Na Kambi Mbwana, Dar es Salaam
BENDI ya Extra Bongo, maarufu kama Next Level, Wazee wa Kiziguo,
imesema kuwa baada ya kusukiwa zengwe katika viwanja vya Garden Breeze,
Magomeni, sasa wanajipanga kutafuta sehemu nyingine ili kuendeleza bonanza lao
kwa ajili ya kuwapa burudani mashabiki wao.
Ally Choki, Mkurugenzi wa Extra Bongo
Akizungumza jijini Dar es Salaam, mapema wiki hii, Mkurugenzi wa
Extra Bongo, Ally Choki, alisema kuwa sehemu hiyo ikipatikana wataendelea na
bonanza lao la kila Jumapili.
Alisema kuwa awali bonanza lao la Magomeni lilikuwa na wapenzi
wengi, ndio maana mahasimu wao kimuziki waliona ugumu wa kupambana nao na
kujikuta wakianza kuwatafutia namna ya kuwaathiri.
“Kwa sasa tunachofanya ni kutafuta namna ya kurudisha bonanza letu
katika sehemu nyingine, ingawa tunafahamu kuwa tulipotoka tulisukiwa zengwe kwa
ajili ya kuiathiri bendi yetu.
“Hatuwezi kuangalia hilo, zaidi ya kujipanga zaidi kwa ajili ya
kuendeleza harakati zetu kimuziki, ukizingatia kuwa tulianzisha bonanza kwa
ajili ya kukutanisha wadau wote sehemu moja,” alisema Choki.
Extra Bongo mbali na kuwa na Choki kama Mkurugenzi, pia imekusanya
wanamuziki wenye uwezo wa kutisha, akiwamo Rogati Hega Katapila, Ramadhan
Masanja Banza Stone, Athanas, Khadija Kimobiteli na wengineo.
No comments:
Post a Comment