MAMBO FULANI MUHIMU
Na Kambi Mbwana, Dar es Salaam
NATUMIA muda huu kuwapongeza waandishi wa Habari duniani
kote, hususan wa Tanzania, baada ya jana kusherehekea Siku ya Maadhimisho ya
Uhuru wa Vyombo vya Habari.
Picha hii ni ishara mbaya kwenye uhusiano wa kimapenzi.
Ni jambo la jema kwa kuwapo watu hawa, maana wamekuwa
wakifanya mengi yanayopelekea faida kwa jamii nzima. Bila vyombo vya habari,
jamii isingejitambua kwa namna moja ama nyingine.
Bila vyombo vya habari na waandishi wao kwa ujumla, hata
uchumi katika kila nchi usingeweza kukua. Bila waandishi wa habari, Dunia
ingeendelea kubaki katika mfumo wa zamani, kiasi cha kushindwa kujua Tanga,
Arusha na mikoa mingine kunaendelea na kitu gani.
Nikiacha hayo, nirudi sasa kwenye dhima ya ukurasa huu wa
Mambo Fulani Muhimu, huku nikiamini kuwa msomaji wangu tutaendelea kuwa pamoja,
tukijadili na kujifunza hili na lile.
Ndugu msomaji wangu, madamu sisi ni binadamu, hutokea
kukorofishana kiasi cha kutuweka katika mtihani mzito. Katika suala la mapenzi,
kugombana na kupatana ni jambo la kawaida.
Waswahili wanasema, kama vikombe kabatini vinagongana
itakuwa sisi binadamu? La hasha. Hata hivyo, katika kuangalia kwanini watu
wanagombana na kufikia kuombana msamaha, yapo mambo muhimu yanayosababisha
kutokea kwa jambo hilo.
Kubwa kabisa ni pale watu hao wanaposhindwa kuanza ukurasa
mpya, yani kuanzisha uhusiano na mtu mwingine. Wapo watu wanaoachana na wapenzi
wao, wake au waume zao, lakini wanaishi peke yao kwa zaidi ya miezi mitano au
mwaka kabla ya kufikiria kuwa na mtu mpya.
Na mtu huyo anaishi peke yake, akimuomba Mungu, kama mpenzi
au mume wake anaweza kujirekebisha katika baadhi ya kasoro zilizojitokeza
katika uhusiano huo uliowaletea usumbufu.
Kwanini mtu huyo asitafute mpenzi mpya au ndoa mpya kwa
haraka wakati ameshaachana na mtu wake? Hakika wapo baadhi ya watu ambao kuanza
upya kwao ni jambo gumu mno.
Anaweza kukutana na mtu mpya, akarubuniwa kwa namna moja ama
nyingine, lakini anapofikiria jinsi ya kukutana uhusiano mpya, akifikiria kila
jambo jipya, damu humchemka na kuona hawezi.
Maswali mengi anajiuliza. Itakuwaje huyo anayetaka kuanza
naye uhusiano mpya akiwa na kero zaidi ya yule aliyeachana naye? Je, atawezaje
kushiriki naye kwenye tendo la ndoa?
Je, ataendelea kuongeza idadi ya wanaume au wanawake aliyofanya
nao tendo la ndoa hadi lini? Je, itakuwaje watu hao wakifikia walau kumi na
kukutana pamoja katika kazi za kijamii au kiburudani.
Fikiria, wewe unakuwa na mpenzi wako disco na kukutana na
watu tisa wamekaa pamoja na wote umewahi kufanya nao ngono? Unajionaje? Hakika
kama ni mtu mwenye busara na heshima lazima utasononeka.
Ndio maana baadhi ya watu wapo radhi kurudiana na wapenzi
wao, waume au wake zao kama waliachana bila matatizo makubwa. Kuna kuachana kwa
aina nyingi na kurudiana kwa aina nyingi.
Kwa mfano, kama ulimfumania mke au mume wako akitoka na mtu
mwingine wa nje, wale wasiotaka umalaya wanaumia kurudiana na watu hao. Lakini
wale ambao walikwaruzana tu kibinadamu, kama vile kutojua wajibu kwa mtu wako,
kutokuwa na upendo kwa ndugu au kushindwa kujiweka katika jamii vizuri na
kuibua kero kwa mpenzi wako.
Haya na mengineyo yanaweza kuleta ugumu wa kuanza uhusiano
mpya na wengine, hivyo kumtafuta mwanamume wako, mke au mpenzi wako na kukaa
naye chini na kujadili tatizo.
Mengi yatazungumzwa na hakika kuzalisha uhusiano mzuri kwa
watu hao ambao waliachana baada ya kutokea kutoelewana. Haya ni machache kati
ya mengi yanayoleta ugumu wa kuanza uhusiano mpya kila siku.
Wanaona bora tu warudiane na watu wao. Tena ni vizuri zaidi,
maana unayemjua utafurahia zaidi kuwa naye kuliko yule unayeanza naye uhusiano.
Ndio maana wanawake wengi wanaojitambua na kujaa heshima
hufikiria uhusiano mpya na hakika wengineo wanalia usiku kucha wakiona ugumu wa
kuanza uhusiano mpya na kutaka kurudiana na watu wao wa zamani.
Tukutane wiki ijayo.
0712 053949-0753 806087
No comments:
Post a Comment