https://tpc.googlesyndication.com/simgad/8045142562622600543


Recent Post

Wednesday, May 15, 2013

Kiongozi wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo Chadema apigwa risasi mkoani Mbeya

Katibu mwenezi wa Chadema wilaya ya Mbeya Vijijini Jackson Mwasenga, ambaye pia ni Mwenyekiti wa kitongoji cha Mzalendo kijiji cha Ndola mjini Mbalizi, akiwa katika hospitali ya Mbalizi Ifisi, akipata matibabu baada ya kupigwa risasi na watu wasiojulikana.(Picha na Gordon Kalulunga)

Na Gordon Kalulunga, Mbalizi
KATIBU mwenezi wa Chama cha demokrasia na maendeleo (Chadema) wilaya ya Mbeya Vijijini mkoani hapa, Jackson Mwasenga, amenusirika kifo baada ya kupigwa risasi nyumbani kwake.

Akizungumza na kikosi kazi cha kalulunga blog katika hospitali teule ya wilaya ya Mbeya, Mbalizi –Ifisi, alisema kuwa tukio hilo lilitokea Mei 10, mwaka huu  alipokuwa nje ya nyumba yake akitokea matembezini.

Alisema siku hiyo alikuwa na wenzake watatu na baada ya kuagana nao alielekea nyumbani kwake na alipojaribu kugonga hodi hakufunguliwa takribani nusu saa.

Alipoulizwa ndani ya nyumba yake alikuwemo nani, alisema kuwa kulikuwa na familia yake akiwemo mkewe.

‘’Nilipofika nyumbani majira ya saa mbili usiku, niligonda hodi takribani nusu saa hivi, kabla sijafunguliwa ndipo walijitokeza watu wawili na mmoja akarudi upenuni kisha yule mwingine akanipiga risasi kiganjani na kwenye paja nikaanguka’’ alisema Mwasenga.

Mwasenga ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kitongoji cha Mzalendo katika kijiji cha Ndola mjini Mbalizi, alisema baada ya kuanguka, alipata ujasiri wa kuanza kumkimbiza aliyempiga risasi huku akipiga kelele za kuomba msaada.

Baada ya hapo anabainisha kuwa alichukuliwa na vijana kwenye pikipiki na kukimbizwa polisi kisha hospitalini ambako anaendelea kupata matibabu na alitolewa risasi kama goroli kwenye mkono wake.

“Nawashukuru watu wote walionisaidia na zaidi madaktari wanaoendelea kunihudumua, tukio hili silihusishi na jambo lolote ikiwemo siasa bali naamini kuwa waliofanya hivi ni wahalifu kama wahalifu wengine’’ alisema kiongozi huyo.

No comments:

LinkWithin

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...