https://tpc.googlesyndication.com/simgad/8045142562622600543


Recent Post

Saturday, May 04, 2013

Lady Jay De na hadithi ya mbwa mwenye mnofu mdomoni mwake

Na Kambi Mbwana, Dar es Salaam
NANI amechafua hali ya hewa? Hii ni kauli inayoulizwa mara kwa mara katika matukio yanayokutanisha jamii pamoja na sehemu za majumbani ikiwa ni utaratibu wa kimaisha.
                           Lady Jay De
Katika suala muziki wa kizazi kipya, swali hili naweza kuliuliza kila ninaposikia malalamiko ya wasanii dhidi ya watu Fulani, iwe ni Kampuni, taasisi au kikundi cha watu wachache.
Ruge Mutahaba, Mkurugenzi wa Utafiti na Matukio wa Clouds Media Group
Sugu na Ruge siku walipokutana kwa mara ya kwanza na kusawazisha mgogoro wao. Kulia ni Tundu Lissu wakati kushoto ni aliyekuwa Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo sasa Waziri wa Mambo ya Ndani, Emmanuel Nchimbi.

Kauli ambayo mara kadhaa pia najaribu kuifananisha na hadithi ya mbwa mwenye mnofu mdomoni. Ngoja niiweke wazi kauli hii. Siku zote mbwa mwenye mnofu hawezi kubweka.
Mkurugenzi Mtendaji wa Clouds Media, Joseph Kusaga

Ni mpole anayejilia vyake. Ila inapotokea mnyama huyo ambaye kwa kawaida ameumbwa na kubarikiwa ukali mnofu wake unatolewa ndipo anapoanza balaa.

Kwa wiki kadhaa sasa, msanii maarufu wa muziki wa Bongo Fleva, Judhithi Wambura Lady Jay Dee amekuwa akiwatuhumu watu, hasa mabosi wa 
Clouds Media Group kuwa wanawanyonya wasanii.

Ni kauli ambayo kwa kawaida imekuwa ikisemwa mara kadhaa na watu ambao, ama katika suala hilo, wamekuwa wakisema bila kuangalia chimbuko halisi la malumbano.

Kwa umri wangu mdogo niliokuwa nao, nimeweza kusikia malumbano ya Clouds na baadhi ya wasanii na kujikuta nikibaki mdomo wazi. Malumbano hayo yaliasisiwa na msanii wa Hip Hop ambaye kwa sasa ni Mbunge wa Mbeya Mjini kwa tiketi ya Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Joseph Mbilinyi, maarufu kama Sugu.

Huyu kweli ni Sugu, maana umwamba wake ulionekana, ingawa baadaye muafaka ulitangazwa kwa Sugu na wahusika wa Clouds, akiwapo Ruge Mutahaba kumaliza matatizo yao.

Katika hilo, najaribu kufikiria kuwa kama watu hao walifikia muafaka, ina maana zile tofauti zilizokuwapo awali, zimefikia tamati, huku nikiamini kuwa matawi yote yalivunjwa pamoja na kuimarishwa ushirikiano kwa ajili ya muziki nchini.

Ikumbukwe kuwa, kabla ya muafaka wa Sugu na wadau wa Clouds, kulikuwa na matusi, kashfa nyingi zilizotengenezwa ili kufikisha kilio au kuonyesha umwamba wao.

Tuliwahi kusikia au kuona hata kwenye mitandao kukiandaliwa video za matusi kama njia za makombora ya vita hivyo. Hata hivyo, wakati ambapo sasa hali imetulia, anaibuka tena Jay Dee kwa tuhuma zilizofanana na Sugu na wadau wake.

Si lengo kuchochea moto huo, ila najiuliza swali, wakati wote wa Sugu analalamikia vitendo alivyoita vya kidhalimu, huyu mwanadada alikuwa wapi? Je, ni kweli kuwa wakati huo wa ukimya wake alikuwa na mnofu mdomoni?

Je, ni kweli kuwa sasa mnofu huo haupo kinywani mwake na kuona njia nzuri ni kuibuka kusipojulikana na kuanza kurusha matusi dhidi ya watu anaowaita wanyonyaji wa haki za wasanii.

Nasema tena, katika suala zima la uchambuzi wa sakata hili, kila mmoja yupo huru kuzungumza kila anachokiamini kwa faida ya sanaa na wasanii wetu wa Tanzania.

Binafsi, nimeshangazwa na maneno ya Jay Dee na hakika ameonyesha namna wasanii wasivyokuwa na mawazo endelevu kwa ajili ya kazi zao. Badala yake, wamebakia kuwa watu wa kutoa lawama hata kwa vitu ambavyo havistahili.

Kwa mfano, unaweza kujiuliza swali hili. Msanii analalamikaa kuwa Clouds inambania kazi zake. Swali, hawa Clouds wanafanya kazi za kufanana hadi na vituo vya Redio vya Radio One, TBC Taifa, TBC FM, Capital Redio, Uhuru FM, Times FM na nyinginezo zote za jijini Dar es Salaam pamoja na mikoa yote kulikozagaa vituo vya redio.

Kwa maana hiyo, kama msanii Mr Blue, Dogo Janja, Madee, Juma Nature na wengineo wanalalamikia dhuluma au kubaniwa na Clouds, wana uwezo wa kupekeleka nyimbo zao kwingine na bado maisha yao yakaenda kama kawaida.

Juu ya suala zima la kupunjwa kwenye shoo zinazoandaliwa na Clouds, likiwapo Tamasha lao la Fiesta linalofanyika kila mwaka, pia si lazima msanii alipwe fedha asizopenda.

Kama Profesa Jay, Fid Q, Linah Sanga, Mwasiti na wengineo wanaona shoo zao hazilipi, wana wajibu wa kukataa na sio kufanya kwa shingo upande au baadaye kuja kutoa maneno ya kashfa.

Labda wasanii hawajajua mbaya wao. Wasanii tatizo kubwa halipo kwa Clouds na Ruge Mutahaba au Mkurugenzi wao Joseph Kusaga dhidi ya kashfa wanazopewa kila kukicha.

Tatizo kubwa lipo kwa serikali kushindwa kuweka mifumo mizuri kwa ajili ya jasho la wasanii. Tujiulize, hawa Clouds ndio wasambazaji wa kazi zote za wasanii?

Jibu si kweli. Kumbe serikali pia inaweza kuweka mfumo mzuri wa kuweka mtambo wa kudurufu kazi za wasanii, kuhakikisha kuwa kila kazi inakuwa na stika kuonyesha uhalali.

Ndio wizi wa kazi upo, lakini si kweli kuwa kila msanii anastahili kuwatukana watu wanapoingia kwenye migogoro ya kibiashara. Lady Jay Dee aliwahi kuwa mfanyakazi wa Clouds FM kabla ya kuingia kwenye sanaa na kupata mchango mkubwa wa wadau wake.

Hata kama leo Jay Dee akikataa, lakini Mungu anajua, ndio maana bado nyimbo zake zinapigwa Clouds. Wasanii wa Tanzania ili wafanikiwe kila mmoja ahakikishe kuwa anaacha fitina na kutenda kazi kama inavyotakiwa kwa ajili ya kuinua kiwango cha sanaa.

Ajabu, wapo wanaoingia kwenye migogoro hii, huku ukiangalia nyimbo zake, hazina ubora kuanzia audio hadi video. Sina shaka na uwezo wa Jay Dee, ila wakati wote huo alikuwa wapi?

Kwanini wenye akili zao wasimcheke ujinga? Vipi wale waliojitoa mhanga kwa ajili ya huo wizi unaotajwa kila kukicha? Hatuwezi kwenda hivyo. Kuna mengi yapo chini ya pazia.

Na kama kila mmoja mwenye nafasi ya kusema akipewa nafasi hiyo, utakuja kugundua kuwa kilichopo si kilio cha wasanii, bali wafanyabiashara, ambao wamegundua ili kuendelea kunyonya damu za wasanii, lazima wawagombanishe watu.

Kwa mfano, kama leo kuna mtu anagonga ‘copy’ za wasanii, hakika ataendelea kuifanya kazi hiyo kwa kujiamini, maana wasanii wakubwa wanaendekeza fitina na porojo zisizokuwa na mpango wowote kwa namna moja ama nyingine.

Kuna kila sababu ya kujisahihisha kwa wasanii wetu. Waone kuwa tatizo lao halipo kwa Clouds na wanaojaribu kupita njia za panya kuwagombanisha au kujigombanisha wenyewe suala hilo likomeshwe kwa ajili ya maisha ya sanaa na wasanii.

Naumizwa mno na tabia hii, hivyo kuna haki sasa wasanii kuwekeza zaidi kwenye kazi zao kwa kutunga nyimbo nzuri, kufanya shoo za aina yake na kujitanua Kimataifa, badala ya kuweka porojo matusi, zisizokuwa na maana yoyote kwa sanaa na wasanii kwa ujumla.

Aidha ni wakati kwa wasanii wote Tanzania kuona hakuna haja ya malumbano zaidi ya kushirikiana wao pamoja na wadau wa sanaa kwa ujumla, wakiwapo Clouds FM, ndio maana kutokana na umuhimu wao kila mmoja anaona bila wao hawaendi, ukizingatia kuwa hata Sugu, aliliona hilo na kufikia kukaa chini na kumaliza tatizo kwa maslahi ya muziki.

Bila hivyo, tusubiri malalamiko makubwa zaidi, vilio visivyokuwa na mashiko, maana siku zote nyumba yenye kelele malaika mzuri haishi humo, jambo linaloweza kuwatafuna wasanii wenye mtazamo huo, waliokuzwa na kulelewa vyema na kufikia umaarufu na kuona dawa ni kuanzisha matusi kwa faida wanazojua wenyewe.
0712 053949
0753 806087

No comments:

LinkWithin

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...