Na Kambi Mbwana, Dar es Salaam
KIUNGO wa timu ya Yanga, Haruna Niyonzima, amesema kwamba amekosa
kabisa hamu ya kukipiga katika klabu ya Simba, ndio maana aliweza kuwakatalia
akijua kuwa bado ana lengo la kuendelea kuwa mwajiriwa wa Jangwani.
Haruna Niyonzima katikati akiwa na viongozi wa Yanga
Akizungumza jana jijini Dar es Salaam, Niyonzima alisema kuwa kila
mchezaji ana ndoto zake, hivyo yeye kucheza Simba ni moja ya vitu ambavyo
hawezi kuviweka mbele hata kidogo.
Alisema ingawa timu nyingi zilikuwa zikimuwinda, ila ndoto za
kucheza Simba hakuwa nazo na hawezi kubadili uamuzi wake, ingawa mpira ni pesa
na lolote linaweza kutokea.
“Nilijua kuwa mkataba wangu upo mwisho, ila kubwa nilitamani
kuendelea kuwapo Yanga kwa msimu mmoja zaidi, ndio maana hata wale niliokuwa
nazungumza nao sikuwapa ushirikiano.
“Mchezaji anayewika uwanjani kufuatiliwa ni jambo la kawaida, ila
ni vyema katika suala hilo mtu kufanya uamuzi wa busara na wenye maslahi katika
maisha yake ya mpira wa miguu,” alisema.
Baada ya kuongeza mkataba wake kwa miaka misimu miwili zaidi,
Niyonzima anajiandaa kurudi kwao nchini Rwanda, kabla ya kurejea baadaye
kuendelea na kibarua chake mitaa ya jangwani.
No comments:
Post a Comment