Mkuu wa Mkoa Kilimanjaro, Leonidas Gama
AWALI ya yote,
nimefarijika kupewa nafasi hii muhimu ya kufungua Kongamano hili la Tatu la
Wanahabari na wadau wa Habari Mkoani Kilimanjaro
Ni matumaini
yangu kwamba Kongamano hili limekutanisha waandishi wa habari na wadau
mbalimbali kutoka hapa Mkoani na kila mmoja kwa nafasi yake ni kama sehemu ya
familia moja katika kusukuma mbele gurudumu la maendeleo ya Mkoa wetu.
Ndugu
Mwenyekiti,
Ili kufikia lengo
la kuinufaisha jamii ya Wanakilimanjaro na Taifa kutokana na huduma
mbalimbali zitolewazo na taasisi tofauti, ushirikiano wa pamoja kati ya
Serikali, Wafanyabiashara wa bidhaa na huduma, wananchi pamoja na vyombo vya
habari ni jambo la msingi.
Ndugu
Mwenyekiti,
Napenda kutumia
fursa hii kutoa pongezi kwa wanachama wote wa MECKI chini uongozi wa mwenyekiti
wa MECKI Rodrick Makundi na kamati nzima ya utendaji kwa kuwa mstari wa mbele
kuhakikisha kuwa Klabu yenu inasonga mbele na kutekeleza majukumu yake kwa
kufuata utaratibu mliojiwekea.
Kama mlivyoelezea
malengo ya kongamano hili, naamini kongamano hili litafungua ukurasa mpya wa
mahusiano yaliyoboreshwa baina ya wanahabari na wadau wengine kwa ujumla wake
kwani kwa kipindi kifupi nilichokuwepo mkoani hapa nimeshuhudia mchango mkubwa
wa vyombo vya habari katika kuisadia serikali kutekeleza vyema wajibu wake
lakini pia kukosoa pale ilipokuwa inaonekana inafaa. Kukosoa na siyo
kulaumu au kulalamika.
Ndugu
Mwenyekiti ,
Kutafuta na kutoa
habari katika nchi yetu ni haki ya kikatiba kama ilivyobainishwa na Katiba ya
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 katika Ibara ya 18(b) inayompa
uhuru Mtanzania kufanya shughuli zake katika tasnia ya habari.
Katiba yetu
kupitia Ibara hiyo inatamka wazi kuwa kila mtu anayo haki kutafuta,kupokea na
kutoa habari bila kujali mipaka ya nchi.
Napenda
niwahakikishie wanahabari wa mkoa wa Kilimanjaro kuwa serikali ya mkoa wa
Kilimanjaro inatambua kuwa kazi zinazofanywa na wanahabari ni kazi halali kwa
mujibu wa Katiba na Sheria za nchi yetu. Fanyeni kazi kwa kuzingatia
weledi na maadili ya nchi yetu.
Hivyo napenda
niwatie moyo kuwa mfanye kazi kwa bidii, kujiamini na uhuru kama wananchi
wengine wanavyofanya shughuli halali katika mkoa wetu.
Ndugu
Mwenyekiti,
Katika nchi yetu
kuna tatizo la watu kutumia vibaya nafasi walizonazo ambazo ni kwa ajili ya
kuutumika umma badala yake wanazitumia nafasi hizo kwa maslahi yao wenyewe au
kutumikia makundi ya wachache katika jamii. Napenda nieleweke kuwa tatizo hili
limeshaanza kuingia katika tasnia muhimu ya habari jambo ambali kwa maoni yangu
naona ni hatari kwa uchumi na amani ya nchi yetu.
Tasnia ya habari
ina mchango mkubwa katika kustawisha maendeleo ya nchi katika nyanja zote
muhimu kama itatumika vizuri kwa waandishi wa habari kusimama katika nafasi yao
ya kuutumikia umma wa watanzania.
Lakini ikiwa
kinyume chake tasnia ya habari itatumika kueneza uongo, fitina, chuki na
uhasama kwa wananchi jambo ambalo madhara yake kwa wananchi ni kukosa
nafasi ya kufikiria namna ya kufanya kazi kwa bidii ili kupambana na umasikini,
badala yake watabaki kunyosha vidole kwa kila mmoja kumuona mwenzie ni adui na
si ndugu tena huku taifa likirudi nyuma baadala ya kusonga mbele.
Madhara makubwa
ya ukiukwaji wa sheria na maadili katika uandishi wa habari ni kuingiza nchi
katika machafuto, jambo ambalo litatugharimu kurudi nyuma katika maendeleo
tuliyofikia, mipango tuliyojiwekea, rasilimali zetu na maisha yetu.
Napenda niwatahadharishe kuwa wapo watu wasio penda mafanikio
ambayo tumefikia. Na wanaweza kuwatumia ninyi wanahabari kupotosha umma
na hatimaye nchi yetu ikaingia kwenye machafuko. Sote ni mashahidi na
tumejionea jinsi vyombo kama hivi vilivyoweza kutumika katika nchi kama Rwanda
na Burundi katika kuchochea fitina, chuki, mifarakano mikongoni mwa wananchi na
hatimaye kusababisha machafuko yaliyogharimu upotevu wa mali na maisha ya watu.
Ni vyema
wanahabari mkazingatia maadili ya taaluma yenu kwa kuhakikisha mnaandika habari
za kweli na zilizofanyiwa utafiti wa kina, kwani kalamu ni sehemu ya silaha
katika uwanja wa vita.
Ndugu
Mwenyekiti,
Nchi yetu ni ya
kidemokrasia, na kila kwenye demokrasia ya kweli haki za msingi za binadamu
zinazingatiwa na hakuna uhuru usio na mipaka. Napenda niwakumbushe wanahabari
kuwa uhuru wa mtu unaishia pale unapoanzia uhuru wa mtu mwingine.
Uhuru wa habari
unaelezwa wazi katika Ibara ya 18 (a) ya katiba ya Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania. Ni kujua kuwa Katiba hii imeweka mipaka ya uhuru huo
katika Ibara ya 16(1) inayompa mtu uhuru wa kuhifadhiwa nafsi yake, maisha yake
pamoja na kuheshimiwa.
Ni matarajio
yangu kuwa wanahabari wa Mkoa wa Kilimanjaro hamtaniangusha kwa kuandika habari
bila ya kuzingatia sheria, haki za binadam na maslahi ya Mkoa na Taifa.
Ndugu
Mwenyekiti,
Tunaelekea katika
kuandika katiba mpya ya Jamhuri ya Mungano wa Tanzania, huu ni wakati wenu
kuwaelimisha wananchi mambo muhimu yanayopaswa kuzingatiwa na kuacha kushabikia
masuala yanayoweza kupotosha mchakato mzima. Wengi duniani hawajaweza
kupata Katiba katika hali ya utulivi na amani. Nawapongeza wananchi wa Mkoa wa
Kilimanjaro.
Msikubali kwa
namna yoyote kuvuruga misingi imara iliyowekwa na waasisi wa Taifa hili,
wakiongozwa na Hayati baba wa Taifa Mwl Julius Nyerere ambaye kwa kipindi cha
uhai wake wote alihubiri na kuamini katika umoja na mshikamano miongoni mwa
watanzania.
Aidha waandishi
wa habari si vyema kujiingiza katika misuguano isiyokuwa na misingi na baadhi
ya taasisi bali ni nyema kila mmoja kwa nafasi yake akatimiza wajibu wake
badala ya kuviziana kwa baadhi ya mambo.
Ndugu
Mwenyekiti,
Pamoja na
waandisi wa habari lakini pia ni wajibu wa wadau kuhakikisha kuwa wanatoa
ushirikiano kwa wanahabari, kwa kuacha kuficha taarifa ambazo zinapaswa
kuwafikia wananchi, kwani jambo hili limekuwa likileta msuguano baina ya wadau
na wanahabari na kufikia hatua ya kuhatarisha mahusiano baina ya pande hizi
mbili.
Mara kadhaa
tumemsikia Rais Jakaya Kikwete akisisitiza taasisi na ofisi za Umma kutoa
habari kwa waandishi ili nao waweze kuihabarisha jamii kulingana na jambo
husika
Ndugu
Mwenyekiti,
Nitoe wito
kwa wadau wote wa habari mkoani Kilimanjaro, itumieni ipasavyo Klabu hii
ya waandishi wa habari (MECKI) katika masuala yenu yanayohusu kuuhabarisha umma
mambo mbalimbali, Watumieni waandishi wa habari kuuhabarisha umma, shirikianeni
na wekeni wazi habari kwa maslahi ya umma kutegemeana na taraibu na sheria za
uandishi wa habari.
Fanyeni kazi kwa
karibu na Halmashauri zetu zote katika mkoa wetu kuripoti habari za maendeleo
ya wananchi hasa wa vijini. Katika eneo ambalo serikali inatenga fedha nyingi
za maendeleo ni halmashauri, hivyo basi habari zinazogusa maendeleo ya wananchi
zipo katika halmashauri zetu.
Moja kati ya
matatatizo yaliyomo katika jamii ni watu kutojua kinachoendelea hasa juhudi zinazofanywa
na serikali na taasisi zingine katika kuwawezesha wananchi kujiletea maendeleo.
Kama kuna kiongozi au mtumishi asiyetoa ushirikiano kwa waandishi mniambie.
Ndugu
Mwenyekiti,
Napongeza mpango
wenu wa maendeleo uliopita na huu mliuiweka wa sasa. Wekeni mipango madhubuti
ya maendeleo na utekelezaji wake.
Sitarajii kusikia
suala la Sacoss likiwasilishwa kama mpango tutakapokutana katika kongamano
lijalo. Nataka kusikia kutoka kwenu juu ya maendeleo ya Sacoss yenu. Mkiwa na
uchumi imara mnaweza kufanya shughuli zenu kwa amani na kujiamini kutokana na
nguvu za kiuchumi zitakazotokana na SACOSS yenu.
Tumieni kongamano
hili kuelezana na kupanga utaratibu mzuri wa kufanya kazi na chombo hiki, na
waandishi wa habari kwa ujumla, ili taarifa zote za maendeleo ziwafikie
wananchi kwa maslahi ya umma.
Mwisho, kubwa
zaidi ni ninyi kama wadau kuwaona wanahabari kama sehemu ya jamii badala ya
kuwaona ni maadui na wenye lengo la kuharibu sifa za taasisi zenu au kampuni.
Vyombo vya habari
vinaweza kujenga kama mtavitumia vizuri lakini pia vinaweza kubomoa kama
hamtaonyesha ushirikiano.
Baada ya kusema
hayo natangaza rasmi kuwa Kongamano hili la Tatu la Wanahabari kuhusu Maendeleo
ya Mkoa wa Kilimanjaro limefunguliwa rasmi.
Ahsanteni sana
kwa kunisikiliza.
No comments:
Post a Comment