DSC09434 (1)

Mkuu wa wilaya mpya ya Mkalama mkoani Singida, Edward Ole Lenga. (Picha na Nathaniel Limu).
***********
Na Nathaniel Limu.
Mwalimu wa shule ya msingi kata ya Msingi tarafa ya Kinampanda wilayani Mkalama Wolter Ponela (32) anatarajiwa kupandishwa kizimbani katika mahakama ya wilaya ya Iramba, kujibu tuhuma ya kumjaza mimba mwanafunzi wa kidato cha pili mwenye umri wa miaka 17.
Mwanafunzi huyo anasoma katika shule ya sekondari Jerumani iliyopo kata ya Msingi.
Mkuu wa wilaya ya Mkalama Edward Ole Lenga amesema ofisi yake imesikitishwa na kitendo cha mwalimu huyo kwa madai kuwa kinachangia kuharibu maisha ya msichana husika.

Amesema vitendo hivyo ni lazima vipingwe vita na wadau wote ili kuhakikisha wanafunzi wa kike wanasoma hadi upeo wao bila vikwanzo.
Katika hatua nyingine, mkuu huyo wa wilaya amekemea vikali tabia iliyoota mizizi ya kumaliza kienyeji matatizo ya wanafunzi kubebeshwa mimba.

Lenga amesema ni lazima sheria zilizowekwa zitumike katika kukomesa tabia za kuwajaza mimba wanafunzi ambazo huwa hazitarajiwi au mimba za utotoni.

Aidha, ameagiza watendaji  kila moja katika maeneo yake aorodheshe majina ya wanafunzi waliojazwa mimba na watu waliochangia uharibifu huo wa mimba za utotoni.

Lenga amewataka walimu kutenga muda kuwaelimisha wanafunzi wa kike madhara yatokanayo na mimba za utotoni kama njia moja wapo itakayosaidia wanafunzi kuchukia vitendo vya mahusiano ya kimapenzi wakati wakiwa wangali shuleni.