Mwenyekiti wa CCM Handeni, Athumani Malunda
Na Kambi Mbwana, Dar es Salaam
CHAMA Cha Mapinduzi (CCM), kipo kwenye wakati mgumu kutokana
na makundi ya vijana kutaka kurudisha fomu baada ya kuwekewa ngumu katika
mahitaji yao, yakiwamo ya kutaka kuita waganga wa kienyeji, maarufu kama
lambalamba kwa ajili ya kutoa uchawi.
Sakata hilo linawasumbua viongozi na watendaji wa CCM katika
wilaya ya Handeni, mkoani Tanga, hasa kutokana na ushawishi wa watu wanaotaka
kurahisisha shughuli hizo za kutoa uchawi.
Habari kutoka katika baadhi ya vijiji vya wilaya ya Handeni,
zinasema kuwa sehemu nyingi za wilaya hiyo, kumekuwa na kelele za wananchi
kutaka kuitisha waganga kwa kufanya kazi katika maeneo yao.
Watu wengi waliozungumza na Handeni Kwetu, walisema kuwa
kama serikali itaendelea kukataa kwa kile wanachokitaka, basi watarudisha kadi
za CCM na kuviunga mkono vyama vingine.
"Sisi kwenye eneo letu tupo wananchi zaidi ya 300 ambao
tunaamini ni wanachama hai wa CCM kwa namna moja ama nyingine, bila kuingiza
wale wasiokuwa wanachama lakini tunaimba wimbo mmoja.
"Kwanini serikali ikatae kila kitu, kwani pesa wanatoa wao?
Kuhusu vurugu, sisi tunataka kufanya mambo yetu kistaarabu kwa kuimalisha
ulinzi sisi wenyewe, inashangaza kwanini serikali inashindwa kukubali mawazo
yetu,” alisema mmoja wa wananchi ambaye hakutaka kutaja jina lake.
Akizungumzia sakata hilo, Mwenyekiti wa CCM, wilayani
Handeni, Athumani Malunda, alisema kuwa serikali haiamini ushirikina kama
isivyoamini dini za wananchi wake.
Ni kweli kuwa maeneo mengi ya wilaya ya Handeni
yanasumbuliwa na mambo hayo, hasa kutokana na wananchi wengi kutaka kuitisha watu
wa kutoa uchawi, kadri ya vile wanavyoamini.
Katika suala hili kuna utaratibu wake, hivyo nafikiri
watendaji wa serikali, akiwamo Mkuu wa Wulaya ya Handeni analifanyia kazi suala
hili kwa ajili ya kuhakikisha kuwa mambo yanakuwa mazuri,” alisema Malunda.
Mbali na Handeni, lakini pia wilaya ya Korogwe inatafunwa na
suala hilo, huku pia maeneo mengi ya jiji la Dar es Salaam kukutana na zogo
hilo la wananchi kuita watu wenye kutoa uchawi.
No comments:
Post a Comment