https://tpc.googlesyndication.com/simgad/8045142562622600543


Recent Post

Friday, May 31, 2013

Ripoti ya kuteswa Mhariri Mtendaji wa New Habari 2006 Ltd, Absalom Kibanda



Abslom Kibanda.

    UTANGULIZI:Usiku wa Jumanne ya Machi 5 kuamkia Machi 6, 2013, Mhariri Mtendaji wa New Habari (2006) Ltd, ambaye pia Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Absalom Kibanda alivamiwa na kujeruhiwa vibaya akiwa nje ya lango la kuingilia nyumbani kwake Mbezi Juu, Dar es Salaam.Tukio hilo liliishtua na kutikisa taifa kwa kiwango kikubwa si tu katika tasnia ya habari nchini, bali pia jamii kwa ujumla hasa baada ya aina ya utekaji, utesaji na usiri uliotumika katika kufanikisha uhalifu huu kufanana kwa karibu na tukio lilomkuta Mwenyekiti wa Jumuiya ya Madkatari Tanzania, Dk.
Stephen Ulimboka lililotokea karibu miezi tisa kabla ya tukio la Kibanda yaani, usiku wa Juni 26, 2012.Ukiacha matukio hayo, miezi sita kabla ya Kibanda kutekwa na kuteswa Mwandishi Daudi Mwangosi, aliuawa akiwa mikononi mwa vyombo vya dola Septemba 2, 2012 huko Nyololo, Iringa akiwa kazini.Tukio la Kibanda limekuwa na sura ya mwendelezo wa mauaji au utesaji wa wanahabari, hasa ikitiliwa maanani kuwa Mwandishi Issa Ngumba (45) wa Radio Kwizera aliyekuwa anafanyia kazi zake katika Wilaya ya Kakonko, Kigoma, Januari mwaka huu, alipigwa risasi na kuuawa katika mazingira ya kutatanisha.Kama hiyo haitoshi, tukio la kutekwa na kudhuriwa kwa Kibanda limetokea mwezi mmoja tu baada ya Mwandishi wa Gazeti la Tanzania Daima, Shaaban Matutu kupigwa risasi na polisi akiwa nyumbani kwake Dar es Salaam kwa maelezo kuwa kimakosa polisi walidhani Matutu ni jambazi.Mazingira ya kutekwa na kuumizwa kwa Kibanda yalitia wasiwasi kuwa upo uwezekano, na dalili zilionyesha kwamba waliofanya kitendo hicho cha kinyama hawakuwa wezi wala majambazi kutokana na ukweli kwamba licha ya kuwa na fedha zipatazo shilingi milioni tatu taslimu ndani ya gari, laptop, simu tatu za gharama (ipad, iphone na Blackberry), watekaji hawa hawakuchukua chochote baada ya kukamilisha uhalifu wao.Kibanda aliumizwa kwa kiwango kikubwa. Alitobolewa jicho la kushoto, akaumizwa vibaya kichwani kiasi cha kusababisha kuvunjika kwa baadhi ya mifupa ya kichwa. Aling’olewa meno mawili na kucha mbili, tena bila gazi. Watekaji hawa, katika unyama wa ajabu kabisa, walimkata pingiri ya kidole cha pete chini ya kucha na kuondokana nayo.Hali hiyo iliibua maswali mengi, watu wengi wakajiuliza na kutafuta sababu za kutekwa na kuumizwa kwa Kibanda kiasi hiki. Kutokana na kuwapo kwa maelezo mengi yanayotofautiana kuhusu tukio hilo, ikabidi Jukwaa la Wahariri Tanzania lifanye uamuzi.Katika kikao cha Machi 8, 2013 Jukwaa la Wahariri Tanzania liliunda TIMU ya watu watano na kuipa hadidu rejea za kufanya uchunguzi wa kihabari juu ya shambulio hilo kubaini limetokana na nini.Timu hiyo iliundwa kufuatia uamuzi wa Jukwaa la Wahariri kufanya uchunguzi huo na baada ya kukubalika kwa ombi la ruzuku ya kufanya uchunguzi huo wa kihabari kutoka Mfuko wa Vyombo Vya Habari Tanzania (TMF). Ruzuku ya TMF ililenga kiujumla kutumia tukio la Kibanda kuwa chanzo cha kutengeneza mazingira salama zaidi kwa waandishi na wahariri na kwamba kiwango cha matukio ya kuteswa, kupigwa na kuuawa kwa waandishi yanapungua kila mwaka. Timu hii imefanya kazi usiku na mchana kwa kwa zaidi ya mwezi. Timu imezungumza na wadau 26. Kati ya hawa yumo Kibanda mwenyewe, mke wake, ndugu zake, wasaidizi wake, waajiri wake wa zamani na wa sasa, viongozi wa kisiasa na vyombo vya dola kutafuta ukweli wa jambo hili. Pia tumesoma matamko na habari zilizochapishwa kwenye mitandao ya kijamii na magazeti ya kati ya Machi 5, 2012 na Aprili 5, 2012 kwa nia ya kufanya ulinganishi wa taarifa tulizozipata kutokana na uchunguzi na habari zilizochapishwa baada ya kutekwa kwake.Vyombo vya dola akiwamo Waziri mwenye dhamana walikataa kuhojiwa wakisema kuna tume ya serikali inayofanya kazi hiyo na kwamba kuhojiwa kungeonyesha kutokuwa na imani na tume hiyo.Leo tunawasilisha muhtasari wa ripoti hii. Ripoti kubwa pamoja na viambatanisho vyake, itachapishwa na kuwekwa katika kitabu kimoja. Utaratibu mwingine wa kuchapisha habari ambazo hazijachapishwa kuhusiana na tukio hili (untold stories) pia utaandaliwa kwa ushirikiano na Jukwaa la Wahariri kwa nia ya kuieleza jamii maajabu juu ya kadhia hii.Tulipewa Hadidu Rejea ziafuatazo:

HADIDU REJEA:1. Kuchunguza mazingira ya kabla na baada ya tukio la kushambuliwa kwake. Kabla ya kushambuliwa kwa maana ya kufahamu kama kulikuwa na viashiria vyovyote vinavyoelekea kuwapo kwa mipango ya mashambulizi dhidi yake.2. Kuchunguza mazingira ya tukio lenyewe kwa kujikitika katika mwenendo wake hasa siku nzima ya Jumanne Machi 5, 2013.3. Kuangalia mazingira ya kazi ndani ya Kampuni ya New Habari (2006), Ltd na nje ya kampuni hiyo kwa kumulika sababu za kuhama kwake kutoka Free Media mwishoni mwa mwaka jana na kuhamia New Habari.4. Kuchunguza jambo jingine lolote linaloweza kutoa mwanga wa sababu za kuvamiwa na kupigwa kwa Kibanda.5. Kuchunguza mazingira ya sasa ya kazi kwa wanahabari na kupendekeza hatua za kuchukua kutokana na kile kitakachobainika

YALIYOJIRI KATIKA UCHUNGUZI:
1.0. Kuchunguza mazingira ya kabla na baada ya tukio la kushambuliwa kwake. Kabla ya kushambuliwa kwa maana ya kufahamu kama kulikuwa na viashiria vyovyote vinavyoelekea kuwapo kwa mipango ya mashambulizi dhidi yake.Timu ya uchunguzi ilitumia muda mwingi katika eneo hili, kubaini iwapo kulikuwapo viashiria, sababu au matukio ya wazi yenye mwelekeo wa kujitokeza kwa shambulio hili. Tuliangalia pia iwapo wapo watu au makundi yaliyokwishapata kuonyesha ishara kwa matendo au kwa kauli juu ya uwapo wa nia hii. Uchunguzi umebaini kuwa kuliwapo viashiria vingi, isipokuwa Kibanda au watu wake wa karibu hawakupata kufikiri kuwa huenda vingeweza kuleta madhara makubwa kiasi hiki kama ifuatayo:-

1.1. Wiki tatu kabla ya Kibanda kuvamiwa, kutekwa na kuumizwa, gari la polisi aina ya gofu Na PT 180 liliwafuatilia kwa muda mrefu Absalom Kibanda na Ofisa Mtendaji Mkuu wa New Habari (2006) Ltd, Hussein Bashe likiwa limeegeshwa nje ya ofisi zao Sinza Kijiweni na baadaye likawafuatilia hadi Sinza Makaburini, ambapo walisimamisha magari yao na kuzungumza na polisi hao waliosema walikuwa wanatilia shaka magari yao. Baada ya kuzungumza kwa muda polisi waliondoka.

1.2. Usiku wa Februari 25, mwaka huu majira ya saa 09:00 usiku, Kibanda walivamiwa na watu walioingia kwenye uzio wa nyumba yao wakavunja kioo cha gari analotumia, lakini kioo kilipovunjwa ‘alarm’ ilipiga kelele, Kibanda akatoka nje na watu hao wakakimbia.

1.3. Kutokana na uvamizi huo, Kibanda na wapangaji wengine katika nyumba zilizopo kwenye uzio mmoja, waliona hatari ya kuvamiwa hivyo wakaanza mazungumzo na kampuni ya Ulinzi ya Kiwango, iliyowataka kufunga kamera za usalama na kuweka walinzi watano. Hadi Kibanda anatekwa, walikuwa hawajahitimisha mazungumzo na kampuni hii ya Kiwango.

1.4. Kuna askari anayefanya kazi Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ) miezi minane kabla alipata kumpa Kibanda taarifa za kinteligensia, kuwa kulikuwapo mpango wa kumteka na kumuumiza. Taarifa kama hizo pia alipewa na wasamaria wanaofanya kazi katika Jeshi la Polisi. Kwa maneno yake Kibanda alisema:“Kuna rafiki yangu askari wa Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ), kama miezi minane au tisa hivi aliwahi kuniambia ‘unaandika sana usidhani kama watu wanakupenda. Chukua tahadhari hasa unapofika getini nyumbani kwako’. Tangu wakati huo nimekuwa nikichukua tahadhari sana.“Wiki mbili kabla ya tukio, niliwahi kuhisi kitu kama hicho [cha kuvamiwa] nikiwa getini. Nilipiga honi wakachelewa kuja kunifungulia, niliogopa sana. Hata nilipoingia ndani nilikuwa nimekosa raha kabisa.“Pia kuna rafiki zangu polisi waliwahi kuniambia kwamba ninatafutwa na kwamba watu wananifuatilia na ikibidi wanitengenezee ajali au kunifanyia kama Ulimboka au Kubenea.”

1.5. Ndani ya miezi mitatu mbele ya mlango wa ofisi yake Kibanda (Free Media Limited) ilikuwa mara kwa mara muda wa asubuhi anapofika ofisini anakuta damu. Haikufahamika kama damu hiyo ilikuwa ni ya binadamu, kuku, ng’ombe, kunguru au mbuzi, bali waliipuuza wakidhani ni masuala ya ushirikina. Mhariri Mtendaji wa sasa, Ansbert Ngurumo, amethibitisha kuwapo kwa tukio hilo.1.6. Mfanyakazi mwandamizi wa Kampuni ya New Habari anakofanya kazi sasa Kibanda ndani ya wiki mbili kabla ya kutekwa na kuumizwa kwake alipata kumwabia Kibanda maneno mazito mara tatu, na hapa tunamnukuhu Kibanda:“Aliniambia Danny Mwakiteleko [aliyekuwa Naibu Mhariri Mtendaji wa New Habari] hakufa kwa ajali, bali alikufa kutokana na blood clotting (kuganda kwa damu). Hivyo ikitokea mtu ukapata ajali au ukapigwa na kuumizwa sana sehemu za kichwa hivi au tumbo, ni lazima madaktari wadhibiti sana blood clotting.“Na kweli, nilivyoletwa hapa Milpark hospitalini, madaktari walikuwa wananidunga sindano sita kila siku kwenye kitovu kuzuia blood clotting. .... (jina linahifadhiwa) aliniambia maneno haya mara tatu, katika mazingira yasiliyotarajiwa na kwa msisitizo ambao sikujua maana yake. Nasema .... (jina linahifadhiwa) naye achunguzwe kwa kina. Inawezekana kuna jambo analijua.”Ofisa huyu, alipishana dakika chache na Kibanda muda wa kutoka ofisini baada ya kipindi cha kwanza cha mechi kati ya Real Madrid na Manchester united kumaliza nusu ya kwanza (half time). Dakika ishirini baadaye Kibanda alishambuliwa.

2.0. Kuchunguza mazingira ya tukio lenyewe kwa kujikitika katika mwenendo wake hasa siku nzima ya Jumanne Machi 5, 2013.2.1. Familia ya Kibanda na Kibanda Mwenyewe hawakuwa na wasiwasi wowote siku hiyo kwani hawakuwa na hisia wala wazo kuwa ungetokea uvamizi huo.

2.2. Kibanda alipopiga honi, mlinzi alisogea langoni kumfungulia. Ghafla akasikia kishindo kikubwa. Akasikia kelele za Kibanda akiomba msaada. Kijana huyu Baraka Ibrahim mwenye umri wa miaka 27, aliogopa. Aliogopa kwa mana hakuwa na silaha yoyote mkononi. Hakuwa na panga, kisu, rungu, wala filimbi. Kwa maneno yake anasema:“Nilivyoona ningefungua geti hata mimi ningekufa, nilikimbia kuwaamsha majirani. Sikuwa hata na namba ya simu ya mtu yeyote kati ya mabosi wangu ninaowalinda. Nilikuwa mimi tu, imani yangu na Mungu wangu.... kutokana na maisha naifanya hivyo hivyo tu. Vinginevyo milele nisingefanya kazi hii ya ulinzi.”Mlinzi huyo alikimbilia kwa majirani katika nyumba aliyoamini yumo mwanaume, lakini akaanza kumwamsha House Girl, ili house girl amwamshe baba mwenyenyumba. Kitendo cha kuamshana na kuwapa taarifa kilichukua dakika tano hadi saba, na ndani ya muda huo, Mlinzi anasema watekaji wa Kibanda walifanyafanya unyama na uasi huo na kuondoka ndani ya muda mfupi kiasi hicho. “Watu hawa wana mafunzo maalumu,” anahitimisha.

2.3. Mke wake alikwenda kazini asubuhi na kurejea nyumbani jioni, lakini tofauti na utaratibu wake wa kawaida ambapo huwa anaangalia televisheni sebuleni hadi Kibanda anaporejea nyumbani, siku hiyo alikwenda kuangalia televisheni akiwa chumbani na usingizi ukampitia. Anasema hakusikia honi wala tukio la Kibanda kutekwa. “Hii inanitesa sana moyoni. Najiuliza kwa nini siku hiyo tu sikukaa sebuleni? Kwa nini siku hiyo tu nimelala mapema kabla Baba Joshua hajarudi (machozi yanamlengalenga). Najiuliza sipati jibu.”2.4. Mmoja kati ya wasaidizi wawili wa nyumbani kwa Kibanda, alisikia kelele za Kibanda akiomba msaada. Alimwamsha mwenzake na kumwambia. “Nasikia Baba Joshua anapiga kelele kama amevamiwa hivi.” Mwenzake alimwambia “Unaota maana kuna kelele za mpira.” Siku hiyo kulikuwa na mechi kati ya Real Madrid na Manchester United.Ni kweli zilikuwapo pia kelele za wanaoshangilia mpira siku hiyo, hivyo Kibanda alipoomba msaada, hata waliosikia walidhani watu wanashangilia mpira. Binti aliwaamsha Angela na mwenzake, wakaenda sebuleni, wakakaa na kuchungulia dirishani, wakaona mwanga wa gari getini, lakini baada ya kutosikia kelele yoyote wakarejea kulala wakidhani siye. Lakini binti mmoja alibaki sebuleni. Baada ya muda jirani mmoja akampigia simu Angela kumweleza kuwa mumewe ameshambuliwa.2.5. Kibanda kwa upande wake, anasema alipofika getini, alipiga honi, ghafla akaona watu wawili wamesimama pembeni mwa gari lake na mtu wa tatu akiwa kwa mbali. Kisha akasikia kishindo kikubwa, akidhani wanataka kuiba gari, aliatokea mlango wa abiria na kuanza kukimbia huku akiita. “Mama Joshua nisaidieeeeee.”Katika kukimbia, aliteleza akaanguka. Huku watesaji wake wakisema mara tatu “Afande piga risasi.” Kibanda alijaribu kupambana, akashika rungu, akawahoji amewakosea nini hadi wampige kiasi hicho, lakini hawakumjibu lolote. Waliendelea kumpiga, hadi akapoteza fahamu. Hakujua jicho limetobolewa saa ngapi, meno yameng’olewaje na wala pingiri ya kidole chake imekatawaje. Ifuatayo ni sauti ya Kibanda mwenyewe. Inasikitisha ila tuwe wavumilivu na tuisikilize.

3.0. Kuangalia mazingira ya kazi ndani ya Kampuni ya New Habari (2006) Ltd na nje ya kampuni hiyo kwa kumulika sababu za kuhama kwake kutoka Free Media mwishoni mwa mwaka jana na kuhamia New Habari.

3.1. Mazingira ya kazi ndani ya New Habari (2006) Limited na Freemedia Limited, yanaacha maswali kadhaa yenye kustahili majibu. Kama ilivyoelezwa kwenye Hadidu Rejea Na: 1, ndani ya kampuni ya New Habari imekuwapo misuguano isiyo na afya kwa kazi ya Kibanda kama mwandishi na tasnia ya habari kwa ujumla.

3.2.Mazingira ya kazi ndani ya Kampuni ya New Habari (2006) Ltd ni utata. Uhusiano katika chumba cha habari si mzuri. Ndani ya kampuni hawaaminiani na imefikia hatua wanatuhumiana kuwa huenda baadhi ya viongozi ndani ya New Habari wamehusika kumteka na kumuumiza Kibanda. Haya yameandikwa ndani ya mitandao ya kijamii, ikidai kwamba kiongozi mmoja ndani ya kampuni hiyo alihusika na utekaji wa Kibanda. Mkurugenzi wa Uhariri, Prince Bagenda anasema waliohusika kusambaza taarifa chafu dhidi ya kiongozi huyo wa New Habari wanatoka ndani ya kampuni hiyo.

3.3. Timu ya uchunguzi ilibaini kuwapo mgawanyiko mkubwa ndani ya New Habari (2006) Ltd kwa kuwapo kundi la ‘Habari Wazawa’ na ‘Habari wa Kuja’. Malalamiko mengi yanajikita katika msingi kuwa ajira hazitangazwi na watu wanaajiriwa bila kuzingatia sifa za kitaaluma.

3.4. Kibanda hakuhama Free Media kwa amani. Uchunguzi unaonyesha kuwa miezi kadhaa kabla ya kuondoka kwake alianza kupoteza mamlaka. Mwenyekiti wa Kampuni ya Free Media Ltd, Freeman Mbowe alianza kumsikiliza zaidi msaidizi wake ambaye alikuwa Naibu Mhariri Mtendaji, Ansbert Ngurumo kuliko yeye Kibanda. Kwa maneno yake, anasema:“Nilihofu kuwa Mbowe anaweza kutugombanisha. Nikaona ni bora niondoke nisije nikagombana na Mbowe au Ngurumo.”Anasema alianza kupoteza mamlaka yake na kutoaminika kwa mwajiri wake baada ya kuandika makala kuhusu Abdulrahman Kinana ambayo kabla ya kuiandika hakuwa na wazo la kuondoka. Yaliyofuata baada ya makala hiyo, yalimshukuma aondoke.

4.0. Kuchunguza jambo jingine lolote linaloweza kutoa mwanga wa sababu za kuvamiwa na kupigwa kwa Kibanda.

4.1. Uchunguzi ulifuatilia masuala mbalimbali ikiwamo miendendo ya watu waliotajwa kwa njia moja au nyingine kuhusinaa na tukio hili. Hata hivyo, karibu watu wote waliohojiwa, akiwamo Kibanda mwenyewe aliyeumizwa walimtaja kwa kutilia shaka mwenendo wa kijana Joseph Ludovick. Hofu yao, iliongezwa nguvu na maandishi aliyoyachapisha Ludovick kwenye mitandano ya kijamii siku ya Machi 6, 2013.

4.2. Usiku aliotekwa na kuumizwa Kibanda, Ludovick katika naye alidai kuwa ametekwa katika eneo la Shekilango na kupelekwa hadi Kigogo. Baada ya kutekwa aliibiwa kila kitu, ikiwamo begi, laptop, simu mbili, fedha taslimu Sh 35,000, akavuliwa nguo na kubaki na chupi tu. Pia alieleza kuwa alitoa taarifa hizo kituo cha polisi Mabibo.

4.3. Maelezo ya Ludovick yalitiliwa shaka na watu wengi hasa baada ya kuleeza kuwa watekaji walitumia muda wa saa mbili kumtoa Shekilango hadi Mabibo, umbali ambao kwa kiwaida mwendo wake hauwezi kuzidi dakika 10. 4.4. Daniel Chongolo aliiambia timu kuwa alfajiri ya Machi 6, siku anayodai kutekwa Ludovick yeye alimuona eneo la Mabibo wakati anatoka Muhimbili. Chongolo alikwenda kituo cha polisi Mabibo na kupewa taarifa kuwa Ludovick alitoa taarifa polisi kuwa alikuwa ametekwa ila akarudishiwa mali zake zote. “Alipouliza amefuata nini polisi, akawambia kama raia mwema amefika kuandikisha kumbukumbu kwa nia ya kuonyesha kiwango cha uhalifu kinavyoongezeka nchini,” anasema Chongolo. Timu ya uchunguzi ilikataliwa kupitia leja ya polisi kama itakavyoelezwa hapa chini.

4.5. Pia taarifa za uchunguzi wa timu hii zinathibitisha kuwapo kwa utata juu ya madai ya kuibwa kwa simu za Joseph Ludovick, kwani simu yake ya tigo (inayodaiwa kuibwa) ilitumika saa 01:21 asubuhi siku ya Machi 6, 2013. Muda huu ofisi za Serikali na Kampuni ya Tigo zilikuwa hazijafunguliwa

5.0. Kuchunguza mazingira ya sasa ya kazi kwa wanahabari na kupendekeza hatua za kuchukua kutokana na kile kitakachobainika.

5.1. Uchunguzi umebaini kuwa maisha ya wanahabari yapo hatarini. Hatari hii inatokana na makundi mengi yenye masilahi kuwaona wanahabari wanaosimamia ukweli kuwa maadui wa masilahi yao haramu. Kuna hatari kubwa inayowakabili waandishi wakati nchi inapoelekea kwenye uchaguzi wa mwaka 2015.

5.2. Uchunguzi umebaini kuwa usiri umepungua katika vyombo vya habari. Tofauti na zamani ambapo habari nyeti ziliandikwa kwa kuhifadhi majina ya waandishi wakitumia jina la MWANDISHI WETU. Simu hizi hata habari za kutisha waandishi wanaweka majina yao na hata wasipoweka, ndani ya vyumba vya habari vingi waandishi wapo tayari kutaja nani ameandika habari fulani.

5.3. Usaliti miongoni mwa waandishi wenyewe ndani ya vyumba vya habari unazidi kuongezeka na usipodhibitiwa hali itazidi kuwa mbaya zaidi. Mwenyekiti wa MOAT, Dk. Reginald Mengi anasema: “Hili ni jambo muhimu sana. Tuache usaliti vinginevyo wengi wataumia.”

5.4. Pia alishauri waandishi wa habari kurejea katika msingi wa taaluma, ambayo inawataka wao kuwa ndio wenye kuendesha vyombo vya habari badala ya kutegemea matakwa ya wamiliki au makundi yenye masilahi binafsi.

6.0. KILICHOBAINIKA:

6.1. Uchambuzi uliofanywa ni timu hii umebaini kuwa hoja nne zinazungumzwa kuhusiana na kutekwa na kuumizwa kwa Kibanda. Hoja hizi ni:-(i) Kazi yake ya uandishi wa habari(ii) Uhusiano wa kisiasa na vyama au wanasiasa mbalimbali(iii)Uhusiano wa kijamii ikiwamo mapenzi(iv) Vitendo vya rushwa.

6.2. Timu imejiridhisha kutokana na majibu ya wengi kuwa dhana ya mapenzi na rushwa, havina nafasi yoyote katika tukio hili. Wote waliohojiwa walieleza pasi na shaka kwamba suala hili la kushambuliwa na kuumizwa kwa kiwango kikubwa kwa Kibanda, halina uhusiano wowote na rushwa au mapenzi.

6.3. Kutokana na yaliyotajwa hapo juu kazi yake na siasa vikiunganishwa vimechangia kwa kiasi kikubwa kuvamiwa kwa Kibanda. Timu imebaini kuwa kuna kutupiana mpira kati ya vyombo vya dola na vyama vya siasa. Mchezo huu mchafu unaweza ukawa mwanzo wa kuumizwa kwa Kibanda na waandishin wengine.

6.4. Baadhi ya waliohojiwa walidai kuwa utekaji huu umefanywa na vyombo vya dola ukiwa sehemu ya mpango mkakati wa vyombo hivi kukihusisha Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) na vitendo vya ugaidi.6.5. Wanayataja matukio ya Uchaguzi Mdogo wa Igunga, maandamano ya Morogoro na Mkanda anaodaiwa kurekodiwa Mkurugenzi wa Usalama wa CHADEMA, Wilfred Lwakatare kuwa vililenga kukifanya CHADEMA kichukiwe na Watanzania kwa kukitaja kama chama cha kigaidi ambacho kinateka watu na kinawaumiza.

6.6. Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe anadai kwamba mpango kama huo vyombo vya dola viliutumia kwa NCCR Mageuzi vikakisambaratisha, Chama cha Wananchi (CUF) kilisingiziwa udini kikapoteza mwelekeo na sasa vyombo hivyo vililenga kukifanya CHADEMA kionekane cha kigaidi mbele ya macho ya jamii ndiyo maana imerekodiwa mikanda kwa nia ya kuitumia kujenga hoja hiyo.

6.7. Wakati Mbowe akisema hayo, baadhi ya watu waliohojiwa wanadai kuwa CHADEMA kimepewa mafunzo na ushauri kutoka nje ya nchi kuwa kikitumia baadhi ya watumishi wa vyombo vya dola wasiokuwa waaminifu kuteka, kuumiza na hata kuua baadhi ya watu maarufu nchini wakiwamo waandishi na wanasiasa, basi wananchi wataamini kuwa Chama Cha Mapinduzi na Serikali yake kimeshindwa uongozi na sasa kimeanza kazi ya kuua wanaowapinga.

6.8. Kwa njia hiyo, inaelezwa kuwa hesabu za Chadema ni kuwa wananchi wataichukia CCM na Serikali yake na kukipa nafasi ya kuingia madarakani. Hapa kauli ya Chadema kuwa NCHI HAITATAWALIKA itakuwa imetimia.

6.9. Dhana nyingine iliyojitokeza ni kuwa wapo wafanyabiashara ambao wana vita binafsi, hivyo wanaamua kuumiza watu wasiowaunga mkono katika mipango yao na hilo ndilo limemkumba Kibanda, baada ya kuwa ameepusha mauaji ya mwandishi mmoja na aliyekuwa ameandaa mpango wa kuua mwandishi huyo hakuridhika hivyo akaamua amshughulikie Kibanda.

7.0. MAPENDEKEZO:
Baada ya Timu kupata taarifa hizi na nyingine nyingi, inapendekeza yafuatayo:-
7.1. Taarifa hii ichukuliwe kama chanzo cha uchunguzi zaidi wa vyombo husika.7.2.

Yanahitajika marekebisho makubwa na ya haraka katika mifumo ya uendeshaji wa vyumba vya habari kwa nia ya kurejesha misingi ya uandishi wa habari inayokubalika.

7.3. Usalama wa wanahabari unapaswa kupewa kipaumbele na wamiliki, wanahabari wenyewe na jamii kwa ujumla. Hapa Timu inapendekeza yawepo mafunzo ya kuwawezesha wanahabari kutambua viashiria vya hatari na kuchukua hatua mara moja.

7.4. Kwa kiwango alichoumizwa Kibanda iwapo mwajiri wake asingejitolea kugharamia matibabu, hatujui hatima yake ingekuwaje leo hii. Tunapendekeza taasisi na mifuko mbalimbali inayojihusisha na masuala ya wanahabari kama Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) , Baraza la Habari Tanzania (MCT), Mfuko wa Vyombo vya Habari Tanzania (TMF) na Umoja wa Klabu za Waandishi wa Habari Tanzania (UTPC) kuanzisha mfuko wa pamoja utakaotumika kugharamia matibabu ya waandishi watakaoumia wakiwa kazini.

7.5. Tukio la kutekwa kwa Kibanda limeonyesha mwanga kuwa wahariri tumegawanyika mno. Habari zilizochapishwa katika magazeti mbalimbali na mitandao ya kijamii zimeonyesha haja ya kuwafanya wahariri kuwa kitu kimoja kwa kuondoa tofauti zao zisizo na masilahi kwa tasnia ya habari.

7.6. Kuna viashiria vingi kuwa kuelekea mwaka 2015 matukio ya waandishi kuumizwa au kutekwa yanaweza kuongezeka kutokana na wanasiasa na vyama kuwania madaraka huku wakitumia baadhi ya watumishi katika vyombo vya dola. Kwa mantiki hiyo, vyombo vya habari na waandishi wa habari wachukue tahadhari kuanzia sasa.

7.7. Taasisi za habari zifanye juhudi za makusudi kukutana na vyama viwili vya siasa vya CCM na CHADEMA haraka iwezekanavyo, kuzungumzia viashiria hivi vya hatari vinavyoelekea kuvuruga amani ya Tanzania.

8.0. HITIMISHO:
Ni dhahiri kuwa kupigwa na kuteswa kwa Kibanda kumejiegemeza katika siasa na kazi yake, hali inayofanya makundi muhimu kuchukua wajibu wa msingi. Kwa upande wa Serikali ni muhimu kufuatilia viashiria katika taarifa hii kwa nia ya kupata ukweli zaidi na kuchukua hatua stahiki za kisheria dhidi ya wahusika.Na kwa upande wa vyombo vya habari na taasisi za kihabari zinapaswa kutambua viashiria vinavyohatarisha usalama wa waandishi wa habari na wahariri na kutengeneza mazingira yatayokuwa salama zaidi kwa waandishi kufanya kazi zao.

9.0. SHUKRANI:

9.1. Tunapenda kulishukuru Jukwaa la Wahariri Tanzania, kwa kufanya uamuzi sahihi wa kuwezesha kufanyika kwa uchunguzi huu ulioanza kuonyesha mwanga wa nini kilitokea.

9.2. Tunapenda kulishukuru Baraza la Habari Tanzania (MCT) kwa kushiriki kikamilifu na kuiwezesha timu hii kwa Rasilimali Watu na Mali kufanikisha kazi hii.

9.3. Tunapenda kuwashukuru Mfuko wa Vyombo vya Habari Tanzania (TMF) kwa uwezeshaji wa ruzuku, uliofanikisha kufanya uchunguzi wa kihabari uliohusisha kwenda nchini Afrika Kusini kufanya mahojiano na Kibanda. Uwezeshaji huo pia unahusisha kutengeneza mwongozo kwa waandishi wenye lengo la kuwaepusha na hatari za kiusalama.

9.4. Tunawashukuru Kibanda, mkewe Angela, wanafamilia, ndugu na jamaa wa Kibanda na wanahabari wote waliohojiwa kwa ushirikiano mkubwa walioutoa kwa Timu hii.

9.5. Tunawashukuru wahariri wote kila mtu kwa nafasi yake, kutokana na ushauri wa mara kwa mara mliotupatia katika kufanikisha uchunguzi huu.

10.0. WAJUMBE WA TIMU:
Timu hii iliundwa na wajumbe watano ambalo ni:1. Deodatus Balile – Mwenyekiti2. Pili Mtambalike – Mjumbe3. Jane Mihanji – Mjumbe4. Tumaini Mwailenge – Mjumbe5. Rashid Kejo – Katibu

No comments:

LinkWithin

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...