https://tpc.googlesyndication.com/simgad/8045142562622600543


Recent Post

Friday, May 31, 2013

Ngwea kulala kwanza Muhimbili kesho akiletwa nchini, wakati P-Funk afunga mdomo juu ya kuwapiga biti Clouds FM



Na Kambi Mbwana, Dar es Salaam
HUKU wakikanusha ripoti  za awali zinazoendelea kusambaa juu ripoti ya kifo cha msanii Albert Mangwea, Kamati ya Mazishi ya msaniii huyo, imesema kuwa inatarajia kuuleta mwili wa marehemu huyo kesho kama ilivyopangwa na kuuaga Jumapili katika Viwanja vya Leaders Club, baada ya kulala katika Hospitali ya Taifa Muhimbili kwa siku moja.
                                 Marehemu Mangwea
Mangwea moja ya wasanii nyota hapa nchini alifariki nchini Afrika Kusini na kuzua huzuni kubwa kwa wadau wa muziki na Watanzania kwa ujumla, hasa kutokana na umahiri wake kwenye kazi hiyo, huku kifo chake kikipokelewa kwa masikitiko makubwa mno na redio zote kusikika mara kwa mara nyimbo zake zikipigwa kama sehemu ya kuomboleza msiba wa msanii huyo nyota.
                               P-Funk Majani
Mara baada ya kuwasili kesho, mwili wa marehemu utafikia kwanza katika Hospitali ya Muhimbili huku siku inayofuata ratiba zilizopangwa kuendelea kwa ajili ya kuustili mwili wake.

Akizungumza jana jijini Dar es Salaam, Msemaji wa Kamati iliyoundwa ya kuratibu shughuli zote za msiba huo, Adam Juma, alisema kuwa maandalizi kwa ajili ya kuleta kwa mwili huo na utaratibu mzima wa maziko yake yanaendelea.

Alisema ili waweze kufanikisha suala hilo, wanaomba msaada wa Watanzania bila kubaguana kwa namna yoyote, maana Ngwea alikuwa mtu wa watu, hivyo hakuna haja ya kuleta propaganda katika suala hilo.

“Tunakabiriwa na changamoto nyingi katika msiba huu, hivyo tunawaomba Watanzania wenzetu waweze kutuchangia kwa namba ya Vodacom, 0754 074323 au Tigo 0658 074324 ambazo fedha zote zitaingia kwenye simu za kaka wa marehemu, Kenneth Mangwea, ambaye ni kama mwenyekiti katika Kamati hii ya kuratibu mazishi ya msanii huyu.

“Kuna vitu vingi vya kufanya na vyote vinahitaji gharama, kama vile kuleta mwili wake, kuuaga sambamba na usafiri wa ndani, bila kusahau safari ya kuelekea Morogoro kwa ajili ya maziko yake,” alisema.

Aidha, Kamati hiyo inayoongozwa na Shirikisho la Muziki Tanzania, chini ya Rais wake, Addo Novemba, ilisema kuwa ripoti iliyoanza kutolewa jana kwenye mitandao ya kijamii si ya kweli.

“Tunaomba Watanzania tuendelee kuwa na subira katika suala hili, maana ripoti iliyosambazwa kwenye mitandao si ya kweli na imeletwa kwa ajili ya kumdhalilisha marehemu Ngwea,” alisema Novemba.

Msiba wa Ngwea umepokelewa kwa masikitiko makubwa na Watanzania, hasa kutokana na mchango wake katika tasnia ya muziki wa kizazi kipya, maarufu kama Bongo Fleva, akitamba na nyimbo nyingi, kama vile Gheto Langu, Mikasi, Speed 120 na nyinginezo lukuki.

Aidha, mtayarishaji wa muziki wa Bongo Fleva nchini, P-Funk, amefunga mdomo kuelezea kwanini aliamua kuwapiga marufuku redio ya Clouds FM kucheza nyimbo alizorekodi yeye na kuimbwa na marehemu Ngwea enzi za uhai wake.

"Kwa sasa sitaki kusema lolote juu ya nyimbo hizo za Ngwea kuchezwa au kutochezwa Clouds FM," alijibu kwa kifupi akiwa na maana ya kuelekeza akili yake kwenye msiba wa msanii Ngwea.

No comments:

LinkWithin

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...