Mtuhumiwa Simon Jumbe anayetajwa kujifanya afisa wa Takukuru. |
TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na
Rushwa (Takukuru) Mkoa wa Mwanza imefanikiwa kumnasa mtu mmoja ambaye
anasadikika kuwa mkuu wa genge la watu wanaojifanya Maafisa wa Ofisi ya
TAKUKURU Mkoani hapa.
Akitoa taarifa kwa waandishi wa Habari ofisini kwake Kamanda wa TAKUKURU Mkoa wa Mwanza Ayubu Akida alisema kwamba kukamatwa kwa mtuhumiwa huyo aliyefahamika kwa jina la Simon Jumbe (32) lakini amekuwa akitumia majina mengie kwa kujiita Mapunda na SP ni kutokana na mtego uliowekwa na maafisa wake.
Kamanda wa TAKUKURU mkoa wa Mwanza Ayoub Akida, akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake leo. |
“Tuliweka
mtego huo kutokana na kuwepo taarifa za siri kutoka kwa raia wema ambapo
walitueleza kwamba kuna wimbi la baadhi ya watu ambao wamekuwa wakiwadanganya
watu kuwa wao ni maafisa na watumishi wa TAKUKURU baada ya kuweka mtego Mei 13
mwaka huu tumefanikiwa kumnasa huyu maeneo ya Kata ya Mkuyuni Wilayani
Nyamagana” alisema Akida.
Kamanda
Akida alieleza kwamba tangu mwezi April na Mei tumekuwa katika hekaheka za
kuwatafuta watu hao baada ya taarifa za kuwepo watu hao wanaojitambulisha kuwa
watumishi na wamekuwa akiwadanganya watu na kufanya kazi ambazo si za ofisi ya
Takukuru ikiwa ni zile za Taasisi zingine za serikali.
Kamanda wa TAKUKURU mkoa wa Mwanza Ayoub Akida |
“Katika
kipindi hicho tuliweza kupokea taarifa za matukio kumi ya kutoka kwa watu
waliotapeliwa katika Wilaya za Misungwi na Jiji la Mwanza ambapo baada ya
kumnasa mtuhumiwa huyu na kumhoji alidai kuwa yeye peke kwa kutumia utapeli huo
ameweza kujipatia kiasi cha shilingi milioni 4,637,000/= kutoka kwa watu kumi
na mbili”alisema Kamanda.
Naye
mmoja wa watu walioathirika na kutapeliwa aliyejitambulisha kwa jina la James
Belindo mkazi wa Nyakato Buzuruga Wilayani Ilemela alisema kwamba alimfahamu
mtuhumiwa kwasababu alikuwa jirani yake naye mtuhumiwa alitumia mwanya huo wa
ujirani akimweleza kuwa kuna magari 12 yameletwa ofisini kwao yaani Takukuru
hivyo kuna nafasi za kazi ambazo anaweza kumuunganishia.
James Belindo mmoja kati ya waliotapeliwa. |
“Alidai
kama nina ujuzi wa kuendesha gari yaani udereva basi nimwambie, nilimweleza
sina lakini kuna jamaa yangu, naye akasema hamna tabu nimpeleke atakuwepo ofisi
ya Takukuru Mkoa, akaomba vyeti na leseni kisha akamweleza kuwa inatakiwa
kufunguliwa majarada matano na kuomba kiasi cha 475,000/- lakini hakupata kazi
hiyo”alieleza kwa masikitiko.
Kamanda
Akida amewatahadharisha wananchi kuwa makini na kundi la matapeli hao
wanaojifanya watumishi wa Takukuru ambao wamekuwa wakiidhalilisha na kuipaka
matope ofisi yake na kuharibu taswira iliyopo kwa jamii na kuwataka kufika
ofisi za Takukuru na kutotoa fedha bila utaratibu wa taasisi hiyo.
Aidha alisema kwamba kutokana na
kuwepo kundi hilo ofisi yake imewataka wananchi kuendelea kutoa taarifa za siri
zitakazofanikisha kunaswa kwa watu hao ambao wamekuwa wakiwadanganya
kuwatafutia kazi,kuwatisha ili wawapatie fedha kunyume na huduma zinazotolewa
na ofisi za Takukuru Wilayani na Mkoa.
No comments:
Post a Comment