Mratibu wa Ruaha Marathon, Albert Sanga
Na Kambi Mbwana, Dar es Salaam
MRATIBU wa mashindano ya riadha
ya Ruaha Marathon, Albert Sanga, amesema kwamba wanaamini mbio hizo
zitafanikiwa kwa dhati kutangaza utalii wa ndani, kwa kushirikisha wanariadha
zaidi ya 2500 kutoka nchi mbalimbali duniani.
Mashindano hayo yamepangwa
kufanyika Mei 25 mwaka huu mkoani Iringa, ikiwa ni mara ya pili kufanyika baada
ya mwaka jana kufanyika pia kwa mafanikio makubwa.
Akizungumza kwa njia ya simu
kutoka mkoani Iringa, Sanga, alisema kwamba lengo ni kuhakikisha kuwa
wanaendeleza mchezo huo pamoja na kutangaza utalii wa ndani kwa kuona kuwa watu
kutoka nchi mbalimbali wanashiriki.
Alisema kuwa Ruaha Marathon ni
kwa ajili ya Watanzania wote, huku lengo lingine ni kukusanya fedha za
kuwasaidia watoto walemavu.
“Mamia ya washiriki kutoka Italia,
Canada, Marekani, Uingereza, Australia, Kenya, Ethiopia, Afrika Kusini na nchi
nyingine wamethibitisha ushiriki wao kwenye mashindano hayo yenye mguso mkubwa
mkoani Iringa na Tanzania kwa ujumla.
“Naamini mambo yatakuwa mazuri
kwa kuona kuwa tunafanikisha mashindano haya kwa kiwango cha juu na kuendeleza
sekta ya michezo pamoja na kutangaza utalii wetu ambao kwa hakika utakuwa na
tija kwa namna moja ama nyingine,” alisema.
Kwa mujibu wa Sanga, watu wa
kada mbalimbali, wakiwamo mawaziri, wabunge na wengineo nao watakuwapo kwenye
mashindano hayo kuangalia kila kitakachojiri kwa siku hiyo maalum ya Ruaha
Marathon mkoani Iringa.
No comments:
Post a Comment