Na Kambi Mbwana, Dar es Salaam
SANAA ni moja ya vitu vinavyohitaji uvumilivu na kujitoa kwa
nguvu bila kuchoka, hasa kama lengo ni kuhakikisha kuwa mafanikio yanapatikana
kwa namna moja ama nyingine.
Fadhili Athuman Soldier, pichani
Wasanii ambao hawana uvumilivu, hushindwa kuhimili
changamoto zinazojitokeza katika tasnia ya sanaa Tanzania, ukizingatia kuwa mtu
anayejiingiza kwa mara ya kwanza huhitaji muda hadi kuweza kutangaza na
kuonyesha kipaji chake kwa hadhira.
Soldier, mkali wa filamu Tanzania
Kwa wale waliofanikiwa kuwa na uvumilivu, ndio hao wanaoishi
maisha mazuri leo majina yao yakitajwa au kuandikwa kila mahali jambo
linaalowapatia heshima kubwa kwenye jamii.
Miongoni mwa wasanii ambao licha ya kukabiriwa na changamoto
za aina yake, lakini bado wanavumilia na kuzidisha uchu wa mafanikio katika
tasnia ya soko la filamu hapa nchini, ni Fadhili Athuman, maarufu kama Soldier.
Kijana huyu kwa yupo kwenye hatua za mwisho kuingiza sokoni
filamu yake ya More Fire, aliyoiandaa kwa umakini mkubwa akiwa na lengo la
kuonyesha cheche zake katika ulingo huo nchini.
Kabla ya kufanikiwa kukamilisha filamu hiyo, Soldier
alishiriki katika tamthilia mbalimbali, ikiwamo ile ya Cinderela, iliyokuwa
inarushwa na kituo cha televisheni cha Star Tv ya jijini Mwanza.
Katika mazungumzo yaliyofanyika hivi karibuni, Soldier anasema kuwa katika tamthilia hiyo na nyingine alizowahi kucheza,
msanii huyo ameweza kuonyesha umakini wa aina yake katika kuigiza, hivyo baadhi
ya watu kumtabiria mafanikio siku za usoni.
“Sanaa ya Tanzania inahitaji uvumilivu na hakika naendelea
kupigania mafanikio kwa namna moja ama nyingine, ukizingatia kuwa nimechagua
sanaa kuwa sehemu ya maisha yangu.
“Hakuna kitu ninachowaza zaidi ya sanaa, hivyo naamini mambo
yataendeleaa kuwa mazuri, hasa kwa kuandaa filamu zenye kiwango cha juu na
kuwaonyesha watu namna gani kazi inatakiwa ifanywe,” alisema.
Katika filamu yake hiyo ya kwanza kuandaa, amewashirikisha
wasanii mbalimbali, akiwamo mnenguaji wa FM Academia, Queen Suzy, Kaila, Bi
Fetty, Zuma, Sacy, Ngamakisi, Ize, Shelii, Todi.
Anasema kuwa filamu hiyo ya aina yake, ameandaa chini ya
Kampuni yake Tanzania One Production yenye maskani yake jijini Dar es Salaam na
iliyopania kufanya vyema katika sanaa nchini.
Msanii huyo anaendelea kusema kuwa kabla ya kuamua
kutengeneza filamu hiyo, alianza zamani kujiingiza kwenye sanaa na kufanikiwa
kucheza tamthilia na filamu za watu wengine.
Anaitaja filamu ya Wema iliyoandaliwa na msanii wa
vichekesho nchini, Senga, huku akishiriki na wasanii wengine nyota na kuiweka
juu filamu hiyo miaka kadhaa iliyopita.
Tamthilia alizowahi kucheza Soldier ni pamoja na Cinderela
mwaka 2011, Ua Jekundu iliyokuwa ikirushwa mwaka 2004, Doa mwaka 2005 katika
televisheni ya Chanel Ten, Zeze TBC 1 mwaka 2007.
Makundi aliyowahi kupitia msanii huyo na kujifunza sanaa ni
pamoja na Fukuto Arts Group mwaka 2002 ambao lilifanikiwa kutengeneza tamthilia
yao ya Ua Jekundu, wakati mwaka 2004 alijiunga na kundi la Dar Talent, huku
miaka miwili baadaye akijiunga na kundi la Sea Breeze.
Hata hivyo, msanii huyo hajaweza kudumu na makundi hayo
kutokana na mpangaranyiko wa kiutawala kwa baadhi ya viongozi wao, hivyo kuamua
kukimbilia Watoto wa Tembo na baadaye Bongo Hood.
“Huko kote nilikuwa napigania maisha yangu kwa kupitia sanaa
ya maigizo na filamu hapa nchini, jambo ambalo lilifanikiwa kuniweka katika
mazingira mazuri na kuuweza ushindani uliopo.
“Ingawa bado sina jina kubwa, lakini wote wanaonijua mimi
wanajua uwezo wangu, huku nikipania malengo ya juu zaidi kuhakikisha kuwa
naweza kupambana kwa namna moja ama nyingine,” alisema.
Soldier anaelezea ushindani uliopo kuwa unachangia kukuza
soko la sanaa kwa ujumla, hivyo ni jukumu lake kuhakikisha kuwa anaweza
kutangaza kipaji chake kwa wadau wa sanaa nchini.
Msanii huyo anasema kuwa japo sanaa ni moja ya sekta
zinazowalipa wasanii, lakini baadhi yao wameshindwa kutumia ubunifu kwenye kazi
zao, jambo linaloweza kuharibu soko lao.
Anasema baadhi ya watu wamekuwa wakitunga filamu
zisizojitosheleza kwa hadithi nzima, mpangilio wa matukio, uongozi na hata
wachezaji kutovaa uhalisia wa mambo kwenye filamu kwa ujumla.
Jambo hili lilifanyika, baadhi ya wadau ambao ndio
wanaoiweka sanaa juu
hujikuta wakiishiwa na mapenzi ya kuwaunga mkono wasanii
wa Tanzania na kuendelea kuangalia kazi
za nje za Nigeria, India na Marekani ambako kazi zao zinaangaliwa na
kila mtu.
“Kwa kulijua hilo, kwenye filamu yangu hii ya More Fire na
nyingine nitakazobarikiwa kuandaa nitahakikisha kuwa wadau wangu wanaendelea
kuniunga mkono kwa kuwapa kazi nzuri.
“Nimepigania sana kulionyesha hilo, hivyo naamini mashabiki
wa sanaa Tanzania ni wakati wao kusubiria na kuitazama filamu hiyo yenye ujazo
wa kila aina kuanzia mtiririko wa matukio na wasanii waliyocheza,” alisema
Soldier.
Msanii huyo aliyezaliwa mwaka 1985 kijiji cha Mzenga,
wilayani Kisarawe mkoani Pwani, anasema kwa sasa hana cha kupoteza zaidi ya
kuongeza ubunifu kwenye kazi zake kwa ajili ya kuonyesha makali yake.
Soldier anawataka Watanzania, mashabiki na serikali
kushirikiana kwa pamoja ili kukuza soko la sanaa Tanzania ili iwe njia ya
kuwapatia maisha bora vijana wanaojiingiza kwenye tasnia hiyo.
Bila hivyo, sanaa itaendelea kusua sua na kuwa mradi wa watu
wachache wasiokuwa na huruma na watu wanaotumia gharama zao kubwa na muda
kuandaa filamu na anayekuja kunufaika ni mtu mwingine ambaye hajui tabu
alizokutana nazo muandaaji.
Soldier ni miongoni mwa vijana ambao wamekuwa na mapenzi
makubwa na sanaa Tanzania, huku nikiamini kuwa huenda akatimiza ndoto zake kama
ataendelea kukaza msuri na kujituma bila kuchoka.
No comments:
Post a Comment