Na Mwandishi Wetu, Ethiopia
BALOZI wa Tanzania
nchini Ethiopia, Joram Biswaro amewataka wachezaji wa Taifa Stars kuhakikisha
wanaipeleka timu hiyo kwenye fainali za Kombe la Dunia zitakazofanyika mwakani
nchini Brazil.
Nyota wa Taifa Stars, Mrisho Ngassa
Ametoa changamoto hiyo
wakati alipotembelea mazoezi ya timu hiyo jana (Mei 29 mwaka huu). Taifa Stars
inayodhaminiwa na Kilimanjaro Premium Lager imepiga kambi nchini Ethiopia na
inafanya mazoezi kwenye Uwanja wa Addis Ababa.
“Watanzania tunafurahi
kutokana na uwezo mnaouonyesha, hasa baada ya kuifunga Morocco mabao 3-1. Kama
mliwafunga nyumbani hata kwao mnaweza kuwafunga. Tunataka kuwaona Maracana
(Brazil) mwakani, mimi tayari ninayo tiketi mtanikuta kule,” amesema Balozi
Biswaro ambaye enzi zake aliwahi kuichezea timu ya Yanga.
Taifa Stars ambayo iko
Addis Ababa tangu Jumatatu (Mei 27 mwaka huu) imeweka kambi katika hoteli ya
Hilton ambapo Jumapili (Juni 2 mwaka huu) itacheza mechi ya kirafiki na Sudan
(Nile Crocodile) kwenye Uwanja wa Addis Ababa.
Balozi Biswaro ameikaribisha Taifa Stars ubalozini Addis
Ababa mara baada ya mechi dhidi ya Sudan ambapo itakutana na baadhi ya
Watanzania wanaoishi Ethiopia kabla ya kuondoka alfajiri kwenda Marrakech,
Morocco kwa kupitia Cairo, Misri.
Kocha Kim Poulsen amesema
kikosi chake kinaendelea na mazoezi vizuri na kitaimarika zaidi baada ya
wachezaji Mbwana Samata na Thomas Ulimwengu wanaochezea timu ya TP Mazembe ya
Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC) kujiunga nacho Juni 3 mwaka huu jijini
Marrakech kwa ajili ya mechi dhidi ya Morocco itakayochezwa Juni 8 mwaka huu.
Wachezaji walioko katika
kikosi cha Stars jijini Addis Ababa ni Juma Kaseja, Aggrey Morris, Mwadini
Ally, Ally Mustafa, Shomari Kapombe, Kevin Yondani, Erasto Nyoni, Haroub Nadir,
Mwinyi Kazimoto, Frank Domayo, Mrisho Ngasa, Khamis Mchana, Amri Kiemba, Salum
Abubakar, Simon Msuva, John Bocco, Vicent Barnabas, Mudathiri Yahya, Athuman
Idd, Haruni Chanongo na Zahoro Pazi.
No comments:
Post a Comment