Mganga wa jadi Aweso Kipaku
ambaye ni diwani wa kata ya Mswaha iliyopo wilayani Korogwe, akiwa ameshikilia
kitu kinachodaiwa ni jini alilolitoa katika moja ya darasa la shule ya msingi
Kwemsala iliyopo kata ya Mtindiro wilayani Muheza juzi, wengine aliyevaa fulana
ya punda milia ni mwenyekiti wa kamati ya shule hiyo Shabani Hamisi.
Na Mashaka Mhando, Muheza
LICHA ya serikali mkoani Tanga kusikika ikipiga marufuku masuala ya utoaji uchawi katika sehemu mbalimbali za wilaya zake mkoani humo, lakini diwani wa Kata ya Mswaha,
iliyopo wilayani Korogwe, Aweso Kipaku ambaye pia ni mganga aliendeleza shughuli hizo katika kijiji cha Kwemsala, wilayani Muheza mkoani Tanga, kwa madai kuwa shule ya kijiji hicho ilikuwa na imani za ushirikina.
Akifanya kazi hiyo, juzi katika
shule hiyo Diwani huyo aliyealikwa na kamati ya shule ya kijiji hicho, alianza
kupita kila darasa la shule hiyo huku akionekana amepandisha mapepo yaliyokuwa
yakimuongoza huku wananchi wa kijiji hicho wakijazana kuona kazi anayofanya
diwani huyo.
Diwani huyo mara baada ya
kukimbizana na vitu vilivyokuwa havionekani kwa macho, alipoingia kwenye ofisi
inayokaliwa na walimu, alipiga kelele kutaka aletewe unga wa sembe, maji na
kuku alipopata vitu hivyo, aliibuka na pembe kubwa iliyokuwa imefungwa vitambaa
vyeupe na vyekundu.
"Wananchi hivi vitu
vilivyotoa mnavyoviona ndivyo vilivyokuwa vikiwasumbua wanafunzi, lakini jini
jingine kubwa limekimbia huko katika makazi...Kazi ya kupambana nalo nitaifanya
kesho (Ijumaa iliyopita)," alisema diwani huyo huku akiwa amekishika
mkononi.
Akizungumza na wananchi mara
baada ya diwani huyo kutoa vitu hivyo, Mwenyekiti wa kamati ya shule Shaban
Hamis alisema tatizo la wanafunzi kuanguka katika shule hiyo lilianza tangu
mwaka juzi na walipoitisha mkutano wa kijiji, viongozi wa dini walisema
wangefanya maombi kuwanusuru watoto hao, lakini hawakuweza kufanya maombi hayo.
"Tuliona watoto wetu
wanaendelea kuanguka wakipelekwa hospitali wanelezwa wana matatizo ya
kisaikolojia, lakini tukiwapeleka kwa waganga wa kienyeji wanatibiwa na kupona,
tukaona ni vema tumlete mganga huyu Kipaku (Diwani) ili awanusuru watoto
wetu," alisema mwenyekiti huyo.
Mwalimu mmoja shuleni hayo
Sophia Msangeni, alisema tatizo la wanafunzi kuanguka limekuwa likisababisha
kushuka kwa taaluma shuleni hapo hatua ambayo ilikuwa ikileta kero na usumbufu
mkubwa mara inapotokea suala la watoto kuanguka ambapo kwa siku wanaanguka
watoto 20.
No comments:
Post a Comment