https://tpc.googlesyndication.com/simgad/8045142562622600543


Recent Post

Monday, May 20, 2013

Bila umakini, mechi za Simba na Yanga zitaleta balaa

SIWEZI KUVUMILIA
Na Kambi Mbwana, Dar es Salaam
KADRI siku zinavyozidi kwenda mbele, idadi ya watu na mahitaji inaongezeka katika kila sekta, ikiwapo ya michezo inayovutia watu wengi. Katika Tanzania ya leo yenye changamoto nyingi, watu wengi wanaona sehemu sahihi kwao ni kuegemea kwenye michezo na burudani.
Mlinda Mlango wa Simba, Juma Kaseja
Katika suala hilo, ili kujiweka katika nafasi nzuri, ni wazi tunahitaji kufahamu mbinu nzuri pamoja na kufanyia kazi zile changamoto zinazojitokeza siku hadi siku kwa maendeleo ya Taifa.

Wakati nasema hayo, Watanzania na wana Uwanja wa kisasa unaoingiza watu 60,000. Idadi hii ni kubwa katika uwanja huo. Pamoja na hayo, inapotokea mechi kubwa kama ya Simba na Yanga, mambo yote huvurugika.

Sehemu zote muhimu kama hushindwa kuwa kwenye mpangilio mzuri. Kwa mfano, barabara moja inayoingia katika Uwanja wa Taifa, kutokea upande wa DUCE, ilikuwa imezibwa.

Angalia, utaratibu uliotumika kuifunga barabara kubwa kama ile, ilisababisha mkanyagano wa kiasi kikubwa kutokana na idadi ya watu wengi waliokuwa wakielekea uwanjani hapo.

Hii siwezi kuvumilia hata kidogo. Mbaya zaidi, hata pale mechi hiyo ilivyokwisha, bado barabara iliendelea kufungwa. Huu ni ujinga wa aina yake. Kama utaratibu unakuwa mbovu, kuna hatari inayoweza kujitokeza siku za usoni.

Nasema hivyo kwasababu ni wazi kila siku klabu za Simba na Yanga zinaendelea kuvuna wanachama wengi na mashabiki wanaokuwa na hamu ya kuhudhulia mechi za timu zao.

Ukiacha hayo, baadhi ya wadau na mashabiki licha ya kulipia tiketi za VIP, lakini hujikuta wakipanga foleni kwa watu wa kawaida, hivyo kuwafanya waone karaha ya kuingia kwenye uwanja huo.

Kwa bahati mbaya, halai hii mara nyingi hutokea kwenye mechi za watani wa jadi, maana hata wale wasiopaswa kusema hulazimisha kwa kujiona wao ndio kila kitu, kitu ambacho si sahihi.

Kutumia utaratibu usioeleweka, ni sehemu ya kuingiza dosari za wasiojielewa kutumia mwanya huo kuharibu miundo mbinu ya kuingia, kutoka au iliyopo ndani ya uwanja huo.

Hakika siwezi kuvumilia. Kila mmoja anapaswa kuelewa kuwa uzuri wa uwanja wa Taifa, hauwezi kudumu kama mipango haitawekwa, sambamba na kuweka utaratibu mzuri wa kuingia na kutoka.

Huu ndio ukweli wa mambo. Kwa mfano, mechi ya Simba na Yanga iliyochezwa Jumamosi iliyopita na Yanga kuibuka na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya hasimu wao, ilijaza watu kuliko kawaida.

Kwa macho yangu, nilishuhudia wengineo wakikaa wawili katika kiti kimoja, au wengine kujistiri kwenye njia za kukanyagia. Kwa mtindo huu, uharibifu wa viti na vitu vingine hauepukiki.

Uharibifu huo unachochewa na wale waliopewa dhamana ya kuulinda na kuuhudumia, ikiwa ni kuandaa utaratibu mzuri unaoweza kuwafanya mashabiki wasishawishike kufanya uharibifu wowote.

Licha ya kuwa na uwanja mzuri wenye hadhi ya aina yake, lakini miundo mbinu ni mibovu, ndio maana mtu inamchukuwa muda mrefu kurejea nyumbani kwake zinapocheza timu kongwe za Simba na Yanga.

Wapo wanaolazimika kutoka uwanjani hadi maeneo ya Ilala Boma, Kariakoo na sehemu nyingine kwa miguu, maana usafiri unakuwa kero kutokana na miundo mbinu hiyo mibovu.

Kwa mtindo huo, inashangaza kuona bado wapo watu wanaoona dawa ni kufunga njia moja, magari, pikipiki zisipite katika njia hiyo, hivyo kuzalisha msongamano kama ilivyokuwa juzi.

Kwa waliobahatika kwenda uwanjani kuangalia mechi ya Simba na Yanga, watakubaliana na mimi kuwa bado hatujui namna ya kuandaa michezo mikubwa kama hao watani wa jadi.

Ingawa ni wepesi sana kuitangaza mechi hiyo kwa namna mbalimbali ili wadau na mashabiki wafike kwa wingi, ila mambo mengi ya kiutawala huwa magumu kufanyiwa kazi.

Kwa hili siwezi kuvumilia na kuna kila sababu ya kuliangalia hilo kwa faida ya mpira wa miguu Tanzania.
0712 053949
0753 806087

No comments:

LinkWithin

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...