NI mtoto tu anayesubiri kuungua kwa kuugusa moto kwa ajili
ya kugundua kwamba unaunguza ama vipi. Ila kwa watu wazima wanaojitambua, hata
kwa macho tu, wataweza kung’amua kilichopo mbele yake, pembeni yake ni moto na
unapougusa madhara yake ni kuungua.
Francis Cheka
Ila, inapotokea mtu mzima anashindwa kujua moto unaunguza ni
ujinga, hivyo kila anayeweza kuwa kwenye mtazamo huo anastahili kuzomewa.
Kinyume cha hapo siwezi kuvumilia.
Siwezi kuvumilia, hasa kila ninapoangalia kipaji cha
mwanasumbwi, Francis Cheka anayetokea mkoani Morogoro kinaangaliwa ovyo ovyo
tu. Kwa miaka zaidi ya mitatu sasa, Cheka ameweza kuwa juu na kupeleka kilio
kwa kila bondia anayekutana naye ulingoni.
Kwa kuangalia hili tu, ni dhahiri kuwa Cheka ni bondia
makini na anastahili kupewa ushirikiano kutoka kwa wadau wa ngumi. Kwa mfano,
serikali pia inaweza walau kumjali bondia huyu kwa kuhakikisha kuwa anafanya
safari kuelekea kwenye mapambano makubwa duniani.
Kwa bahati mbaya, serikali yetu imekuwa ikifanya mambo
kiujanja ujanja tu. Hata Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo siku
zote imekuwa ikifanya mambo ambayo si yenye kukuza michezo.
Angalia, kila kipaji katika Taifa hili kimeibuka kwa juhudi
zake. Hakuna hata mmoja aliyetokea kwenye mikono salama. Ni tofauti na baadhi
ya nchi zilizoendela duniani.
Kila siku mabondia wa Tanzania, wadau wao wamekuwa wakilia
wimbo wa kukosa wadhamini wa uhakika. Licha ya kujaa kwa makampuni ya kila aina
na taasisi za muhimu, lakini ni chache zinazojitokeza kudhamini mchezo wa
masumbwi, japo kutoa Milioni moja au mbili.
Mapromota wa masumbwi ambao nao wanasumbuliwa na ukata,
wanatumia muda mwingi kusumbukia fedha za kuandaa pambano, huku wakitarajia
faida ya viingilio vya mashabiki.
Hakuna mipango wala ushirikiano hapa. Waswahili wana msemo
wao, supu ya mbwa inanywewa ikiwa ya moto. Kutokana na hilo, Cheka akitumiwa
vyema na wadau pamoja na serikali anaweza kufanya makubwa duniani katika sekta
ya masumbwi.
Watu watauliza au kushangaa. Ndio, maana watakumbuka kuwa
sio Cheka peke yake aliyewahi kutesa katika masumbwi hapa nchini. Ukiacha Said
Kinyong’oli, pia alikuwapo Rashid Matumla, akitokea katika familia ya wacheza
ngumi ambao hadi leo wanatamba.
Mwili wa Matumla ungeweza kutumiwa vyema, hakika angeweza
kupanda ulingoni kushiriki mapambano makubwa duniani. Lakini hao wote waliwika
kwa miaka michache na kupotea.
Naweza kusema sisi hatuna akili ya kuendeleza watu wenye
vipaji kwa ajili ya maslahi ya Taifa. Tumebaki kuwa wapiga makofi na
kushangalia ujuha wetu katika kila jambo hata kama halina tija.
Wakati huu, ni dhahiri kuwa kama Cheka hajajiweka sawa zaidi
kwa juhudi zake, huenda baada ya miaka miwili au mitatu ijayo kutoweka. Hakika
siwezi kuvumilia hata kidogo.
Ni wakati wetu sasa kukaa chini na kuangalia mwenendo wetu.
Tumtangaze Cheka nje ya nchi pamoja na mabondia wetu wengine kwa ajili ya
kupata mapambano makubwa na yenye soko.
Tutafate nafasi ya kujichomeka katika Mataifa makubwa, ili
iwe njia nzuri ya kukuza na kuendeleza sekta ya masumbwi. Kwa sasa Cheka naweza
kusema kuwa hana mpinzani Tanzania.
Atacheza na nani sasa? Kila anayeingia naye ulingoni
anampiga kama mtoto wake wa kumzaa. Juzi, Thomas Mashali aliyejigamba sana,
aliweza kutandikwa, huku Cheka akiwa anasumbuliwa na mkono.
Naamini huu ni wakati wa kuangalia mwenendo wetu kwa ajili
ya kusonga mbele katika kona ya masumbwi. Ili aweze kutimiza malengo yake,
inahitaji muda kidogo wa kujiandaa ili kuongeza uzito wake.
Huo ndio ukweli wa mambo. Kinyume cha hapo tuendelee na
porojo zetu, mzaha wetu, huku vipaji vyetu vikizidi kutumbukia katika shimo la
ufukara.
Tunaomba radhi kwa usumbufu, hasa kwa makala haya kukujia leo Alhamis badala ya Jumatatu kama ilivyokuwa kawaida yake.
No comments:
Post a Comment