Na Dorine Otinga, Eldoret, Kenya
Kama
nilivyoelezea juma lililokwishapita juu ya kura za maoni ya wananchi wa Kenya
wanaosadiki wagombea wao. Nikumbushe tu, wakenya 328 walioulizwa kwenye zoezi
la kura za maoni juu ya uchaguzi walikuwa na mitazamo mbalimbali.
Watu
92% wamekubali kuwa mdahalo kwa njia ya runinga ulisaidia kujua mbinu na uwezo
wa kujieleza wa wagombea wao. Wengine 24% walilazimika kubadili mawazo yao kwa
ajili ya wagombea waliodhani watawachagua.
Wapigakura hawa 34% ina maana
wamebadili mawazo kutoka kwa mgombea mmoja kwenda kwa mwingine. Wakenya 27%
wanadhani Uhuru Kenyatta atashinda uchaguzi.
Wakenya
26% wanaamini Peter Kenneth atashinda kutokana na kufanya vizuri kwenye
mdahalo. Vilevile 22% ya wakenya wanaamini Raila Odinga atashinda uchaguzi na
yeye ndiye bingwa wa ushawishi hadi sasa akiwa na mgombea mwenza, Kalonzo
Musyoka.
Halafu kuna 12% wanapenda kuona Martha Karua akishinda kuchukua
uongozi. Hata hivyo, kuna baadhi ya wakenya ambao hawajaamua iwapo
watapiga kura au la. Waangalizi wa kimaitaifa wameshaanza kuwasilia hapa Kenya
na wanatahadharisha ongozeko la watu watakaoacha kupiga kura.
Sababu
zinazotolewa juu ya baadhi ya wakenya kuacha kupiga kura ni kutokana na yale
machafuko ambayo yalitendeka mwaka wa 2007 na kusababisha maafa makubwa kwa
wakenya. Wengi wao ni walioathiriwa na ghasia baada ya uchaguzi ambao
wamekuwa na uchungu kutokana na mambo yaliyotokea baadaye, huku Uhuru Kenyatta
na William Ruto wakifunguliwa mashtaka huko The Hague, nchini Uholanzi.
‘’Sisi
tulifukuzwa shambani kwetu kule Molo, na tumeishi katika hema kwa muda wa miaka
mitano.Tulijuta sana. Bado sijaamua iwapo nitapiga kura’’, alisema mwanamke
mmoja aliyekuwa katika kambi ya wakimbizi. Ingawa serikali ilifanya juhudi
ya kuwapa wakimbizi hawa mahali pa kuishi kwa muda na kukabiliana na maisha
mapya yenye changamoto kubwa kuliko hali ile waliyozoea kabla ya machafuko.
Nje
ya Kenya wetu wanadhani shamrashamra za siasa katika uchaguzi mkuu zimekuwa
kwenye sura ya mdahalo na upigaji kura pekee. Lakini ukweli ni kwamba watpo
watu wenye uchungu kwa hali iliyotokea.
Mpaka
sasa hivi, bado wengi wao hawajaamua iwapo watapiga kura tena ifikapo Machi 4,
licha ya wapigakura milioni 14.3 kuandikishwa na kupata sifa zote za kuchagua
viongozi. Hili limekuwa kero kubwa kwa Tume huru ya Uchaguzi, na inaelekea
Mkuu wa Tume hiyo, Isaac Hassan atakuwa na jukumu lingine kuwaelezea wakenya
umuhimu wa kushiriki kikamilifu zoezi la kupiga kura.
Baadhi
ya vituo vya habari vimeungana kwa nguvu kubwa sana na kuanzisha midahalo
isaidiayo wakenya kujua ni kiongozi yupi atakayefaa kuchaguliwa ifikapo Machi
4. Juhudi hizi zimeongeza usikivu mkubwa sana kwa vituo vya habari, kwani
vimefanya kazi ya kueneza uzalendo wa wakenya.
Kulingana na mdahalo wa
kwanza ambao ulihusishwa na runinga ya Citizen na vituo vingine, mgombea
Mohamed Abduba Dida, ambaye ni mgeni katika ulingo wa siasa aliweza
kuinua umaarufu wake kutokana na uwezo wake wa kujieleza, kipaji chake cha
kushawishi hadhira na vile vile ucheshi wake ambao uliamsha hisia za wananchi.
Raila
odinga na Uhuru Kenyata walisalia maarufu zaidi kutokana na kuwa kwenye ulingo
wa siasa. Mpaka sasa Odinga na Uhuru wanachuana vikali, huku taasisi za utafiti
zikionyesha wanakaribiana sana kwa kujipatia ushindi.
Mathalani, duru za
kisiasa zinasema kwamba Uhuru Kenyatta na William Ruto hawatahudhuria mdahalo
wa mwisho utakaofanyika kabla ya uchaguzi. Jambo hili limezua mjadala mkubwa
hapa Kenya, ambapo wengi wanajiuliza kulikoni wasiweze kupanga njia za
kufanikisha mdahalo badala yake wanakataa kuhudhuria?
Lakini
kwa upande wao Uhuru na Ruto wanasema licha ya Changamoto ambazo zimewakumba,
ikiwemo kesi katika mahakama ya ICC, wao wanaendeleza kampeni zao bila wasi
wasi. Ilikuwa ni afueni kwao, baada ya Mahakama Kuu ya Kenya kusema
kwamba, haiwezi kuwazuia kugombea kiti cha Urais, na kwamba uamuzi huo ungeweza
kuamuliwa na Mahakama ya rufaa. Akielezea sababu za kujitoa
kwenye mdahalo wa mwisho, Uhuru Kenyatta alisema kuwa katika mdahalo
uliomalizika hakutendewa haki hivyo haoni sababu za kushiriki tena.
Uhuru
akielezea hilo amesema kitendo cha kuingizwa kesi iliyoko ICC kiliudhi kambi
nzima ya Jubilee hivyo anastahiki kufuata ushauri wa kambi hiyo kujiondoa
kwenye mdahalo wa mwisho kabla ya uchaguzi. Aidha, kumekuwa na tetesi
kutoka kwa wanachama wa ODM, ambacho kinaongozwa na Raila Odinga, kwamba
wanachama wa Jubilee wana mpango wa kuhakikisha mgombea wao Uhuru Kenyatta anashinda
kiti cha urais kwa hali yoyote ile.
Suala
hili limewatia wakenya tumbo joto kwani hawataki ghasia, wanaona kitendo cha
wanachama wa Jubilee kung’ang’ania kupata ushindi kwa namna yoyote ile ni
kutaka kuchochea ghasia miongoni mwa wakenya ambao wanataka
utulivu. Wanachama wa ODM wanadai kuwa Jubilee wanataka kuiba kura ili
mgombea wa Jubilee, Uhuru Kenyatta ashinde kiti hicho, jambo ambalo
hawajathibitisha hadi sasa.
Hii
imekuwa kashfa ya kwanza kutolewa kwenye kampeni za uchaguzi zinaoendelea hapa
Kenya. Aidha, hawa ODM hawasemi ni namna gani Jubilee ya Uhuru Kenyatta
watakavyoiba hizo kura, bali wanaendelea kushutumu na kuchochea matumbo moto
kwa wapigakura. Chama cha Jubilee ambacho kinaongozwa na Uhuru Kenyatta na
mgombea mwenza Wiliam Rutto, kimejaribu kufanya kila njia kupinga tetesi
za wanachama wa ODM wanaoongozwa na Raila Odinga kwamba walitaka kuiba
kura.
Wengi
wanasema haifai kwa ODM na Odinga kueneza fitina kama hii ambayo haina chembe
ya ukweli. Wanasema kama Odinga hakujifunza kwa Uhuru Kenyatta na Ruto juu
ya mashtaka yao kule ICC, ni vema akachunga kauli zake uchwara ambazo
zinachochea uharibifu wa amani kwa wapigakura.
Kulingana
na utafiti ambao umefanywa na baadhi ya kampuni nchini Kenya, Raila Odinga
anamshinda Uhuru Kenyatta kwa asilimia chache sana, huku wakifuatwa na wagombea
wengine. Wagombea hawa wawili wanafuatana uso kwa uso na wakenya
wanatarajia mmoja wao kuibuka mshindi baada ya uchaguzi wa Machi 4, mwaka huu.
Huku
uchaguzi ukikaribia, serikali iliamua kuunda Tume ya Taifa ya Uwiano na
Utangamano, ikiwa na lengo la kuwaunganisha Wakenya na kuwachukulia hatua
wakali wanasiasa na wananchi wanaotoa matamshi ya kichochezi. Mwenyekiti
wa tume hiyi ni Mzalendo Kibunja, ambaye amesema Tume yake haitamuonea aibu mwanasiasa
na mwananchi yeyote atakayeleta uchochezi kwa wakenya. Wengi wanakumbusha
ikwemo hatua ya ODM, kusema Jubilee wataiba kura, kuwa inabidi Mzalendo Kibunja
achukue hatua kali zaidi dhidi yao.
Katika
mahojiano na mwanahabari Jimmy Gathu wa kituo cha Citizen hapa Kenya, Mzalendo
Kibunja, alisema kuwa wale wote wanaoeneza matamshi ya kichochezi na chuki
watachukuliwa hatua kali.
Hatua
ya tume ya Uwiano na utangamano, imekwenda mbali zaidi na imewaonya wanaotumia
mtandao wa facebook na Twitter kuwa makini kwa maandishi yao wanayowaeleza
wenzao kuhusu uchaguzi mkuu wa hapa Kenya.
Uhuru Kenyatta
Jaji
mkuu wa Kenya Dk. Willy Mutunga ametangaza kuwa anatishwa na baadhi ya
wanasiasa, hali ambayo inamfanya asiwe na amani na kukisia kuwa huenda uchaguzi
huu unaweza kuwa na machafuko pia. Jaji Mutunga anadai kuwa vitisho hivi
vinamshinikiza kutekeleza maslahi yao badala ya kujali uamuzi wa wakenya kwenye
uchaguzi.
Hata
hivyo, Jaji huyo alisema kwamba vitisho dhidi ya Idara ya Mahakama
havitawafanya majaji kutekeleza maslahi ya kundi fulani la watu. Jaji alisema
kwamba alipokea vitisho hivi karibuni wakati wa kesi iliyowahusisha Uhuru
Kenyatta na William Rutto ilipokuwa ikisikilizwa huko nchini Uholanzi.
Alieleza
jinsi ujumbe wa barua aliyoipokea ilivyokuwa ikimtisha, na kwamba angetendewa
jambo baya na kundi haramu la Mungiki, iwapo angetoa uamuzi wasioupendelea
katika kesi ya wawili hao.
Mwaka
wa 2007, ilisemekana kwamba Uhuru Kenyatta alitumia kundi hili
kuwaangamiza Wakalenjin Mkoani Rift Valley. Jaji Mutunga analaumu serikali kwa
kumdhulumu baada ya kuamrishwa na afisa mmoja wa uhamaji, kusafiri kwenda Dar
es Salaam kwani hakuwa na idhini ya mkuu wa Umma, Francis Kimemia.
Jaji
mkuu ameeleza hofu yake ya majaji kutishwa kisiasa huku uchaguzi ukikaribia
kwani inahatarisha usalama wao na kuiweka nchi kwenye hatari ya
machafuko. Jaji huyo alitangaza msimamo wake kuwa hatatishika na kama
mmoja wa wapiganaji wa demokrasia, yuko tayari kwa lolote.
Jambo
jingine ambalo linafanyika katika uchaguzi huu ni matayarisho ya karatasi za
kupigia kura yanayofanywa na Tume Huru ya Uchaguzi (IEBC). Pia IEBC imeamua
kuachana na majaribio ya uchaguzi yaliyopangwa kufanyika mapema Februari
24.
Katibu wa IEBC, James Oswago alisema kuna kazi ngumu kufanya majaribio
badala ya uchaguzi kamili. Hivyo mashauriano yalifanyika kwamba majaribio
yafanyike Februari 18 yaani Jumatatu iliyopita ili kuwaruhusu wananchi
kupigakura kwa ufasaha ifikapo Machi 4.
Naye
meneja wa Elimu kwa wapigakura IEBC, Nixon Ng’ang’a alisema kwa mara ya kwanza
katika historia ya hapa Kenya, wapigakura watakuwa wanpiga kura kwa nafasi za
uchaguzi sita na siyo tatu, hivyo watahakikisha zoezi linakwenda
vema. Kwingineko ni shamrashamra zinazoendelea hapa, kwani IEBC imesema wagombea
wote nane wanatakiwa kufanya kampeni za amani ili kuwalinda wakenya dhidi ya
machafuko.
Dorine
Otinga ni mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Egerton nchini Kenya na atakuwa miongoni
mwa wasimamizi wa uchaguzi huo.
No comments:
Post a Comment