Na Kambi Mbwana, Dar es Salaam
MISS Tanzania mwaka 2012,
Brigitte Alfred, amewakumbusha wanaopenda kushiriki mambo ya urembo kuhakikisha
kuwa wanakuwa na malengo kabla ya kujiunga kwenye tasnia hiyo duniani.
Miss Tanzania 2012, Brigitte Alfred
Akizungumza jijini Dar es Salaam juzi, Brigitte alisema kuwa malengo ndio silaha ya kumuwezesha mtu kutimiza
kile anachokihitaji katika kipindi cha maisha yake.
Alisema wapo mabinti wazuri na
wenye sifa zote, ila wanashindwa kuendelea na kufika nafasi za juu kutokana na
kutoweka malengo tangu mwanzo wanapojiunga kwenye sanaa hiyo ya urembo.
Brigitte ambaye anashikilia
taji hilo kubwa la urembo Tanzania, alitumia muda huo kuwakumbusha washiriki na
wasichana wanaotaka kuwa warembo kuhakikisha kuwa wanapigania ndoto zao.
“Mimi tangu mwanzo nilisema
nakwenda Tanzania kushiriki Miss Tanzania, nikitokea Kenya ambako nilikuwa
masomoni, jambo ambalo hakika nimelifanikisha kwa kiasi kikubwa.
“Wakati huu ambao naelekea
kukabidhi taji kwa mrembo mwingine, naendelea na harakati zangu maana
ukishaingia kwenye sanaa hii na kushika taji ni mwendelezo wa maisha mengine
kwa kutumia mgongo huu ambao wengi wanautamani japo baadhi yao wanakosa
malengo,” alisema Brigitte.
Brigitte kwa sasa anaelekea
kukabidhi taji hilo kwa mrembo mwingine, hasa baada ya kinyang’anyiro cha
kuelekea Miss Tanzania 2013 kushika kasi kutokana na sehemu mbalimbali kuandaa
mashindano hayo ambayo baadaye yatahusisha mikoa, Kanda na baadaye fainali za
Taifa zitakazofanyika jijini Dar es Salaam.
No comments:
Post a Comment