SIWEZI KUVUMILIA
Na Kambi Mbwana, Dar es Salaam
NDIO hapo ninaposhangaa kuona waliokuwa kwenye nafasi za
uongozi wanaona njia nzuri ni kuweka siasa kwenye suala zima la michezo,
ukiwamo mpira wa miguu Tanzania.
Juma Kaseja, mlinda mlango wa Simba
Hili kwa kiasi kikubwa linasababisha mpira wa miguu uzidi
kupumulia mashine kila siku, licha ya kuwa na wachezaji wazuri na wenye vipaji
vya aina yake.
Hii siwezi kuvumilia kamwe. Kuna kila sababu ya wadau wa
michezo wakiwamo wa mpira wa miguu kuacha tabia hiyo haraka iwezekanavyo kwa
ajili ya maendeleo yetu.
Nasema hivi nikiangalia zaidi mfumo wetu. Mfumo ambao
kuanzia kwenye klabu hadi kwenye Shirikisho la Soka nchini TFF ni siasa tupu
zinazoendelea kufanywa.
Hii haiwezi kukaa sawa. Angalia, klabu ya Simba imekuwa
chanzo cha kushindwa kuwika katika soka kutokana na siasa. Mwenyekiti wake
Ismail Aden Rage wakati mwingine anashindwa kujibu hoja zenye mashiko, hasa
wanachama wake wanapohoji yenye kuleta maendeleo.
Katika hilo, jibu kubwa analoweza kutoa mwenyekiti huyo ni
kutangaza taratibu za muda mfupi, kama vile kujenga uwanja, licha ya kujua kuwa
hakuna kinachoweza kufanikiwa.
Kwa miaka kadhaa sasa Simba ikiwa na viongozi tofauti
tofauti imekuwa ni watu wa porojo. Porojo ninazofananisha na siasa, maana ndizo
zinazotuharibia kila siku.
Sio Simba tu, ila hata Yanga, ndio wanayofanya kila siku,
jambo ambalo linatakiwa liangaliwe upya kwa faida ya soka Tanzania. Wakati hayo
yanakera kwa klabu zetu, TFF nao ndio aina yao ya maisha, kuweka siasa
kusipowezekana.
Suala la Uchaguzi wa TFF liliingiwa na siasa za kutisha,
hadi kufikia serikali kwa kupitia Waziri wa Michezo kuzuia Uchaguzi huo. Jambo
hilo lilisababisha ujumbe kutoka Shirikisho la Mpira wa Miguu duniani kutua
kuweka mambo sawa.
Kitendo cha kuja kwa watu hao, kumetoa majibu kuwa sisi
hatuwezi kujiendesha bila wazungu. Na hiyo ni kwasababu tunapenda sana kuweka
siasa hata pale pasipohitaji.
Leo hii ujumbe huo wa FIFA umetuma salamu na kutoa mwongozo
wa Uchaguzi kufanyika baada ya kuweka mambo sawa hasa katika baadhi ya kanuni
pamoja na kuundwa Kamati ya Nidhamu.
Kamati hii iliwahi kupigiwa kelele na wadau wa michezo,
akiwamo Michael Wambura aliyekuwa akililia haki yake ya kuchaguliwa katika
Shirikisho hilo nchini TFF.
Wambura alikuwa akiyalilia hayo kwasababu mapungufu
yalionekana sambamba na kuwekewa siasa katika kila anapokwenda au kutaka
kufanya kwa ajili ya kumkwamisha.
Ajabu ni kuwa leo hii kwasababu Wazungu wametangaza hayo
yafanywe, TFF wanakubali. Kwanini? Hii inaonyesha jinsi Watanzania
tusivyojitambua na kusubiriwa kupangiwa na Wazungu hata pale tunapoweza
kufanikisha ya kwetu.
Hii haiwezi kuwa sawa hata mara moja. Lazima tukubali kuwa
tumekwamishwa na tabia zetu za kupenda siasa hata pale pasipohitaji siasa kwa
namna moja ama nyingine.
Huu ndio ukweli wa mambo. Kuna kila sababu ya kutambua
kasoro zetu kama lengo ni kujenga na kuweka tija katika harakati zetu. Mpira ni
kazi inayolipa fedha nyingi.
Watoto wa wenzetu wanachezea fedha nyingi kwa muda mchache,
wakati sisi Watanzania hilo hatulioni na tumeona kuwa porojo ndio mahali pake
na kubaki kama tulivyo.
Hii si njia nzuri hata kidogo. Ni wakati wa kutambua uozo
wetu kwa ajili ya maendeleo ya soka Tanzania. Kwa bahati mbaya, wachache wao
wanaposema ukweli, huonekana wazandiki.
Kila siku nimekuwa nikisema, muhimu ni kufahamu mtu
alipojikwaa na sio kuangalia zaidi alipoangukia. Hatari hii itaendelea kuota
mizizi kila siku ya Mungu, hata baada ya Rais Leodgar Tenga kumaliza muda wake
na kurithi mwingine atakayechaguliwa.
Nchi za wenzetu wamefahamu makosa yao na leo wanasonga
mbele, wakati sisi tupo kama tulivyo licha ya kuwa na watu wengi wenye vipaji
kama vile Mrisho Ngassa, Juma Kaseja, Mwinyi Kazimoto, Nadir Haroub Cannavaro
na wengineo wengi.
Ndio maana nasema ni wakati wetu wa kuacha siasa kwa ajili
ya kufanya kazi kwa moyo ili tuendeleze soka letu kwa maendeleo yetu pamoja na
Taifa letu kwa ujumla.
Kinyume cha hapo badala ya kwenda mbele tutarudi nyuma na
hatuwezi kwenda mbele hata kama klabu zetu au vyama vyetu vya soka viongozwe na
malaika.
0712 053949
0753 806087
No comments:
Post a Comment