Na
Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
WAKATI watu wakiwa kwenye wasiwasi kwa kipindi kirefu sasa katika sanaa ya muziki wa Bongo Fleva, hatimae uongozi wa Clouds Media Group kwa kupitia Mkurugenzi wa Utafiti na Matukio, Ruge
Mutahaba, umemtaka msanii wa Bongo Fleva, Judith Wambura, Lady Jay Dee kujipanga na kupokea changamoto badala ya kutafuta mahali kwa kujiegemeza kwa kueneza
matusi kwao hali inayochafua heshima yao katika jamii.
Clouds
Media wamefungua mdomo kwa mara ya kwanza kwa kipindi cha miezi mitano
tangu Jay Dee alipokuwa akiwarushia makombora kwa madai kuwa wameharibu soko la
muziki wa Bongo Fleva sambamba na kuitangaza bendi ya Skylight kwa ajili ya
kuiangamiza Machozi Bendi iliyoanzia katika mgongo wake.
Ruge Mutahaba
Akizungumza
jana jijini Dar es Salaam ambapo pia alikuwa akirushwa moja kwa moja katika
redio ya Clouds FM, Mutahaba alisema Jay Dee amekuwa akilalamikia mambo mawili
ambayo ni bendi ya Skylight na matangazo yake yaliyoshindwa kurushwa hewani
japo alilipia Sh 240,000.
Lady Jay Dee
Alisema
suala hilo walilimaliza baada ya kumueleza kuwa redio yao haiwezi kukataa
matangazo kwakuwa ndiyo wanayowafanya waendelee kuwa kinara katika suala zima
la kuiendesha Clouds FM.
“Nilimwambia
kamwe hatuwezi kukataa matangazo na kama kuna lolote limefanyika, basi ni kwa
bahati mbaya, ukizingatia kuwa tayari alishafanya kazi nyingi pamoja na kupewa
urahisi kwenye kazi zake kwa kupitia Clouds FM.
“Pamoja
na yote hayo, bado matusi na kejeli yaliendelea hasa katika mitandao ya kijamii
jambo lililotufanya tuamuwe sasa kujibu japo hapo kabla tuliamua kubaki kimya
kwa ajili ya kulinda hadhi ya kazi zetu,” alisema.
Kuhusu
shutuma za kuitangaza zaidi Skylight Bendi, Ruge alisema bendi hiyo si mali ya
Joseph Kusaga, Mkurugenzi wao wala yeye, kama madai hayo yanavyotolewa bila
kufanya utafiti, isipokuwa ni mali ya Sebastian Ndege.
“Kama
kuna mvutano kati ya Machozi Bendi na Skylight basi ni wa kibiashara maana wote
wanalipa fedha za matangazo na kama chanzo ni Jay Dee kuporwa wanamuziki wake,
hilo si jambo geni kwenye muziki.
“Dada
yangu Asha Baraka asingekuwa makini angelia sana, maana kila bendi
inayoanzishwa au kuendeshwa lazima ichukuwe wanamuziki kutoka kwake,
ukizingatia kuwa ni jambo la kawaida hivyo tumuomba Jay Dee atumie busara
katika hili pamoja na kuumiza kichwa kupokea ushindani na changamoto kama hizo
za kuchukuliwa wanamuziki,” aliongeza Ruge.
Aidha,
Ruge alisema Clouds FM ni redio ya watu binafsi, hivyo si ina utaratibu wake
katika utendaji wa kazi, ikiwapo kuchagua nyimbo au kuacha kupiga kama kuna mtu
amekwenda kinyume, hasa wale wanaopita nje na kuanza kuwatusi, kuwakejeli bila
kukumbuka fadhira walizofanyiwa kabla ya kuwa maarufu wao.
Pia
alisema Clouds FM ipo tayari kufanya majadiliano ya wazi na mtu yoyote mwenye
hisia tofauti juu yao, huku ikiwataka wasanii waongeze bidii katika kazi zao
ili wasimlaumu mtu wanapoanguka na kuwapisha wengine, maana muziki unaonekana
ni wa kupokezana vijiti.
Maneno
ya Ruge huenda yakapoza moto uliowashwa na Lady Jay Dee akiwatuhumu kuwa
wamedhamiria kuangusha kipaji chake na bendi yake, huku akitumia sana njia ya
mitandao ya kijamii kupambana vita hiyo na kuwaacha watu njia panda.
No comments:
Post a Comment