Na Mwandishi Wetu, Dodoma
NAIBU waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu Tawala za Mikoa na
Serikali za Mitaa, Kassim Majaliwa, amesema kwamba wameamua kurudisha masuala
ya michezo mashuleni, ikiwa ni njia ya kuwafanya watoto washiriki kikamilifu,
sambamba na kutangaza vipaji vyao wakiwa wadogo.
Naibu Waziri TAMISEMI, Kassim Majaliwa
Majaliwa alitumia nafasi hiyo kuwakumbusha walimu na
wazazi juu ya masuala ya michezo mashuleni, ikiwa ni ajenda muhimu ya kuwaweka
sawa wanafunzi kutambua kuwa michezo ni muhimu katika maisha yao.
Akizungumza katika mchango wake kwa Bajeti ya Wizara
ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Majaliwa alisema kuwa wanaamini kwa
serikali kurudisha michezo mashuleni, itakuwa na faida kubwa kwa Watanzania
wote.
“Natumia fursa hii kuwakumbusha walimu na wazazi juu
ya kutia mkazo katika jambo hili la michezo katika shule za Tanzania, tukiamini
kuwa utasaidia kwa kiasi kikubwa kutangaza pia vipaji vya watoto wetu,”
alisema.
Aidha Majaliwa pia alitumia muda wake kuipongeza
wizara ya Habari kwa kuweka sera nzuri pamoja na kufanya kazi kwa bidii katika
suala la michezo na utamaduni kwa maendeleo ya Taifa.
No comments:
Post a Comment