Na Albert Sanga, Iringa
Nafahamu kuwa wengi
kama sio wote tunakubaliana kuwa fedha zina umuhimu mkubwa sana katika maisha
ya mtu, tunachotofautiana ni imani kuhusu fedha. Mitazamo kuhusu fedha ndio
inayoamua kiwango cha fedha alichonacho kila mmoja. Hii ina maana kuwa kila mtu
anamiliki kiwango cha pesa sawa sawa na imani ama mtazamo wake kuhusu fedha.
Albert Sanga, Mjasiriamali
Kimsingi ni kwamba
zipo imani zinazosapoti watu kuwa na fedha za kutosha na zipo imani na mitazamo
inayozuia watu kuwa na fedha ama inawafanya waishi maisha ya kupungukiwa
nyakati zote! Imani na mitazamo hii kimsingi huzalishwa kutokana na malezi, utamaduni na mazingira. Mtazamo wa
mtu kuhusu fedha tunaita, “Money blue print” (Kila nitakapotumia neno hili la
kimombo litakua limebeba maana hii).
Mathalani, ukiwa
mikoa ya Nyanda za juu kusini kuna mivumo, ‘myths’ kuhusu kabila la Wakinga
(bahati nzuri na mimi ni Mkinga). Watu wengi kutoka kabila hili wanasifika sana
kwa kufanya biashara na matajiri wengi katika mikoa hii ni Wakinga. Pamoja na
sifa hii, Wakinga wanatajwa kuwa ni mabingwa wa kutumia ushirikina katika
biashara zao.
Hivyo utabaini kuwa
kwa mtu anaewatazama wakinga na utajiri wao, akiamua kuchukua ‘myth’ hii; basi
ataunganisha fedha na uchawi. Hii itakuwa kichwani kwake kwamba, ili uwe na
fedha nyingi (tajiri) ni lazima uwe mchawi na hii ndio itakuwa, ‘Money blueprint’
yake.
Mfano mwingine
unawahusu rafiki zangu Wachaga. Wapo watanzania wengi ambao wanaamini mchaga
yeyote anayetajirika ni lazima awe ametumia wizi ama udhulumaji. Kwa watanzania
wenye mtazamo kama huu, ni wazi kuwa
wanapoitazama fedha wanaiunganisha na wizi ama udhulumaji. Kwao hawa hii ni
‘blue print’ yao.
Ukiiangalia mifano
hiyo yote miwili utabaini kuwa ni mitazamo
inayozuia mtu kuwa na fedha nyingi (hata kama mwenye mtazamo huo akiwa hajijui).
Na hii ni kwa sababu watu wengi hawapendi uchawi, hawapendi wizi na wanauchukia
ujambazi. Kwa kuwa wameunganisha fedha na uchawi, wizi na ujambazi,
‘automatically’ wataichukia fedha bila hata kujijua ikiwa wanaichukia fedha!
Matokeo ya chuki zao dhidi ya fedha yanadhihirika katika kiwango cha fedha
wanazomiliki. (Nakuthibitishia eidha wanakuwa ni masikini ama ni watu wenye
kuhangaika milele kwa kupata fedha isiyowatosha-hata kama wawe ni wenye vyeo vikubwa!).
Ingawa mtu kuwa na
fedha nyingi sio kipimo cha utajiri lakini ukweli ni kwamba hakuna mtu aweza
kusema ni tajiri ikiwa hana fedha (hata kama iwe katika maumbo mengine). Kwa
maana hii tukiongelea fedha kwa namna moja ama nyingine tunakuwa tukiiunganisha
na utajiri (ingawa kuna watu hawataki kabisa kuwa matajiri-hawa nao blueprint
zao ndivyo zinavyowaelekeza!).
Kiuhalisia ni kuwa
utajiri ama umasikini wa mtu haupo katika wingi ama uchache wa mali au fedha anayomiliki.
Tofauti kubwa iliyopo kati ya masikini na matajiri ni ile ya kifikra. Masikini huwaza
kimasikini, tajiri huwaza kitajiri. Utajiri ama umasikini wa mtu huanzia katika
fikra na mitazamo yake.
Kwa mfano, fikra za
kitajiri huamini kuwa ukiwa na fedha ya
kutosha utaishi kwa furaha, amani na upendo kwa wengine hivyo utatimiza agizo
la Mungu kuwa mpende jirani yako kabla ya kumpenda Mungu. Fikra za kimasikini
zitajinenea hivi, “sio vizuri kuwa na fedha nyingi, kwa sababu hautampendeza
Mungu”
Kama alivyosema,
Mchungaji Pepe Minambo kutoka Kenya ndivyo na mimi ninavyoamini kuwa ni vigumu
kwa masikini kuingia mbinguni. Sababu za uwezekano wa masikini kuikosa Mbingu
zipo wazi; kwanza masikini ni mlalamikaji na mnung’unikaji (na Mungu hapendi
walalamishi na wanung’unikaji), masikini ana wivu na masikini hajiamini.
Msomaji usisahau
kuwa hapa siongelea masikini wa roho aliowasema Yesu Kristo, ila naongelea
masikini wa fikra chanya. Ni vema tukafahamu kwamba, tajiri huwa tajiri kabla
hajamiliki kitu na masikini huwa masikini kabla ya kudhihirika kwa hali yake;
kwa vile umasikini na utajiri vyote ni matokeo ya kuwaza.
Vile vile nigusie
kundi maarufu sana la uchumi wa kati “middle class”. Hawa ni watu ambao hawana
fedha nyingi na wala sio masikini kabisa. Kundi hili ni sumbufu sana kifikra na
ndilo ambalo husambaza fikra hasi kuhusu fedha. Kundi hili, hupenda kuridhika
mapema na hupendelea sana usalama “comfort zone”.
Kinachosikitisha
zaidi ni kwamba kuna wanasiasa wanadai
kupigania uwepo wa watanzania wengi katika kada hii ya watu wa kati; wakati
mfumo na uchumi wa dunia unawafuta kwa kasi kubwa. Mfumo wa uchumi wa dunia
uliopo (na utakaoendelea kuwepo kwa
mamia ya miaka ijayo) unawabeba watu wa aina mbili tu, masikini na
matajiri.
Ni ama uchague kuwa
masikini au uchague kuwa tajiri. Kazi ni kwako msomaji kama unaamini na
kutamani kuwa mtu wa kada ya kati. Kwa wanaofuatilia duru za kiuchumi kwa
umakini hawashangazwi na hali iliyopo ya matajiri kuendelea kuwa matajiri na
masikini kuzidi kuwa mafukara, sio Tanzania tu lakini ni katika dunia nzima.
Kwa kuwa ninaongelea kuhusu imani kuhusu fedha ni
vema nikagusia imani iliyochimbika miongoni mwa baadhi ya wakristo. Katika
Biblia kumekuwa na maandiko ambayo, tafsiri (nasisitiza kuwa ni tafsiri kwa
sababu Biblia ipo ‘perfect’) zake zimekuwa na ‘Money blue print’ ambazo
hazisapoti mtu kutafuta na kunia kumiliki fedha. Nitataja maandiko mawili; la
kwanza ni lile lisemalo, “Huwezi kumtumikia Mungu na mali” na la pili ni lile
lisemalo, “Kupenda fedha ni shina la maovu yote duniani”.
Si kusudio langu kuhubiri
(ingawa nina karama ya kuhubiri pia) lakini nifafanue kidogo kuhusu maandiko
hayo. Neno mali (ama Biblia zingine zimeandika fedha) limetafsiriwa kutoka
katika neno ‘Mamos’ linalomaanisha ‘roho inayotawala mali’. Kwa maana hii,
kimantiki ilitakiwa kueleweka kuwa, “Huwezi kumtumikia Mungu na roho
inayotawala mali”.
Kuhusu fedha na
maovu ninachoamini ni kuwa ikiwa pesa itatumika vibaya itazalisha maovu na
ikiwa itatumika vema inaleta tija. Ni kama kisu kilichopo jikoni, kinaweza kukata
mboga na kinaweza kutumika kuua ama kumdhuru mtu. Kusema kisu ni chanzo cha
‘mauji yote ya jikoni’ itategemea umeangalia upande upi wa matumizi!
Kwa upande wa malezi
na utamaduni wetu nako kumezalisha imani na mitazamo mingi iliyo hasi kuhusu
fedha. Kwa mfano; jamii zetu zinaamini kuwa wanaume ndio wanastahili kuwa na
fedha kuliko wanawake. Ndio maana mwanamke anapotajirika migogoro hutokea
ikilinganisha na mwanaume anapotajirika.
Wanawake wengi
waliomatajiri utasikia habari kuwa ama
hajapata kuolewa, ama aliolewa akaachika ama ndoa aliyonayo ina mgogoro mkubwa.
Unajua tatizo linapoanzia? Nitaeleza hapa chini, lakini kabla nataka niseme
jambo hili; imani ya jamii kuhusu fedha
ndio husababisha wanawake wanaotajirika kuonekana kuwa hawapo sawa.
Katika familia
nyingi watoto wanapokua, huwa kuna mazoea ya kuomba fedha kwa mama. Mama zetu
mara nyingi tukiwaomba fedha huwa wanasema kauli kama hii, “Msubiri baba yako,
akija ndio atakupa fedha”. Kinachojengeka katika akili ya mtoto ni kuamini
kuwa, wanawake hawana na hawastahili kuwa na fedha! Hii ni ‘Money blueprint’
hatari sana na imechangia sana wanawake wengi kuwa nyuma kujitafutia fedha na pengine
kutajirika.
Kutoakana na
‘blueprint’ hii ndio maana huwa sishangai ninapoona mabinti wakijiorodheshea
vigezo vya wanaume wanaowataka; katika vigezo hivyo hawaachi kuweka, ‘mwenye
kazi nzuri (moja kwa moja atakuwa na fedha)’, ‘mwenye fedha za kutosha’, ‘aliye
maarufu (umaarufu kwa kiasi fulani huleta fedha)’ na vigezo vya kufanana na
hivyo.
Zipo imani na
mitazamo mingine mingi ambayo imewaathiri watu wengi bila kujijua na
imesababisha kuishi katika maisha ya uchache badala ya utele wa kifedha. Kwa
mfano wapo watu ambao wanaamini kuwa haiwezekani watu wote tukawa matajiri.
Wanachosahau kujiuliza ni hiki, “Ni wapi imeandikwa kwamba wewe fulani, bin
fulani utakua masikini?” Kama dunia inaendelea kuzalisha matajiri, kwa nini
usiwe mmoja wao na badala yake unajivisha haki ya umasikini?
Wapo watu wengine
ambao wanaamini kuwa matajiri ni mabahiri; kwao hawa utajiri ni ubahili na
wengine wanajiridhisha kuwa fedha haiwezi kununua furaha. Ukweli ni kwamba
matajiri wengi wana nidhamu ya matumizi ya fedha (ndio maana wanazidi
kutajirika) na uhalisia ni kwamba ingawa fedha sio kigezo pekee cha mtu kuwa na
furaha lakini siku za masikini hutawaliwa na huzuni kutokana na kutopata
anavyovitaka. Kupata unachokitaka ni moja ya mihimili ya furaha. Na mtu una
uwezekano wa kupata unachokitaka kwa sehemu kubwa ikiwa utakuwa na fedha
Msingi mwingine wa
kupata fedha (na mafanikio mengine yeyote) ni kuzingatia kile unachokipenda na
sio kile usichokipenda (focus on what you want and not on what you don’t want).
Hii inatokana na kanuni mbili za kiubongo na kiasili; ambazo ni hizi(Nitatumia
kiombo kidogo).
Kanuni ya kwanza
inasema“What you focus expands-yaani unachozingatia hukua” na ya pili inasema
“Your eyes will see what your mind has prepared to see-macho yako yataona kile
ambacho fikra zake zimejiandaa kukiona”. Iko hivi, ukitaka fedha zingatia utele
(namna ya kuongeza fedha) na usizingatie uchache (kuishiwa, kufilisika)!
Nihitimishe makala
haya kwa kudurufu mambo machache. Mosi
ni kuwa kila mtu anayo nafasi sawa
(equal channce) ya kuwa na fedha za kutosha kumpa uhuru wa kiuchumi. Pili
hakuna raha wala sifa ya kuendelea kuwa masikini, kwa sababu masikini ni mzigo
kwa dunia. Masikini na umasikini wake hata awe ni mtakatifu na mwema kiasi gani
ni kwamba anaitesa dunia (kwa sababu anahitaji kusaidiwa). Tajiri (ama niseme
mwenye fedha za kutosha) hata kama ni mchoyo ama bahiri bado ni msaada kwa
dunia (kwa sababu anajisaidia).
Pamoja na haya yote,
sio kusudio langu kuwabeza masikini na tena sio kusudio langu kuwataka
watanzania wote wawe matajiri (japo ikiwa hivyo nitafurahi pia-manake nami
nitakuwa mmoja wa matajiri); lakini ninataka kila mmoja apokee changamoto ya kutamani kuwa na uhuru wa kifedha na
kiuchumi. Na hili linawezekana ikiwa mitazamo na imani za wengi kuhusu fedha
zitabadilika na kuwa zinazosapoti badala ya kuvuruga nafasi ya mtu kupata
fedha.
Kila mtanzania
anastahili ushindi wa kifedha!
0719 127 901, stepwiseexpert@gmail.com
No comments:
Post a Comment