https://tpc.googlesyndication.com/simgad/8045142562622600543


Recent Post

Wednesday, May 22, 2013

Mtwara kwatikisika mabomu, wananchi wahamasishana kwa meseji za simu na nyumba kwa nyumba, watu wanne wahofiwa kufa


Na Mwandishi Wetu, Mtwara
SAA chache baada ya Waziri wa Nishati na Madini, Mheshimiwa Sospeter Muhongo kusoma Bajeti ya Wizara yake Bungeni, hali imelipuka ghalfa mkoani Mtwara kutokana na watu kuingia barabarani na kuanza upya vurugu zao, huku ikidaiwa kuwa hadi muda huu huenda watu wanne wamepoteza maisha.
 Askari
Wananchi hao Mkoani Mtwara wameamua kuingia barabarani na kuanza kufanya fujo zilizopelekea polisi kuanza kufyatua mabomu ya machozi kwa ajili ya kuwatawanya waandamanaji hao wanaoshindana na serikali kwa miezi kadhaa sasa.

Awali, wananchi wote mkoani Mtwara siku ya leo ilikuwa kufuatilia mambo ya Bunge yanavyokwenda, huku wakiwa na hamu ya kuona nini kitaamuliwa katika Bajeti ya Muhongo, wakitaka kuona mkoa wao unapendelewa zaidi kwa uwapo wa gesi.

Baada ya kuona bajeti hiyo ipo tofauti na dhamira yao, waliamua kurudi tena kwenye harakati zao kwa ajili ya kushinikiza malengo yao kwa serikali juu ya gesi.

Hadi sasa, mabomu yanaendelea kulipuliwa mjini hapa na wengi wasiokuwa na uwezo wa kushiriki, hasa wazee wakiwa wamejichimbia majumbani mwao.

Sera ya mkoani Mtwara ni gesi kwanza, uhai baadaye, moja ya kauli mbiu zinazotumika kuwapa kiburi wananchi. Tangu kuzuiwa kufanyika kwa mikutano ya hadhara, wananchi wanatumia mbinu mpya ya kuhamasishana kwa njia ya meseji na vipeperushi na wakati mwingine kwa njia ya usafiri wa umma na kwenye maduka.

Taarifa zaidi zitaendelea kukujia ikiwa ni pamoja na maddhara ya vurugu hizo mkoani Mtwara.

No comments:

LinkWithin

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...