanga, lakini msimu ulioisha ubingwa umekosekana ndani ya timu yao sambamba na kufungwa bao 2-0 na mtani wao wa jadi.

Hapa tu, utagundua kuwa uwepo wao ndani ya timu ulikuwa na manufaa makubwa. Sitaki kuorodhesha wachezaji ambao kiwango chao si kizuri, ila wanaopewa kufanya usajili wachunge na tabia yao ya kusajili kwa kupitia magazeti.

Tukifanya hivyo, soka letu litaendelea kubaki kama lilivyo. Nitawaona wa maana hasa kwa Sima, wakiendelea kuelemea kwenye soka la vijana kama njia ya kuvuna vijana wenye mfano wa Shomari Kapombe, ambaye kwa sasa amekuwa nyota.

Nani anapinga uwezo wa kijana huyu? Je, hatukubali kuwa wapo wenzake wengi katika Tanzania hii wenye uwezo mkubwa ambao wakitumiwa wataitangaza nchi Kimataifa.

Je, nani anaona usajili wa magazeti ndi kila kitu? Je, hatuoni huu ni wakati wetu sasa kufanya kazi zetu kwa mipango, usajili wenye tija kwa Taifa badala ya kuchukua makapi nab ado tunayafanyia matangazo makubwa kwenye media ili jamii ione imelamba dume?

Nayasema haya, huku nikiamini pia si mbaya pia kwa timu za Tanzania, zikilinda mikataba kwa wachezaji wazuri kwenye vikosi vyao kwa ajili yaa kendelea kubaki kwao.

Vinginevyo siwezi kuvumilia hata kidogo. Maana, kila siku tutaendelea kupiga porojo, kurushiana makombora na wenzetu nje ya nchi wanazidi kuchanja mbuga.

Huu si wakati wa kufanya usajili wa magazeti. Ni wakati wa kuona kila anayepewa jukumu la kuongoza, basi anashiriki kwa namna moja ama nyingine kuweka mikakati imara kwa sehemu husika.

Nadhani kwa kulisema hili, viongozi au mabosi wa Simba na Yanga, akiwamo Hans Pope, watajua namna gani ya kufanya kwa ajili ya kukuza soka letu, maana usajili ndio kitu muhimu ndani ya klabu za soka kwa ajili ya kupatikana soka lenye ushindani, lenye ubora na viwango.

0712 053949
0753 806087

No comments:

LinkWithin

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...