SIWEZI KUVUMILIA
Na Kambi Mbwana, Dar es Salaam
WASWAHILI wana msemo wao maarufu unaosema kuwa siku zote wa
moja havai mbili. Msemo huu kama ni uongo, basi upo karibu na ukweli. Binafsi
nauamini msemo huo nikiorodhesha na matukio yetu kwenye jamii.
Mrisho Ngassa, akiwa kwenye jezi ya timu ya Taifa, Taifa Stars
Matukio ambayo yanaendelea kutokea na kutuacha tunajiuliza
maswali kede kede, ukizingatia kuwa kila mtu ana maoni na mtazamo wake. Mapema
wiki iliyopita, aliyekuwa mshambuliaji wa Simba, Mrisho Ngassa alitambulishwa
kwenye uongozi wa Yanga, kuwa amesajiliwa kwa ajili ya kukipiga kwenye timu
hiyo msimu ujao wa ligi.
Ngassa ni kama amerejea tu Yanga, maana aliwahi kukipiga
kwenye timu hiyo kabla ya kutimkia katika timu ya Azam FC na baadaye kusajili
Simba, alipoitumia kama njia ya kumrejesha Jangwani.
Si vibaya kwa Ngassa kurudi Yanga, maana katika mazungumzo
yake na wanahabari alisikika akisema kuwa ana mapenzi na klabu hiyo. Ni mnazi
mkubwa wa Yanga.
Anaipenda kuliko kitu chochote duniani. Sawa, ila Dunia ya
leo mipra ni kazi na sio unazi tena. Kama unazi, basi mchezaji wa aina hiyo
hawezi kusonga mbele katika soka la Kimataifa.
Ndio, hivyo siwezi kuvumilia, ndio maana Ngassa ameonekana
kucheza soka kwa ajili ya Tanzania tu. Kamwe hana maono ya kufika mbali. Hana
lengo lolote la kuwa nyota Kimataifa.
Mchezaji huyo ambaye amejizolea umaarufu mkubwa kwa wadau wa
soka Tanzania, alikataa dau nono la timu ya El Merreikh ya Sudan. Kama
angekubali kwenda huko, huenda ingekuwa njia yake ya kusonga mbele.
Lakini bila sababu za kueleweka, aliamua kuikataa ofa hiyo.
Watu walijuliza maswali lukuki. Maswali ambayo sasa yamepata majibu kuwa hana
anachoangalia zaidi ya soka la Simba, Yanga na Azam FC.
Hii ni aibu kubwa. Aibu ambayo itaendelea kumsumbua Ngassa
miaka nenda rudi, maana hata mapato ya Tanzania na Sudan ni tofauti. Kwa
kawaida, anaposajiliwa kwenye timu moja, ni njia ya kwenda kwingine.
Kama Ngassa angeenda Sudan, huenda angepata nafasi ya
kuonekana nchi nyingine na kuonyesha uwezo wake. Labda amejijua kuwa hana tena
muda mrefu uwanjani.
Kwamba uwezo wake unaelekea ukingoni? Hapana, mbona hadi leo
Athumani Idd Machuppa yupo nje anacheza soka? Ni mipango tu. Umri wa Ngassa
hauna tofauti kubwa na kiungo wa Tanzania, Henry Joseph Shindika anayecheza
soka la kulipwa nchini Norway.
Huyu Ngassa ana mshauri kweli? Nani ameshika funguo ya
mafanikio ya kijana huyu ambaye Taifa bado linamuhitaji? Hatukatai kucheza soka
la ndani, lakini kwa Ngassa ameshavuka.
Ilitakiwa aende kwanza nje kucheza soka, kabla ya kurudi
nyumbani kumalizia soka lake kama inavyojulikana. Je, kurudi kwake Yanga, ndio
kusema amefanikiwa?
Ina maana amenufaika na maisha yake ya kusajiliwa kwa gari?
Wenzake Ulaya wanaishi kwa fedha nyingi mno. Gari ambalo mara nyingi
linaonyeshwa kama danganya toto, ila soka la kulipwa lina manufaa makubwa mno.
Kwanza hata usajili wake si wa kiubabaishaji. Uliona wapi
Dunia ya leo mchezaji anawekewa mezani milioni 20 na akishapewa kuishia kwa
madalali, waliompigia chapuo kusajiliwa kwenye timu hiyo?
Hatuwezi kukubali wachezaji wetu wa Tanzania washindwe
kutumia fursa kuwafilisi mabosi wa soka duniani. Hakika siwezi kuvumilia. Mtu
kusajiliwa Azam na kuonyesha mapenzi kiasi cha kiubusu jezi kama sababu ya
kuachwa ni ujinga wa kutupwa.
Bila hata kumsifu mchezaji huyo, anapaswa kuambiwa kuwa amefanya
makosa makubwa, kiasi cha kulazimisha kurudi kule ulipotoka. Soka la Tanzania
ni wazi lipo kwa Simba, Yanga na sasa kwa Azam.
Hivyo kama timu zote hizi umevaa jezi zao, kwanini usikwee
pipa kutafauta maisha mengine ya soka? Kila la kheri Mbwana Samatta, Thomas
Ulimwengu, Ivo Mapunda, Shindika, Danny Mrwanda na wengineo mnaohaha kutafuta
maisha katika soka, maana Bongo ni porojo tu.
Tukutane wiki ijayo.
0712 053949
0753 806087
No comments:
Post a Comment