Mwandishi Wetu, Moshi
KATIKA kuelekea mchezo wa jana dhidi ya Flamingo FC ya Arusha, Machava FC
ambo ndio mabingwa wa ligi daraja la Tatu, mkoa wa Kilimanjaro, wamekabidhiwa
vifaa vya michezo na uongozi wa chama cha Mapinduzi CCM wilaya ya Moshi.
Machava FC walikabidhiwa vifaa hivyo ambavyo ni mipira mitano na Jezi,
kama sehemu ya mchango wa Chama hicho kwa timu hiyo ambayo kwa sasa ndio
inayobeba Roho ya mkoa wa Kilimanjaro katika medani ya soka.
Akizungumza baada ya kukabidhi vifa hivyo vilivyotolewa kwa timu hiyo na
Mjumbe wa Halmashauri kuu CCM, Jerry Silaa, Katibu wa CCM wilaya ya Moshi Mjini
Aluu Segamba aliwahakikishia wapenzi wa soka mkoani hapa kuwa wako tayari
kushirikiana nao hadi mwisho wa Safari.
“Leo tunatimiza ahadi yetu kwa wawakilishi wetu, mabingwa wa Mkoa timu ya
Machava, tunaamini kuwa timu hii kama roho ya kilimanjaro katika mchezo wa soka
itafanya makubwa na kinachotakiwa ni kuwapa sapoti inayostahili,” alisema
Segamba.
Naye Makamu Mwenyekiti wa klabu hiyo Abuu Masoud, baada ya kupokea msaada
huo kutoka CCM, alisema kutokana ushirikiano unaoneshwa na wadau wa soka kwa
timu yao wanaahidi kufanya vizuri katika michezo yao yote na kuwapa raha
wapenzi na mashabiki wa Machava mkoani Kilimanjaro.
Kwa upande kocha msaidizi wa machava aliwaondoa hofu mashabiki wa timu
yake kuhusu hali ya Afya ya mshambuliaji wa kutumainiwa wa klabu hiyo, Isa
Kipese na kuelekea mchezo wa jana na kuongeza kuwa kinachosubiriwa ni ripoti za
madaktari wanaomshughulikia mchezaji huyo.
Machava FC ambayo inauwakilisha mkoa katika michezo ya Mabingwa wa mikoa
imekuwa ikipokea sapoti kutoka kwa wadau wa michezo mkoani hapa ambapo hivi
karibuni tu Mbunge wa Moshi Mjini, Filemon Ndesamburo na Mstahiki Meya wa
Moshi, Jafary Michael walitembelea kambi ya timu hiyo na kuchangia fedha
taslimu shilingi laki saba.
Katika hatu nyingine chama cha Mapinduzi CCM pia imetoa msaada wa
vifaa vya michezo kwa timu ya Gillete Fc ya kata ya Kaloleni kama sehemu ya
utekelezaji wa ilani ya chama hicho za kutoa fursa nyingi za ajira kwa njia ya
michezo.
Akikabidhi vifaa hivyo, mipira
miwili na Jezi kwa diwani wa kata ya Kaloleni, Michael
Mwita, Segamba alisema kuwa wanalenga
kuunganisha umma wa mkoa wa Kilimanjaro, kupitia michezo na kuongeza kuwa
katika swala la michezo watu wote ni ndugu bila kujali itikadi zao.
No comments:
Post a Comment